How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 25 October 2022

Ruzuku iwe kwa huduma za kijamii, si kwenye siasa

Kwanza, nikiri. Sikuwa najua kuwa ima kaya yetu ni tajiri au fujaji. Sikujua kuwa kumbe kila mwaka walipa kodi wetu kapuku wanakamuliwa kugharimia siasa kana kwamba tunakula na kunywa siasa! Kumbe kuna wakati viinchi vyenye ujambazi wa wazi wa kisiasa kama majirani zetu vinasevu njuluku lukuki? Hii stori ukimwambia jamaa kama M7 anakucheka na kuanguka kwa kicheko. Kamwambie na yule rafiki yake Tolu, atazimia kwa mshangao. Sina ugomvi na ulaji wa kisiasa. Si afadhali uupate baada ya kusota kwenye debe baada ya kuwahadaa wapika kura ya kula kuliko kupewa kila mwaka bila kufanya lolote. Hawa waliopendekezwa kuruzukiwa, tunawaruzuku kwa lipi na nini? Nadhani hata chama twawala hakipaswi kuruzukiwa. Wafanye kazi wapate kula badala ya kula wapika kula. Niliposikia hili pendekezo, nilijiuliza kama ambavyo Bi. Mkubwa mwenye kaya alijiuliza. “Vingine nilikuwa nasema ilo kweli? Lakini ni maoni ya kikosi kazi.” au urabu tu, manjonjo na njaro?
         Pili, mie ni mpenzi wa demokrasia japo si mlevi wake. Pili, mie si mwanasiasa bali kapuku, mchambuzi, msomi, na mtunzi. Tatu, huwa siamini katika ndoto bali uhalisia. Naona yule anaanza kuumka na kulaani. Tuliza bori rafiki yangu. Najua. Nitakachoandika hapa kitawakera na kuwakwaza wengi hasa wale ambao ulaji wao unategemea longolongo na madudu kama hayo.
Nije kwenye hoja yenyewe. Juzi, nilisoma mapendekezo ya kikosi kazi kisicho kazi hata hivyo kuwa vyama vya siasa vipewe asilimia 10 ya ruzuku inayotengwa kila mwaka kama riziki, sorry, ruzuku. Tunatenga hii njuluku kwa utajiri gani? Kwanini isitengwe na kupewa wakulima wetu badala ya wapiga soga? Kutenga asilimia kumi ni jambo jema japo halina wema kama hatatuangalia yafuatayo:
Mosi, je kwanini hiyo njuluku isipelekwe mahospitalini na mashuleni kwanza? Je ina maana siasa ni mali kuliko elimu na siha zetu? Je inakuwaje tunataka kuwekeza sana katika longolongo badala ya mambo ya muhimu zaidi kama afya na ujuzi?
        Tatu, je hitajio la kwanza na muhimu kwa wabongo ni demokrasia aka siasa au mambo mengine wezeshi kama vile miundombinu? Ningekuwa nimeshauliwa au nasikilizwa, ningesema, vyama vya siasa vingoje kidogo japo tuhakikishe kila hospitali na zahanati zina madawa ya kutosha, wafanyakazi wa kutosha, mishahara mizuri na marupurupu mengine. Niviasa vyama kula pini kwanza ili kuhakikisha shule zetu zote zina madawati, walimu, vitabu, na nyumba za walimu vya kutosha mbali na maslahi yanayoingia akilini kwa walimu.
        Nne, kabla ya kumwaga neema na ulaji kwa wanasiasia, ningehamishia hilo dau kwenye barabara za vijijini na wilayani ambako ndiko uhai na uzalishaji wa taifa vipo. Huko ndiko madiko diko tunayopwakia kila uchao na mazao ya kibiashara yanayotuingizia uchache wa kigeni yanazalishwa. Nani anaweza kula sera au siasa na kelele za majukwaani au kwenye majumba ya ibada? Nani anautafuta ufalme wa mbinguni ilhali amezama kwenye ujinga na umaskini vya kunuka? Nani huyo asiye na busara anayetaka kuvisha uso kabla ya makalio? Hebu tuelimishane jamanini msijedhani tunatukana au kutetea utopolo na ukandamizaji. Basi kama hiyo pesa imekosa la kuifanyia hadi kuiruzuku na kuwazawadia wana siasia basi itumike kuwapekelekea maji au umeme hawa wahenyekaji ambao jasho na nguvu yao ndivyo vimekuwa injini za taifa tangu kupata uhuru wa bendera. Kama maji yameshindikana, basi tumia fedha hiyo lau kupambana na ukosefu wa ajira kwa kujenga mazingira wenzeshi ya kutengeneza ajira binafsi au za kuajiriwa kwa vijana wetu wanaopoteza muda madarasani na kuishi kuwa machinga wakati wakati wanasiasia na matapeli wengine wakiotesha vitambi kutokana na kuruzukiwa wasipostahiki au kuvuna ambako hawakupanda kwa kupiga domo na kulilisha domo.
        Tano, tujiulize. Hii njuluku inayopendekezwa kuwapa wapiga siasa inatoka kwenye kodi ya makapuku wanaozidi kuhenyeshwa na ugumu wa maisha uliyoikabili dunia hata wale wenye nazo au? Je ni haki kuwaacha walipa kodi wengi vijijini bila hata vijibarabara vya changarawe na kuwaruzuku wanasiasa?
        Leo sichongi sana. Tukubaliane tena kuelewana. Kwa usawa huu, kwa yeyote mwenye akili timamu, siyo wakati wa kuruzukiana kwa kupiga mikelele. Tunatapanya uchache––––tena mwingi utokanao na kubomubomu­­­­––––kwa utajiri upi zaidi ya udhalili tunaouonea fahari kiasi cha wengi kutucheka na kudhani ima tu hamnazo au tuna maradhi ya kichwa? Kuna haja ya kuweka vipaumbele kwenye mambo ya lazima na maana badala ya kuendelea na mazoea yale yale. Wapika kula na walipa kodi wetu hawali siasa. Wanahitaji huduma bora. Wanahitaji barabara, hospitali, shule na zahanati bora na siyo uboreshaji wa ulaji wa wanasiasa ambao hata sera bora hawana.  Msinielewe vibaya. Wangekuwa na sera bora tungekuwa kaya kapuku kama tulivo. Tieni akilini na kufikiri na kufanya maamuzi magumu. Tuonane wakati mwingine na mwinginewe.
Chanzo: Jamhuri leo.

No comments: