VYOMBO vya habari vilimkariri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akipiga kampeni ambazo wakosoaji wake waliziita chafu na za kichovu kuhusiana na pendekezo la kuwa na serikali tatu.
Wengi waliona kama anachofanya ni kuingiza siasa na fitina makanisani, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. CCM wamekuwa wakitutahadharisha kutochanganya siasa na dini. Wakosoaji wa Lukuvi wanahoji: “Kwanini wapinzani wakifanya kama alivyofanya Lukuvi wanaonekana kama wamechanganya dini na siasa, lakini CCM wakichanganya vitu hivi tena kichovu inakuwa halali?”
Lukuvi alikaririwa hivi karibuni akijivua nguo yeye na bosi wake Rais Jakaya Kikwete alimvumilia hata baada ya kutuhumiwa kughushi sifa za kitaaluma akisema: “Mimi nataka serikali mbili kwa sababu tumeshazoea kusali chini ya miti tukiwa na amani na tukiwa na serikali tatu tutasali kwa mtutu.
Kama umeshindwa kuwatunza wanawake wawili ulionao, je, huyo wa tatu ambaye humjui tabia yake utamtunzaje?” Jibu la swali lake ni rahisi. Kama umeshindwa wake wawili basi baki na mmoja au kuwaacha wote.
Hata hivyo, hapa kusali chini ya miti na mtutu wa bunduki vinaingiaje kama si kuishiwa na kufilisika kifikira hata kisiasa kwa Lukuvi na wenzake wanaotaka kutumia kampeni na propaganda uchwara kuwahadaa wananchi?
Je, bado wanadhani kuwa Watanzania ni majuha na mataahira wa kutishiwa kwa kila upuuzi? Kwanini Lukuvi na mabwana zake hawataki kutambua kuwa kizazi cha sasa ni kipya cha ‘dot com’ kilichoelimika na kisichotishwatishwa kipuuzi?
Licha ya kuonyesha utovu wa nidhamu, busara na hekima, Lukuvi amemdhalilisha bosi wake Rais Kikwete. Kimsingi amebainisha kuwa uwezo wa kufikiri unaonekana kuwa mdogo kutokana na elimu kidogo.
Hata hivyo, Kikwete anapaswa ajilaumu. Kwani zilipotolewa tuhuma za kughushi vyeti vyake vya kitaaluma, hakumchukulia hatua zaidi ya kujifanya hasikii.
Sasa anaanza kujifichua kiasi cha kumuacha Kikwete bila nguo. Je, kwanini Kikwete alinyamazia tuhuma hizi? Je, aliamua kuwaacha mawaziri waliotuhumiwa kughushi kwa kuhofia kuwa na watu mahiri na makini kwenye baraza lake la mawaziri ili wasimfunike?
Katika kampeni zake chovu na mfu Lukuvi aliongeza: “Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena, angalieni nchi ya Korea Kusini na Korea Kaskazini ambao waligawanyika na sasa ni maadui wakubwa wanaokaa mipakani wamenyoosheana bunduki.”
Lukuvi angeonyesha ukweli na mashiko ya madai yake kwa kufafanua ni kwanini hali itakuwa hivyo. Tumuulize Lukuvi, anamaanisha nini? Je, kuna mpango wa CCM kutumia jeshi kupora madaraka au ni kuishiwa na kufilisika kisiasa au vitisho vya kutaka kuendelea kuwa madarakani?
Huwezi ukalinganisha Korea Kaskazini na Korea Kusini nchi ambazo ziligawanywa na nguvu ya nje, lakini si wananchi wenyewe, vinginevyo unaonyesha usivyojua historia ya nchi hizi au kile unachosema.
Hata wakati wenyewe na sababu ya kugawanywa kwa Korea mbili ni tofauti kabisa na kinachoendelea Tanzania.
Sijui kama Lukuvi anajua anachosema au ameamua kwa makusudi kupotosha ukweli huku akitoa vitisho vya kitoto. Huenda anamaanisha anachosema kutokana na elimu na uwezo kiduchu wa kufikiri.
Kama wananchi wanataka serikali tatu hakuna wa kuwatisha wala kuwazuia. Hata hilo jeshi analoongelea ni lao. Isitoshe tangu Umoja wa Mataifa uharamishe mapinduzi, nani aogope jeshi kuchukua madaraka?
Inaonekana Lukuvi hajui hata kitu rahisi kama hiki. Mambo ya kutishia nyago na nyau yeshapitwa na wakati na anayeyatumia ima ni mshamba au mjinga anayepaswa kuwa shule.
Wakati wa kuanzisha utaratibu wa vyama vingi, wachovu kama Lukuvi walikuja na vitisho hivyo. Bahati nzuri Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisikia huu upuuzi na kuingilia kati na kushauri vyama vingi viruhusiwe kwa vile vilikuwa haviepukiki.
Kadhalika Lukuvi na wenye mawazo mgando kama yeye lazima wajulishwe. Serikali tatu haziepukiki. Hivyo, watafute sababu nyingine ya kutumia fujo kuendelea kuwa madarakani kwa kuhofia kuondolewa wakaishia gerezani kutokana na dhuluma, ufisadi waliofanya kwa muda mrefu.
Lukuvi aliendelea kujivua nguo alipokaririwa akisema: “Unajua jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha. Hiyo serikali ya tatu ambayo jeshi litakuwa chini yake haina vyanzo vya mapato vya kueleweka, sasa hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu watakubali kuishi bila fedha?” Pesa inaingiaje hapa? Je, jeshi letu linaendeshwa kwa utii kwa wananchi au kuhongwa fedha au kuabudiwa kama anavyotaka kubainisha Lukuvi? Kwanza, anapaswa aliombe jeshi msamaha huku akipelekwa mahakamani kwa uchochezi na hata uhaini.
Laiti Rais Kikwete asingekuwa mtu wa kuvumilia mambo ya ajabu kama haya, Lukuvi angeozea gerezani. Ni upuuzi na ujinga wa hali ya juu kusema kuwa jeshi linaweza kuwazuia wananchi wanachotaka au kuwaamria jinsi watakavyotawaliwa.
Hilo jeshi halilipwi mishahara toka mfukoni mwa CCM bali wananchi wenyewe. Lukuvi alipaswa abanwe aeleze ni jeshi lipi linalotaka kuleta vurugu kwa kupinga msimamo na chaguo la wananchi ili livunjwe hata kushughulikiwa. Maana Tanzania ni nchi ya kidemokrasia isiyopaswa kutishwa na yeyote ndani na nje.
Wanaosema eti serikali tatu hazitakuwa na vyanzo vya mapato ni wendawazimu au wanahitaji kupimwa akili zao. Ukiangalia pesa ambayo imekuwa ikipotea chini ya utawala mbovu wa CCM, kuanzia misamaha ya kodi, kutosimamia mapato, matumizi mabovu hasa ufujaji, wizi na kila aina ya jinai, zinatosha kuendesha hata serikali kumi. Lukuvi anadhani wananchi hawajui ukweli huu?
Kama Lukuvi angekuwa ameelimika, angejua kuwa serikali tatu au mbili au moja zina vyanzo vya mapato kwa vile haziongozi hewa bali pande la nchi liitwalo Tanzania, lenye kila rasilimali kuanzia watu, ardhi, mito, maziwa, madini na kila kitu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 23, 2014.
1 comment:
Naona huyu Bwana yeye amehamua tuu kusema wazi ambacho wengine wanazunguka wanazunguka mmbuyu kuongea hayo mambo ya idadi za seraili katika Muungano,
Ambapo wengi wao kutoka sirikali wamwahamua kutokuwa wa wazi kwenye hili.
Post a Comment