Baada ya Jobless Nduguy kutangaza vifaa vyake vitakavyotumika kutubamiza mkenge Mjengoni, Kijiwe kimestuka na kuamua kutoa tamko kama taasisi inayoheshimika sana Kayani kikionya kuhusu muendelezo wa ujembuzi na ujambazimbuzi.
Baada ya kuweka gazeti mezani, Mpemba leo ndiye analianzisha. Anabwia kahawa yake na kung’ata kashata na kumwaga pwenti.
“Jamani mmeona njama za Chama Cha Maulaji (CCM) kuendelea kutubamiza nkege kwa kuwapa ulaji watuhumiwa wakubwa wa Escrew? Inatisha na kusikitisha kiasi cha kuanza kunfanya nistukie hata huu utumbuaji wa majipu wakati mabusha yakidekezwa wallahi,” analalamika Mpemba.
Kapende anadaka mic, “Mimi tangu alipochaguliwa huyu Jobless Nduguy imani na Mjengo ilitoweka. Sioni tofauti ya Jobless na yule manzi kidhabi aliyepachikwa na mafisadi baada ya Mjengo kuonyesha unaweza kung’ata. Kama tofauti ipo basi ni jinsia zao lakini si zaidi ya hapo.”
Baada ya Kapende kumwaga pwenti, Msomi Mkatatamaa anakula mic. Kabla ya kutoa ya moyoni anachukua gazeti na kuonyesha kichwa cha habari kisomekacho, “‘Vigogo kashfa ya Escrew’ kuongoza Kamati za Mjengo.” Anaweka gazeti pembeni ambako linanyakuliwa na Mchunguliaji. Anasema, “Mwanzoni niliposoma kuwa Daktari Kanywaji kamteua Sossie Muongo sikuamini. Kwanza, nilidhani ni uongo. Baada ya kugundua ni kweli nikamvuita pumzi. Sasa hili la kuteua waescrow waje watuumize limenimaliza kabisa ukiachia kuondoa imani yangu na haya mazingaombwe na sanaa vinavyoendelea. Hivi kweli mzee wa Joni Chenga aka mzee wa Vijisenti au Bill Ngereza ukiachia mbali Hawa wana Ghasia anayetuhumiwa kuwa nyuma ya wizi wa UdA wana nini cha kutoa zaidi ya kuendeleza libeneke hata kwa kuanzisha Escrew nyingine?”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachomekea, “Kumbe wewe hujui! Hawa licha ya kulindana na kupeana ulaji, wanakatiana.”
Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi ananyakua mic na kuzoza, “Hebu tiambie tieewe. Wanakatiana nini hawa na nani anamkatia nani?”
Msomi anajibu, “Wanakatiana wao kwa wao. Wapo wanaomkatia Nduguy ambaye naye anao anaowakatia. Hapa ni kukatiana kila kitu au vipi.” Msomi huwa si mtu wa utani. Hii ya leo mpya na inaacha kijiwe hakina mbavu kutokana alivyowaunganisha katika kukatiana huku ambako kimsingi ni balaa kwa Kaya.
Mipawa anaamua kutia buti, “Mie wote wangechaguliwa kusingekuwa na shobo. Lakini kuteuliwa kwa hawa ngosha wawili na Hawa wana Ghasia hata Mery Nyago kumeniumiza sana. Kwani lazima wakatiane wao au ni ile roho mbaya kama siyo kulinda ufisadi wao?”
Mijjinga aliyekuwa anamaliza kuongea na bi Mkubwa wake anayeonekana kuwa na ugomvi, anakwanyua mic na kuzoza, “Hapa hakuna chamabadiliko na kama yapo ni ya kuelekea kulekule tulikotaka kutoka. Hata hivyo, tusisahau kuwa hii ni CCM bwana. Hamuoni vifaa kama Mzito Kabwela vilivyotupwa nje. Kama Nduguy angetaka kutenda haki, tulitegemea vifaa kama Joni Munyika, Saed Kube na Halima Mndee viwemo uone ambavyo mafisadi wangejinohino kwenye nguo zao. Sasa jamaa yangu Muongo anatesa na kuchelea.”
“Hapa bila shaka waliofanya uteuzi siyo Nduguy. Nadhani ni akina Singasinga na Jimmy Rugemalayer ambao kimsingi ndiyo Escrew yenyewe,” anachomekea Kapende.
Mheshimiwa Bwege hajivungi. Anakula mic, “Kumbe hamjui! Escrew siyo hawa gendaeka wa kinshomile na kigabacholi. Hawa wanatumiwa na wazito wenyewe akiwemo Njaa Kaya na Ben Tunituni wenyewe. Hata Dk Kanywaji pamoja na mbwembwe zake, hana ubavu wa kuigusa Escrew. Ataonea vibaka wa bandarini lakini hatawagusa majambazi papa wa Escrew. Hata hivyo, tunapaswa kufahamu kuwa nyani wote ni wale wale tena kwenye mstitu ule ule. Tutegemee nini?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic, “Tangu wavunje nyumba ya mjomba wangu wala sina hamu nao wala cha kutumaini toka kwao. Wanapeana ulaji huku wakiwaacha wanyonge wakinyongeka bila kujali. Hili nalo ni balaa jingine kwetu walalahoi. Sijui nani atatupigania iwapo mambo yenyewe ni haya?”
Msomi anarejea tena, “Kuna haja ya kuangalia chanzo cha tatizo ambacho –nionavyo mimi –ni mfumo mzima ambao unahitaji kufumuliwa na kusukwa upya. Na bila kuhanikiza kurejea mchakato wa Katiba ya wanakaya, yote tufanyayo ni kutwanga maji kwenye kinu. Wataendelea kutuibia huku wakikatiana kama ilivyojidhihirisha kwenye sanaa hizi za Nduguy. Huwezi kurejesha wezi watupu na gendaeka wabovu ukategemea mabadiliko wala maendeleo. Tuatendelea katika kutokuendelea huku walaji na mafisadi wetu wakijiridhisha na kutuhadaa kuwa wameleta maendeleo wakati wanachofanya ni maanguko matupu.” Kabla ya kuendelea kirongaronga chake kililia hivyo akaamua kupokea simu na kuchonga kidogo.
Kanji kuona hivyo kapata upenyo. Anabwia mic, “Sasa kama nakata katana hivi, si wataumiza vatu dogo ya chini jamani? Sasa ile zee ya jisenti nakwisa iba juuku nyingi wanaongezea laji ya nini kama siyo chezo chafu nyuma ya pazia?”
Kijiwe kikiwa kinashika kasi si lakapita shumbwengu la Nduguy. Acha tulimwagie kahawa ya moto!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 31, 2016.
No comments:
Post a Comment