The Chant of Savant

Thursday 13 October 2011

Mnywa gongo amkumbuka Mwalimu

Siku ya leo, walevi wote wamkumbuka shujaa wao

Wamkumbuka shujaa wao mwalimu Nyerere

Wanalia na kusononeka kwa kumkosa mtetezi wao

Hasa wakati huu ambapo mafisi na ngedere

Wameamua kuuza na kurarua utu wao

Rudia mara mbili kabla ya kupiga funda tatu za gongo

Pamoja na jeuri yangu ya kunywa gongo na ubishi wa kisomi kutokana na usomi wangu kuhusiana na haya mazabe yanayoendelea, bado namhusudu marehemu mzee Mwalimu Juliyas Mchonga Kambarage Mussa Nyerere kwa jeuri, utaua na uadilifu wake. Hakuwa fisi wala fisadi. Hakuwa kihiyo wala bwege. Jamaa alikuwa amepiga vitabu hadi kunyakua Masters yake. Kwa sisi wenye Masters na PhD tunajua ugumu wa kupata vifaa hivi. Wengi wanaviogopa hasa kama akili hazichemki kama zangu na Mzee Mchonga. Mwalimu hakuwahi kutumia shahada ya heshima hata siku moja ingawa alikuwa nazo utitiri acha hawa wenye kimoja pale na kingine pale tena vya kulazimisha. Ndiyo maana pamoja na usomi wake hakufa na cheo cha dhuluma cha kujiita Daktari wakati udaktari wenye ni wa heshima. Mwalimu hakupenda makuu wala kupenda kupewa shahada hata na vyuo ambavyo havina sifa kama wale wengine muwajuwao wapendao kuitwa madaktari wakati hawataki kwenda shule wala kufikiri kisomi.

Juzi nilikuwa nikisikiliza hotuba yake ya Mei 1995 kule Mbeya alipotabiri kuwa uongozi wa Bongo utakuja kugeuka biashara, ujambazi na kila aina ya jinai, niliridhika kuwa kumbe hotuba zake bado ni bora na zenye mantiki kuliko za walio hai. Kwa hiyo hapa nikiongelea usomi wa Mwalilmu hata kama mimi ni mnywa gongo na mvuta bangi, tunaelewana. Hebu ukitaka kujua ninachomaanisha, chukua hotuba moja ya Mwalimu uichambue ki maana na maanawia halafu ulinganishe mihotuba mirefu ya wengine utajua ninachomaanisha vilivyo.

Leo nani ana ubavu wa kuwafokea wezi achia mbali kuwatimua badala ya kula nao? Leo nani anaweza kupata madaraka bila kuhonga, kuiba kura, kudhaminiwa na fedha chafu na upuuzi mwingine? Mwalimu aliweza kuyaepuka na kuyatabiri haya pale aliposema kuwa Ikulu si sehemu ya kufanyia biashara ya njugu, ubwabwa, bwimbwi wala sanaa.

Ukiachia mbali usomi, kuona mbali, uadilifu na ushujaa, Mchonga alijenga nchi wengine wakabomoa. Wangeshindwaje kuibomoa wakati hawana uchungu nayo? Kujenga nchi kunahitaji moyo na kuibomoa kunahitaji uchoyo na upgo. Hii ndiyo tofauti ya Mwalimu na wahujumu wa kazi zake. Alilinda raslimali za umma mafisi wakatapanya. Wengi wa mafisi na mafisadi unaowaona wakiibukia ni matunda ya fikra na sera za mwalimu hata kama ni wezi wa fadhila. Wengi baba zao hawakuwa na uwezo hata wa kuwapeleka hata mama zao kujifungua hospitali hao wezi wao. Ndipo mwalimu akaleta huduma za bure za jamii. Baada ya kuanza kutembea akawapeleka shule bure wengine wakasoma hadi kupata PhD wanazotumia kuibia umma. Wakati wa mwalimu hapakuwa na mawaziri wa kughushi shahada kama ilivyowahi kutokea huko nyuma. Hapa kinachotukera hasa sisi wanywa gongo ni kuona jinsi vitegemezi vyetu vinaposumbuliwa na kunyimwa au kupewa mikopo wakati wanaofanya hivyo walisoma bure. Huu nao ni ufisadi na ujambazi wa aina yake. Kwanini, k ama kulipia elimu ni mali, wao wasilipe pesa iliyotumika kuwasomesha?

Mwalimu alikuwa kiboko. Hakujilimbikizia wala kuabudia mali kama jamaa zangu magamba. Hakuwa mpuuzi wala msanii bali mtoboa siri kama mimi. Mna habari kuwa ingawa mwalimu hakuwa mlevi wa gongo alilewa utu? Mna habari mimi nimechukua tabia zake kuliko hata watoto wake? Naona niishie hapa msije kuanza kumpakazia kuwa alizaa mwanaharamu nje ya ndoa ambaye ni mimi kama yule jamaa chovya chovya mwenye watoto wa kuokota hapa na pale mia kidogo. Hayo tuyaache.

Leo ni siku maalum ya kumuenzi nguli mwalimu Kambarage Burito baba wa Tanzania. Hivyo nitaongea kilevi lakini kwa heshima na taadhima vya namna yake kwa ajili ya heshima ya nguli huyu.ninapoandika wanywa gongo pale Uwanja wa Fisi walishajiandaa kukaa kimya kwa dakika kumi kabla ya kunywa gongo ili kumkumbuka Mwalimu wa walimu.

Tunajua mwalimu alipotutoka hakuacha baadhi ya misamiati kama vile mafisi, magamba hata wasanii. Hivyo tunachukua fursa hii kumuomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi kwani alimpenda zaidi kwa kumchukua kabla ya kushuhudia kufuru na uchafu ambavyo kama angeviona huenda angejitoa roho kama siyo kuzimia.

Kwa namna ya pekee, juzi walevi wa Buzwagi, Mara, Shinyanga na kwingineko ambako mbwa mwitu wameshambulia walituomba tushirikiane kumkumbuka na kumuombea nguli huyu wa uadilifu na baba wa ujamaa. Kweli mwalimu alikuwa baba wa ubinadamu na adui mkubwa wa ufisi na ufisadi. Hakutufanyia biashara wala kutuchuuza kama ilivyokuja kutokea. Pamoja na mapungufu yake, leo ukitamka jina Mwalimu kila mmoja anatia akilini hata sisi wanywa gongo na wavuta bangi. Jina la Mwalimu ni machukizo na tishio kwa vibaka wakubwa wakubwa na wale wote wanaokula bila kunawa kwa miguu na mikono huku wakivuna pale ambako hawakupanda.

Manadhani Mwalimu angekuwa hai hawa majambazi kama hawa wanaotaka kulipwa mabilioni kwa kusambaza kiza wangefurukuta? Hakuwa na mchezo wala kuchekacheka mbele ya maafa. Kweli paka akiondoka panya hujitawala. Shujaa Mwalimu ameondoka, mafisi, mafisadi, mapapa, vinyamkera na kila kinyama cha kizani vinatuchezea mahepe. Hata hivyo kuna siku yao isojina vitalia na kusaga meno.

Natamani niandike hadi kesho. Acha niende kwa Mama Betty nimlilie Mwalimu wetu hata kama ni kwa kupiga funda moja. Mwalimu we shall miss you greatly even though those hyenas you left behind have tried unsuccessfully to founder your name.

Chanzo: Dira Oktoba 13, 2011.

1 comment:

Jaribu said...

Unajua wakati mwingine hum-appreciate mtu mpaka akiondoka. Enzi hizo nilikuwa simuelewi vizuri nikawa namuona mkali sana. Lakini hiyo ndiyo inayotakiwa, someone to run a tight ship. Hawa bozos wa siku hizi wanapenda madaraka, lakini hawajui kuyatumia.