The Chant of Savant

Wednesday 14 April 2010

Mpendazoe ni gunia la misumari, Sitta ni nini?

WAKATI mwingine unaweza kudhani watu fulani wamepevuka na wana akili za kutosha kumbe unakosea.

Sijaelewa mantiki, kwa mfano, kwa baadhi ya asasi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachodai ni mhimili wa demokrasia nchini kumkejeli mbunge wa zamani wa Kishapu, Fred Mpendazoe.

Wamemkejeli kuwa hakuwa na tija kwa chama zaidi ya kuwa gunia la misumari ya moto kwa vile aliamua kuhama chama hicho.

Sijui wanaomuona Mpendazoe kama gunia la misumari ya moto kama wao si kasuku wanatumia midomo kufikiri na kujipendekeza kwa wakubwa lau wasikike?

Inashangaza CCM kuwanyamazia kasuku hawa wenye madai yanayopingana na dhana ambayo CCM imekuwa ikitaka tuamini kuwa ni mhimili na muasisi wa demokrasia nchini. Ingekuwa hivyo basi wanachama wake wangejua kuwa kuhama chama si jinai bali haki ya mwananchi ya kikatiba.

Licha ya kuwa ujuha ni unafiki kwa wana CCM kumlaani Mpendazoe. Mbona tuna wanasiasa wengi tena wachumia matumbo waliohama toka upinzani na hawaandaliwi maandamano? Je, dhambi ni kuhama CCM kwenda vyama vingine na baraka na halali kuhama upinzani kuingia CCM?

Leo bila aibu mkoa mzima unaandaa maandamano kuonyesha ujuha na CCM ngazi ya taifa wanauvumilia! Tumefikia wapi?

Hivi, kwa mfano, leo upinzani ukiandaa maandamano ya kulaani baadhi ya viongozi wa upinzani walioamua kujitembeza kwa CCM kwa kuipigia kampeni CCM italaani na kuona wanatishia amani hata demokrasia!

Kwanini sasa inaruhusu uhuni huu wakati ikiwa imeishachafuliwa na ufisadi hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi? Je, bado CCM inaendelea kuwaona Watanzania kama majuha wasioweza kufikiri bali CCM yenyewe?

Sasa jinai hii kuelekea uchaguzi ni ya nini kama si kufikiri hivyo?

Je, CCM chama kilichomezwa na ufisadi kiasi cha kushindwa kuwakomboa wananchi? Je, CCM si lege lege iliyoishiwa mikakati kuchakaa na kuganda kimawazo kama alivyosema Mpendazoe? Je, kuacha wahuni watoe majibu ya kihuni si ushahidi tosha?

Je, kwa kumchukia Mpendazoe kwa vile aliuchukia ufisadi si kuthibitisha madai kuwa CCM ni chama cha mafisadi?

Kwa chama makini chenye uongozi na sera makini, nguvu zingeelekezwa kujibu hoja za Mpendazoe badala ya kujiruhusu kuingia kwenye ulingo wa kashfa, kejeli na kukwepa maswali mazito ambayo Watanzania wangetaka kupewa majibu yake.

Bahati mbaya kwa CCM haikuwa hivyo! Ni aibu na pigo kiasi gani kwa chama kinachojiita mhimili wa demokrasia na siasa na nchi? Je, huu si mwanzo wa kuchakaa na kuishiwa?

Hebu tuangalie madai ya Mpenzoe ambayo hata hivyo si mapya ila yanaonekana mapya kutokana na kutamkwa na mtu aliyekuwamo ndani, tena jikoni.

“Nimeishi kwa matumaini ndani ya CCM kwa muda mrefu na sasa natangaza wazi kuwa nakihama chama hicho na kuhamia chama mbadala ambacho ni CCJ,” alisema.

Kama mbunge aliyekuwa akipokea mamilioni ya shilingi ameishiwa matumaini huyu mwananchi kapuku amebaki na nini kama tutaacha kudanganyana na kuwekana sawa ukiachia mbali kuchuuzana?

Je, kusema hivi ndiyo kuwa gunia la misumari ya moto? Je, kipi bora kati ya gunia la misumari ya moto (Mpendazoe) ambayo ukiipoza waweza kujengea na pakacha (hawa wanaojibu hoja kwa kejeli na maandamano ya kihuni)? Inatisha kama tumejiachia kuwa wahuni tena kama chama.

Hebu tuangalie hoja ya msingi ya Mpendazaoe kujitoa CCM: “Serikali iliyotokana na rushwa hutumwa na matajiri walioiweka madarakani... ni serikali kiziwi; haiwezi kusikia kilio cha wananchi wake; ilipewa nafasi ya kujisafisha kuanzia kikao cha NEC kilichofanyika Butiama na kamati ya Mwinyi haikufanya hivyo kwani hadi leo hakuna maamuzi yoyote.”

Hapa maswali ya kujibu ni je, serikali ya sasa haikutokana na pesa chafu za mafisadi hasa wizi wa EPA? Je, CCM haijatekwa na matajiri ambao walianza kufanya hivyo hata kabla ya mwanzilishi wake kufariki?

Mzee Joseph Butiku alisema viongozi wa sasa ni watumwa wa mafisadi akaambiwa na wehu fulani kuwa ni mwehu. Je, CCM ya sasa haiendeshwi na matajiri hawa hawa wanaoweza hata kuvunja Benki yetu Kuu na kuiba na bado wakaendelea kuitwa waheshimiwa na wanafanyabiashara maarufu wakati ni majambazi maarufu?

Mara zote ilipokabiliwa na shutuma kuwa CCM ni chaka la ufisadi imekuwa ikikanusha kwa kutoa majibu rahisi na ya kejeli kama njia ya kukwepa ukweli na kuwajibika, ukiachia mbali kuua mjadala.

Leo mfano anatokea kinyamkera aliyening’inia mgongoni mwa baba yake na kusema eti Mpendazoe ni wa kuja! Ukimwangalia anayesema hivi si chochote wala lolote, bali kupe alaye kwa mgongo wa baba au mama yake!

CCM imekuwa ikitumia vitisho vya kuwatimua wanachama wake wanaoonyesha kupingana na madudu inayofanya. Ila kadiri siku zinavyokwenda, mbinu hii haitafua dafu zaidi ya kuwa mwiba.

Kujitoa kwa mbunge wa zamani wa Kishapu-CCM Fred Mpendazoe kumefichua unyafuzi hata unyanyapaa wanaokumbana nao wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, hasa wale wasiopenda ufisadi.

Kwa mujibu wa uzoefu wa Mpendazoe hali ni mbaya. Maana anasema aliishi kwa matumaini yasiyokuwapo hadi mambo yakamshinda akaamua kuachana na CCM angalau awe huru, ukiachia mbali kushiriki vilivyo kuwaondoa wananchi kwenye makucha ya chama hiki nyemelezi.

Ingawa wengi wanachelea kuthubutu kama alivyofanya Mpendazoe, kuhofia kupoteza ulaji mnono wa dezo, ukweli ni kwamba huu ni woga tu. Maana wanasiasa wana yanayoinyima CCM usingizi kama Dk. Willbrod Slaa, Freeman Mbowe, walitoka huko na wakafanya makubwa kwenye upinzani kiasi cha kujizolea heshima ya hali ya juu.

Kitu kingine kilichojitokeza kutokana na kuhama kwa Mpendazoe ni kuthibitika kwa madai ya muda mrefu kuwa CCM sasa ni kimbilio na chaka la wafanyabiashara mafisadi ambao wameamua kusaka ubunge ili kulinda madhambi yao.

Cha mno ni ule ujasiri wa Mpendazoe kuirushia dongo serikali ya sasa akisema ilitokana na rushwa na pesa chafu kiasi cha kuendelea kuwa mtumwa wa mafisadi walioingiza madarakani.

Tuhitimishe kwa swali. Kama Mpendazoe ni gunia la misumari ya moto, kina Sitta ni nini?
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 14, 2010.

No comments: