How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 29 December 2016

Kijiwe chashanga kaya kubinafsishwa kwa magabacholi

Mpemba anaonakena ana ishu inayomkera. Ameingia akiwa na gazeti mkononi huku akisonya nakutikisa kichwa. Kwa waliomzoea, wanajua kuna jambo linamkera.
Mbwamwitu anamuuliza “Mgoshi mbona unaonekana kukereka kunani tukusaidie?”
            “Yakhe we niache. Kwani hukusikia eti magabacholi wawili wamedai wilaya na Nkuranga ni mali yao? Kama hujasoma basi chukua gazeti usome.” Anampasia Mbwamwitu gazeti la Danganyika Daima.
Kichwa cha habari gazeti kimeandika “Magabacholi Wawili Wadai Wana Hati Milki ya Wilaya ya Nkuranga.”
            Habari inayofuata inasema “Magabacholi wawili Mahanji na Kahanji wametoa notisi kwa wakazi wa Wilaya na Nkuranga kuhama mara moja ili kuondoka kwenye ardhi wanayosema wamekuwa wakiimilki tangu walipogawiwa na Nkoloni.”
            Kapende anaamua kutia guu na kusema “mimi nilidhani kaya yetu ilikuwa huru tangu mwaka 61 kumbe nilikosea! Sasa inakuwaje magabacholi wawili, tena bila aibu, wanaweza kudai kuwa wilaya nzima ni mali yao? Hapa lazima kuna tatizo tena kubwa.”
            Msomi Mkatatamaa naye hangoji. Anakula mic “usemayo kaka yana mashiko. Lazima kutakuwa na tatizo tena kubwa tu. Nadhani nichukue fursa hapa kumtaka rais Joni Kanywaji awatumbue hawa jamaa ili waende kwao India na kudai ardhi kule. Ni ajabu. Hawa inaona hawaheshimu uhuru wetu tulioupata toka kwa manyang’au waliotuletea balaa hili la mijitu mibaguzi inayodhani sisi ni manyani wasio na akili hata kujua kuwa hii kaya ni mali yetu tuliyopewa na Muumba mwenyewe. Hapa bila shaka kutakuwa na wapiga dili waliowapa hizo hati feki. Je kwanini tusiwatokee na kuwatimua kama lisirikali linawagwaya kama ambavyo limekuwa likifanya siku zote?”
            Mipawa anakula mic “wala mie sishangai. Tumejiruhusu kuchezewa na kudhalilishwa kama vile tu hamnazo. Inakuwaje wanahizaya hawa wanaweza kudiriki kututia midole machoni bila woga wala aibu? Lazima kuna namna. Haiwezekani magabacholi wadiriki hata kuwafukuza viongozi wetu wastaafu wasiwe na kinachowapa hiki kiburi cha ajabu. Sasa kama wanaweza kudai wilaya nzima ni mali yao, watashindwaje kusema hata ikulu ni mali yao?”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu na kuronga “habari hii imenitia kichefuchefu na kuharibu siku yangu. Hapa lazima wanene wetu watueleze: kunani kama si ubwege na kutojiamini? Hamkumsikia yule gabacholi Maanji anayejidai kuwa bilionea alivyopeleka mikataba feki kwa pilato. Hii ni dharau kiasi gani wajameni? Hapa lazima wanene watueleze haraka kabla hatujachenchiana pakachimbika bila jembe.”
            Mgoshi Machungi anakatua mic “hapa azima tiangaie nani anawapa kibui hawa wanahizaya ii naye timshughuikie kikamiifu ii iwe somo kwa engine wanaodhani kaya yetu ni shamba la bibi. Mimi napendekeza kwa wazii Ukuvi afute hii hati miiki inayowapa kiburi haafu achunguze na kuwakamata hawa magabachoi ii wafie upango.”
            Mzee Maneno anakwanyua mic “Tulishawaambia kuwa tumeuzwa japo tunajidai kuwa tunaimilki kaya ambayo tunaiita yetu wakati ina wenyewe. Kama siyo siasa za kuendekezana, hawa jamaa walipaswa kufia lupango. Wallahi leo hii imenifanya nimkumbuke jamaa yetu marehemu Chris Mtikisa aliyewatikisa na kuwatia aibu. Hata hivyo, niseme wazi. Dokta Kanywaji hatawaacha watende haya makufuru. Lazima watakwenda na mtu hawa.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic na kusema “kumbe wakati mwingine unaweza kudhani unaota wakati si kweli! Hata kama ni jeuri ya njuluku, jamani hii imezidi. Bila kujitambua na kuwatambua na kuwatumbua wabaya wetu, kuna siku tutaambiwa tufunge virago na kutafuta pa kwenda baada ya kuambiwa hii kaya si yetu.” Anamaliza huku akimkazia jicho Kanji ambaye naye anamtazama kwa mshangao.
            Kanji naye anaamua kula mic “hii iko sangaza mimi sasa dugu zangu. Kama dugu bili nasema namilki wilaya, hiyo vatu nazaliwa pale takwenda wapi?”
            Kabla ya kujibu, Mchunguliaji anajibu kiuchokozi “India.”
            Kanji anajibu “veve iko jua India au natania. Kule iko mtu mingi sana dugu yangu. Kama veve nakwenda India hapana kaa hata siku moja takimbia kama napata kurutu veve.”
            Mpemba anakatua mic “yupo jamaa yangu alokuwa akienda kule kununua bidhaa. Alintonya kuwa kule watu wababana hadi kujisaidia kwenye madebe tokana na ukosefu wa sehemu ya kuchimba vyoo. Yule jamaa aliongeza kuwa hata hii hali ya kuchoma  maiti wafarikipo yatokana na ukosefu wa ardhi ati.”
            Kapende anajibu “usemayo Ami ni kweli japo hawa magabacholi wa hapa kaya wanajifanya kutojua ugumu wa maisha unaoendelea kule Ugabacholini. Huoni wakiwa hapa wananenepeana wakati kwao wakondeana?”
            Msomi anarejea “nadhani walidhani tutaendelea kutojua kinachoendelea kwao. Kwenye kizazi hiki cha mitandao wataficha nini.” anachomoa kisimu chake na kuanza kutafuta video kuonyesha ugumu wa maisha huko India. Mara video inaanza kucheza ikionyesha magabacholi maskini wanavyosoteshwa na ukapa kule.
            Msomi anaendelea “kama wanene wetu wangejua kuwa tunajua kila kitu, wala wasingeendekeza kunguru yoyote zaidi ya kutupa lupango. Napendekeza twende zetu Nkuranga na kuungana na wachovu wa huko ili tuwahamasishe wadai magabacholi wote warejeshwe kwao au kwa Kwini aliyewaleta hapa kutengeneza reli na si kudai umilki wa kaya na ardhi yetu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la gabacholi mmoja. Acha tulitoe mkuku ili kumtia adabu!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.
 

No comments: