The Chant of Savant

Wednesday 14 April 2010

Mama Mpayukaji anusurika kifo

SIJUI kwanini matukio mengine hutokea pamoja, ingawa yote hayatangazwi kutokana na nani aliyeko nyuma yake? Mna habari mke wangu kipenzi Salama Mpayukaji alinusurika ajali ya barabarani sambamba na ile iliyohusisha msafara wa mke wa rais?

Ingawa ajali hii haikutangazwa kutokana nami kuwa mkuu wa kijiwe, ilitokea. Bi mkubwa alikuwa amekwenda kwenye kijiwe cha Kyabakari kule Ilala kunipigia kampeni. Siku hizi tunawatumia wake zetu kutupigia kampeni kabla ya kipenga cha kampeni kupulizwa.

Tunatumia mali za umma ili wanakijiwe kuukwaa. Kwa upande wangu, situmii pesa ya kina Kagodoka walioiba pesa ya kahawa na kashata.

Badala yake natumia NGO ya Bi mkubwa ya MAWAWA, yaani Maulaji ya Wake za Wakubwa tofauti na mke wa yule.

Alivunga kwenda kule kukagua miradi yetu ya kisiasa kutokana na uchafuzi kuwa mlangoni.

Lazima kila kamba ifungwe ili walevi waingie mkenge upya watupe kura ya kula.

Kwa sasa tutawaonyesha mapenzi ya ajabu ili wakishaukwaa mkenge walie na njia wakati sisi tukiwasanifu kwa ujuha wao.

Hii ndiyo sababu mnawaona Bi mkubwa wangu na kitegemezi changu wakizungukia vijiwe kila uchao. Ingawa hatuna magazeti, habari zetu ziko kila mahali kwani nasi tuko kila mahali tukipiga kampeni hata kabla ya kipenga kupulizwa.

Nilitaarifiwa kuwa kuna bajaj ilikuwa imebeba pombe haramu na bidhaa za magendo iliyokuwa ikiwakwepa ndata ndipo ikaugonga msafara wa baiskeli na pikipiki uliokuwa umembeba bi mkubwa.

Yeye hakuwa na mashangingi. Maana sisi kijiweni hatuna ubavu wa kutembelea mashangingi zaidi ya baiskeli na vikwata. Ingawa wengi wananilaumu kuanza kampeni kabla ya wakati, hawajui hizi ndizo siasa nasi ndio wanasiasa?

Kutokana na kutaka kuwa mkuu wa vijiwe vyote kayani, huwa namtuma bi mkubwa kuwahonga wapiga kura, sorry kuwasaidia kitu kidogo kama vigogo wenu wanavyofanya kwa kutoa saruji na upuuzi mwingine kipindi hiki kuelekea kwenye uchafuzi.

Kuna wanaosema eti bi mkubwa wangu alistahiki kwa vile alikuwa akitenda dhambi kubwa kunipigia kampeni mimi. Eti wanasema hakuna haja ya kulaumu ile bajaj ya mfanya magendo kwani wote walikuwa wakifanya magendo - huyu ya siasa na yule ya maisha!

Kumbe siku hizi waja hamna huruma kiasi hiki! Kosa lake nini? Kuwahonga na kuwatumia washirika wenu wa bedroom siyo?

Wanaongeza kuwa Godi alisikia vilio vya walevi tunaowadhulumu! Tunawadhulumu au wanajidhulumu kwa ujuha na uroho wao? Ni uvivu wa kufikiri kuhoji pesa anazotumia bi mkubwa wangu zitokako wakati kijiwe kimejaa mianya lukuki ya kutengeneza njuluku.

Hawa wahajui kutesa kwa zamu? Mie sijajitwalia hata meza moja ya kahawa. Mbona waliojitwalia migodi wanaendelea kutanua huku walevi wakiendelea kukodoa mimacho kama bundi? Mwenye wivu ajinyotoe roho na kuacha sisi tufaidi vya walevi. Hayo tuyaache.

Na kama si kuwa na msafara mrefu wa pikipiki (ambazo kwa kijiwe ni kama mashangingi) kama sabini hivi, mambo yangekuwa mabaya zaidi.

Wapo walevi kijiweni wanaosema eti asisafiri na misururu mirefu ya pikipiki na baiskeli kwa vile anakera watumiaji wa barabara!

Hivi angekuwa anatumia mashangingi hawa wangejinyotoa roho? Ebo, hawa hawanitakii mema. Nani mwenye hizo barabara zaidi ya mimi na ufalme wangu? Zitafungwa mtake mistake. Huu ndiyo ukuu ati.

Siwezi kufanya kosa kumzuia bi mkubwa kutanua kama mkuu wa kijiwe. Maana tunavyowaliza walevi, akisafiri kwa pikipiki moja si watamnyotoa roho. Kwanini hawataki kukubali ukweli kuwa mke wa mkuu wa kijiwe naye ni mkuu wa kijiwe kwa vile anajua siri nyingi za mkuu hasa za bedroom?

Mbwa wa mfalme ni mfalme wa mbwa wote. Walinena wahenga. Hawajui kuwa umbea wote ninaoupata kuhusiana na wabaya wangu hupitia kwake?

Hawajui kuwa familia yangu ni serikali ndani ya serikali kijiweni? Kwa taarifa yenu kama mnapasuka pasukeni. Hata vitegemezi vyangu vinasafiri na misururu ukiachia mbali kutumia pikipiki yangu iliyonunuliwa na kijiwe kwa bei mbaya.

Ningekuwa mkuu wa kaya naye angesafiri na dege langu huku akijinoma. Msikonde si ndege bali ungo wangu. Ingawa wakosoaji wanasema kuwa wake zetu wanapenda vya dezo kama maiti na kwanini mke wa Obama hatumii Air Force One kwenye biashara zake, wanakosea.

Ile ni Marekani iliyojaa wajuaji. Si kama kijiwe chetu ambacho kinaongozwa na mlevi na mpenda raha mimi kilichojaa walevi na majuha. Isitoshe Marekani ina jina kubwa lakini si tajiri kama kijiwe chetu. Kwani hamjui?

Angalia ninavyotanua na kina Mbwamwitu, Ewassa, Kanji na wengine wakihomola. Sisi tumejaliwa utajiri wa kahawa ambayo lazima wakubwa tuinywe na kula kashata na familia zetu na nyumba ndogo kwa amani.

Marekani hawana amani kama kijiwe chetu. Wao wanatishiwa na Al-Qaida. Kama kuna adui yetu si mwingine bali majuha na wale wenzetu ambao wameanza kutuhama na kujiunga na maadui zetu.

Wazushi wanasema eti vibaka walimtegeshea ili wamnyofoe migold yake ambayo tangu niukwae anaikoga kama maji.

Thubutu! Vibaka hawana dili kali kama akina Kagoda na Meremeta. Hivi yule jamaa waliohomola pesa ya HEPA wameishia wapi; mbona hawaunganishwi na Lumba Maumba au wakubwa wanaogopa watawaumbua? Kwanini walevi wasihangaike na hawa badala ya mke wangu chifu wa kampeni zangu za siri au hadi shehe ubwawa atabiri?

Kwa vile viherehere wamezidi, nitaamuru bunge la kijiwe litunge sheria ya kulinda ulaji wa mke wangu kwa vile naye ni mkuu kama mimi. Au wanataka nifanye kama M7 nimteua kuwa waziri kwenye kijiwe?

Mlitaka pikipiki yangu atumie Lyatongolwa kwenda Moshie kujidai kama yule waziri uchwara aitwaye
aliyekwenda kwa ndege na kuamuru shangingi lake limfuate ili awaonyeshe washamba wa kwao kwenye mibuni?

Sasa kama viroho vinawatweta kwa roho mbaya zenu kulilia mali ya umma ambayo haiumi, nitafuga mbwa naye, kama mke wangu na vitegemezi vyangu awe anafaidi kupandishwa kwenye pikipiki ya kijiwe atanue kwa vile ni mbwa wa dingi wa kijiwe.

Alijisemea Mama Yoyo. Unajua alisemaje kwa Kiswahili chake mbofu mbofu? “Misaili haina akili. Yeye nakula vitu dongo dongo kwa chaguzi lafu nachagua mizi naleta kelele! Sisi nachagua Muringe inaua yeye na kuleta Ewassa lafu nalalamika!”

Leo sitachonga sana. Kwani nina safari kwenda kumpongeza Mpende azoe kwa kuachana na ukale na ubabaishaji wa nambari wahedi.

Pia nikirejea nakwenda kumzaba makonde yule mtabiri uchwara wa kijiwe aitwaye shehena Njaa aliyetabiri kuwa hakutakuwa na uchafuzi mwaka huu. Kumbafu huyu. Anataka ninyimwe kura ya kula na walevi? Khalas kweisine.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 14, 2010.

No comments: