How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 5 April 2014

Mlevi apendekeza tuvunje muungano

                               
Baada ya kutoa somo la Katiba Mpya kule Dodoma wiki jana na wahusika kujifanya hamnazo, leo nimekuja na wazo mujarabu la kuepusha kupoteza muda na njuluku za walevi.
Baada ya kugundua kuwa chama twawala kinataka kupandikiza katiba yake ya mazabe na mizengwe, ili kiendelee kuwala walevi, nimegundua. Lazima nitumie ujuzi wangu niliupata wakati nikifundisha ‘Constitutional Law’ kwenye chuo kikubwa cha Harvard kutatua tatizo hili ‘once and for all.’
Hakuna ubishi. Chama Cha Mizengwe na Ukale (CCMU) kingependa kuvunja kila kanuni kuhakikisha siri kali mbili zinaingizwa kwenye Katiba.   Hii licha ya kuhujumu na kuvunja Katiba yenyewe, inavunja muungano kirejareja. Lazima muungano uvunjwe kitaalamu na kwa kuridhiana na kila mtu kuchukua hamsini zake kwa raha mstarehe au vipi?
Wapingaji nao wanataka kuongeza siri kali kuwa tatu jambo ambalo CCMU hawataki hata kusikia.
Siri kali nyingi za nini kwa kaya kapuku na ombaomba ambayo mdingi wake kila siku yuko kiguu na njia ughaibuni kubomu lau naye apate cha kukwapua kama si ‘per diem’?
Je! tunahitaji siri kali nyingi au ni wenye kupenda kula kutokana na siri hizi ndiyo wanaotuzuga na kutaka tuwaunge mkono?
Siku zote huwa napenda siri kali na kuu moja tu hasa ikizingatiwa kuwa sisi ni kaya moja, dugu moja, jamii moja. Vunjeni kila upande uwe na siri kali moja mchezo uishe.
Hawa wanaokinzana wakilipana njuluku zetu wapo tayari kuvunja kanuni hata kuruhusu ka-mchezo ka kuviziana na kusingiziana kama alivyofanya Njaa Kaya hivi karibuni Sam Sixx alipovunja kanuni kumruhusu amshambulie jaji Jose Waliboa aliyeonekana kuboroka sana tokana na kitendo hiki cha kihuni.
Kitaalamu kinachoendelea huitwa ‘protracted conflict’. mgogoro wa kudumu ambapo wenye kuushiriki wako tayari kuhujumiana hata kuhujumu wengine wasiohusika kama vile vizazi vijavyo.
Hivyo, tunapaswa kuingilia kati ili kuepusha usaliti, uzandiki, uhuni, upogo hata ulimpyoto unaoweza kuiweka kaya rehani zaidi tena kwa miaka mingi ijayo.
Hivyo basi, napendekeza tuvunje muungano ambao kimsingi unaonekana kuwa mgongano.
Tukifanya hivyo tutatenda haki kwa CCMU na wale wanaotaka sirikali tatu. Kufanya hivyo pia hakutasaidia ‘parties to conflict’ bali kaya nzima ikizingatiwa kuwa:
Kutatoa fursa kwa kaya mbili kupata nafasi ya kupumua na kutafakari kuungana upya kwa masharti mapya au la.
Hakuna haja ya kung’ang’aniana wala kupoteza njuluku na muda wa walevi kwenye jambo ambalo linaweza kupewa uamuzi wa haraka na kila mtu akachukua chake na kudunda, au vipi?
Tukivunja muungano tutatoa fursa kwa pande zote mbili kuishi bila kuungana na kuona madhara au faida zake.
Mfano, malalamiko ya kunyonyana na kubebana yatakufa na kila mtu atakaa kivyake na kuona ukweli ambao hakuwa ameuona kabla ya kupeana talaka.
Tukivunja muungano, tutaokoa muda wa malumbano na upotevu wa pesa za umma ambavyo vimekuwa vikiendelea kule Dodoma.
Kaya yetu ni ombaomba na kapuku isiyopaswa kupoteza njuluku kwenye mambo ya kipuuzi kama malumbano yasiyo na kichwa wala miguu hasa ikizingatiwa kuwa rasimu ilishafanya kila kitu ilichoagizwa na walevi.
Ukiachia mbali kuondoa malumbano uchwara na ufyole na ulimpyoto visivyo na tija, walevi wa pande zote mbili, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1964, watapata fursa si ya kufaidi kaya zao asilia bali hata kujua matatizo yake zinapokuwa nje ya muungano.
Licha ya kufaidi kaya zao katika uasilia wake, walevi watapata fursa ya kutumia uraia wao bila utata wala kuutelekeza mwingine.
Walevi hawakupenda kuishi kwenye kaya moja yenye uraia pacha yaani wadanganyika au wabarawa na wazenj au wapwanie.
Huu ni unafiki ambapo umekuwapo kwa zaidi ya nusu karne unaopaswa kukomeshwa mara moja.
Pia ifahamike, kama tutavunja muungano, tutaepusha muungano wa migongano na mashaka ambao umekuwa ukimomonyolewa taratibu kama alivyobainisha jaji Waliboa hivi karibuni aliposema, “Waasisi walituachia mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano.
Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na Katiba.” Haya madai makubwa kweli kweli.
Ajabu wale ambao wamekuwa wakivunja katiba na muungano waliendelea kuitwa watukufu na waheshimiwa wakati ni watukutu na waishiwa waliopaswa kushitakiwa kwa makosa ya uhaini ambayo adhabu yake ni kunyongwa hadi kunyotoka roho.
Faida nyingine ya kuvunja muungano ni ile hali ya pande mbili kuweza kufaidi uhuru wa kuwa mbali na mwingine. Hili litaweza kusaidia kutafakari na kuyaangalia mambo bila uwepo wala ushawishi mawazo wala masharti ya mwenza.
Huu ni wakati mzuri wa kujipima na kutafakari nini cha kufanya tofauti na mazoea ya kabla ya kuvunjika kwa ndoa. Huu ni wakati muafaka wa kudurusu kila hatua iliyopita na ijayo na kufanya uamuzi wa maana.
Kwa walevi kama mimi huu ndiyo wakati wa kupiga kanywaji na kuvuta bangi sana ili kupata mastimu ya kuweza kufanya uamuzi mulua, au siyo? Wenye ndoto za kugundua wese na kuwa matajiri kama nchi za ghuba ruksa.
Wenye kusema tumetua mzigo hasa ikizingatiwa kuwa kipande kidogo cha kaya kilikuwa na maulaji mengi na makubwa kama uwaziri, ulinzi na kila makandokando watapata fursa ya kuona ukweli hata kama ni mchungu au vipi.
Ninachosisitiza ni kwamba tusifanye mambo kichovu. Tukiamua tuamue tukiwa tayari kufaidi au kusota. Maana nijuavyo, hakuna kisicho na faida hata kama ni kidogo kiasi gani. Kadhalika hakuna kisicho na hasara hata kama ni kizuri kiasi gani.
Hivyo, uamuzi wa kuvunja muungano usitoke kwangu. Ninachofanya ni kutoa ushauri tu tena wa kilevi. Akha mie simo!
‘If you think education is expensive just try ignorance’. Kadhalika, ukidhani ndoa ni kero jaribu talaka. 

Chanzo: Nipashe April 5, 2014.

2 comments:

Jaribu said...

Hii hadithi ya Muungano inanikumbusha mkasa wa rafiki yangu mmoja kutoka Cameroon. Alileta mke kutoka kwao, na huyo bibi hakuchukua hata muda akaanza kumponda mmewe, "Huyo rafiki yako ni mshamba sana!" Miaka ikapita visa kila siku lakini jamaa yeye akawa anadai kuwa ndoa ni muhimu lazima aimarishe. Jamaa miaka minane wanatafuta mtoto hawapati, akasema tatizo ni mume wake kwa sababu yeye kashatoa mimba nne! Akazaa mtoto ambaye akafa alipozaliwa, akawa anawaambia watu kuwa mtoto hakuwa wa mmewe; alivyoona jamaa bado anang'ang'ania akakwangua akaunti yao ya benki, akakimbilia kwao huku akimwonya jamaa kuwa aondoke kabla yeye hajarudi.

Jamaa akapata picha, akatimka, kapata mwanamke mwingine, na within two years mke wake mpya akamzalia watoto wawili.

Moral of the story ni kwamba Waswahili hatupendi mabadiliko, ndio maana tuko nyuma. Nakumbuka jamaa niliyokuwa nasoma naye Ilala Boma, "Baba yangu alifeli, mama alifeli na hata babu yangu alifeli. Halafu unategemea nitakwenda sekondari!"

Wakati mwingine inabidi kila mtu ashike lake.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Your are so funny Jaribu. Hizi mbili ulizotoa zimeniacha nikicheka huku bia yangu ikitaka kunitokea puani. Ni kweli Waswahili tunaogopa mabadiliko vinginevyo kijipande cha ardhi ambacho hata hakilingani na wilaya ya Lushoto kisingetuhenyesha na kututoa jasho wakati kinatunyonya. Nakumbuka mwl Nyerere aliwahi kusema kuwa kama ingekuwa amri yake vile visiwa angevisukumizia mbali. Kimsingi Visiwani wanajua kila kitu. Tukigangamala tunaibuka na mikoa miwili ya Pemba na Zenj. Ningekuwa president ningewaambia wajeshi wetu walioko kule kutangaza kuwa ni mikoa na kuunganisha nchi. Hata ukifanya hivyo haitakuwa kama Russia na Crimea kwa sababu Zenj ilishakufa na kusahaulika. Otherwise Jaribu shukrani kwa stori tamu.