Kila mpenda mageuzi na haki angetamani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kishindwe kwenye uchaguzi ujao au hata kikishinda siyo kwa kishindo kama kilivyiozea. Baada ya waziri mkuu wa zamani aliyeachia ngazi kwa shinikizo la kubainika kushirika kashfa ya Richmond, Edward Lowassa kujiunga na upinzani, alizua mtafaruko ambapo wapo walioona kama ni neema kwa mageuzi na pia walioona kama ni laana kwa upinzani.
Kadiri siku zinavyokwenda, upande unaopinga kujiunga kwa Lowassa na upinzani unazidi kupata mashiko huku nchi ikitikisika si kidogo. Kwa hesabu za haraka haraka ni kwamba katika mtanange huu wanaoonekana kunufaika ni CCM hasa ikizingatiwa kuwa sintofahamu baina na miongoni mwa kambi ya upinzani vinawapa nafuu. Maana, wengi walidhani wapinzani wangeshupalia maovu ya CCM badala ya kugeukana na kukimbiana wao kwa wao. Je hapa kosa ni la nani?
Wapo wanaolaumu upinzani kwa kumpokea Lowassa na kumpa kila alichotaka huku wenyewe ukionekana wazi kukosa kile ulichojiandalia. Mfano, Profesa Lipumba alikaririwa akisema kuwa dhamira na nafsi vyake vilimsuta hasa baada ya kugundua kuwa UKAWA walishindwa kusimamia maadili waliyokuwa wakiyatetea. Alisema kuwa alishangaa kuona wale waliouzuia kuandikwa kwa katiba mpya ya wananchi ndiyo wamegeuzwa waleta mageuzi yale yale waliyozuia na kuua. Hapa, Lipumba ana hoja. Amejitahidi kifalsafa kuonyesha yuko upande gani.
Hata hivyo, Lipumba aliwachanganya wengi pale alipokiri kuwa alishiriki mchakato mzima wa kumpokea na kumkweza Lowassa. Wengi wanashangaa kwanini sasa na si wakati ule au kuna mkono wa mtu? Kwa siasa za Tanzania lolote linawezekana. Swali kubwa linaloulizwa ni: Je kuna kitu au vitu UKAWA wanaficha juu ya kukubaliana kum-import Lowassa?
Iweje mtu mzima, msomi na mwenye akili timamu ashiriki mchakato halafu aupige teke baada ya kukamilika kama hakuna namna? Je kuna kitu kimetembea hapa au ahadi ambazo zimewaacha wengine nje? Maana ukiangalia mantiki ya kumpa Lowassa tiketi haraka haraka bila hata kushauriana na wanachama unashangaa kila kitu. Je kujiondoa kwa Lipumba ni jambo la kawaida ingawa kuhama vyama kwa wanasiasa ni jambo la kawaida? Nadhani kuna tofauti kidogo hasa ikizingatiwa kuwa Lipumba hakuwa anapambana na upinzani ndani ya chama chake wala hakuwa akigombea cheo kingine kama vile ubunge kiasi cha kulazimika kuhama ili kufanikisha alichokitaka. Lazima kutakuwa na jambo tena kubwa tu ambalo wahusika hawataki kuliweka wazi. Maana, kama ni kusutwa na dhamira na nafsi, ilibidi kutokee siku Lipumba alipopokea taarifa ya kuwepo mpango wa kumkaribisha na kumpokea Lowassa. Je kuna ahadi za vyeo ambapo wapo walioahidiwa unono wakati wengine wakiachwa nje? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Baada ya Lipumba kujiuzulu, wasioona mbali wameanza kumuandama wasijue ngoma bado mbichi. Je kama kuna yaliyofichika na Lipumba akasongwa na akaamua kuyaweka hadharani, upinzani utakuwa na lake hapa? Je kuondoka kwa Lipumba kutawapa wangapi moyo kufanya maamuzi magumu kama haya? Je jibu la kuondoka Lipumba ni ubabe au busara zaidi na kuheshimu mchango wake kwenye kulea na kukuza upinzani?
Hata hivyo, kujiuzulu kwa Lipumba na ile sintofahamu inayoendelea kuhusiana na mustakabali wa Dr Wilbrod Slaa kwenye chama chake ni ushahidi tosha kuwa vyama vyetu bado si huru. Bado ima vinamilkiwa na waanzilishi au ndugu zao au watu wao au bado vinaendeshwa kichama kimoja. Maana, kama kungekuwa na uhuru na demokrasia ya kweli, tungesikia nukta ambapo wahusika wameshindwa kukubaliana au kukubaliana. Ukiangalia wazungumzaji wakubwa katika sakata hili, unashangaa kugundua kuwa wahanga wa ujio wa Lowassa walikuwa wemevishwa kilemba cha ukoko wakati wanaoendesha vyama wako nyuma ya pazia. Nataka anayeona dhana hii ni potofu anipe mantiki ya Lipumba na Slaa kuonekana kama wasio na thamani wala mamlaka ikilinganishwa na wengine. Je wapo wenye vyama wanaovuta kamba nyuma ya pazia? Je vyama vya namna hii vinaweza kutuvusha au kufanya mambo tofauti na CCM?
Laiti Lipumba angeyasema yote yaliyomkwaza hadi akajipiga mtama hasa ikizingatiwa alivyokiri kuwa alishiriki mchakato mzima lakini akaupiga chini kwenye saa za mwisho. Laiti na Slaa angefanya maamuzi magumu na kueleza kila anachojua, huenda wananchi wangepata faidi kwa kujua sura hali ya upinzani wetu ambao kipindi hiki umejitahidi kujionyesha ulivyo sawa na CCM.
Ukitathmini uzito wa Lipumba kama mwenyekiti wa chama na nguzo mojawapo ya UKAWA na sintofahamu ya Dk Slaa, unagundua kuwa mizani inalalia upande wa UKAWA. CCM wamempoteza Lowassa ambaye tokana na alivyokwishachafuka angewapa kibarua kigumu kumsafisha wakati UKAWA wameondokewa na kiongozi wa chama tena asiye na tuhuma hata moja. Lowassa hakuwa mwenyekiti wa chama wala mwenye ushawishi mkubwa serikalini baada yakupoteza uwaziri mkuu. Tayari alikuwa majeruhi ambaye CCM wakiamua kupiga kwenye donda atajeruhika zaidi kiasi cha kuzua wasi wasi kuwa anaweza kuzama na upinzani wote jambo ambalo –Mungu apishe –mbali ni hasara kwa mageuzi nchini. Hata akishinda ana jipya gani ambalo CCM hawana? Inashangaza ni kwanini upinzani hakuliona hili kiasi cha kujiweka rehani kwa Lowassa kana kwamba yote uliyokuwa ukisema ili kuwa ni danganya toto au changa la macho. Haiwezekani watu waliojiandaa miaka yote hii watundike daruga kwa mtu mmoja huku wakiwa tayari hata kusambaratika bila kueleza kilichopo nini cha mno.
Tumalizie kwa kuwataka wahusika wazidi kutupa mwanga juu ya kuendelea kuvunjika kwa ndoa yao huku mchumba mpya akipeta bila maelezo pamoja na mapungufu yake.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 16, 2015.
11 comments:
Ninavyofahamu, Lowassa hajabainika kushiriki kashfa ya Richmond. Ushahidi haujatolewa na yeyote, popote. Jambo la pili ni kuwa Lowassa ana wafuasi wengi sana huko CCM, kuanzia wazito hadi walalahoi, na tunajionea wanavyomwagika kuingia UKAWA.
Lipumba na Slaa wamejiweka kando, lakini hatujaona umati ukiwafuata. Sioni kama UKAWA imepata hasara. Badala yake, naona Lipumba na Slaa ndio wamejiumiza.
Kwa anaekusoma mlolongo wako wa makala dhidi ya CCM kisha Lowassa na sasa hivi UKAWA anashindwa kukuelewa nini unachotaka na ili iweje.Sisi wananchi tunataka mabadiliko kwa nchi yetu mabadiliko tuwe huru tutoke katika ukoloni wa CCM na ni sisi wenyewe wananchi ndio wahusika wa kuleta mabadiliko hayo ya kumuweka tunaemtaka madarakani na tumeshakuwa wenye mwamko wa kutosha wa kufanya hivyo, tumechoka na CCM kwa miaka yote iliyotawala tumekuwa ni walala hoi na tumeendelea kuwa walala hoi imetosha!Lete fikra mbadala kwa manufaa ya nchi na wananchi ya kuleta mabadiliko tunayoyataka na usiwe mwenye kukatisha tamaa kwa kukosoa kwa kila majuhudi yanayofanywa na wale ambao wanaotaka kuing'oa CCM mbadarakani.
Inawezekana kumbe wahaaribu upinzania ndiyo waliohamua kujitenga ingawa hao wote dhahiri walishiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kumkaribisha Lawassa!
Mbele na anon shukrani kwa kuacha unyayo hapa. Nianze na Mbele, ni kweli kuwa Lowassa hajakutwa na hatia na mahakama. Bahati nzuri hili si jipya. Ulishaliongelea na nikalitolea ufafanuzi kuwa mahamakama ya kisiasa ni tofauti na ya kisheria na isitoshe kwenye nchi iliyomezwa na ufisadi sitegemei kama haki inaweza kutendeka kwa viwango vya kimataifa. Hivyo, hoja hii tuliishaifunga kwa kuitolea ufafanuzi. Kuhusiana na umati wa watu, hata Mrema alipata umati tena mkubwa tu. Kwa hiyo umati bado si kigezo hasa ikizingatiwa kuwa hata mgombea wa CCM hajaanza kampeni kama alivyofanya Lowassa.
Anon wa kwanza siwakatishi tamaa wala kumshambulia UKAWA. Kimsingi mimi rafiki yangu ni haki bila kujali anayeitenda au kuivunja ni nani. Hivvyo, kwa vile nilishambulia CCM msitegemee nilikuwa UKAWA. Mimi ni mchambuzi,yeyote atakayefanya jema au baya kwa faida au hasara ya wananchi wa Tanzania mimi ninaye. Nadhani tumeelewana.
Anon wa pili hadi sasa hatujui nani anaharibu upinzani kati ya waliopinga kuja kwa Lowassa na waliomkaribisha hadi matokeo ya uchaguzi mwakani ndipo tutaongea vizuri. Ni mapema sana kuamua. Tuwe na subira ila tusikimbiane wakati muafaka ukifika.
Ndugu Mhango
Msimamo wangu kuhusu tuhuma za ufisadi wa Lowassa sijaubadili na sitaubadili. Ninasisitiza kuwa kuna kitu kinachoitwa utawala wa sheria, na kuna tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Kufuatana na misingi hiyo ni kwamba Lowassa ana haki ya kuhesabiwa kuwa hana hatia, hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.
Tukianza kupindisha misingi hii, au kuendekeza ulegevu wowote katika uzingatiaji wa misingi hii, tutakuwa tunaenda njia moja na mafisadi. Kuna sababu gani kuukemea ufisadi iwapo sisi wenyewe hatuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria? Hitimisho ulilotoa wakati ule ni lako, sio letu. Hitimisho kwa upande wangu ni kwamba kumwita Lowassa fisadi ni kumkosea haki, kwa sababu hakuna mahakama ambayo imethibitisha kwamba yeye ni fisadi.
Kaka Mbele nakubaliana nawe ila nashangaa kwanini hukuchukua msimamo huu Lowassa alipokuwa CCM au ni kwa vile mwenye mapenzi haoni ingawa macho anayo? Hata hukumu yako kuwa CCM ni bonge ya dampo kubwa ambayo niliisoma kwenye uga wako basi utakuwa umekosea. Maana hakuna mahakama iliyosema hivyo. Hatuwezi kuacha kutumia akili zetu tukataka kila kitu tufuate maandishi hata kama hayaingii kwenye hali fulani. Si vibaya kuwa na msimamo na kuushikilia kama unaweza kuutetea. Iweje CCM wahukumiwe ufisadi bila kufika mahakamani na hao hao wakiondoka huko wawe wasafi? Nashangaa kuona umegeuka mtetezi wa Lowassa wakati zama zile akiwa CCM uliwaponda wote. Kupanga ni kuchagua. Mimi sitatea mtu bali haki bila kujali mhusika yuko upande gani. Ndiyo maana nasema, Lowassa ni fisadi kama alivyokutwa na Kamati teule ya Bunge hadi akaamua kujitia kitanzi mwenyewe. Kama hakuwa amefanya huo ufisadi kwenye kashfa ya Richmond, ilikuwaje akaachia ngazi kwa hiari yake? Inajulikana kuwa aliogopa mengi yasiwekwe hadharani hivyo akaamua kufunika kombe mapema kabla hajakaangwa.
Nsdugu Mhango
Shukrani kwa ujumbe wako. Ukipitia tena ule ujumbe wa CCM kuwa dampo kubwa la takataka, utaona nilijenga wazo hilo kutokana na matamshi ya CCM wenyewe. CCM wamekuwa wakisema kwamba hao wanaohama kutoka CCM kwenda upinzani ni makapi na "oil chafu."
Sasa kwa kuzingatia jinsi hao wanaoitwa makapi na "oil chafu" wanavyoendelea kumwagikia upinzani, na kwa kuzingatia kuwa CCM inasema kuwa pamoja na wimbi hilo la wahamaji, CCM ni imara, nilichosema ni kuwa iwapo hayo wanayosema CCM ni ukweli, basi ni wazi kuwa CCM ni dampo kubwa la takataka. Sikutunga kitu. Nimejikita katika yale wanayoyasema CCM wenyewe.
Kaka usemayo ni kweli kuwa walioanzisha mchezo wa matusi ni CCM sawa na ambavyo wapinzani walianzisha kuita akina Lowassa Mafisadi. Hivyo, nasi tunaposema ni mafisadi hatutungi wala kuzua bali kutumia maneno yao kama ambavyo wewe umetumia ya CCM bila kujali kama kufanya hivyo ni kinyume na imani yako ya haki za binadamu na uamuzi wa mahakama kuhusiana na ukweli wa jambo. Nimefurahishwa na utetezi wako.
Ndugu Mhango
Sijui wengine wana mawazo gani kuhusu suala hilo tata. Ningefurahi kuwasikia.
Hata mimi simfurahii huyo Lowasa lakini wakati mwingine siasa inahitaji kuwa "pragmatic", inabidi ulale kitanda kimoja na watu wanaokuchefua. Kama kumkumbatia Lowasa kutafanya CCM ibwagwe, mimi siwezi kulia sana.
Unaweza kuona mfano wa wenzetu. Kwenye Vita Vikuu vya Pili, nchi za kibepari za Magharibi ziliungana na Urusi ambayo walikuwa hawaipendi, kwa sababu adui wao alikuwa mmoja, Hitler. Na baada ya vita kuisha, nchi za Magharibi zilipoona kuwa Urusi inawageuka, basi na wao badala ya kuwanyonga majasusi na wanasayansi wa Hitler wakaamua kuwaajiri wawasaidie kwenye upelelezi wa maadui wa muda huo, Warusi na vile vile kwenye utafiti wa roketi. Maslahi mapana ya taifa ni tofauti na maadili ya kanisani. Kama Mandela aliweza kukaa na kuongea na makaburu waliompa kifungo cha muda mrefu, sembuse Lowasa.
Na kuhusu Lowasa, hata kama yeye anahusika na Richmond, Godfather mwenyewe ni Profesa Tezi Dume. Hizo hela anazopoteza kwenye safari zake zisizoisha ni zaidi hata ya Richmond. Ukiongezea na wizi mwingine uliotokea baada ya Lowasa "kujiuzulu", unakuta gharama ya Richmond haifui dafu ukilinganisha na Dowans, Escrow na mengineyo.
Jaribu kwanza karibu baada ya muda mrefu. Kwa kiasi fulani nimeyakubali maoni yako ingawa bado nina shaka kama wapinzani wana mfumo na utaratibu tayari wa kuweza kumdhibiti Lowassa baada ya kulibwa zimwi. Laiti wangeonyesha hili, ningemuunga mkono na hata mguu mgombea wao. Usemayo ni kweli ingawa haya apply kwa hali ya Tanzania ambapo watu hasa wanasiasa binafsi kwa mujibu wa katiba yetu wanaweza kuliburuza taifa bila kuwa na namna ya kuwadhibiti hivyo kujiunga na adui kukawa balaa kubwa na maafa zaidi kama ilivyotokea kwa Mrema na upinzani.
Post a Comment