Hivi karibuni Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imefanya kitu ambacho kimewashinda na kuwashangaza wengi. Ni pale ilipovunja majumba yaliyojengwa kinyume cha sheria kwenye maeneo ya Mwenge na Kunduchi. Kadhalika halmashauri nyingine za Ilala na Temeke zilivunja majumba yaliyojengwa kiholela kwenye maeneo ya akiba ya barabara. Hili ni jambo jema. Lazima watanzania wajifunze au kufundishwa kufuata na kuheshimu sheria. Tunashauri ubomoaji huu usiwe nguvu ya soda au kufanya kazi kizimamoto. Lazima upanue wigo wake na kubomoa na kuwatoza faini wote waliojenga kwenye maeneo ya wazi au yasiyoruhusiwa.
Pia ubomoaji uhusishe majengo mengi jijini yaliyojengwa chini ya viwango. Kwani –majengo haya ni mabomu yanayongojea kulipuka na kuua watu wengi wasio na hatia kam ilivyotokea miaka ya nyuma ambapo jingo la mitaa ya Uhindini liliporomoka na kuua watu wasio na hatia. Tunadhani ni wakati muafaka kuitaka Manispaa ya Ilala kuhakikisha jengo pacha lililokuwa libomolewa wakati wa utawala uliopita na lisibomolewe kufuatia. Pia tunashauri majengo ya vigogo yanayojulikana kujengwa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa yavunje. Mfano mdogo ni jengo la Getrude Rwakatare ambalo mbunge mmoja aliwahi kudai lilipaswa kuvunjwa lakini sheria ikamuogopa mhusika. Chini ya utawala mpya wa rais John Pombe Magufuli, tunaamini majengo husika yatabomolewa.
Pia yapo mahoteli yanayojulikana ambayo nayo yanapaswa kubomolewa na wahusika kutozwa faini hata kufungwa kwa kuvunja sheria. Haiwezekani tugeuke taifa la wavunja sheria. Lazima tabia hii ikomeshwe bila kuangalia sura ya mtu.
Kama serikali mpya itarudia makosa yaliyofanywa na serikali goi goi na ya kishikaji iliyopita, itapoteza imani kwa wananchi. Hivyo, ingekuwa vizuri zoezi la kubomoa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria kutoangalia sura wala hadhi ya mhusika bali sheria kama ilivyo. Kwa kubomoa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria bila kujali thamani yake wala hadhi za wamilki, serikali ya awamu ya tano itakuwa inatoa onyo na tangazo kuwa mambo ya kufanya mambo kwa mazoea yamekwisha wakati wake. Wananchi waisiadie serikali kuikumbusha pale inapojisahau ili itende haki kwa watanzania wote bila kubagua.
Kitu cha msingi mno hapa ni kufuata sheria kuhakikisha kuwa watakaobomolewa nyumba zao wasiende mahakamani na kudai fidia na kushindwa. Hapa nadhani serikali inabidi kuitupia jicho wizara ya ardhi. Kama kuna watakaokuwa na hati milki za maeneo husika basi wabanwe waeleze walivyozipata au waliowapatia ili nao wachukuliwe hatua. Kwa njia hii tunaweza kuwabaina wafanyakazi wabovu, wala rushwa na wezi hata kama wamefanya madudu haya kwa muda mrefu na kuwachukulia hatua. Hili nalo litatoa onyo kwa wale wanaotarajia kurudia mchezo huu.
Hili la kumlika wizara ya ardhi ni muhimu sana. Maana tokana na ufisadi, ufisi, ubinafsi na upogo imefikia mahali hata wageni wanauziwa na kumilkishwa ardhi kinyume cha sheria kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo raia wa Uswisi anayeishi nchini Kenya Dk. George Hess alikuwa akiuza viwanja nchini kiasi cha kuzua gumzo jinsi mgeni huyu alivyoweza kumilkishwa ardhi ambayo anaifanyia biashara. Je wako akina Hess wangapi nchini? Je walipataje uhalali wa kumilki ardhi husika? Lazima washirika wa wahalifu hawa wajulikana ili kuepusha kuhatarisha usalama wa taifa na maslahi ya watanzania. Haiwezekani mgeni aje na kujua wapi kuna viwanja na akapata hati ya kuvimilki bila kuwa na watu ndani ya mfumo.
Tunaamini kuwa kama manispaa husika zitachukua hatua ya kubomoa majumba yaliyojengwa kinyume cha sheria na kutoa taarifa serikalini kuwachukulia hatua wahusika, tunaweza kuokoa ardhi na fedha nyingi za taifa.
Tokana na utawala wa kibabaishaji na fisadi, taifa letu liligeuzwa shamba la bibi ambapo watu tena wageni huja na kujifanyia kila watakacho hata kama kinakinzana na sheria zetu bila kuchukuliwa hatua. Chini ya utawala mpya ulioanza kujitofautisha na tawala mbovu za nyuma, watanzania wanategemea kuona mambo yakibadilika na sheria kufuatwa na kuheshimiwa vilivyo.
Tumalizie kwa kuitaka serikali kushirikiana na Manispaa si za Dar es Salaam bali zote nchini kubaini wezi wa ardhi za umma na kuwachukulia hatua zinazostahili. Tunashauri zoezi hili ligeuzwe kuwa operesheni ya nchi nzima ili kuokoa fedha nyingi za umma na mali zake.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli kuingilia haki kuhakikisha mali na ardhi vya umma havichezewi tena wala kuwa chanzo cha utajiri kwa wahalifu waliotamalaki serikalini. Kiundwe kikosi madhubuti cha kurejesha ardhi ya umma nchi nzima na zoezi hili liwe endelevu na la kudumu. Tunazipongeza halmashauri za manispaa husika kwa kuonyesha mfano. Muhimu zisiangalie ardhi ya akiba ya barabara bali ardhi yote ya umma iliyotwaliwa tokana na utawala fisadi huko siku za nyuma.
Heko manispaa za Dar es Salaam kuonyesha mfano. Tunarajia halmashauri nyingine nchini zitaiga mfano huu wa kizalendo na kimaendeleo. Tumechoshwa na nchi shamba la bibi ambapo kila nyani anaweza kuja na kujilia mahindi atakavyo kwa vile bibi mwenyewe ima ni kipofu au hana nguvu za kuhami shamba lake.
Chanzo: Tanzania Daiam Nov., 29, 2015.