How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 9 August 2015

Lowassa angejisaidia na kuusaidia upinzani kama

Kwa hali ilivyo ni kwamba waziri mkuu wa zamani aliyeondoka madarakani kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa amepania kupata anachotaka, urais. Baada ya kuenguliwa kwenye mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutimkia upinzani na hatimaye kuchukua fomu, inawezekana Lowassa akajaribu karata yake japo akiwa nje ya CCM. Je atafanikiwa hasa ikizingatiwa kuwa anacheza kwenye timu ngeni dhidi ya timu ya nyumbani?
Kama Lowassa anataka kunufaika na kuunufaisha upinzani kuondoa wabaya wake, basi angepaswa kufanya yafuatayo kuliko kukimbilia kuchukua fomu za kutaka apitishwe kupeperusha bendera ya UKAWA.
Kwanza, angeachana na ndoto ya kuwa mgombea. Kwani –kama uchaguzi wa ndani ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) utafanyika kwa haki, Lowassa hawezi kupata kura akamshinda yeyote kwa vile ni mgeni. Hivyo, tukubaliane kuwa kama Lowassa atashinda, lazima iwe ni kupitia uchakachuaji. Maana, hana chama wala wafuasi. Hata kama hawa aliotoka nao CCM hawezi kufua dafu kwa wafuasi wa CHADEMA na wale wa vyama washirika. Hivyo, kama atapitishwa –kama inavyoonekana baada ya kuchukua fomu peke yake –lazima kanuni na demokrasia vifinywe ili kumwezesha kusimama kwenye uchaguzi jambo ambalo ni pigo kwa upinzani. Maana, watakuwa wameonyesha mfano mbaya kuhusiana na ushindani wa kidemokrasia. Hapa ndipo swali kuu la: Je Lowassa ni mradi wa nani katika UKAWA?
Pili, alipaswa kujikita kwenye kuelezea anachojua kuhusiana na Richmond huku akisema ukweli kwa kueleza ni kiasi gani rais Jakaya Kikwete alishiriki. Maana kusema, “Nilijaribu kuvunja mkataba oda ikatoka juu” bila ushahidi unaonekana kama usanii wa kawaida na kutapatapa au kutaka kufa na mtu.
Tatu, ili kuwashawishi wananchi na hasa wapiga kura, Lowassa anapaswa kueleza namna serikali ilivyoficha ukweli kuhusiana na kashfa nzima. Hata kama kufanya hivyo kulilenga kumuokoa yeye baada ya kuwajibika kama namna ya kuepusha serikali nzima isianguke. Lakini kama Lowassa ataendelea kutoa shutuma na ushahidi nusu nusu, atazidi kuchafuka zaidi     na hivyo, kukosa kilichomtoa CCM. Nadhani kama hii itatokea Lowassa atazama na upinzani wote isipokuwa vyama vidogo vilivyopo nje ambavyo kimoja chao kitanufaika kama ilivyokuwa kwa CHADEMA baada ya Mrema kuizamisha NCCR-Mageuzi na hatimaye TLP.
Nne, Lowassa anapaswa kujibu tuhuma zote bila kificho. Hii itamsaidia kujionyesha kama mtu mkweli anayeweza kuomba msamaha na akabadilika na kuaminika tena.
Tano, akishaeleza anachojua juu ya Richmond, atapaswa kuomba msamaha kwa watanzania. Kwani atakuwa –licha ya kuwapa ukweli ambao wanauhitaji –ameonyesha alivyo na nia ya kujirekebisha na kujutia makosa yake. Hivyo, ombi lake la msamaha litakuwa na maana zaidi hasa ikizingatiwa kuwa yeye si malaika.
Sita, aeleza mengine anayojua kwa muda wote aliokuwa kwenye serikali na CCM na namna machinery ilivyokuwa ikifanya kazi kuhujumu juhudi na raslimali za watanzania. Hili nalo litamjengea heshima. Kwa vile atakuwa amefichua mbinu chafu ambazo hazitarudiwa hapo baadaye.
Saba, baada ya kufanya hayo hapo juu, anapaswa aeleze mchango aliokuja nao kwenye upinzani kisera na kimkakati na anavyopanga kusonga mbele mbele baada ya kutubu na kuomba msamaha. Hapa lazima aeleze sera zake binafsi na za chama chake akizipambanisha na za CCM huku akirejea kwenye mema aliyofanya kwa wakati wote alioutumikia umma.
Nane, ahakikishe anataja mali zake na za mkewe bila kuficha kitu ili aendelee kuwathibitisha wananchi kuwa sasa ameuona mwanga na kuamua kujirudi na kutubia.
Tisa, ashiriki kikamilifu kumnadi mgombea wa UKAWA ambaye sharti awe mtu mwingine. Afanye alichofanya mwenzake wa Kenya Raila Odinga. Alipoenguliwa na rais wa zamani Daniel arap Moi, alijiunga upinzani na kumuunga mkono mgombea wa umoja wa wapinzani, Mwai Kibaki na kuiangusha na kuifuta kabisa KANU alipokuja na kauli yake maarufu, “Kibaki Tosa” yaani Kibaki anatosha.
Kumi, Lowassa anapaswa kukubali ukweli kuwa huwezi kupata kila unachokitaka duniani kwa namna na wakati unapotaka. Nadhani kwa kuunga mkono mgombea wa upinzani, atafanikiwa kuwaadhibu wabaya wake na kuonyesha umuhimu wake katika upinzani na siasa za Tanzania na jinsi mchango wake ulivyo mkubwa. Ila kama ataendelea kusikiliza tamaa zake za urais, amini usiamini, atashindwa tu na kuishia alipoishia Mrema japo tofauti ni kwamba Lowassa atakuwa amehujumu upinzani kwa kulazimisha kusimama na akazamisha vyama vinne vilivyo kuwa tegemeo nchini.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 9, 2015.

3 comments:

Mbele said...

Ni muhimu kuzingatia pia kwamba UKAWA walimtaka na wanamtaka Lowassa, na walitaka awe mgombea wao wa urais. Hili si suala la upande moja. UKAWA wanatambua nguvu ya Lowassa, na walitaka, na wameridhia kuwa yeye awe mgombea wao wa urais. Wanatambua kuwa kwa yeye kuwa mgombea urais, kuna uwezekano mkubwa wa kuing'oa CCM madarakani.

CCM yenyewe inatambua tishio hilo, na ndio maana inafadhaika sana. Baada ya Lowassa kuhamia UKAWA, upepo wa kisiasa unazidi kuvuma kuelekea UKAWA. Kila kukicha tunasikia wazito wa CCM na wanachama wa CCM wanakimbilia UKAWA. Hili si suala la kubuniwa, ni hali halisi inayoonekana siku hadi siku.

Lowassa hayuko UKAWA kwa ajenda yake binafsi. Atakuwa anasimamia maazimio na matakwa ya UKAWA. Ila tu ni kwamba ajenda na matakwa ya UKAWA na yale ya Lowassa ni yale yale kwa kiasi kikubwa. Ndivyo walivyoanza. Huko mbele ya safari, katika kufanya kazi pamoja, katika kufahamiana zaidi, katika kuelimishana, na katika kurekebishana, wanaweza wakaondoa tofauti zao, kama ziko, wakawa kitu kimoja thabiti.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele shukrani kwa mchango wako japo sikubaliani na jinsi ulivyorahisha mambo. Nadhani tunapaswa kuangalia upande wa pili wa shilingi--kama CCM haitadondoka nini kitafuatia? Je UKAWA wanaootea kuiondoa CCM kwa kumeguka? Umenifurahisha na kunichekesha kusema eti maslahi ya Lowassa ni sawa na UKAWA. Naweza kukubaliana nawe kama ungesema lengo lao lakini si maslahi. Pia naweza kukubaliana nawe ukisema ni maslahi binafsi na si ya taifa. Ila kusema wanataka kuing'oa CCM kwa maslahi ya watanzania kidogo inatia shaka. Najaribu kumtathmini Lowassa kwa upande mwingine, mfano kama angepitishwa na CCM unadhani angekuwa mpole na MKAWA kama unavyomuona? Nadhani UKAWA wamethibitisha kitu kimoja au viwili. Kwanza, wanaweza kuchukua risk jambo ambalo ni zuri na hatari kisiasa. Pili, wamekuwa wakweli kuwa miaka yote walikuwa wanapiga siasa na kubangaiza. Maana haiwezekani mtu mmoja awe na nguvu kuliko vyama vinne na hivi vyama vikwa na maana kama tutakuwa wakweli.
Naona niachie hapa nisiandike makala ndani ya makala.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Hii mijadala, na uchambuzi wa kila suala la kipengele ni muhimu. Inatoa mwanga kwa kila anayeshiriki au anayefuatilia. Siku na saa na dakika itakuja ya kupiga kura, kuamua kunyoa au kusuka. Ningekuwa mpiga kura, kwa hali ilivyo sasa, na kama hakutakuwa na mabadiliko yasiyotarajiwa, kura yangu ningempa Lowassa.

Ni uamuzi wa kusuka au kunyoa. Hatuna malaika kati ya wagombea. Hilo ni wazi. Kila mpiga kura atajijua mwenyewe.