How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 1 January 2016

Mlevi aaga, atafsiri na kukaribisha mwaka


      Japo mlevi si muumini wa dini yoyote zaidi ya ulabu na mibangi, anamshukuru Subhanna kuumaliza na kuanza mwaka bila ya kuuawa na mibangi na mma ukiachia mbali kutotupwa lupango kwa kusakiziwa kesi feki na ndata. Siku hizi ndata nao wanaipatapata hasa wanapofikiria kasi ya kufichua ufisadi ambao wengi wao wanaufanya na kuwa matajiri wakati mishahara yao ni kiduchu.
             Pia anachukua fursa hii kumtakia mafanikio rahis mpya mwenye mapya, Dk Joni Kanywaji Makufuli, kuingia na kasi ya kuridhisha. Dua hizi ni zinatoka moyoni na ni za dhati. Mimi si kama matapeli wanaojitia kumuombea Dk Kanywaji na kaya wakati wanachofanya ni kutafuta ukaribu naye ili awape ulaji. Mie mibangi na mipombe yangu inanitosha. Kwa Dk Kanywaji wamekwama. Si mpenda sifa.
            Pia nachukua fursa hii kumshukuru Kahari kuniwezesha kushiriki uchaguzi wa maana ulioleta kidume aliyerejesha heshima ambapo sasa mambo yanaanza kubadilika. Nazidi kuomba ipatikane haki badala ya kuwa imemilkiwa na wakubwa na mafisadi huku wakituacha walevi tukipigika bila sababu tokana na ukwapuzi na uzembe wao.
            Nimshukuru God kwa kutuwezesha kuachana na utawala kidhabi uliopita. Maana uliigeuza kaya yetu danguro la mafisadi na shamba la chizi. Nichukue fursa hii kushukuru kwa kunusurika kutawaliwa na fisadi aliyetuachia machungu baada ya kuua upinzani tokana na upogo na uchoyo na uroho wa wakubwa wake wachache wasioona zaidi ya usawa wa matumbo na pua zao. Sipati picha kama tungepata fisadi mwingine aliyebadili chama baada ya fisadi wa chama kikongwe hali yetu ingekuwaje. Ama kweli Mungu si Mlevi! Alhamdullillahi aametuvusha salama kwa kupata kifaa au jembe la “Hapa kazi tu.”
            Habari mbaya ni kwamba mlevi alibomolewa mjengo wake kule kwenye bonde la Mkwajuni tokana na kuingizwa mjini na mafisadi waliomuuzia kiwanja kumbe kanyabwoya.
            Mwaka uliopita ulikuwa mgumu kwa mlevi kutokana na kasi ya Dk Kanywaji kumkumba mfadhili wake aliyezoea kumpa ofa za mapupu bangi na kanywaji. Hata  hivyo, hajutii sana. Kwani uwajibikaji na maadili yakirejea kwa kuondoa madili huenda naye akakomaa na kuukata.
             Baada ya kutoa tathmini binafsi ya mlevi, ngoja nizame kwenye matarajio ya mwaka mpya. Kwanza, mambo makubwa yatatokea ambapo kaya itarejea kwenye mstari na kila mlevi atakula na kunywa jasho lake. Waliozoea kuja kujiibia watakavyo wakishirikiana na panya na mchwa wa kayani sasa watakoma. Hakuna kilichokuwa kinaniumiza kama kuona kaya iliyojaliwa neema lukuki kuombaomba huku magabacholi, sorry wachukuaji wakichukua na kwenda kuneemesha kwao.
            Tokana na kasi ya Dk Kanywaji, nashauri ahakikishe mibaka, vibaka, mafisadi, mchwa, makuadi, panya na wote waliokuwa wakitukwamisha wanafilisiwa na kufia lupango.
            Pili, namshauri abadili mfumo wote hasa kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ili malengo yake yawe na ulinzi na uhalali kisheria ukiachia mbali kuwa endelevu. Lazima tuheshimiane. Tumechoka na wezi kutukoga kwa utajiri waliouchuma kwa kutuibia.
            Mwaka mpya utaanza na mambo mapya kama vile:
            Walevi wote kutakiwa kutaja umaskini na utajiri wao kaya nzima. Pili, walevi watachapa kazi hata kama ni kwa kuogopa spidi ya Dk Kanywaji na kaya itasonga mbele.  Mfano, wale waliozoea kugeuza ofisi za umma vijiwe na vijiko vya kuchotea ulaji wasahau kabisa. Wapenda kuzurura ughaibuni wakilipana per diem kiama chao kinaanza. Walioficha njuluku Uswizi wakae mkao wa kuliwa. Wote wenye utajiri wa kutia shaka lazima watie maji vichwani. Wauza bwimbwi watatangaziwa kiama muda si mrefu.
            Habari njema, heshima na uchumi wa kaya vitaumka kama vile vimwekwa hamira. Wale waliokuwa wakijiona ni untouchable wakimilki ukwasi wa kaya na kuutoroshea nje wakae mkao wa kuliwa. Misheni town wote waliozoea kushinda bandari wakikuwadia maadui wa uchumi wetu wataanza kuuza nyanya. Jingine la kushangilia ni kwamba vyanzo vyetu vya maji vitakuwa salama ukiachia mbali miji yetu kuanza kuwa na mpangilio.
            Utabiri: Japo mlevi si tapeli kama wale wanaojifanya watabiri, acha atabiri kidogo. Mwaka unaoanza utaanza upya na mambo mapya ambapo hata wale usiotegemea kuguswa waliochezea dhamana zao kwa umma kuanzia nambari wani hadi chini wataguswa na kutikiswa. Pili, maisha ya walevi yatabadilika na kuboreka huku ya wale waliozoea kuiba yakizidi kuwa mabaya. Kiwango cha uombaomba kitapungua kiasi cha wafadhili kuanza kulalamika kwanini wakubwa wetu hawaendi kuwaramba makalio kama ilivyokuwa kwenye awamu tatu zilizopita.
            Mwisho, natabiri kuwa wakuu wengi wa mashirika, ubalozi, wilaya, mikoa na popote kwenye ulaji walioteuliwa kishikaji wataporomoka kama nyumba ya karata. Dk Kanywaji atafanya vitu ambavyo havikuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miaka 30 tangu mzee Mchonga (Mungu amrehemu) alipotundika daruga.
            Kwa ufupi ni kwamba mwaka 2016 ni mwaka wa Danganyika kurejea kwenye hadhi.
Chanzo: Nipashe Januari 2, 2016. 

No comments: