Baada ya waziri mkuu aliyeachia ngazi tokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa kuhamia rasmi kwenye upinzani, bado amezidi kuongeza utata juu ya utata. Wapo wanaoona kama Lowassa amefanya maamuzi magumu na kuchukua hatua mujarabu. Pia wapo wanaopinga hatua hii na kuona ni kama matokeo ya tamaa urais kwa upande wa Lowassa na uchumia tumbo kwa upande wa upinzani.
Wale wasiokubaliana
na uamuzi wa Lowassa wanaona kama amejimaliza na kuuchafua upinzani kiasi cha
kukosa kuaminiwa na umma tena hasa kutokana na jinsi ulivyokuwa ukimsakama na
kumuonyesha kama mtu asiyefaa kushika madaraka makubwa kama haya hasa kutokana
na kuhusishwa na ufisadi wa kutisha.
Sasa si uvumi
tena. Lowassa ametua CHADEMA. Wengi wanangojea kuona hatua nyingine atakayopiga
Lowassa kwenye nyumba yake mpya. Hata hivyo,
maswali ni mengi kuliko majibu. Wapo wanaohoji: Je asingeahidiwa kuwa mgombewa kwa
tiketi ya upinzani angehama? Je hapa nani
anamtumia nani na matokeo yake ni nini kwa watanzania? Je ikitokea wakamkatalia
kugombea atarudi CCM na je CCM watampokea au ndiyo utakuwa mwisho wa Lowassa
kisiasa?
Kimsingi,
wengi wanashuku ndoa hii ya mkeka kati ya Lowassa na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA). Kwani inakuwa vigumu kuwaelewa upinzani hasa namna watakavyoweza
kuweleza wananchi haya mapenzi ya haraka na imani vimetoka wapi na sababu yake
ni nini. Kitendo cha upinzani kumpwakia na kumpokea Lowassa kiasi cha kukiuka
yale waliyohubiri kwa muda mrefu kimefanya kuwepo hata hisia zaidi ya siasa. Maana wapo wenye hisia kuwa huenda kuna
biashara nyuma ya pazia ambapo mhusika amenunua tiketi toka kwenye upinzani
ambao umethibitisha kuwa kumbe ulikuwa ukipiga kelele tu. Haukuwa na mkakati wa
kuweza kukishinda Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiasi cha kulazimia kuramba
matapishi yake tena ya jana. Je ujio wa Lowassa kwenye upinzani ni Baraka au
laana ambayo matokeo yake yatazidi kuudhofisha na kuunyima heshima mbele ya
watanzania?
Ukiangalia sababu
za Lowassa kujiengua CCM na kuelekea upinzani unagundua kuwa hata kama
akibahatika kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya upizani na akashinda
uchaguzi, anaweza kuwa tatizo zaidi ya suluhu. Je Lowassa amehama kulipiza
kisasi, kutimiza ndoto ya urais au kujikoa kisiasa baada ya CCM kuonyesha wazi
kumchoka na kumtosa kwa mara nyingine?
Je nini
sababu ya UKAWA kumpokea na kumkweza Lowassa kiasi cha kuwaacha walio wengi
midomo wazi? Je ni ile hali ya kujua kuwa hawakuwa na ubavu wa kuishinda CCM?
Je ni mbinu ya kuishi kisiasa? Je hatua hii itazaa matunda au kuumaliza upya
upinzani?
Kwa namna
upinzani ulivyokuwa umembomoa Lowassa, utakuwa na kibarua kigumu kuwashawishi
wapiga kura na watanzania ili auzike. Wengi wanadhani Lowassa asipewe tiketi na
badala yake atulie kwenye upinzani akiusaidia kuiangusha CCM huku akibakia kuwa
mtu muhimu katika upinzani na kwa taifa. Kama wote wataendekeza maslahi
binafsi, uwezekano wa Lowassa kugeuka laana kwa upinzani ni mkubwa kuliko
kugeuka baraka. Itakuwa jambo la ajabu kama wote wawili hawataiona hatari hii
wakashikilia siasa za majaribio (Experimental politics). Maana inashangaza
kuona magwiji wa upinzani tena madaktari wa falsafa kushindwa kutambua jambo
rahisi kama hili. Kwanini Lowassa apate anachokitaka wakati upinzani ukose
ulichopigania na kujiandalia kwa muda mrefu?
Nadhani, kama Lowassa atapitishwa kuwa mgombea wa upinzani atakuwa –licha
ya kupata nguvu ya ajabu na haraka –na kila sababu ya kuuburuza kama alivyowahi
kufanya Augustine Mrema ambaye kuhamia kwake NCCR-Mageuzi kulikiua chama na
akageuka kuwa laana badala ya baraka. Je ni upofu kiasi gani kwa magwiji kama
wa upinzani kushindwa kuisoma historian a mafunzo yake? Ama kweli tamaa mbele
mauti nyuma walisema wahenga.
Kwa wenye
kujua malengo binafsi ya Lowassa na malengo ya kitaifa ya upinzani, inakuwa
vigumu kuona namna ya kusuluhisha tofauti hizi kimilengo na kimkakati.
Ukisoma maoni
mengi ya watanzania karibu kila sehemu, wenye shaka na ndoa ya Lowassa na UKAWA
ni wengi kuliko wanaoiunga mkono. Kinachofanya ndoa hii kuwa ngumu ni ile hali
ya wachumba kuwahi kutuhumiana mambo mengi machafu ambayo si rahisi kuyasafisha
ndani ya muda mfupi. Na kama sikosei, CCM wataitumia hali hii vizuri kuzidi
kumuumbua Lowassa kiasi cha upinzani kuishia kujilaumu baadaye baada ya uchaguzi ujao. Kumpokea si jambo baya.
Maana, ni haki ya kila anayetaka kujiunga au kujitoa kwenye chama. Jambo linaloonekana
kuwa baya ni kile kinachoonekana kama upinzani kuvunja kanuni zake na ahadi
zake kiasi cha kumpa nafasi na hadhi ambayo Lowassa kimsingi hastahili. Je wamempima
na wana uhakika gani kuwa kama atashindwa kupata anachokitafuta hatawafanyia
kama alivyowafanyia CCM? Ama kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo.
Lowassa ni mtu anayejiona kuwa na nguvu kuliko chama. Hivyo, upinzani hauna
namna ya kuipunguza au kui-control nguvu hii tokana na kumkubalia kila kitu
haraka. Hata hivyo, tungoje tusikie vigezo vitakavyotolewa na UKAWA juu ya
kumpokea na hata kumpitisha awe mgombea wake.
Tumalizie kwa
kuwashauri Lowassa na UKAWA kuepuka maslahi binafsi na badala yake waangalie
alama za nyakati na ukweli wa mambo kwa kuidurusu hali hali ya siasa za Tanzania.
Nakumbuka, hata Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani wa Kenya alipohamia
upinzani toka KANU hakugombea urais zaidi ya kutumia umaarufu na nguvu yake
kuunga mkono mgombea wa upinzani Mwai Kibaki na kushinda baada ya kutamka kauli
yake maarufu KIBAKI TOSHA. Tunadhani hata Lowassa alipaswa kusema, MGOMBEA WA
UPINZANI TOSHA badala ya kuhangaika na kugombea urais mwenyewe. Hii inaweza
kufanya safari yake ya matumaini kuishi kuwa safari isiyo na matumaini chochote
bali anguko jingine la kisiasa.
Chanzo: Dira
No comments:
Post a Comment