How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday 31 December 2016

Mlevi kuanzisha kanisa la Upasho na Vitisho na Mipayuko

            Baada ya kuona walevi wenzangu tena vihiyo na wasio na ujanja hata nusu yangu wakianzisha madhehebu yao na kuukata, nami nimeamua nianzishe kitu hii lau niweze kuendesha michuma ya “zawadi’ nitakapowakuna kwa vituko na ulevi wangu kama jamaa yangu Lusekelela. Nani asiyetaka kuukata hata kama ni kitapeli? Kuukata ni kuukata bila kujali umepata namna gani.
            Baada ya kuanzisha dhehebu langu likalaoitwa Upasho, nitajipachia cheo cha Mtume ili kuvutia wateja wa biashara yangu hii mpya. Kama haitoshi, nitatangaza kuwa natenda miujiza kupitia maombi. Mimi ni specialist wa kuombea wagumba, maskini na wanaougua miwaya.
            Baada ya kuwa nimepata njuluku ambazo zitamwagika kama mana kwa wana wa Israel mwenda usiku, lazima nichape kanywaji kama sina akili nzuri. Niatakuwa na uwezo wa kukata bia na whisky na siyo mataputapu niliyozoea pale Kwa Mfuga Dog na Uwanja wa Hyena.
            Najua kuna wanoko wengi wanaoitwa waandishi wa habari. baada ya kuwa nimepiga mma, hata kama nitaangusha gari na kufanyiwa kitu mbaya wao inawahusu nini?
 Nitoe onyo. Watakaoniandika vibaya nawapiga mkwara kuwa watakufa ndani ya miezi mitatu. Ili kuhakikisha wananyotoka roho lazima niwakodishe wanyotoaji roho wawanyotoe roho halafu nitangaze kuwa nilitabiri vifo vyao ambavyo vitatokana na kunishfu mimi mlevi wa God.
            Tokana na kaya yetu kutoa misamaha kwa madhehebu ya kidini, nitaanza kuwasaka wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi ili watumie dhehebu langu kuingizia biashara zao ambazo nitazitangaza kama misaada kwa dhehebu langu. Kwa vile hakuna cha bure duniani, mie nitawatoza kodi kidogo na kuukatata. Bila shaka hapa nitapata midola na kununua migari ya bei mbaya halafu nawahadaa walevi kuwa nimepewa zawadi na watoaji ambao hawapendi kutangazwa majina yao.
            Ili kuputa njuluku lazima mbali na kutegemea kupitishia wafanyabiashara mizigo yao, lazima niuze bwimbwi kama sina akili nzuri. Nikichanganya na njuluku nitakazowatoa wasaka miujiza, bila shaka nitaukata haraka iwezekanavyo. 
            Kuna kipindi nilipanga nilipanga kuingia kwenye siasa na kuanzisha chama cha familia yangu ambapo mimi nitakuwa mwenyekiti wa maisha na ndugu na jamaa zangu vigogo wa chama. Lakini tokana na kuwa kule kuna kukaguana namna mlevi alivyochuma, siendi.   Baada ya kuingia kwa dokta Kanywaji, naona kama siasa hazilipi kama mwanzo. Sitashangaa kusikia siku moja akiweka masharti juu ya namna ya kutumia ruzuku vipatavyo vyama vya kisiasa. Hivyo, nimeonelea kuanzisha dhehebu badala ya chama.
            Kwanza, kuendesha chama ni ugonjwa wa moyo hasa unapokuwa king’ang’anizi kama mimi. Kule wanataka demokrasia wakati kwenye neno la Bwana unakuwa wewe ndiyo kila kitu.
            Pili, kwenye vyama kuna fitina kibao. Wanaingia na kutoka tokana na kila mmoja kuwa na misheni yake kwenye siasa. Kwenye dini ukishajipachika cheo chako bab kubwa, hakuna mpinzani wala wa kukubughudhi. Unakusanya kodi mwenywe, unatumia mwenyewe; na hakuna wahasibu wa lisirikali kuja kuumbua ulaji wako. Hata ukinunua mchuma wa bei mbaya na kujipa kama zawadi halafu ukatangaza kuwa umepewa zawadi, hakuna sheria ya maadili itakayokubana kama wanasiasa. Huku ni madili matupu. Wakati kweney siasa ni maadili matupu. Kwenye dini unabukanya kama utakavyo huku ukizidi kuwahimiza waumini kutoa sana ili Mungu ‘awazidishie” hata kama si kweli. Who cares?  Afadhali nianzeshe dhehebu langu la upasho na vitisho na mipayuko huku nikiendelea kupiga kanywaji kama sina akili nzuri.
            Kwa vile nimemaliza na kuanza mwaka mpya, haya ndiyo maazimio yangu ya mwaka mpya. Huu ni mwaka wa upasho, kupiga kanywaji na kuendesha michuma ya bei mbaya nitakayonunua na kudanganya nimepewa zawadi. Tuonane wiki ijayo kwa mipango mingine babu kubwa.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: