BAADA ya kumdhalilisha, kumvizia na kumhujumu Jaji Joseph Warioba, na tume yake, wengi tulidhani Chama Cha Mapinduzi (CCM), lau, kingeona aibu na kuona inatosha. Lakini wapi! Wameonja asali sasa wanataka kuchonga mzinga.
Nani angeamini kuwa aliyejinadi kuwa mtu wa viwango angekuja na viwango dhaifu (substandards) na vya ajabu na hovyo? Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, ameanza kuonyesha sura yake halisi ambayo wengi hawakuijua.
Kwa heshima aliyokuwa amejijengea alipokuwa spika wa Bunge la Muungano, wengi walidhani angeilinda kwa gharama yoyote.
Je, Sitta, alijijengea heshima kwa bahati mbaya au kupitia njia ya kuwaondoa wapinzani wake ili baadaye agombee urais?
Je, Sitta anaendeleza harakati zake za kuusaka urais hata kwa kujitoa kafara na kuwa tayari kutumiwa na CCM kama itakavyo bila kujali utu na heshima yake? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Mtu hata jamii wanaweza kuingia kwenye matatizo zaidi hasa pale wanapolinganisha majanga mawili ili kuchagua moja. Hii ndiyo iliyotokea kuelekea kwenye mchakato wa kumpata mwenyekiti wa Bunge la Katiba.
Watanzania walitumia falsafa hii ya kulinganisha majanga mawili kumsaka mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Sitta alikuwa akichuana na Andrew Chenge, ambaye alionyesha kupingwa sana kutokana na historia ya kuhusishwa na ufisadi, rushwa na kutorosha fedha nje ambayo hajawahi kuyatolea majibu yanayoingia akilini.
Walipopambanishwa wawili hawa, wengi walionekana kumpendelea Sitta (naye kutokana na historia ya utendaji wake hasa alipokuwa spika wa Bunge la Muungano).
Kilichompiga jeki Sitta ni ile hali ya kuruhusu Bunge, mwaka 2008, kumkaanga waziri mkuu wa zamani aliyeachia madaraka kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa. Pamoja na Sitta kupata umaarufu asiostahili, wengi walisahau sifa moja muhimu: Sitta na Chenge ni wana CCM tena makada waliowahi kuonyesha kutumiwa wazi wazi na chama kiasi cha kuwatelekeza wananchi.
Walisahau kuwa Sitta alifanya aliyofanya ima kwa bahati mbaya au katika harakati za kujisafishia njia kuelekea ikulu ukiachia mbali kuhongwa uwaziri baada ya kuficha mambo nyeti kuhusiana na kashfa ya Richmond ambayo bila shaka kama yangewekwa hadharani, serikali ya Rais Jakaya Kikwete ingeanguka. Lakini badala yake, wawili hawa walimtwisha mzigo Lowassa ambaye hakuacha kulalamika kuwa hakutendewa haki.
Ukiachia kuhongwa uwaziri baada ya kutupwa nje toka kwenye uspika kwa kumpachika Anne Makinda, Sitta alituhumiwa katika kuanzishwa kwa Chama Cha Jamii (CCJ) alichokikana na kukitelekeza baada ya kupewa uwaziri. Huyu si mtu wa kuaminika hata kidogo.
Ni mtu aliye tayari kulitelekeza taifa kwa maslahi binafsi tokana na ushahidi huu hapa juu. Ni bahati mbaya kuwa euphoria ya kumkaanga Lowassa imetulewesha na kuendelea kumuamini uenyekiti wa Bunge la Katiba analohujumu kwa kutumiwa na Kikwete na CCM.
Sitta alionyesha sura yake halisi pale alipovunja kanuni ya Bunge la Katiba kwa kumruhusu Rais Kikwete, amhujumu na kumdhalilisha Jaji Warioba na tume yake ukiachia mbali kupotosha umma juu ya faida na ulazima wa kuwapo serikali tatu kama zilivyopendekezwa na wananchi.
Wahenga walisema: Nyoka ni nyoka hata abadilishe ngozi vipi anabakia kuwa nyoka. Baada ya kuihujumu tume, jambo ambalo ni kuuhujumu umma ule ule uliopendekeza muungano wa serikali tatu na umma ule ule unaolipia vikao vya Bunge la Katiba.
Sitta, kwa mara nyingine, ameonyesha rangi yake halisi kwa kufanya upendeleo dhahiri katika uteuzi wa wajumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge la Katiba hivi karibuni. Hata alipobanwa aeleze ni kwanini ameendeleza hujuma, hoja na majibu aliyotoa havikuingia akilini.
Kinachogomba kuhusiana na idadi ya serikali ni ile hali ya baadhi ya wafujaji wa pesa ya umma kujifanya eti wanauonea huruma. Hivi karibuni Rais Kikwete alikaririwa akisema kuwa serikali tatu ni gharama.
Ni ajabu. Hivi Kikwete ndiyo leo anaona gharama wakati anasifika kwa kuunda mikoa na wilaya nyingi zenye maslahi kwa watu wake na chama chake?
Mbona hakuona gharama ambazo ameliingiza taifa tangu awe rais ambapo ataondoka na sifa moja kuu—- kuzurura dunia nzima hadi anafananishwa na bazazi Vasco da Gama, Mreno aliyesifika kwa ujambazi na uzururaji wake? Je, ni kweli anachohofia Kikwete na CCM ni gharama au ni machozi ya mamba tu?
Kitu kingine wanachohofia CCM eti ni kudhoofika hata kuvunjika kwa muungano. Uvunjike mara ngapi iwapo wamekuwa wakifanya mambo kwa kificho tena bila kufuata sheria kama alivyothibitisha Kikwete hivi karibuni? Kikwete alitaja uraia kuwa suala la muungano.
Ajabu aliposema hivyo alisahau kuwa badala ya uraia mmoja uliokubaliwa kwenye muungano, sasa tuna uraia wa aina mbili, yaani Utanzania na Uzanzibari. Hapa bado hawajavunja muungano?
Kutokana na kazi maalumu ya kuhujumu Bunge la Katiba iliyofanywa na Sitta, wengi wameanza kukosa mantiki ya zoezi zima kiasi cha kutaka Bunge livunjwe ili kuepuka kupoteza muda na pesa ya umma kwa vitu ambavyo havina manufaa kwa umma.
Hujuma za Sitta ziligundulika wazi pale alipoteua wajumbe wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Katiba kwa kumteua Profesa Ibrahim Lipumba aliyeukataa uteuzi na kusema, “Nimesikitishwa na mpango maalumu mlionao wa kulifanya Bunge hili Maalumu kuwa Bunge la CCM.”
Wengi wanashangaa ni kwanini Kikwete ameamua kuhujumu mchakato aliouanzisha yeye mwenyewe. Je, alilazimika? Je, hakujua matokea yake? Je Kikwete, CCM na Sitta watafanikiwa kuhujumu umma kwa kuupa katiba pandikizi yenye lengo la kuendeleza fikra mgando na utawala wa kibabaishaji?
Je, umma utafanya kosa kuendelea kuwaamini wawili hawa ambao wameishaonyesha wazi wasivyotaka katiba itokanayo na utashi wa wananchi ambao, kimsingi, ndiyo wenye katiba na nchi?
Je, CCM na Kikwete wanaogopa nini? Ama kweli! Ukistaajabu ya Kikwete, utaona ya Sitta! Ukishangaa ya wawili hawa utaona ya CCM—kiama cha taifa letu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 2, 2014.
No comments:
Post a Comment