The Chant of Savant

Saturday 27 June 2009

Hongera Kikwete kumteua Pita Noni


Japo watu wengi wametilia shaka uteuzi wa ‘mchapakazi’ Pita E M Noni kuwa mnene wa Benki ya Raslimali (TIB), nachukua fursa kuwapongeza wote wawili yaani mteuzi na mteule kwa kutuacha hoi. Si haba. Vitu vyao tumeviona na ujumbe umefika. Sasa mapambano dhidi ya ufisadi yameiva.

Kwanza , ikumbukwe. Noni, kwa wakubwa na maslahi yao , ni mchapakazi hakuna mfano duniani. Alisimamia vilivyo zoezi la EPA kiasi cha kutoacha mwanya wa makosa. Maana hata sanaa za kuwafikisha wahusika mahakamani, zinavyoonyesha, zitaishia kama watuhumiwa wa Richmond ambao hivi karibuni waziri wa bora utawala alisema hawawezi kuwajadili kwa vile sheria za kubuni haziruhusu. Kituko zaidi ni pale mama waziri mwenye jina la mnyama anayetisha alipoongopa eti Richmond haikupewa hata ndururu!

Pamoja na Noni kutajwa vibaya kwenye wizi wa EPA naye asikanushe, bado kwa wakubwa anafaa sana . Wengi walidhani angeingia kwenye kundi la akina Iman Mwankosya. Wamenoa. Haingii mtu mwenye connections.

Rais Jakaya Kikwete amekuwa bingwa wa kuteua watu wanaoamsha hisia na mjadala. Alianza na swahiba yake Edward Lowassa. Bahati mbaya hakudumu baada ya kuonyesha sura yake halisi. Kwa waliojua uhusiano wao na shutuma alizoziacha marehemu Mwalimu Julius Nyerere, walikuna vichwa kiasi cha kuota ukurutu walipotaarifiwa kuwa jamaa angekuwa waziri mkuu. Na kweli, mwanaharamu hata umuweke kwenye chupa atatoa kidole, hakuchelewa kufanya vitu vyake kiasi cha kutimka kabla ya wakati wake!

Uteuzi mwingine ulioamsha hisia na mijadala ni ule wa Joe Mgosi Makamba bingwa wa mipasho kuwa katibu mkubwa wa chama chake. Hadi sasa hakuna anayejua siri na sababu ya kumteua mtu tata kama huyu ambaye si haba amekijenga chama kwa njia ya ‘bomoa tutajenga kesho’. Amesababisha mijadala mingi ndani na nje ya chama. Hii ni kutokana na mipasho yake ambayo kuvuka mipaka hata kuwaudhi walengwa ni jambo la kawaida. Jamaa mwenye breki moja linapokuja suala la kupayuka.

Pia uteuzi wenye kusisimua ni ule wa aliyekuwa waziri wa miundo mbinu na mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge. Akiwa ameboronga sana kwenye utawala kidhabu wa Benjamin Mkapa, hakuna aliyetarajia mtu yeyote mwenye uchungu na nchi, busara na uelewa wa mambo angemteua mtu kama huyu. Lakini alimteua na ukweli ukajidhihirisha baadaye alipogundulika kuwa ametutika mabilioni ya shilingi kisiwani Jersey aliyoyaita vijisenti. Hadi sasa ni ajabu ya maajabu kwa jamaa huyu kuendelea kuwa mheshimiwa huku akilalia mabilioni ya shilingi toka kwenye dili la rada.

Huo ndiyo uteuzi wa bingwa wa kuteua ambaye kwa msimamo hana tofauti na ruba aamuapo lake. Wengi, hadi leo, hawajui siri ya silka hii. Jamaa atakuchekea hata umuudhi vipi ilmradi mwisho wa siku lake linakuwa .

Uteuzi ambao unaweza kuingia kwenye kitabu cha maajabu cha Guiness ni ule wa Rweka Mka-ndala, kada maarufu wa CCM kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Manzese. Madhira ya blanda hii wanayajua wengi hasa wanafunzi. Migomo, migongano juu ya mikopo ya elimu ndiyo usiseme.

Uteuzi mwingine ni ule wa Kingungi Ngombaru Mweru kuwa mshauri wa rais na mbunge. Jamaa kwa umri wake, kama tutamtendea haki, alipaswa kukaa nyumbani akacheze na wajukuu. Maana ukiangalia kwenye safu za uongozi nchini, hakuna rika lake hata mmoja.

Uteuzi mwingine uliowaacha wabongo vinywa wazi ni ule Basie Pesatatu Mramba kuwa kwenye baraza la mawaziri huku akiwa anajulikana alivyovurunda kwenye awamu ya tatu. Na hapa si Mramba peke yake, karibu wengi wa waliokuwa wakitiliwa shaka kwenye utawala uliopita aliwateua na anaendelea kufanya vitu vyake nao! Jamaa hatutamsahau hasa kwa nyodo zake za kutwambia tule majani ili anunua dege la rais na ten percent ifanikiwe.

Ukienda kwenye uteuzi mwingine kama vile wa mabalozi na majaji hata wakuu wa wilaya na mikoa unabaki kukuna kichwa na kuugulia. Wapo wanaompakazia Kikwete kuwa katika uteuzi wake huwa anaangalia mitandao, imani na wapi mtu atokako. Sie hatukubaliani na hili. Tunajua wazi kwa katiba yetu uoza na viraka, rais anaweza kumteua mkewe hata bibi yake kushika wadhifa wowote atakao kumpa iwe ni fadhila, takrima au vinginevyo.

Uteuzi mwingine ambao uliwaacha wabongo hoi ni ule wa mkurugenzi wa mawasiliano ikulu, Silva Rweye ambaye hakuna ubishi kuwa wakati wa kampeni aliitumia kalamu yake kumjenga Kikwete huku akiwabomoa wengine. Ingawa kufanya hivyo ni kinyume cha taaluma, si haba anapeta ukiachia mbali kuzua utata kutokana na majibu yake ambayo ukiyapima vizuri unahoji what’s up upstairs. Mfano aliwahi kusema kuwa kama serikali ingemtaka Daud Ballali ingemkamata. Ajabu wakati akipayuka hivyo, Ballali alikuwa akitakiwa atiwe mbaroni kujibu tuhuma za ujambazi wa EPA. Hata hivyo maneno ya Rweye yalikuja kuthibitika kuwa ya kweli pale Ballali alipopatikana na kufa kifo cha utata hadi kesho.

Jamaa huyu enzi zake kabla kalamu haijawa biashara mnadani aliweza kuitumia kumtoa fisadi yeyote roho kwa ugonjwa moyo. Wahenga walisema: mchawi mpe mtoto. Baada ya kuonjeshwa mahanjumati ya ukuu na ulaji wa dezo mbona aliweza kuyalamba manonihino yake bila hata chembe ya aibu! Kweli njaa ni ugonjwa mbaya sana hasa inapopanda kichwani.

Bado kuna uteuzi wa wazito kama Daudi. Matakataka, na vunja mbavu huu wa Noni ukiachia mbali ule wa Larensi Masha ambaye licha ya kuwa na uhusiano na mwanae kampuni yake iliguswa kwenye kashfa ya EPA.

Kinachofurahisha ni kwamba awamu ya kwanza ya utawala wa Kikwete umefanya yote haya ukijua changamoto yake kwa wapiga kura. Je kwenye ngwe lala salama tutaona maajabu gani? Ni suala la kukaa na kungoja. Muhimu ni kwa wapiga kura kufikiri mara mbili kama watataka kuepuka na kadhia na jinai kama hizi. Kimsingi dawa ya haya yote wanayo wapiga kura.



Tusisahau uteuzi wa Kikwete kwenye msimamo wa kumkingia kifua mtangulizi wake Benjamin Mkapa na hata harakati za sasa za kutaka kuchota pesa ya wanuka njaa wa Bongo kuipa Kiwira .

Utuzi wa mwisho wa Kikwete uliovutia wengi ni pale alipojiteua hivi karibuni kugombea urais kwa tiketi ya chama hata kabla ya muda kufika!

Tumalizie tulikoanzia. Kwa wale wanaoohoji na kushangaa Noni anakwenda TIB kwa sifa na kazi zipi wakumbuke. TIB ndipo zitakapowekwa pesa zilizorudishwa na majambazi wa EPA ambao Noni anawafahamu vizuri. Hakuna shaka huko nako atazishughulikia pesa hizi na kufanikisha uchaguzi mwakani. Nani hajui kuwa na siasa hasa vyeo vya juu ni investment tosha?

Hongera Kikwete kumteua Noni na wengine tuliowataja hapojuu. Si haba vitu vyako tunaviona na hakika kwa timu kama hii lazima tufike Misri kabla ya kuelekea Kanani.
Chanzo: Tanzania Daima, Juni 24, 2009.

No comments: