The Chant of Savant

Saturday 2 January 2016

Uenyekiti CCM:Kikwete uliachiwa muachie Magufuli


             Baada ya rais Jakaya Kikwete kustaafu na kuendelea kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapindizi (CCM) mengi yameanza kusemwa ya maana na yasiyo ya maana. Yanasemwa mengi baada ya kupatikana rais mpya Dk John Pombe Magufuli ambaye –kutokana na spidi yake ya kupambana na maouvu na uzembe –wangetaka apewa rungu la mwenyekiti wa CCM ili asafishe taifa na kulirejesha kwenye mstari kama lilivyokuwa wakati wa marehemu baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.  Baadhi ya vyombo vya habari vimeishaandika kuwa CCM inapanga kuchelewesha utaratibu uliozoeleka tangu zama za baba wa taifa Mwl Nyerere wa kuachiana wenyekiti wa chama kabla ya kufikia mwisho ili kumwezesha rais ambaye pia anakuwa mwenyekiti wa chama kuteleza mipango na ahadi zake.
            Kwa kuelewa na kutambua umuhimu wa nyadhifa hizi mbili, rais na mwenyekiti, Mwl Nyerere aliamua kwa hiari kumwachia mrithi wake Ali Hassan Mwinyi ili avae kofia mbili na kupanga nguvu za kukamilisha aliyopanga kwa taifa. Kwa busara zake, baada ya Mwl kuwa akimshauri baadhi ya mambo Mwinyi ambayo wengi waliona kama alikuwa akimwingilia kwenye madaraka yake au kutaka kutawala kupitia mlango wa nyuma, alianzisha utaratibu wa kuachia madaraka kabla ya wakati wake ili kumpa mrithi wake fursa ya kufanya na kutekeleza yale aliyokuwa ameyapanga.  Pia, Mwl Nyerere aliepuka mgongano unaoweza kutokea baina ya rais na mwenyekiti wa chama chake. Hivyo, hata baada ya Mwinyi kuingia na kustaafu –kwa lengo hilo hilo la kuepuka mganganyiko na kufanikisha malengo ya chama na ya rais –alimuachia mrithi wake Benjami Mkapa aliyemuachia rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye anaonekana kunogewa na uenyekiti kiasi cha kuruhusu mengi yasemwe bila kuachia madaraka wala kutoa ufafanuzi. Wengi wanauliza anahofia nini au kunani?  Wasio na subira au wenye wasi wasi kuwa kuna watu wa ndani ya chama wanaotaka kumkwamisha au kuogopa kasi ya rais Magufuli wameishaanza kusema mengi na wengine kuuliza: “Sasa unangoja au unaogopa nini kumwachia ukanda Magufuli ili afanikishe mipango yake kama rais na kutimiza ahadi zake ambazo kimsingi ni za chama?”
            Kuondoa dhana potofu kuwa Kikwete anaogopa mabaya yake yasifuchuke, anapaswa kuendeleza utaratibu wa kuachiana uenyekiti ili kumpa nguvu na uwezo Dk Magufuli kuikomboa nchi iliyokuwa imezama kwenye uhovyo, ufisadi, uvivu na ujinga bila sababu ya msingi. Kikwete nimjuaye ni jasiri. Hivyo, asikubali kuonekana fisadi au mhalifu kwa kuogopa kuacha uenyekiti kwa Magufuli ili atekeleze ahadi zake. Ninaamini Kikwete aliangushwa na wasaidizi wake. Hivyo, si vibaya kutoa fursa ili mambo yarejee kwenye mstari. Uzuri ni kwamba hata Magufuli analijua hili na aliwahi kulitamka wazi alipomlaumu Kikwete kwa kula na wanafiki tokana na huruma yake. Kwa vile Kikwete ametamka wazi wazi kuwa anaunga mkono juhudi za Magufuli –ili asionekane mnafiki na muongo –wapo wanaosema amwachie uenyekiti Magufuli ili arekebishe chama na taifa kwa mpigo.
            Japo Kikwete ana haki ya kuendelea kuwa mwenyekiti hadi ukomo wake wa kikatiba, kuna uwezekano kuwa ung’ang’anizi na ukiukaji wake wa utaratibu uliozoeleka ima kumchelewesha rais au kuzua kutokuelewana kiasi cha wawili kukwamishana –kama itatokea. Hali hii, hata hivyo, inaweza kuwa na madhara mabaya kwa Kikwete zaidi ya Magufuli hasa tukizingiatia mambo mawili. Mosi, rais wa Tanzania ana nguvu nyingi kikatiba kuliko mwenyekiti wa chama tawala. Pili, tukirejea kilichotokea nchi jirani ya Malawi pale rais mstaafu Bakili Muluzi alipotaka kutumia uenyekiti wa chama tawala kumkwamisha mrithi wake marehemu Bingu wa Muthrika. Nini kilitokea? Rais alitumia umaarufu na madaraka yake kuanzisha chama chake na kukihama chama kilichomwingiza madarakani kiasi cha kukiua kirahisi. Tuombe Mungu ili lisotokee. Na hapa jibu si kuomba Mungu bali kumshauri Kikwete amwachie uenyekiti wa CCM Magufuli ili afanikishe mipango yake ambayo pia ina tija kwa chama chake hasa ikizingatiwa kuwa maandilizi ya uchaguzi ujao ndiyo yanaanza pindipo rais mpya anapoapishwa.
            Kama Kikwete ataamua kumaliza muda wake na kufanya hivyo kukawa kikwazo kwa mipango ya Magufuli kuna sababu moja au mbili za kutegemea kilichotokea Malawi kwa sababu Kikwete hana mpango wa kugombea tena urais. Hivyo, hana sababu yoyote ya msingi ya kuendelea kuwa mwenyekiti vinginevyo kuwapo na mambo mengine nyuma ya pazia kama wabaya wake wanavyodai ambayo anataka yasifichuke. Kwanza, Magufuli kwa sasa anakubalika kuliko watangulizi wake isipokuwa baba wa taifa. Pili, Magufuli si mtu aliyepata urais kwa kismati. Alijiandaa kwa muda mrefu. Tatu, Magufuli si mbabaishaji wala mtafuta sifa. Ana malengo ya mbali na mapenzi makubwa kwa taifa –kama hatabadilika au kukwamishwa na huu mgawanyo wa madaraka.  Hata hivyo, kwa udhubutu wake, spidi yake, sera zake na tabia yake, Magufuli si mtu wa kushindwa kirahisi. Hivyo–kama Kikwete atang’ang’ania –lolote laweza kutokea ambapo mwenye kupoteza atakuwa CCM na Kikwete zaidi ya Magufuli.
            Tuhitimishe kwa kumtaka Kikwete ima aendeleze utaratibu alioukuta au atoe angalau maelezo ni kwanini anataka kuupinda utaratibu uliozoeleka. Tunaamini hatawapa nafasi wakosoaji wake kuendelea kudai kuwa anaogopa mabaya yake yasifumliwe akaishia pakanga.
Chanzo: Tanzania Daima, Januari 3, 2016.

No comments: