The Chant of Savant

Wednesday 14 December 2016

Kijiwe chasheherekea na kutathmini uhuru

      Image result for sherehe za uhuru

      Wakati wapo waliosherehekea kumbukumbu za miaka 55 za uhuru kwa kununa tokana na kutokuwapo makulaji na posho, kijiwe kilisherehekea kwa tafakuri na tathmini nzito.  Wakati wengi walikuwa kwenye uwanja wa taifa wakishuhudia gwaride, kijiwe kilichegama sehemu ambayo ni siri kubwa ili kutathmini uhuru husika na ikiwezekana kuwasuta baadhi ya wenzetu.
            Baada ya kukusanyika tukiwa kwenye mood ya kuwa huru, Mpemba ndiye anayelianzisha.
            Anakula mic “hongereni ndugu zangu wa bara kwa kusherehekea miaka 55 ta uhuru wenu.” Kabla ya kumaliza Kapende anampoka mic “tunashehekea uhuru au udhuru? Nadhani wanaosherehekea ni wala nchi lakini si waliwao kama sisi. Je kama uhuru huu ni wa bara siew a pwani wetu ni lini? Maana naona wasema wabara kana kwamba kila ntu ni mbara. Sie Ntwara, Lindi, Dar na Tanga si wabara kama unavyosema.”
            Mpemba anajibu haraka “nilimaanisha msio wa visiwani kama siye. Sie kwetu kila aniotokea mahali pasiyo kisiwa humwita mbara bila kujali yua aishi bara pwani au bara ndani.”
            Kapende anakula mic tena “sasa nimekuelewa. Je kwenu visiwani haliwi kama hapa hasa wale wasiokuwa kwenye ulaji? Maana usipokula hapa shurti uliwe vinginevyo uwe mpiga dili, muuba bwimbwi, mfanya biashara au mfanya ujambazi.”
            Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungu anachokea kwa kuonya “Kapende angaia hiyo ugha. Wewe ni wa kutwambia eti tunaiwa! Kama kuiwa dii basi iwa wewe.”
            Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisikiliza huku akisoma jarida kubwa la kimataifa ambalo jina lake nimelisahau, anaamua kuingilia ili kuikoa mjadala.  Anakohoa kidogo na kusema “jamani tuweni makini na tunavyotafsiri mambo. Sioni kama kuna sababu ya kutumia uoni mmoja kutafsiri kila jambo. Nadhani, kimsingi, Kapende na Mgoshi mnongelea kitu kimoja sema kwa uoni tofauti. Nadhani kuliwa hapa anamaanisha wanaonyonywa.”
            Anakohoa tena na kumtazama da Sofia Lion aka Kanungaembea na kuendelea “najua kwa tafsiri mbaya hata kunyonywa laweza kugeuzwa tusi. Hata hivyo, huko nisingetaka niende.”
            “Kaka Msomi wala huna haja ya kujitetea. Kwani kuna mtu ambaye hakunyonya? Wasingenyonya wangekuwapo hapa?”
            “Nashukuru sana. Dada hapa nimekupata na nadhani kila mmoja amepata ujumbe. Ngoja nijikite kwenye mada baada ya kuondoa utata wa tafsiri na uoni. Nadhani tunachopaswa kufanya leo ni kuangalia mambo yafuatayo. Mosi, je kweli sis tuko huru au walio huru ni baadhi yetu wenye nazo? Pili, je tangu tupate uhuru, tumefanikiwa kufika kule tulikotaka na kutarajia kufika kwa wakati na kasi inayotakiwa? Tatu, je uhuru maana yake ni nini? ni nyimbo, gwaride na hotuba au maisha kwa ujumla? Yapo mengi ya kuangazia na kutoa tathmini ya haki na kisayansi kwa kuangalia uzoefu wetu kama wana kaya.”
            “Profesa Msomi nikushukuru sana kwa lecture yako fupi lakini yenye kusheheni nondo. Ndiyo, lazima tujiulize: je ni wanakaya wangapi hawajahi kutumia umeme kiasi cha kuwa chanzo kizuri cha uharibifu wa mazingira na afya zao ukiachia mbali kuwachelewesha kimaendeleo kibinafsi na kitaifa? Tusiishie hapo. Twende mbele na kuhoji. Je ni wanakaya wanagapi hawajawahi hata kukanyaga barabara ya lami achilia mbali kuzifaidi? Je hawa nao wanasherehekea miaka 55 ya uhuru au udhuru?” anauliza Mipawa huku akiinua kombe lake na kubwia kahawa.
            Mgoshi naye anaamua kupoka mic na kuronga “ninakuabaina ya maangaizo yako profesa Mipawa. Nataka nikuchomekee kidogo tu kwa kuongeza kuwa tihoji ni wangapi wamesoma vilivyo ukiachia hawa wanaoghushi na vihiyo wengine wa kuchapia chapia kama kiswangiish? Je timejiandaaje kwa ajiii ya kesho? Je sisi tiko huu kwei kwei au tinajidanganya hasa ikizingatiwa kuwa baa letu bado ni tegemezi?”
            Kanji anaamua kula mic “vengi nasema kweli kwelikweli. Mimi ona kama tangu napata huru iko endeleo kuba sana. Naona Swahili mingi endesa gari na kujenga jumbani kubakuba. Zamani gari na jumba kubakuba ilikuwa ya hindi tu. Sasa naona ikobadili sana. Witu wingi nachenji. Kila mtu sasa naveza waa wivalo paka napendeza sana. Naona jumba nyingi Kariakoo . Hata kama sisi hapana endelea kama Europe, iko piga hatua sana.”
            Mpemba anaamua kurejea. Anakatua mic na kuronga “tusemapo twahitaji wote kuwa huru, twamaanisha maendeleo. Pia niseme wazi, haya maendeleo tuniotaka si njini tu bali kaya nzima. Kama yawezekana kuwapelekeni Pemba muone tulivopigwa, nadhani wengine wasingesema waniyosema japo haki yao. Naungana na Nsomi kusema wazi kuwa twapaswa kuhoji maana ya uhuru wetu ili kujua kama uhuru kweli au udhuru. Haiwezekani maendeleo yakapimiwa njini na kusahau mashambani ambako waishi watu wetu wengi na ambao shughuli zao zaendesha kaya hii. Hivi nkulima akiacha kazi nani aweza kaa hapa njini?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si linakuja shangingi la muuza bwimbwi maarufu mtaani akipiga honi kushangilia miaka 55 ya uhuru! Mara anashuka na kutumwagia mabulungutu ya njuluku. Tukiwa tunashangaa jamaa anadandia mchuma wake na kuondoka. Ndipo Kapende anasema “hawa kweli ndiyo wako huru ingawa zao zinahesabika.” Je wewe ni huru kwa maana ya uhuru au kwa maana ya kisiasa? Soma na kutia akilini na kutafakari ili kujiletea uhuru wa kweli wewe na kaya yako na vizazi vyako.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: