The Chant of Savant

Thursday 13 October 2022

Kwani dhambi ‘wanene’ kupanda daladala?

Baadhi ya marais wa Afrika akiwamo Samia Suluhu Hassan (wa tatu kulia) na William Ruto wa Kenya wakiwa katika basi la pamoja walipoenda kuhudhuria mazishi ya Malikia Elizabeth II yaliyofanyika London, Uingereza.

         



    
  By Nkwazi Mhango

Picha zionyeshazo baadhi ya marais wa Afrika wakiwa wamekwea ‘daladala’ kwenda kwenye maziko ya mama yao - malkia wa Utashani, Elizabeth II aliyezikwa hivi karibuni zilizua mijadala, mishangao, shutuma, songombingo, usongo na usungo wa kisiasa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari. 

    Wapo waliosema kuwa ‘wanene’ wetu walidhalilishwa huku wakichekelea kama mnene aliyeingia ulaji hivi karibuni wa kaya jirani aliyeonekana akikenua utadhani alikuwa akifurahia kukumbushwa alikotoka na atakakokwenda baada ya kuachia unene. 

    Je, ni kweli walidhalilishwa, kuzidiwa akili, au kulazimika? Je, walikuwa na jinsi ya kuepuka ‘fedheha’ hii sorry, kumbukizi hili la maisha? 

    Je, kama hivyo ndivyo, mbona braza Joe Biden na wengine wenye vifua hawakukwea daladala? Je, ingetokea magaidi wakalifanyia vitu vyao hilo daladala walilopanda si kaya nyingi zingeishia kwenye mitafaruku? 

        Kwanza nikiri kwamba simjui paparazzi aliyenasa picha hii. Kama ni Mswahili, ajue amefanya kosa kuwaumbua ‘wanene’. Kama ni mtasha, amefanya kazi yake kuwaumbua ‘wanene’. Hata hivyo, nampongeza kwa kutupa picha halisi ya ubinadamu. Pia nawapongeza marais kukubali kukumbuka walikotoka, ukiachia mbali wanakoishi wengi wa wananchi wao ambao ndio waajiri wao. 

        Baada ya kugusia kwenye kilichojiri kwa ‘wanene’ wenu wapendao misafara ya magari lukuki na ushufaa huku wakizungukwa na mbwembwe zisizo na sababu wala maana kana kwamba wao si binadamu tena, naomba tuangalie yafuatayo kuhusiana na kadhia/kisa cha ‘wanene’ kudandia daladala kwenda kumzika mtesaji wao mkuu ambaye ndiye aliyekuwa mkuu wa utumwa na ukoloni ulioicha Afrika, na Tanzania ikiwamo hohehahe na maskini. 

        Ni huyo huyo aliyewaachia ‘wanene’ wetu kufuja na kupenda madaraka kwenye mgongo wa walipa kodi maskini. Ndiye aliyeanzisha woga bandia wa ‘wanene’ wetu kuwaogopa watu wao wakati ni hao hao waliowapikia kula kwa kupiga kura huku wakiendelea kugharimia matanuzi yao. 

        Kwanza, tujiulize; je, ‘wanene’ wetu wapendwa na waheshimiwa sana si binadamu kama wewe na mimi? Huoni walivyokuwa wakichekelea kupata lifti kwenye daladala majuu? Nawashukuru kwa kuonyesha ubinadamu na ukomavu wao wa kuminya na kujifanya walifurahia kwa njia mbili; mosi, kutabasamu na kucheka kana kwamba ni kweli. 

        Pili, kuuchuna baada ya kupandishwa mchuma huku wakiwaacha mabodigadi wao na manjonjo pembeni kwenda kumzika yule aliyewapa unene na kuwafundisha namna ya kuutumia kujifurahisha, kujineemesha na kujitukuza. Tukubaliane. Wanene wetu ni binadamu, tena dhaifu kama wengine. Sasa ni ajabu gani kupanda/kupandishwa daladala? 

        Kwa tunaoishi ughaibuni, kilichofanyika wala si ishu wala habari. Kwanza, ‘wanene’ wa huku si watanuaji. Pia, hawanyonyi wala kuwatumikisha watu. Hivyo, hawana maadui wa kweli na kufikirika kama huku Kusadikikani kwetu. Hivyo, wakipandishwa mchuma si dili. Pia wapo uneneni kuwatumikia, si kuwatumia wale waliowaamini na kuwakasimu madaraka. 

        Ndiyo maana hawana maadui wala hawahofii maadui wasiokuwapo kama wale wa ‘wanene’ wetu zaidi ya magaidi na vichaa. ‘Wanene’ wa huku hutumia kiakili na kiuchumi kweli kweli. Hawatanui hata kidogo. Hata wakitaka kutanua, walipa kodi wa huku hawatawaruhusu. Wanaishi kama sisi akina apeche alolo. 

        Mtasha huwezi kutumia fedha yake kujilisha pepo kama wafanyavyo ‘wanene’ wetu wasijue ni mambo ya kizamani na kikoloni waliyorithi wakati waliowarithisha walikwisha kuachana nayo ili wasionekane malimbukeni na washamba. 

Mbali na wanene wetu kuwa wanadamu, tena wengi wakiwa vitegemezi vya maskini, tujiulize; je, kabla ya kuukwaa unene, utukufu na utukutu, walikuwa wakipanda nini waliposafiri lau kwenda skuli? 

        Wapo waliokuwa wakipanda punda, achia mbali kwenda kwa miguu, tena peku peku kama alivyowahi kusema Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alibeba viatu vyake visichafuke. Unadhani gwiji huyu alikuwa mjinga au mshamba zaidi ya kuwa mwanafunzi wa maisha?  Ukiachia akina Mzee Mwinyi waliobeba viatu, badala ya viatu kuwabeba, wapo waliolala kwenye tembe wakila michembe na matobolwa, achia mbali waliokuwa wakilala chini na kulala bila kula. 

        Wapo ‘wanene’ hata waliolalia ngozi ya kondoo, ukiachia kunonihino vichakani na mengine mengi ambayo nisingependa kukumbushia ili wasiumbuke bure na kuonekana ni wavivu wa kujifunza kutokana na historia zao.  Kama waajiri wake - yaani wapika kula na wanuka jasho wanapanda mabasi, yeye ni nani asipande au kupandishwa basi? 

        Hata hivyo, kutokana na kujisahau kwa binadamu, wapo watu wanaopata madaraka na kusahau walikotoka. 

        Pili, wale wanaoshangaa au kulaumu ‘wanene’ wao kupandishwa mchuma waambiwe. Wanene wao nao wana wanene wao pia. 

        Tumalizie: Kama wachovu wanapopanda pipa hujipiga picha na selfie, kuna kosa gani wanene wakifanya kinyume na kupanda, sorry kupandishwa mchuma, kwa nini nao wasipigwe picha? Kimsingi, tuwapongeze ima ‘wanene’ wetu au wale waliowapandisha daladala kwa kujikumbusha au kuwakumbusha walikotoka kama si walikowasahau wale waliowapa ulaji. Tuonane baadaye. 

Chanzo: Jamhuri leo.


No comments: