The Chant of Savant

Wednesday 5 February 2020

TATHMINI YA MIAKA 43 YA UHAI WA CHAMA CHA MAPINDUZI


Tarehe  5  Februari  2020;  wana-CCM  wanaadhimisha  miaka 43  ya uhai wa Chama chao. Tunapofanya  sherehe  hizo,  ni   vema   tujikumbushe   kule  tulikotoka,   yaani  safari  nzima iliyotufikisha  hapa  tulipo;  pamoja na   matarajio  ya  baadaye.                   
Kuhusu  suala  la tulikotoka,  kuna  mambo   muhimu    kadhaa   ya   kuzingatia,  ambayo   ni   pamoja   na haya   yafuatayo:                                                                                                          
USHIND  WA  CCM  KATIKA  CHAGUZI  MBALI  MBALI.
(i)   Kwamba   katika  kipindi  chote  hiki;   Chama   cha   Mapinduzi   kimeendelea   kuwa   ni   Chama Tawala ,   kutokana  na   kwamba  kimekuwa   kikipata   ushindi   mzuri  katika   chaguzi   zote zilizofanyika,   ikiwa  ni  chaguzi  zilizifanyika      ndani    ya   mfumo   wa   vyama   vingi   vya   siasa   tulio nao.                                                                                                         (ii) Lakini  pia  yafaa  izingatiwe  kwamba  kulingana   na takwimu za matokeo ya  Chaguzi  hizo;     kiwango   cha  ushindi  wetu  ( ambacho  ndio  ushahidi  wa  kukubalika  kwa  Chama  chetu  kwa   umma wa Tanzania),  kimekuwa   kikipanda,   na   kushuka.  Kilipanda   sana  katika  miaka  kumi ya  mwanzo baada ya kuingia katika mfumo   wa vyama vingi vya siasa:    Tukianzaia   kwenye  uchaguzi   Mkuu  wa  kwanza  wa  vyama  vingi   wa   mwaka  1995, ushindi wa Chama chetu    uliongezeka   katika   uchaguzi mkuu   uliofuata   wa mwaka 2000; na   ushindi  wetu   wet   uliongezeka   zaidi   katika   uchaguzi   mkuu wa mwaka 2005.   Lakini baada ya hapo, kiwango cha ushindi, hasa katika uchaguzi wa Rais wa nchi, kilianza kushuka   katika uchaguzi wa mwaka 2010, na kiliendelea  kushuka katika uchaguzi  mkuu  uliopita   wa mwaka 2015.
ITIKADI  YA  UJAMAA.
(iii) Kuhusu  utekelezaji  wa  Itikadi  ya  CCM  ya  UJAMAA,   yafaa  Wana-CCM  tuwe  wawazi  na  wakweli,  kwa  kukiri  kwamba  tulishindwa.  Kwani   siasa  ya  Ujamaa  sasa  imebaki  katika  maandishi tu  ya  vitabu  na  baadhi  ya  nyaraka  za  CCM;   hususa  katika  kitabu  cha  Azimio  la  Arusha  lenyewe;  lakini  siyo  katika  utekelezaji.
Lakini  yafaa  pia  sababu  za  kushindwa  huko  zielezwe  wazi,  kwamba  kubwa    zaidi   ni  kwamba  tulijaribu  “kujenga  Ujamaa  bila  kuwa  na  Wajamaa  wa  kuujenga”.
Ufafanuzi    wake  ni  kwamba,  kama  Azimio  la  Arusha  lenyewe  linavyosema  katika  ukurasa  wa  4;  kwamba  “Ujamaa  ni  imani.  Hauwezi  kujijenga  wenyewe.  Hauna  budi  kujengwa  na  watu  wanaoamin  na  kufuata  kanuni  zake”.   Basi  ukweli  ni  kwamba  hatukuwa   na  watu wa  aina  hiyo (waliokuwa  tayari  kufuata  Kanuni  za  Ujamaa).   Hiyo  ndiyo  sababu  kubwa  iliyotufanya  tushindwe  kutekeleza  ile  DHANA   (theory)   yasiasa  ya  Ujamaa.
(iv)  Lakini  yafaa  bado  tujipe  moyo,  kwamba     MOYO  WA  UJAMAA  (the  Ujamaa  spirit)  uliojengeka  miongoni  mwa  Watanzania  kutokana  na  mafundisho  mazuri  ya  Azimio  la  Arusha,  tumebaki  nao  moyo  huo   hadi  sasa;   na   unaendelea   kuonekana  dhahiri  katika  maisha  ya  kila  siku  ya  Watanzania  wa  leo.  Ipo  mifano  mingi  ya  kuthibiisha  hilo.                      
Kwa  mfano,    Dhana   ya  siasa  ya  Ujamaaa  inasema  hivi:   “Katika  nchi  ya  Ujamaa  kamili,  hakuna  unyonyaji.   Mtu  hamunyonyi  mtu  mwenzake;   bali  kila  awezaye  kufanya  kazi,  hufanya  kazi”.     
Eneo  hilo  la  dhana   ya  siasa  ya  Ujamaa’,    limeendelea  kutekelezwa  vizuri  hadi  hii  leo; kwani  vijana  wengi    sana   hii  leo,   wanajituma  kufanya  kazi  halali,  za  aina  mbali  mbali,  ambazo  zinawapatia  riziki  kwa  nguvu  zao  wenyewe.   Hao    ni  pamoja  na ‘Wamachinga’,   kina   ‘Mama  Ntilie’;  na  vyama   vingi   vidogo  vidogo  vya  ushirika,  vinavyopewa  mikopo  na  Halmashauri  za  Wilaya.
Lakini  zaidi  ya  hayo,  moyo  wa  Ujamaa,   wa  kuheshimiana  kwa  misingi  ya  usawa  wa  binadamu;  pia  unaonekana   dhahiri  katika  maisha  ya  kila  siku  ya  Watanzania.  Kuna  vikundi  vingi  vya  watu  katika  jamii  yetu,  vilivyoundwa  kwa  hiari  na  watu  husika  wenyewe;    vya  kusaidiana  katika  maisha,   nyakati  za  furaha  na  nyakati  za  shida.   Ndiyo  sababu   kuna  vyama  vingi  vya  Ushirika  vya  ‘Saccos’  na  ‘Vikoba’  vilivyounndwa   na  watu  wenyewe,    vya  kusaidiana  kiuchumi;   na  pia  kuna  vyama  vingine  vingi,  hasa  Vijijini,   vya  kusaidiana  nyakati  za  shida,  hususan  vinapotokea  vifo.   Kule   kwetu  Ukerewe,   vinaitwa  ‘Luguyo”.
Hii  yote  ni  mifano  inayothibitisha  kwamba,  hata  kama  DHANA  ya  Ujamaa  ya  “kuishi  pamoja  na  kufanya  kazi  pamoja  kwa  faida  ya  wote”,  ilishindikana  kutekelzwa;   lakini  MOYO  WA  UJAMAA  uliojengwa  na  Azimio  la  Arusha,  unaendelea  kushamini  miongoni  mwa  Watanzania.
TATIZO  LA  KUFUTWA  KWA  MIIKO  YA  UONGOZI.
Lakini  kuna   tatizo  kubwa   lililosababishwa   na  uamuzi   maarufu  uliofanyika  Zanzibar  mwezi  Januari  1991,  uliofanywa    na  Halmashauri  Kuu  ya  Taifa ya  CCM,  ambao   kwa  bahati  mbaya  ulipotoshwa  sana  wakati  ule,  kwa  madai  kwamba,   eti,   uamuzi  huo  “uliua  Azimio  la  Arusha”.     
Kwa  hakika,  huo  ulikuwa  ni  upotoshaji  mkubwa;    kwa sababu,  uamuzi  huo  kamwe   haukuua  Azimio  la  Arusha.  Hii  ni  kwa  sababu,    jambo   pekee  lililobadilishwa katika  Azimio  la  Arusha   na   kikao hicho cha Zanzibar;  ni  jambo  moja  tu,  ambalo   ni  ile   ‘Sehemu ya Tano’  ya  Aziio  hilo   peke  yake,  ambayo   inayohusu  “Miiko ya Uongozi”.                Sehemu  zake  nyingine  zote;    yaani   kuanzia   Sehemu ya  Kwanza   hadi   Sehemu   ya   Nne,   na muhimu  zaidi  ni   ile  ‘Sehemu ya  Tatu’   inayozunumzia   suala la  KUJITEGEMEA, (ambayo   ndiyo sehemu  kubwa  zaidi  kuliko zote  katika  kitabu  cha  Azimio la Arusha), hazikuguswa kabisa na  Kikao hicho cha Zanzibar. Kwa  hiyo,  kudai  kwamba  “Azimio  la  Ausha  liliuawa  Zanzibar”,  ni  upotoshaji  mkubwa.  Yapasa  tuachane  nao.
TUZINGATIE   MABADILIKO  MAKUBWA  YA  SERA  ZA  UCHUMI.
(v)   Ni muhimu vilevile kuzingatia  kwamba uamuziwa  kikao hicho cha Zanzibar, ulifuatiwa mara moja na uamuzi  mwingine muhimu,  wa kubadilisha sera zake za uchumi, ambapo  mnamo mwezi  Februari mwaka huo huo wa 1991, Chama  kilitangaza  “mwelekeo wa sera zake za Uchumi katika miaka ya Tisini” 
Mwelekeo huo mpya wa sera zake za kiuchumi  ndio ulioruhusu  sekta binafsi  iweze kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wan chi yetu;  ambalo   lilikuwa  ni  jambo  jema;  kwani  kushirikisha  sekta  binafsi  kulisaidia  sana  katika  kuimarisha  uchumi  wa  nchi  yetu,  hasa  kwa  upande  wa  upatikananji  wa  bidhaa  mbali  mbali  zinazohitajika  kwa  matumizi  ya  kawaida  ya  watu.   
MIIKO  YA  UONGOZI  ILIWEKWA  KWENYE  SHERIA  ZA  NCHI.
(iv) Ni  muhimu  pia  kuzingatia,   kwamba,  pamoja  na  kuvurugwa    kwa  suala  la  ‘Miiko  ya  Uongozi’   kulikofanywa  na  Kikao  hicho  cha  Zanzibar  cha  Halmashauri  Kuu  ya  Taifa  ya  CCM;   Miiko  ya  Uongozi  ilihamishiwa  katika  sheria  za  nchi,  na  kuongezewa  makali  yake,  kwa  kuwekewa  adhabu  kwa  wale  watakaovunja  mashari  ya  sheria  hiyo.  Kwa  hiyo  Miiko  ya  Uongozi  iliendelea  kuwapo.
KUPOROMOKA  KWA  MAADILI   MIONGONI  MWA   VIONGOZI.
(v)   Katika  tathmini  yetu,  yafaa  pia  tukiri  kwamba  kumekuwapo  na  tatizo  la  kuporomoka  kwa  maadili  miongoni  mwa  Viongozi  wetu.  Nionavyo  mimi,  ni  kwamba  kuna  sababu  mbili  kubwa  ambazo zimechangia katika uporomokaji huu wa maadili   miongoni  mwa   Viongozi  wetu.
Ya  kwanza,  ni kusitishwa kwa mafunzo ya maadili, ambayo yalikuwa yakitolewa katika vyuo vya Chama vya Kivukoni College, pamoja na vyama vyake vingine sita vya kanda,  vilivyokuwapo katika Mikoa mbali mbali.                                                                
Lakini  ni  vizuri  kwa  wanachama  kufahamu  sababu  ya  kuchukuliwa  kwa  hatua  hiyo  ya  kufunga  vyuo  vya  Chama  wakati  huo.     Ni  kwamba,   hatua  ya   kufungwa kwa  vyuo hivyo vya Chama ,  ilitokana  na   kuingia  kwetu    katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.   Tukio  hilo  kubwa  la  kisiasa,   lilisababisha  pia    mabadiliko   mengine  makubwa   kufanyika  katika mwelekeo, pamoja na malengo ya kisiasa  ya  Chama   chetu;   ambayo  sasa  yalibadilika na kuwa  ni ‘kutafuta ushindi katika chaguzi za viongozi wa Dola’. 
Ndiyo sababu,   hata Katiba ya CCM ilibadilishwa kwa kuwekewa kifungu kipya katika sehemu yake  inayozungumzia malengo muhimu ya Chama.  Kifungu hicho kipya ni kifungu cha 5, ambacho kiliweka lengo  jipya  kabisa, ambalo lilikuwa ni:   “kushinda katika chaguzi za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa”.                                                                      
Ushindani   huo  ndio  hasa uliosababisha kuwapo  kwa  tatizo  linguine  la  RUSHWA   katika uchaguzi;  kwani  wagombea walio wengi , hususan katika hatua ya kura za maoni za kutafuta mshindi atakayegombea kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi  unaohusika, wakaanza  kutumia mkakati wa kutoa rushwa kwa wapiga kura wao, kama njia ya kujitafutia ushindi.
 Sababu ya pili  ya  kuchukuliwa  kwa  hatua  ya  kufungwa  kwa  vyuo  vya  Chama  chetu  vilivyokuwapo;    pia  ilitokana  na  kuingia  kwa  nchi  yetu  katika  mfumo  wa  vyama  vingi  vya  siasa,  mnamo  mwaka  1992.   Ni  kwamba,  baada tu   ya kuingia katika mfumo huo wa vyama vingi vya  siasa;   ile  ruzuku iliyokuwa inatolewa na Serikali kwa Chama kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo  katika Vyuo vya Chama vya Kivukoni College, na katika vyuo vyake  sita vya kanda vilivyokuwa katika Mikoa mbali mbali;  ILISITISHWA.                    
 Hali hii ya kutokuwapo kwa msaada wa  fedha  za  mafunzo   hayo ya maadili na uadilifu kwa viongozi,  pia ilichangia katika kuporomoka kwa maadili ndani ya Chama,   kwa sababu ilibidi sasa kila kiongozi   alazimike kutumia akili zake  mwenyewe  tu,   katika shughuli zake za uongozi.  Na  kama wasemavyo Waswahili,  “akili ni nywele, kila mtu ana zake”.
  Taswira ya jumla   ya  Chama cha Mapinduzi.Hadi kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Chama cha Mapinduzi kilikuwa katika hali nzuri sana.   Ndiyo   sababu katika uchaguzi wa mwaka huo, Chama chetu kilijipatia ushindi mnono na  wa kishindo kikubwa.  Lakini mara  baada ya hapo, taswira ya Chama cha Mapinduzi  machoni pa wananchi  walio wengi, ilianza kuathiriwa sana,   na mambo yafuatayo:
 (a)  Migogoro iliyojitokeza kwa kasi  miongoni mwa  viongozi, hususan baina ya makundi yaliyokuwa yakizozana na  kuhasimiana miongoni mwa Wabunge wa CCM.                                                               
Image result for photos of msekwa"(b)  Kuwapo  kwa  tuhuma  kali    za   UFISADI,   ambazo  pia  zilitokana     na   uhasama huo miongoni  mwa  Wabunge  CCM.   Ilitokea  kwamba   Chama chetu kilibebeshwa mzigo wa kuwa ni Chama kinachokumbatia  mafisadi.  Jambo  ambalo  lilituathiri  sana.                                           
 (c)  Kujipenyeza,   tena  kwa kasi  kubwa, kwa  wafanya biashara  wasio waadilifu,  katika baadhi ya Vikao muhimu  vya Chama vinavyofanya  maamuzi .
(d) Chama  kupoteza  sifa yake yake ya asili,  ya kuwa ni Chama kinachojali wanyonge; na kwa hiyo kikabebeshwa  mzigo wa kuitwa  eti ni ‘chama cha matajiri’.   
 Lakini  kwa  hivi  sasa,  wanachama  tunayo    sababu  ya  kufarijika,  kutokana  na  kwamba  shutuma  zote  hizo  sasa  hazipo  tena,  kwani  zimefutwa  na  kazi  nzuri  sana  ya  kujirekebishwa,  iliyofanywa,  na  inaendelea  kufanywa,  na    viongozi  wa  Chama  waliopo  sasa
Matarajio ya baadaye.
Kazi  nzuri   inayofanywa  na  viongozi  waliopo  sasa,   imeleta matumaini mapya  miongoni mwa wanachama walio wengi.  Kwa hiyo matarajio ya baadaye yanapaswa kuwa mazuri. 
Hata  hivyo,   yafaa   ikumbukwe  kwamba  Chama cha  Mapinduzi, ni Chama  kikongwe, kwa maana ya kwamba kimekuwapo, na  pia kimekuwa madarakani   mfululizo,  kwa   miaka yote tangu nchi yetu ilipopata uhuru wake.
Jambo hili la ukongwe wa Chama  chetu,   lina faida zake, lakini pia lina hasara zake. Faida yake ni kwamba kwa sababu ya uzoefu wake huo wa miaka mingi, kina fursa  kubwa  ya kuendesha shughuli zake vizuri, na kwa hiyo kuendelea kupata ushindi katika chaguzi zijazo.                          
 Lakini kwa upande mwingine,  kuwapo huko kwa muda mrefu kunaweza kusababisha hatari kubwa.  Hii ni kwa sababu ya kwamba,   kutokana na hulka ya binadamu ilivyo, wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu ya uongozi wa nchi, hata kama Chama kilichopo madarakani kinafanya vizuri kiasi gani.                                  
Maana yake ni kwamba,   watu wanaweza kuchoka tu kuendelea kuwa chini ya uongozi wa Chama kile kile,  miaka nenda miaka rudi!  Na hatari hiyo inakuwa ni kubwa zaidi pale ambapo matendo ya viongozi  wake  yatakapokuwa mabaya kiasi cha kuwaudhi  watu.       
Kwa ajili hiyo, Chama cha Mapinduzi hakina budi,  hususan kupitia viongozi wake, kioneshe kwamba kinaweza  kuleta mabadiliko yenye tija, yenye kuleta matumaini mapya  miongoni mwa wananchi walio wengi. Kiongozi mpya wa Chama  chetu  na  Serikali,   Rais  aliyetokana na CCM,  Dr. John Pombe Magufuli,  ameleta matumaini hayo mapya miongoni mwa wananchi walio wengi. Kwa hiyo matarajio ya baadaye  ni  mazuri,  kwamba CCM itaendelea kupata ushindi na kushika Dola kwa kipindi kingine kirefu  kijacho.
KIDUMU  CHAMA  CHA  MAPINDUZI.
Chanzo: Cde Msekwa Mwenye.

No comments: