Kwa wapenzi na watunzi wa vitabu kama mimi, mtu anapoandika kitabu huwa anatengeneza kitu ambacho kitaishi muda mrefu hata baada ya yeye kuwa ameondoka. Mmoja wa watu wanaonivutia sana walioamua kutumia fursa na uwezo wao kutengeneza urathi usiochuja si mwingine ni rafiki yangu mzee wangu na mtunzi mwenzangu mzee Pius C. Msekwa ambaye baada ya kustaafu anautumia utajiri wake wa maarifa kuelimisha jamii kupitia makala na vitabu. Hapa komredi Msekwa anaonekana akizindua kitabu chake kiitwacho Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye hakuwa mwalimu wake tu bali mentor wake; ambaye kadhalika mchango wake kwa taifa si haba.
Juzi juzi alipoteuliwa kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Mbeya cha
Sayansi na Teknolojia, nilisoma kwenye mtandao wa Jamii Forums watu wengi
wakilalamika kuwa inakuwaje Komredi Msekwa awe na vyeo viwili tofauti na
falsafa ya rais John Pombe Magufuli aliyemteua. Hata hivyo, wakosoaji walisahau
kitu kimoja; Komredi Msekwa si mtu mwenye njaa wala mwenye tamaa ya madaraka na
mali. Nadhani, kwa tunaomfahamu unyenyekevu wake na kujitolea, alipokea wadhifa
huu kwa sababu ya kumheshimu rais. Nakumbuka alipoteuliwa, alinitaarifu. Kwa wanaomjua, Komredi Msekwa hajapewa ajira
wala ulaji bali mzigo wa kusaidi taifa kutokana na utashi, utayari na uzoefu
wake. Kitu ambacho wengi hawakifahamu ni
kwamba nyadhifa alizo nazo Komredi Msekwa si ajira bali heshima inayomgharimu
muda wake wa kustaafu. Kama Komredi Msekwa angelikuwa mpenda madaraka si
angeendelea kugombea ubunge na kupita tu. Mbali na hayo, Komredi amejitofautisha kama mpenda jamii ambaye
anapohitajika huwa hakatai. Isitoshe, tukiangalia kizazi cha sasa kilichojaa
wapigaji, kwanini tusimpongeze Komredi Msekwa kwa kuwa tayari kutwishwa majukumu.
Nadhani hili linajibu swali ambalo wachangiaji wengi kwenye mtandao wa Jamii
Forums waliuliza: Inakuwaje rais amteue mtu mwenye umri zaidi ya miaka 80 na
kumuondoa profesa Mark Mwandosya mwenye umriu wa zaidi ya miaka 60? Nani kasema ujuzi inazeeka? Isitoshe wote wawili si wasaka ajira bali viongozi waliotumikia taifa kwa uaminifu na ufanisi mkubwa
na kwa muda mrefu. Hivyo basi, kwa kusherehekea na kuonyesha kufaa kwa Komredi
Msekwa, nimeamua kumpamba kwenye blog hii leo lau watu waweze kutambua uwezo
wake mkubwa si wa kuongoza tu bali hata kufikiri na kuweka fikra zake kwenye
maandishi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kwa namna
komredi Msekwa anavyojituma au tuseme anavyo-punch laptop yake kama asemavyo, sijui taifa letu lingeneemeka vipi
kama viongozi wetu wote wangemuiga? Kwa kuangalia namna Komredi Msekwa
alivyochangia katika uongozi wa taifa letu, nimechagua picha hii iwe picha
maalumu na muhimu ya kufungia mwaka. Komredi Msekwa aka Rock, nangoja kwa hamu
kusoma vitabu vyako viwili ambavyo najua uko unavimalizia. Komredi Msekwa,
hongera kwa kazi pevu na tafadhali, endelea kuelimisha umma kupitia maandishi
na mchango wako visivyo kifani.
No comments:
Post a Comment