Baada ya kugundua na kushuhudia kuwa kuombea Kaya imekuwa fasheni ukiachia njia ya siri ya wahusika kujisogeza karibu na wenye ulaji na kuchangisha sadaka nyingi. Kwa mlevi huu ni mkenge ambao lisirikali na Kaya kwa ujumla vinapaswa kuuepuka kwa gharama zote. Mbali na kuwasogeza wahusika karibu na wenye ulaji, mkenge huu husaidia kuwafanya wahusika kupata umaarufu kwa mgongo wa wanasiasa maarufu kama rais. Utakuta wengi wakitafuta nafasi adimu ya kupiga picha na wazito wa serikali kama vile rais –ambaye hata hivyo, haonyeshi kushabikia ujinga huu –mawaziri na wazito wengine wenye umaarufu ambao unaweza kuchotwa na makapuku ombaomba wasiojulikana. Hivyo, ni juu ya wahusika kupokea tahadhari hii toka kwa mlevi mwenyewe ambaye ameshastukia dili zima. Hii nayo ni aina ya ufisadi wa kimfumo inayoanza kujengeka. Nani kawambia kuwa Kaya tajiri kama vile Marekani, Japan na Uchina yameendelea kutokana na kuombewa zaidi ya kuchapa kazi kwa juhudi na maarifi huku uwajibikaji na kutenda haki vikiwekwa mbele?
Tokana na mvuto wa maombi, si ajabu kusikia wafanya fujo wakiombea amani au wezi wakiombea haki. Hapa dawa si kuomba au kufunga bali kuacha maovu. Dawa si kuomba ni kuchapa kazi. Dawa ni kuwajibishana na kutendeana haki badala ya kuingizana mkenge. Wapo wanaoombea eti kuongezeka kwa joto, kuongezeka mafuriko, kuongezeka ubomoaji wa nyumba za mabondeni na mabalaa mengine yatokanayo na maumbile na shughuli za ngurumbili. Dawa hapa si kuomba bali kuacha kukata miti hovyo. Dawa mujarabu hapa ni kupanda miti na kutunga sheria zinazozuia uchafuzi wa mazingira utokanao na ufisadi na upogo na uwepo wa serikali mbovu kama iliyopita ambayo iliacha kila kitu kwenye autopilot.
Kesho utasikia wakiombea vijana waache kubwia madawa ya kulevya. Dawa hapa ni kuwakamata na kuwanyonga wauza unga. Mchezo huu hatari na mchafu hauishii hapa. Wapo wanaoomba kurejea kwa maadili mema. Hapa dawa si kuomba bali kupambana na uchafuzi wa maadili utokanao na ulimbukeni , miigizo, ujinga, unywanywa na ujinga. Badala ya kufungia magazeti yanayofichua maovu, fungieni magazeti ya udaku ambayo Mlevi hupenda kuyaita magazeti ya uchafu. Kwani, magazeti haya –licha ya kuuza na kusambaza ujinga na uchafuzi wa maadili sana –yamegeuza taifa letu kuwa taifa la wadaku, wambea na wapuuzi bila sababu. Nenda mkaone nchi za jirani. Hazina utitiri wa magazeti ya udaku kwa vile si mataifa ya wadaku na wapuuzi. Yote fanyeni, msije kuingilia bangi na ulabu wetu. Hatuhitaji kuombewa tuache ulabu. Kwani Mwana wa Maria aliyegeuza maji kuwa mvinyo mnadhani alikuwa njinga kama nyinyi siyo? Acha tujipigie ulabu na kututika mibangi. Kwani ndiyo nyenzo pekee tulizobaki nazo za kujiliwaza tokana na kunyonywa na kupigika kwa muda mrefu.
Wapo wanaombea hata wenye kesi kama zile za makontena bandarini ili serikali iwasahau wao na mali walizojilimbikiza. Hapa dawa ni kuiambia serikali kuwakamata, kuwafilisi na kuwanyonga. Dawa ni kufichua ajira za kujuana ambapo watoto wa vigogo wanajazwa kwenye sehemu nyeti kama Bandari, Viwanja vya ndege, Mipakani, Benki kuu, Uhamiaji, Biashara, Madini, Utalii, Mafuta na sehemu nyingine nyeti zenye ulaji wa haraka.
Mlevi yeye si bingwa wala muumini wa kuomba omba bali kusema sema hasa kuwapa vidoge wanaohitaji.
Siyo siri, tumegeuka taifa la ombaomba, wavivu na washirikina bila sababu. Huwezi kuombea amani ikawapo kama hakuna haki. Huwezi kuomba joto lipungue duniani wakati ukikata miti na kujenga kwenye vyanzo vya maji.
Huwezi kumwombea rais wakati hufuati falsafa yake ya “Hapa kazi tu”. Sidhani kama rais Kanywaji anaamini kama kuomba ni kazi zaidi ya kuchapa kazi na kuachana kuombaomba. Rais Dokta Kanywaji nakustua, unapaswa kuwastukia hawa ombaomba wa kiroho wenye uroho wa kutaka kukutumia kujitajirisha kwa njia ya kujifanyia mambo yao. Inakuwaje hawa na njaa zao waingize kaya yetu kwenye udini wao? Lisirikali halina dini na halipaswi kuwa nayo. Hivyo, halipaswi kuombewa bali kuambiwa litende haki kwa ngurumbili wote wa kaya hii ya Danganyika. Kaya yetu hahihitaji kuombewa. Wanaombewa maiti si walio hai. Kama kuomba ni dili basi kila mtu aombe kivyake na kwa imani yake. Kwanini mtulazimishe kufuata dini zetu hasa sisi ambao dini zetu ni kanywaji na si hizo zenu za kimamboleo?
Tumalizie kwa kumnukuu Bwana mkubwa Mwana wa Adamu aliyesema, “Waache wafu wazike wafu wenzao,” (Mathayo 8:22-23). Hata profesa Paulo alisema kuwa asiyefanya kazi asile. Kwani hakujua nguvu ya maombi kama ingekuwapo kweli?
Nami profesa Ayatolah, Daktari, Ustaadh Mlevi wa Mvuta bangi nasema tena kwa kinywa kipana, “Waache ombaomba wawaombee ombaomba wenzao lakini si kaya yetu.”
Chanzo: Nipashe, Januari 23, 2016.
2 comments:
Salaamu Mwalimu Mhango,
Biashara ya dini imeaanza tangu zama za kale pale mwanadamu alipoaanza kujielewa kuwepo kwake hapa dunia na kuanza kujiuliza na kutafuta maana hiyo ya kuwepo hapa duniani.Tukiangalia kwa mapana zaidi maana ya dini kuanzia uchawi na makuhani wake,dini ya mababu na makuhani wake hatimae dini zinazojulikana za mbiguni au za ardhini na makuhani wake,tunakuta tu kwamba mfumo wote wa dini hizo za aina mbali mbali zimekuwa zenye kuanzisha biashara kubwa ya kidini tangu zama hizo hadi dunia itapokwisha.
Ukweli usiopingika ni kwamba dini ni biashara kubwa na mtaji wake ni uwongo unaopambwa na kuonekani ni kweli na wateja wake ni wale ambao hawana wakati wa kutafakari kuhusu biashara hiyo na kuwaachia makuhani wa dini hizo kutafakari kwa niaba yao na makuhani hao wamefanikiwa katika biashra hiyo baada ya kuwahakikishia na kuwakinaisha waumini wao kwamba wao kama makuhani wanauhusiano mkubwa sana na wakaribu sana na miungu yote ya dini hizo mbali mbali,na baada wateja hao kufikia imani hiyo wamejikuta wakiibiwa mchana kweupe ili hali wenyewe wakiridhika. kwa kutoa sadaka ambazo haziwafikii waungu wa dini hizo wala haziwahudumia wao kama ilivyokuwa inapaswa.
Jambo la kushangaza zaidi la makuhani wa dini zote hizo tangu zama hizo hadi hii leo ni kujisogeza kwao sana kwa watu wenye madaraka na nguvu za kiuchumi na kisiasa ujisogezaji ambao umewafanya wawe kitu kimoja katika kuwakandamiza wananchi wao kwa kutumia biashara hiyo ya dini.Wenzetu wa bara la ulaya katika karene ya 15 waliishitukia na hatimae waliikataa biashara hiyo baada ya kuwagunduwa makuhani hao ni mizigo isiobebeka tena katika jamii na kuiondoa biashara hiyo kabisa na waliokuwepo madarakani hawakuwasogeza tena makuhani hao karibu yao zaidi ya huduma zao ambazo zinachukuliwa ni kama huduma za kijamii tu ndani ya makanisa yao,hii ukiondoa nchi kama Marekani ambapo biashara hiyo ya kidini imkuwa ni kubwa mno lakini tofauti yao na sisi waafrika kwamba wanaoibiwa huko Marekani ni waumini wa kawaida ambao wametawaliwa na kuzongwa na maisha ya Mada(materialism) na hatimae hawana pa kukimbilia isipokuwa mikononi mwa makuhani hawa wa kidini.
Mwalimu Mhango,tatizo la kwetu Afrika au kwa nchi za ulimwengu wa tatu ni kwamba makuhani takriba wote wanajipendekeza kwa watawala kwa imani tu kwamba wakiwa karibu na watawala hao biashara yao itazidi kuwaletea faida ya kiuchumi,kuzidi kukubalika kwa jamii kubwa na kuzidisha haiba yao ya kidini na kijamii,Ilikuwa juu ya viongozi wetu wawaone tu kama ni wafanya biashara tu wa dini ambao wanataka kujitajirisha kupitia migongo yao,lakini kwa bahati mbaya viongozi wetu wengi wanajikuta wamekamatwa na makucha ya wafanya biashra hao kwa vile malezi yao ya awali ya kijamii hayatofautiani sana na wale waumini wa kawaida na hatimae wamejikuta na wao ni wateja wazuri tu kwa makuhani hao.
Mwalimu Mhango,ebu na tuuone ukweli huu kwamba dini ni uhusiano wa yule anaeamni,anachokiamini na anachokiabudu tunakuta tu kwamba ni uhusiano binafsi(private) ambao muumini huyo inabidi awe mwenye kujiamini na kuwa huru kuabudu anachokiabudu na kuomba anachokiabudu bila ya kuingiliwa na mtu mwingine katikati na kumuombea kwa niaba yake kwa hicho anachokiabudu kwa njia yyote ile anayoiona ni muwafaka,lakini inapotokea kuwapa makuhani haki ya kuwaombea wengine kwa niaba au kufikia mpaka ujasiri wa kuiombea Kaya au kumuombea mtawala awe Rais au Mfalme hapo sasa ndio utapeli wa wazi na wa hali ya juu ambao biashra hiyo ya dini inakuwa na mafanikio makubwa.
Inaendelea........
Mwalimu Mhango,
Swali la kujiuliza ni hili endapo hawa makuhani ni wanadamu kama wanadamu wengine na wanaaamini kama wanavyoamini wanadamu wengine iweje leo tuwape makuhani hao haki ya kutuombea au kuombea Kaya?Je ni wapi walipopewa uhakika kwamba maombi yao yanakuwa na nguvu au uhakika au dhamana ya kujibiwa huko wanapo omba?Je kwa nini tuwape nguvu hiyo ya maombi makuhani hao kama si sisi wenyewe kuamini kwamba kumekuwa na makubaliano kati yao na hao miungu yao kwamba wakiomba hawatokataliwa maombi yao au na wao ni sehemu ya miungu hiyo ambayo inaishi na sisi duniani katika maumbile ya kibinadamu?
Naam,Mwalimu Mhango,umefafanunua vya kutosha na umehadharisha vya kutosha na msemo wako wa "uvivu wa kufikiri"ndio unaosababisha biashara hii ya kidini kuendelea kuwa kubwa na kuna mzsemo mwingine wa mababu zetu waliosema kwamba "wajinga ndio waliwao"na tuwaondolee wafanya biashra hii ya dini uvivu wa kufikiri inawezekana ikapatikana nafuu kubwa sana kama walivyo waobdelea watu wa bara la Ulaya wafanya biashara hawa.Je tutaweza kufanikiwa hilo katika jamii yetu ambayo mihimili yote ya Primitive Society bado inatutawala hata kama tunaishi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia na wengine wetu tunamiliki shahada za juu za kielimu?
Post a Comment