How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday 5 June 2010

Masauni, ubaguzi na uonevu wa CCM

BABA wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere, alituachia urithi bora japo tunaufuja kwa ujuha na upogo wetu. Hakuwa mnafiki wala kigeugeu. Alichukia ubaguzi, ufisadi, uroho, ubinafsi, ubepari, ufisi na mambo mengine kwa namna ya pekee.

Hakuna dhambi iliyomuumiza kichwa kiasi cha kukamua hazina yetu kama ubaguzi. Rejea mchango wa Tanzania kwenye kuikomboa Afrika ya Kusini. Bado tunakumbuka wimbi la wakimbizi waliopewa hifadhi na fursa toka Afrika ya Kusini.

Watu wa Mazimbu ilipokuwa kambi maarufu ya wakimbizi hawa ya Solomon Mahlangu, wanakumbuka vizuri.

Nyerere alilaani ubaguzi na kupigana nao kwa matendo.

Aliishi na kulitimiza hili kwa kiwango cha juu. Sijui wanaojua hili wanajisikiaje wanapoona Watanzania wanaanza kubaguana kwa misingi ya mitandao, vyama, dini hata makabila vitu vinavyopingana na dhamira ya mwanzilishi wa taifa hili?

Uonevu na ubaguzi wa hivi karibuni dhidi ya mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Hamad Yusuf Masauni, ndio umenisukuma kudurusu hali halisi kuhusiana na jinai hii iliyohalalishwa hivi karibuni nchini mwetu.

Kuna madai kuwa Masauni alighushi cheti cha kuzaliwa, hatua iliyomwezesha kuchaguliwa kushika wadhifa huu adhimu chamani. Wadhifa huu ni muhimu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kutona na vijana kuwa kundi kubwa nchini.

Kama Masauni alighushi au la hilo ni suala la polisi na mahakama kuchunguza na kuamua ingawa kutokana na vigogo walioko nyuma ya sakata hili ukweli ni kwamba Masauni keshahukumiwa tu.

Je, Masauni ni wa kwanza kutuhumiwa kughushi? Jibu ni hapana. Alianza kutuhumiwa Mbunge wa Buchosa, Samuel Chitalilo. Wakati tuhuma hizi zikitolewa, Rais Jakaya Kikwete wakati ule akiwa mgombea alimtetea kwa kusema kelele za mlango hazimzuii mpangaji kulala, kwa maana kelele za wapiga kura hazimzuii mbunge kufanya vitu vyake.

Wengi wanashangaa. Kwanini Kikwete ambaye mtoto wake Ridhiwan anatuhumiwa kuwa nyuma ya sakata la Masauni- hakusema kelele za mlango? Au ni yale ya uchungu wa mwana? Wengi wanajiuliza. Je, huu si ubaguzi wa wazi tena utendwao na wale tuliowaamini madaraka na ofisi za umma.

Pia sakata la Masauni limeuvua nguo utawala wa Kikwete na kuuonyesha kama usio makini.

Kwani ndiye aliyempitisha kuwa mwenyekiti bila kuwa na uhakika na historia yake. Je, wako wangapi kama Masauni waliopitishwa na utawala huu ilhali hawafai?

Baada ya hapo mwanaharakati Keinerugaba Msemakweli aliwatuhumu vigogo wengine wa CCM kwa kosa hilo hilo.

Waliotuhumiwa tena kwa kutungiwa kitabu ni ni mawaziri na wabunge Dk. Makongoro Mahanga (Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana), Dk. Mary Nagu (Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko), Dk. Diodurus Kamala (Waziri wa Afrika Mashariki) na Dk. Emmanuel Nchimbi (Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).

Wengine ni Mbunge wa Ismani ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (William Lukuvi), Victor Mwambalaswa (Lupa-CCM) na Dk. Rafael Chegeni (Busega-CCM).

Baada ya kuzuka madai na manung’uniko kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, alimlazimisha Masauni kujiuzulu Mei 18, kwa shinikizo la chama, Makamba alijitetea na kusema kuwa jukumu la kushughulikia tuhuma za Masauni limo mikononi mwa polisi.

Wengi wanaamini Masauni ametimuliwa baada ya kugusa masilahi ya wakubwa fulani. Wanajiuliza mantiki ya tuhuma za Masauni kukimbiziwa polisi ilhali tuhuma za Chitalilo zilishughulikiwa na polisi hao hao zikawekwa chini ya busati. Wanashangaa kwanini Masauni aachishwe uongozi wakati watuhumiwa waliotajwa hapo juu hawakuwajibishwa ukiachia mbali kutoshughulikiwa na polisi?

Katika kukwepa aibu, hivi karibuni vyombo vya habari vilimkariri Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Naibu Kamshna wa Polisi, Peter Kivuyo, akisema suala hilo linafuatiliwa na polisi kwa karibu.

Kivuyo alisema “Kuhusu mawaziri kughushi vyeti polisi imeanza uchunguzi na hatua kali zitachuliwa kwa wahusika iwapo watabainika kufanya makosa hayo ili iwe fundisho kwa wengine.”

Ahadi ya hatua kali kuchukuliwa imeishakuwa wimbo wa jogoo. Kwanini wasiwajibishwe kwanza ndipo hatua zifuate kama kweli kuna utashi wa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria?

Suala la Masauni linachunguzwa na polisi wakati la vigogo waliotajwa muda mrefu na rais akawanyamazia linafuatiliwa siyo linachunguzwa!

Hapa unaweza ukaona ubaguzi na kulindana kwa dhahiri. Tunakwenda wapi iwapo vyombo vya dola vinaanza kutumika kama asasi za watu binafsi kulindana na kupeana kinga?

Hapa tunapigwa changa la macho. Anayebisha ajiulize tuhuma zenye kila aina ya ushahidi za kughushi zinazomkabili Mbunge Chitalilo ziliishia wapi baada ya Kikwete kumkingia kifua kuwa kelele za mlango haziwezi kumzuia mpangaji kulala?

Je, kiongozi wa namna hii anayetenda kwa upendeleo anaweza kutuvusha au kutuzamisha?

Hii maana yake ni kwamba anatawala kifamilia na ushikaji. Hivyo watu wake wa karibu wakiguswa sheria itapindwa na kuwahami.

Wako wapi kina Kagoda, Deep Green Finance, Meremeta na wezi wengine wa EPA, CIS, rada, ndege ya rais na wengine wengi walio karibu na wakubwa?

Swali ambalo litaiandama CCM ni mantiki ya kumwajibisha Masauni ambaye ni dagaa huku mapapa wakiendelea kukata mawimbi.

Kituko na kufichuka kwa unafiki wa CCM ni ukweli kuwa ilimpitisha Masauni ikijua madhambi yake. Kosa hapa kwa CCM si kughushi vyeti vya kuzaliwa bali kugusa masilahi ya wakubwa fulani.

Maana kama kughushi kungekuwa kosa kwenye macho ya CCM watuhumiwa vigogo wangekuwa wameishawajibishwa zamani gani!

Je, wako wangapi walioghushi lakini wakaendelea kuwa kwenye ofisi za umma kwa kinga ya kujikomba kwa na kulinda masilahi haramu ya CCM?

Je, kuna ufisadi na ujambazi kuliko huu? Je, hapa mfumo wetu haujaoza kiasi cha kugeuka kansa?

CCM, polisi na umma tutende haki. Wananchi tuwashinikize wahusika kuacha mchezo mchafu wa kutumia sheria kibaguzi. Na wahusika watuhumiwa na washitiri wao wajue fika. Mambo yameanza kubadilika.

Kuendelea na jinai hii mtaamsha hasira za umma kiasi cha kuleta vurugu. Jinai ya CCM. Polisi na Masauni na vigogo walioghushi iwe somo kwetu. Amkeni tuibadili jamii yetu kwa faida yetu.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 2, 2010.

No comments: