The Chant of Savant

Thursday 8 April 2010

Wafanyakazi watendewe haki

KWA mtu anayejali kujua ugumu na mazingira magumu wafanyakazi wetu hasa wa kada ya chini wanavyopambana navyo huku wakizalisha na kushuhudia uchumi ukifujwa na wanasiasa, ana kila sababu ya kuunga mkono mgomo uliopendekezwa na wafanyakazi nchi nzima.

Wengi walidhani serikali ingechukulia tishio hili kwa uzito unaostahiki badala ya kutoa majibu yasiyo na mashiko.

Wengi walidhani serikali ingekubali lawama zote kutokana na wanasiasa kutumia vibaya rasilimali na jasho la wafanyakazi na wakulima wa taifa hili, ukiachia mbali mipango mibovu na sera za kuazima na kubabaisha.

Kwa wanaojua madhara ya mgomo hasa kwa uchumi unaosuasua kutokana na usimamizi na matumizi mabovu ya serikali, maneno ya Rais Jakaya Kikwete hayatoi jibu zaidi ya kutapatapa na kuwekana sawa. Je, hili ni jibu linaloingia akilini?

Hivi karibuni Rais Kikwete alikaririwa akisema: “Nayasema haya kwa kuwa naamini kwa dhati kuwa huo ndio uamuzi wenye maslahi kwa taifa letu na kwa wafanyakazi pia.

Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kufikia kwenye malengo yenye masilahi kwao na kwa waajiri wao.” (Hapa alimaanisha majadiliano).

Kusema ukweli majadiliano yameishapitwa na wakati. Yalianza wakati wa serikali ya awamu ya pili. Lakini tabia ya serikali kukaidi ahadi zake na kukiuka taratibu imeendelea kuwapo kwa zaidi ya miaka 20.

Hatuwezi kuendelea hivi wakati wafanyakazi wakijituma huku watawala wakiongeza ukubwa wa serikali matumizi bila ulazima wala kujali wale wanaozalisha hicho wanachofuta.

Rais aliambiwa kabla ya kuingia madarakani kuwa mtangulizi wake alikuwa ameunda serikali kubwa. Yeye alipoingia kwa kiburi na kutojua madhara yake kwa uchumi aliunda kubwa kuliko iliyokuwa ikilalamikiwa.

Rais ameishaonywa na vyama vya upinzani na wataalamu wa uchumi kuwa ziara zake na matumizi yasiyo na nidhamu na ufisadi ni vikwazo kwa uchumi wetu.

Amefanya nini kuhusu haya zaidi ya kuziba masikio na kuendelea kufanya yale yale?

Nchi ndogo jirani ya Rwanda na hata Kenya wamepiga marufuku matumizi ya mashangingi. Tanzania waliahidi wangefanya hivyo. Lakini katika kipindi hicho hicho ziliripotiwa taarifa kuwa walikuwa wameagiza mashangingi!

Pamoja na wakati ule serikali ya nchi fukara kuwa na mashangingi 6,000 na ushei waliweza kuendelea kuagiza mengine kinyemela kana kwamba umma hauna macho.

Hivi ni wafanyakazi gani vichaa watakaokubali madai kuwa serikali haina fedha wakati inasamehe mabilioni ya EPA, Kagoda, Richmond, TICTS, Meremeta, CIS, Kiwira ukiachia matumizi mabaya na ufisadi na kuchanganya siasa na uchumi?

Je, wafanyakazi watasikiliza ushauri wa rais ambaye huwa hasikilizi ushauri wa Watanzania?

Je, rais anadhani wafanyakazi ni vipofu wasioweza kuona nchi, rasilimali zao vinavyofujwa? Je, rais anadhani wafanyakazi hawaoni yanayofanyika? Tutoe mfano.

Katika sakata la uzembe na uhujumu wa Kampuni ya Kihindi ya RITES, wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli waliweza kujikusuru na kufufua baadhi ya vichwa vya treni lakini serikali ikawaangusha hadi maji yalipozidi unga.

Je, wafanyakazi kama hawa rais atawaridhisha na nini zaidi ya kutimiza madai yao? Hawa si wapumbavu kama wanasiasa wanavyowachukulia.

Wanajua wenzao waliostaafu hasa wale wa Jumuia ya Afrika Mashariki walivyodhulumiwa na kuhujumiwa na serikali hii hii inayotaka waingie kwenye mazungumzo iwazidi kete. Walimu wanajua ninachomaanisha hapa.

Serikali haina sifa ya kuaminika katika ahadi na makubaliano yake. Ni mara ngapi serikali imeingia makubaliano nao na baadaye ikawageuka?

Leo tuna wanasiasa wanaolipwa mamilioni wakati madaktari, walimu na wafanyakazi wengine wakikopwa mishahara yao ukiachia mbali kuhujumiwa haki zao.

Mara nyingi wafanyakazi wameingilia bila mafanikio kuzuia wezi wachache katika serikali kuingia mikataba inayohujumu nchi kama ile ya uwekezaji uliogeuka utumwa na hujuma kwa taifa. Nani anawasikiliza badala ya kusikiliza ten percent?

Rejea wafanyakazi wa iliyokuwa NBC walivyojaribu kunusuru benki yao bila mafanikio, ukiachia mbali wa TANESCO lilipoletwa kampuni la kikaburu lililoiacha ikiwa mkangafu kama alivyowahi kukiri mkurugenzi wa zamani wa shirika hili.

Uliza serikali inadaiwa pesa kiasi gani na mamlaka ya maji safi na taka na TANESCO? Bila serikali na wakuu wake kuwajibika hatuwezi kupata jibu la kero za wafanyakazi.

Kuondokana na kero za wafanyakazi ni kuwatendea haki kwa kulipa haki zao na kuwa na nidhamu ya matumizi.

Serikali inayotumia mara mbili ya kipato chake haiwezi kufanya hivyo zaidi ya kuleta siasa na longo longo, vitu ambavyo vimepitwa na wakati.

Kinachokera ni kwamba pamoja na uchungu wa wafanyakazi, wanasiasa wanajifanyia mambo kana kwamba wao hawaishi katika nchi hii.

Ukitaka kujua ninachomaanisha, jikumbushe ni misamaha mingapi ya kodi ilishatolewa na serikali ya awamu ya nne ukiachia mbali kipengele kinachotoa mamlaka kwa waziri husika kuendelea kutumika wakati tukijua wazi ni uchochoro wa kuhujumia uchumi na taifa letu.

Leo hatutaandika mengi. Kumsaidia Kikwete na chama chake na serikali yake ni kumgomea ili aone madhara ya kufuja rasilimali na mali za umma ili atie akilini.

Bila kugoma siasa na sanaa zitaendelea huku wafanyakazi hata wananchi wetu wakizidi kugeuzwa punda vihongwe na kikundi kidogo cha watu kilichojaa mafisadi na wafujaji. Wafanyakazi msikubali maneno, maana maneno matupu hayavunji mfupa na matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.

Kuhusu kutatua tishio la mgomo. Kikwete anapaswa kufikiri upya na kuja na matendo na si mijadala. Mbona anapata muda wa kuwakingia kifua mafisadi na waharifu wengine, tena kwa jasho la wafanyakazi lakini kwanini anashindwa kutimiza madai ya wafanyakazi?
Tanzania Daima Aprili 7, 2010.

No comments: