The Chant of Savant

Wednesday 5 August 2009

Ngeleja, Mkapa na usanii wa Kiwira


TAARIFA zilizotolewa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuhusiana na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kurejeshwa serikalini kinyemela haziwezi kupita bila kulaaniwa na kupingwa.

Pia uzushi kuwa ANBEN, Kampuni ya Anna Mkapa na Benjamin Mkapa ilijitoa mwaka 2005, haziwezi kupita bila kushutumiwa na kukalipiwa.

Kwanza ifahamike, waziri anataka kuuhadaa na kuupotosha umma kwa kudai kuwa Mkapa na mkewe walijitoa kwenye mradi wa kuhujumu Kiwira. Waziri anataka kumgeuza nani bunga? Mkapa na mkewe watajitoaje iwapo watoto wao na Kampuni yao la Fosnik wamebaki?

Je, walijitoa kwa sababu gani, tena ndani ya kipindi kifupi cha kuasisi dili hili huku Mkapa akiwa bado yu madarakani? Je, ni kweli walijitoa au ni danganya toto na mazoea ya usanii wa watawala wetu waliopo madarakani?

Kuonyesha habari hizi zilivyo sanaa na ujambazi wa mchana, eti waziri anasema serikali itawafidia wezi waliojitwalia mali ya umma kinyume cha sheria! Hawa ni watu wa kufikishwa mahakamani na kuitwa wahujumu wa uchumi moja kwa moja hata kama wana madaraka.

Wanalipwa kwa jema gani iwapo mradi mzima uliibiwa kutoka mikononi mwa umma kwa bei ya kutupwa? Je, waziri anadhani umma umesahau jinsi Mkapa na wenzake walivyojitwalia mgodi wa Kiwira kwa bei ya karibu na bure?

Hebu fikiria mali ya 4,000,000,000 inauzwa kwa bei ya shilingi 70,000,000. Huu ni wizi na uhujumu uchumi hata upakwe mafuta vipi. Na huu ni ushahidi kuwa utawala wa sasa ni fisadi na mshirika mkuu wa jinai hii.

Mkapa na mkewe wanaweza kuwa wamejitoa vipi iwapo maswahiba wao bado wanaendelea kushirikiana na watoto wao katika dili hiyo?

Je? serikali imeamua ‘kuitwaa’ Kiwira ili kumuepusha Mkapa kupambana na hasira ya umma na kumkingia kifua kama alivyoahidi Rais Jakaya Kikwete au kuna namna wakubwa wa serikali ya sasa walifaidika na mradi huu au ufisadi huu? Je, watawala wetu wanalipa fadhila kutokana na Mkapa kuidhinisha benki yetu kuu ivunjwe ili kupata mtaji wa kuingilia madarakani?

Je, wanaamua kufanya hivyo kwa kuogopa Mkapa asiwafichue kuwa nyuma ya wizi na ujambazi wa EPA na Richmond? Hivyo wanaona wamuhifadhi kabla hajawaumbua? Je, kwa serikali kama hii inayoshirikiana na wahalifu kweli tunaweza kupamba na ufisadi unaozidi kugeuka donda ndugu nchini?

Je, wakuu wa serikali ya sasa wana mpango wa kufanya kama alivyofanya Mkapa, mkewe, watoto na marafiki ili baadaye wajilipe fidia kama wanavyopendekeza kwa Mkapa? Maswali ni mengi kuliko majibu.

Ikumbukwe. Kabla ya Ngeleja kuja na dili la kurejesha Kiwira serikalini, aliwahi kulihadaa Bunge na taifa zaidi ya mara nne akisema angefichua wamiliki wa Kiwira. Sasa badala ya kutimiza ahadi yake anakuja na sanaa nyingine za kumuokoa bosi wake Mkapa! Je, umma wa Watanzania wenye mali watakubali kugeuzwa majuha na kuchezewa mahepe mchana kweupe?

Hebu angalia sanaa za waziri kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari. Inatia kinyaa na inatisha kama wananchi wenye mali wataukubali upuuzi huu ambao kimsingi ni wizi wa mchana.

“Januari mwaka 2005 (siku 13 tangu kuanzishwa kwa TPR), ANBEN iliondolewa kuwa miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa TPR, hivyo wamiliki wa TPR waliobaki walikuwa wanne.”

Haiwezekani Rais Mkapa na mkewe washindwe kulipia hisa zao lakini watoto wao waweze. Huu ni uongo wa mchana na waziri hakufanya ‘home work’ yake vizuri katika kutunga uongo huu unaolenga kuhalalisha uhujumu wa taifa.

Tuambizane ukweli bila kumung’unya. Ukweli ni kwamba dili hili linaihusisha Serikali ya Awamu ya Nne moja kwa moja na ndiyo maana Mkapa na wenzake wamekuwa na kiburi cha kutotaka kutoa maelezo. Kwani wanajua nyuma yao kuna nani. Na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete aliamua wazi wazi kumkingia kifua bosi wake wa zamani na mshirika wake zilipofumka tuhuma za uhujumu na ufisadi.

Kwani katika maelezo ya Ngeleja kuna ukweli usiopingika kuwa mwizi mkuu hapa si Mkapa pekee, bali hata serikali. Alibainisha kuwa, mkataba wa kuendeleza mradi wa Kiwira kati ya serikali na Kampuni ya KCML, uliingiwa Machi 24, 2006 kwa kutia saini makubaliano ya makusudio (Agreement of Intent-Aol) na mikataba ya Power Purchase Agreement (PPA), Implementation Agreement (IA), Escrow Agreement (EA), Transmission Line Facilities Agreement (TLFA) na Facility Transfer Agreement (FTS), ilitiwa saini Agosti 2006.

Je, serikali iliingiaje mkataba na kampuni ya kijambazi huku umma ukipiga makelele kama si mhusika mkuu? Je, serikali iko tayari kutoa maelezo kwanini imekuwa ikiwakingia kifua mafisadi kila wanapobainika?

Rejea kuendelea kugeuka muujiza kwa kampuni dokozi la Kagoda, kuendelea kutoshitakiwa kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na wenzake, kutokana na kubainika walishiriki ufisadi, kutofikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wa ufisadi wa EPA na wengine na yote katika yote, kutaka kulipa fidia kwa wezi wa Kiwira.

Je, serikali ya namna hii si fisadi wa kutupwa? Ingawa Ngeleja, bosi wake, Mkapa na wengine wanaweza kujiridhisha kuwa wametua mzigo, ukweli ni kwamba mzigo bado ni mbichi na historia itawahukumu kwa ukali wote siku moja.

Nani alijua kuwa mtawala mbabe kama Mkapa angetiwa adabu kiasi cha kutegemea kulindwa na rais huku akiendelea kuishi maisha ya aibu? Tunaitaka serikali iwafungulie mashitaka wezi wa Kiwira badala ya kuwazawadia pesa yetu.

Baada ya kugundua kuwa kisingizio cha Mkapa kuwa na kinga hakiwezi kuwaokoa mkewe na wanawe, sasa serikali imeamua kuua ushahidi kwa kuutwaa mgodi wa Kiwira huku ikitenda kosa moja ambalo siku moja italijutia-kuwafidia kwa unyakuzi wao.

Ngeleja, mwakani unakabiliwa na uchaguzi. Kama umma utaweka nukta, Mkapa amekutoa kafara, kwani huna sababu ya kurejea bungeni kuendelea kuwatetea mafisadi huku ukiwatelekeza wananchi.

Ukistaajabu ya Musa utaona ya Filauni. Hakika huu ni usanii wa Ngeleja, Mkapa na serikali kuendelea kuuibia umma bila aibu. Na hakika, huu ni ushahidi tosha kuwa serikali yetu haina nia ya kupambana na ufisadi ambao mazingira yanaonyesha inautenda tena bila aibu.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 5, 2009.

No comments: