Baada ya rais John Magufuli kuridhia kufunguliwa ubalozi wa tanzania nchini Israeli, wengi walishangaa hata wengine kumlaumu wakiona kama anakwenda tofauti na msimamo wa Tanzania bila kujua kuwa mambo yamebadilika tena sana. Kwani, alichofanya ni tofauti na msimamo wa Tanzania ulioasisiwa na baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Hivyo, wengi waliona kama anakiuka miiko ukiachia mbali kuonekana kama anaangalia ndani (inward looking) akipuuzia uhusiano wa kimataifa. Rais Magufuli alikaririwa hivi karibuni akisema “nimeamua kurudisha uhusiano na Israeli, kwa kumteua Balozi tu umekuja ujumbe wa watalii wapatao 600 kutoka nchi hiyo, fedha zimeingia.”
Katika kudurusu hili, nitatoa sababu zifuatazo:
Mosi, siasa za sasa na za wakati wa akina Mwl Nyerere ni tofauti sana. Wakati wa Mwalimu, dunia ilikuwa kwenye kile kinachoitwa vita baridi (Cold War) kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti wa Kirusi (USSR) kama mataifa mawili kandamizi na koloni bila kujali nani alikuwa upande gani. hata hivyo, baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin hapo 9 Novemba,1989 dunia ilibadilika kwa kiwango kikubwa baada ya upande wa Magharibi ukiongozwa na Marekani kufanikiwa kuuangusha upande wa Mashariki ukiongozwa na Urusi. Hivyo, siasa za wakati ule ni tofauti kabisa na za sasa. Wanaoona kama ni ajabu kuanzisha uhusiano na taifa la kizayuni lenye sifa ya kuwakandamiza Wapelestina, inabidi waelewe hili.
Pili, tujiulize. Hivi kama Palestina ingekuwa huru na sisi tukiwa tunatawaliwa ingekuwa tayari kutoa sadaka ya uchumi wake eti kwa sababu ya taifa la Kiafrika kama Tanzania? Hili sitalijibu. Jibu lake unaweza kulipata mwenyewe kwa kuangalia ima uhusiano baina ya masalia ya waarabu yaliyoko Tanzania au tabia za nchi za kiarabu dhidi ya waswahili. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa nyingi za vifo vya waswahili huko Mashariki ya kati vya wafanyakazi wa ndani wa kiswahili tokana na ubaguzi na ubaguzi, ujinga na unyanyasaji wa waajiri wao ambao bado huamini kuwa mtu mweusi ni mtumwa au abid. Mbali na hilo, rejea namna hawa wapalestina tunaowakingia kifua walivyotuuzia ndege mbovu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere pamoja na kuwaamini na kuwatetea.
Tatu, ili kujua kuwa kwa sasa kila nchi inaangalia maslahi yake, rejea kitendo cha nchi ya kiarabu kama Misri kusaini mkataba na Israeli maarufu kama Mkataba wa Camp David uliofanyika huko Camp David mnamo tarehe 17 Septemba, 1978 baina ya rais wa zamani wa Misri Anwar El Sadat na waziri mkuu wa zamani wa Israeli, Menachem Begin. Kumbuka. Wakati Misri ikiingia mkataba na Israeli, mataifa yote ya kiarabu yalikuwa yameapa kutohusiana na Israeli. Lakini baada ya Misri kuona hatua hii inaathiri uchumi wake, iliamua kuingia mkataba wa makubaliano na ushirikiano na Israeli. Kama waarabu ambao ndiyo ndugu wa wenzao wa Palestina waliona madhara ya uhafidhina wao, sisi ni nani? nadhani tulichelewa.
Nne, ukiachia mbali Misri, hebu angalia Palestina yenyewe inavyoshirikiana na Marekani ikitegemea itatue mgogoro taifa ambalo ndiyo mhimili mkuu wa uwepo na ustawi wa Israeli tokana na kuipa fedha nyingi za misaada kuliko nchi yoyote ulimwenguni. Hapa hujaongolea kuiwezesha Israeli kijeshi na kijamii. Tanzania ni nani kuendelea na misimamo ya kikale? Ni vizuri kufahamu kuwa mahusiano ya kimataifa ya sasa yamejikita sana kwenye uchumi kuliko siasa na mambo mengine kama ilivyokuwa hapo zamani. Siasa za kisasa zinataka hivyo.
Tano, kwa wanaokumbuka namna Tanzania na nchi nyingine zilizokuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi wa Afrika Kusini zilivyoathiri uchumi na maisha ya watu wao kuhakikisha makaburu wanang’olewa, ni mashahidi kuwa namna ambavyo Afrika Kusini sasa inawatenza watu wao ni somo tosha juu ya kuhatarisha uchumi na maisha ya nchi kwa ajili ya siasa za nchi nyingine. Hakuna anayeunga mkono ukaburu unaofanywa na Israeli dhidi ya Palestina. Hata hivyo, pia hakuna ambaye yuko tayari kuhatarisha uchumi wa taifa lake kwa ajili ya taifa jingine. Hii maana yake ni kwamba, badala ya nchi moja moja kujitoa mhanga kuhakikisha Palestina inapata uhuru wake, nchi zote zinapaswa kuungana pamoja na kukabili mataifa ya magharibi ambayo kimsingi ndiyo mihimili mikuu ya ukaburu unaoendelea nchini Palestina. Kwa nchi maskini kama Tanzania, kuendelea kuitenga Israeli na kupoteza fursa za kiuchumi, ni kujitia kitanzi kwa ajili ya jambo ambalo halitafanikiwa kutokana na hatua kama hiyo. Siasa za mapenzi ya mshumaa zimepitwa na wakati kama tulivyoeleza tokana na kuanguka kwa ukuta wa Berlin.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli kuhakikisha anafanya biashara na Israeli lakini siyo kugeuzwa mmojawapo wa watu wa kutumika kuhalalisha ugaidi na unyama inaowafanyia wapalestina. Aeleze wazi wazi msimamo wake kuwa lengo lake ni mahusiano ya kibiashara lakini si kujiingiza kwenye siasa za ndani katika mgogoro huu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.