How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 7 August 2015

Mlevi atoka UKAUA na kuanzisha UKOME

Baada ya siasa za kuuzana na kununuana kuchukua sura Bongolalaland–ambapo ngurumbili wachafu wanasafishana ili kupata ulaji–Mlevi nimestukia dili zima. Japo sikuwa nimeitaarifu dunia kuwa nilikuwa miongoni mwa wanaounda Umoja wa Kukomboa Umma wa Apechealolo (UKAUA), ijulikane. Nilikuwa mmoja wa waanzilishi na wanachama. Sikupenda kutangaza kwa vile kile chama twawala–kama kingejua kijogoo nimo–kingeuandama umoja ule kuliko kilivyofanya kwa vile kinajua nguvu yangu ya hoja na kukubalika kwangu. Tofauti na wale walioharibu kila kitu kwa tamaa zao za urahis na wale waliowanunua hadi wakajivua nguo hadharani tena wakiramba matapishi yao, mimi najulikana kwa msimamo wangu na sera za nguvu.
 Kuanzia leo natangaza rasmi kuwa nitaanzisha umoja wangu na walevi utakaojulikana kama United and Keen Organization Meant for Emancipation (UKOME) ili kuwakomesha wanaofanya biashara ya siasa kwa mgongo wa upingaji.
Kabla ya kujitoa na kufikiria kuanzisha UKOME, niliwauliza washirika zangu yaani Porofedheha Ibra Pumba, Freeguy Mboe, Eddy Mkaidi na Mbatie sababu zenye mashiko za kukubali kujigeuza nepi ya Eddie Luwasha waliyekuwa wamemfichua na kumpaka wenyewe wasipate jibu. Nilipozidi kuwabana wanieleze kama amewakatia uchache ndiyo walizidi kuchanganyikiwa na kunichukia kiasi cha kuniona kama nawaharibia kitumbua chao.
Baada ya kuamua kujitoa wapo walionishauri nijiunge na Chama chaMafisadi (CcM). Kwa vile mimi si fisadi na nauchukia ufisadi kuliko hata ukimwi, nimeamua liwalo na liwe. Sasa naanzisha zana yangu ya kuwakomboa walevi.
Nina sababu za kufanya hivi.
Mosi, ni kutaka kulipiza kisasi kwa kusalitiwa na wenzangu.
Pili, nataka kutimiza yale tuliyokuwa tumeahidi kabla ya kidudumtu kutuvamia na kumwaga sumu yake itokanayo na ukwasi wake wa kukwapua toka kwa walevi.
Tatu, nataka kuonyesha kuwa bado kuna watu wenye udhu na maono ya mbali ambao si rahisi kununuliwa wala  kubabaishwa na yeyote hata awe na mshiko na sifa kiasi gani. Kama jamaa angekuwa dili ilikuwaje akapigwa kibuti kwenye chama chake?
Nne, nataka kutumia fursa hii kuanzisha nguvu ya tatu yaani UKOME ambayo itanufaika na anguko la UKAUA hapo Oktoba kama ilivyotokea mwaka 1995 ambacho chama cha ENISISIARA Mageuko kilimpwakia Augus Lyatongolwa Mlemavu akaishia kukizamisha kirahisi. Mimi ni gwiji la historia. Hivyo, licha ya kujua kusoma alama za nyakati, najua kuitafsiri na kuitumia historia vizuri. Siko tayari kugeuzwa kama chapati na fisadi aliyekubuhu.
Hakuna kitu kiliniudhi nusu ya kujinyotoa roho kama kushuhudia jamaa akivaa magwanda ya upingaji badala ya jela. Huyu alipaswa kuwa lupango kama si kushamiri kwa mchezo wa kulindana na kuwekana nyumba ndogo. Baada ya UKAUA kuwekwa kimada na jamaa, nimeamua nijiondoe na heshima zangu badala ya kufanya siasa za maji taka na kuramba matapishi kama wale waliojimaliza wakidhani wamepata wasijue wamepatikana.
Kila nikikumbuka muda, mawazo na njuluku nilivyotumia UKAUA na kuishia kuuawa kishenzi, natamani nichukue bakora nichape watu. Hata hivyo, kwa vile mimi ni mpenda amani na asiyeyumba, naamua kujitoa rasmi ili nisichafuliwe na huyu bata waliyempwakia wasijue si chochote wala lolote bali zigo la hasara.
Hakuna waliponiacha hoi kama kufanya mambo ya chama kimoja kwa kumruhusu ngurumbili tena fisadi mmoja achukue fomu pekee. Yako wapi mabadiliko? Iko wapi demokrasia wanayotaka kuanzisha iwapo wanarejesha ufalme tena wa kifisadi kwa mlango wa nyuma? Hivi miaka yote ya maandilizi mlijiandaa kwa aibu hii ya kuwekwa kinyumba mchana kweupe? Hata kunguru wanawacheka kwa jinsi mlivyoingia choo ya kike. Na hakika itabuma na kula kwenu. Siku hiyo ndiyo nitacheka na kushangilia japo siwapendi magamba.
Sioni tofauti ya magamba na UKAUA kwa sasa kwa vile wote wanaua demokrasia. Kwa vile nimestukia mchezo, nitapeleka mswada bungeni kutunga sheria itakayomtaka mgombea wa urahis kwa tiketi cha chama chochote shurti awe amekaa kwenye chama husika bila kutoka si chini ya miaka mitano ili kuwakomesha virukanjia wa kisiasa wanaokimbiza maslahi yao huku wakitelekeza ya kaya.
Japo mie si mtabiri kama yule kidhabu aliyekuwa akitumiwa na mgamba kututisha, Shehena Yaya kabla ya kurejesha namba, naweza kutabiri kwa uhakika kuwa sasa Dk Kanywaji Makufuli atapeta kama hana akili nzuri. Maana, tulidhani tungempa upinzani wa kuua mtu. Kwa vile wenzangu wameamua kuuza mechi –piga ua –lazima Dk Kanywaji apete huku akishinda ki-Tsunami. Naona yule anacheka na kutikisa kichwa kwa sababu anaugua ugonjwa wa mapenzi kibubusa. Japo wote tulitaka magamba yadondoshwe, si mwaka huu. Ama kweli ukishangaa ya Mlemavu utaona ya Luwasha! Sijui jamaa kawapa nini jamaa zangu hadi wapagawa hivi? Ama kweli penye udhia penyeza rupia. Nadhani akina Jimmy Rugemalayer, Singasinga na Roat Tamu na mafisi na mafisadi wengine sasa wanachekelea wasijue ndiyo kiama chao kama Dk Kanywaji atapeta. Na lazima apete kutokana na uzembe, upogo na uroho ulioonyeshwa na wenzangu ambao kwa sasa nawaona kama nepi kama sio diaper kisiasa.
Hawa jamaa wamejua kututenda. Yaani waliuanika huo msukule wao pale Mwemba Yanga 15 Septemba, 2007. Nakumbuka nilikuwapo nikasikia na kuona kila kitu kwa macho na masikio yangu hata kama niliutwika mma. Nakumbuka wakiongozwa na Dk Silaha walivyokuja na list of shame wasijue wataishia kuwa politicians of shame!

Tena kabla ya kusahau, ngoja nichukue fursa hii kumkaribisha Dk Silaha kwenye UKOME. Maana tangu zengwe hili lianze sijamuenga popote wala hajatoa tamko ya nini kitafuatia hasa baada ya wenzake ambao wanajiona ndiyo wenye vyama kumtosa. Je naye atakubali kudhalilisha utu wake na kuramba matapishi yake hasa ikizingatiwa kuwa ndiye aliyetoa list of shame? Sijui ataweka wapi uso wake. Daktari Silaha ndugu na rafiki yangu, huna haja ya kufa kwa ugonjwa wa moyo wala kujivua nguo hadharani. Njoo UKOME tuwakomesha hawa vidhabu waliotupotezea muda na mechi.
Chanzo: Nipashe Agosti 8, 2015.

No comments: