Baada ya lais Joni Kanywaji Magufuli kumteua waziri mkuu Ka-telephone Majaliwa, Kijiwe kimemkubali na kinamtakia majaliwa mema yenye ufanisi katika wadhifa wake mpya kama jina lake.
Mpemba anaingia akiwa na bashasha. Bila shaka ana jambo la kutupasha. Baada ya kuamkua anabwaga gazeti la Danganyika Daima mezani na kusema, “Wallahi mwenzenu leo nna furaha ile mbaya.”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea, “Una furaha ya nini au ulinusurika kichapo cha bi mkubwa baada ya kuchelewa juzi?”
Mpemba anajibu, “Mbwamwitu tuheshimiane wallahi. Kama wewe wachapwa na bi nkubwa wako usijedhani wote twapigwa ati.” Kijiwe kinacheka na Mbwamwitu ananywea.
Mijjinga anakula mic, “Hebu basi Ami tumegee hicho kilichokukuna kiasi cha kuja umefurahi kiasi hiki nasi tufurahi nawe angalau.”
“Kwani we huwa husomi magazeti na kusikiiza vyombo va habari?”
Mijjinga anajibu, “Kwani kusoma magazeti na kusikiliza vyombo vya habari ndiyo sababu ya furaha wakati vyombo vingi vya habari vinaonyesha maafa ya ugaidi kama yale yaliyotokea Misri, Mali na Ufaransa?”
Mpemba anachukua gazeti na kuonyesha picha ya waziri mkuu brand new, Majaliwa akitafuna kiapo kule Idodomya.
Mgosi Machungi aliyekuwa amebung’aa anasema, “Kumbe unaanisha uteuzi wa huyu jamaa yangu Majaiwa! Kwei una sababu ya kuwa na fuaha hasa baada ya vigogo na vitegemezi vyao kama yue kitegemezi wa mgosi mwenzangu kupigwa chini waahi.”
“Watu wengine kwa roho mbaya sina mfano! Badala ya usononeke kwa kitegemezi cha mgosi mwenzio kukosa ulaji nyeti hivi unashangila! Roho mbaya nyingine bwana! Ndiyo maana sisi waswahili hatuendelei,” analalamika Sofia Lion aka Kanungaembe.
Mheshimiwa Bwege wala hamkawizi, anakula mic, “Mgosi yuko sahihi. Tumechoka na ufalme wa kuingizwa kwa mlango wa nyuma. Hata ningekuwa mimi nisingefurahi.”
Kanji anachomekea, “Veve heshimiwa Bwege hapana danganya sisi bwana. Iko furahi sababu Jaliwa natoka sehemu moja yenu.”
Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic tena, “Ni kweli Majaliwa ni ndugu yangu tena wa damu kama hamjui, nafurahi si kwa sababu tunatoka sehemu moja bali nafurahi kwa sababu Dk Kanywaji ameanza na sura mpya kama vile kimwana Tulia aliyetua mjengoni ingawa bosi wake Jobless Nduguy ni kapi lile lile sijui hapa chama kimshika shati Dk Kanywaji ili asizidi kukiumbua hata sijui.”
Kapende aliyekuwa anateta na Mipawa anaamua kupoka mic, “Hata mimi ni mtu wa Kusini lakini simshabikii Majaliwa kwa vile twatoka kumoja. Mbona nilimpa wakati mgumu Ben Tunituni pamoja na kutoka sehemu moja. Nadhani tukubaliane kuwa umma umechoka na makapi yale yale na usanii ule ule. Nadhani Dk Kanywaji analijua fika hili kwa vile amekuwa nao kwa muda mrefu.”
Kabla ya kuendelea, Mipawa anakula mic, “Naungana mkono na Dk Kapende kwa vile sisi wanakijiwe tunachukia ufalme wa mlango wa nyuma, kujuana, kulindana na kufadhiliana kwa kupeana ulaji. Nadhani hapa Dk Mwenzangu homeboy Kanywaji ameanza kuionyesha dunia kuwa ameshika usukani.”
Msomi aliyekuwa anasoma tabu kubwa sana jeusi analiweka chini na kula mic, “Sikuwa na mpango kuchangia leo kutokana na kuwa na kibarua cha kufanya utafiti kuhusiana na kushamiri ugaidi. Lakini mchango wa Dk Mipawa umenikuna kiasi cha kutia guu. Kwanza, nakubaliana na wale wanaoona kama Dk JPM anataka kujitofautisha na utawala mbovu uliopita kwa kufanya mambo tofauti na ulivyokuwa ukifanya. Kwani amejifunza kuwa utawala kidhabu uliopita ulikuwa ukifanya makosa mengi bila sababu. Hivyo,hataki kurudia makosa. Ingekuwa pigo kubwa kwa imani ya wananchi kwa JPM kama angeteua makapi kama Jan Makambale au Billy Lukuuvi. Nani anataka makapi usawa huu wa mageuzi?”
Anapiga chafya na kuendelea, “Wale wanaosema kuwa uteuzi wa Majaliwa unaweza kuwa siasa za gesi, so be it kama utendaji wake ni mzuri. Hata ningekuwa JPM ningemteua bila kujali wanywanywa watasemaje. Maana kaya sasa inataka sura mpya, nguvu mpya na zenye mawazo mapya ili kuondoa huu uoza wa kunuka ulioachwa nyuma na Njaa Kaya.”
Mzee Maneno anakula mic kinamna, “Hata mimi kusema ukweli naunga mkono uteuzi upya ingawa jamaa mwenyewe hajulikani. Naamini timu ya Dk Kanywaji –kama haitakuwa zimamoto au nguvu ya soda –inaweza kuleta mageuzi ambayo wengi wanayatarajia.”
“Hili la utendaji kazi wala usitie shaka mzee mwenzangu. Jamaa yangu mmoja wa Uhasama wa Kaya amenitonya kuwa jamaa ni mchakazi usipime, ni kichaa wa kazi kama JPM. Hebu fikiria mtu anatoka uwaziri mdogo na kuvuka uwaziri na kuwa waziri mkuu. Unadhani huyu ni mchapakazi wa kawaida?” anachangia Kapende huku akikatua kashata yake.
Hoja hii imekumkuna Kanji kiasi cha kudaka mic, “Hata mimi iko kubali neno ya Pende. Kama hii Jaliwa nakuwa waziri dogo na sasa naruka yote na kuwa vaziri kubwa lazima iko chapa kazi kweli kweli.”
Mheshimiwa Bwege anakumia mic tena, “Nikienda kumpongeza kwa kuteuliwa nitampa vipande vyake kuwa asiliwe ulaji kama wengine na kuharibu sifa yake. Kwanza, nitamtaka anahakikisha watu wa Kusini tunaona manufaa ya gesi yetu vinginevyo tutamuandamania aondolewe kama atashindwa jambo rahisi na wazi kama hili.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si waziri mkuu Majaliwa katia timu kijiweni kupata kahawa kwa vile ni mwanachama wetu wa muda mrefu!
No comments:
Post a Comment