Kwa niaba ya mafyatu wote duniani bila kumsahau Bi Mkubwa wangu na yule wa kaya, kwa huzuni, majonzi, na simanzi, kubwa, nakupa sala na salamu za mwisho za mfayatu wenzio. Natoa rambirambi kwa familia hasa Bi Sitti na Khadija, Dk Hussein, marafiki, na taifa kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika uongozi, utumishi, na historia vya taifa letu.
Shehe Ali, hukuwa ila mja safi mnyenyekevu, mwenye heshima hata kwa waliokuwa chini yako. Ulipewa mikoba mwaka 1985 wakati taifa likiwa kwenye hali mbaya kiuchumi si kutokana na uongozi mbaya bali ubazazi na ukatili wa mabepari walioichukia na kuihujumu kwa vile haikukubali kulala nao kitanda kimoja. Iliyotaka moyo wa chuma kuibadili. Ulitumia mbinu na weledi wako kama mwanadiplomasia mbobezi kusema “sasa na itoshe tubadilike na kukubali dunia inavyokwenda hata kama hatutaki.” Pamoja na uzuri wake, hukuona aibu wala woga kukiri na kutambua kuwa siasa za Ujamaa zilikuwa zimefikishwa ukingoni na kuanzisha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.
Shehe Mwinyi, nenda. Kazi umeifanya, vita umepigana na kushinda. Umeondoka msafi na hazina kwa taifa. Mafyatu tunakumbuka bashasha na utani, busara, uchangamfu, ucheshi, utani, na upendo wa kweli kwetu. Japo hukujitangaza, ulikuwa fyatu. Kwani, ulifyatua kitu kiitwacho rukhsa kilichogeuka mhuri na kitambulisho chako. Cha mno, ulifyatua daktari Hussein mnene wa Visiwani. Tunakukumbuka kama kiongozi bora na mahiri aliyeangushwa na wale aliowaamini akidhani walikuwa na imani na udhu kama wake.
Maalim Nzasa, hukuwa mjivuni, mchoyo, wala mpenda sifa. Hukupenda kutukuzwa wala kusifiwa. Hukujitutumua hata ulipofanya makubwa kwa sababu ulikuwa mcha Mungu aliyeamini kuwa Mungu pekee mtukufu asitahikiye sifa zote nzuri na kubwa. Hakika, Mwinyi, umeondoka na kutuachia tunu nyingi ikiwemo amani, mshikamano, nahau, na maridhiano ambavyo, hata hivyo, machawa, mafisadi, waroho, na wenye roho mbaya, matapeli wa kisiasa na watenda jinai wengine ambao hawajui wala kukubali kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho wameanza kuvihujumu.
Nisomapo historia yako na vimbwanga kama kununuliwa pea ya kwanza ya viatu ukaacha kuvivaa ukaibeba ukitembea pekupeku ili visichafuke nafarijika. Nakumbuka falsafa yako adhimu kuwa binadamu anapaswa kutahadhari asiwe kichwa cha mwendawazimu walevi kujifunzia kunyoa. Sijui kama wengi walikuelewa ulichomaanisha kuwa umma ukikupa dhamana, kazi yako ni kuutumikia siyo kuutumia. Hukupenda ubwana wala ushaufu na utukufu feki na uchwara zaidi ya unyenyekevu na utumishi kwa wanyonge. Pamoja na kutunikiwa udaktari wa heshima na vyuo mbalimbali, kama Ben na JK, hukuwahi kukubali wala kupenda kuitwa daktari. Ulijua athari zake yaani, ujivuni, ukihiyo, na ulimbukeni.
Pamoja na madaraka makubwa, hukuyalewa wala kuyatumia vibaya kibinafsi ila kujitoa kuutumikia umma kindakindaki na kiungwana. Cha mno, hukuogopa kukosolewa japo wakati mwingine ulichukia ilipotokea kudhalilishwa au kuonekana dhaifu kama kiongozi.
Nakumbuka sana ulivyoitikia mwito kwa unyenyekevu baba wa taifa Mwalimu JK. Nyerere alipokufyatua kuwa ikulu siyo pango la wezi mbali au ulipowatimua wanachuo walipoonyesha dharau. Bila kupayuka wala kufyatuka, ulivunja baraza la mawaziri tena bila kutoa hata notisi, ukajipanga upya na mambo yakaenda vyedi na mafyatu wakafurahi kunufaika. Haimanishi utawala wako haukuwa na kasoro. Tokana na kutokuwa na uzoefu na sera hasidi za kinyonyaji na kinyanyasaji za kibepari, wapo waliotumia madaraka na upole wako kupiga njuluku na baadaye ilibainika, binafsi, kuwa hukuwa fisadi au roho ya fisi ya kuuibia umma. Umeishi maisha ya faida na heshima kiasi cha kuacha urathi uliotukuka kama baba, kaka, binadamu, na yote katika yote, kama rais aliyependwa na kuheshimika “si haba.”
Alhaj Mwinyi, hukuwa mdini wala mhafidhina. Ilipotokea kasheshe ya mabucha ya nguruwe mwaka 1993, japo kwako ni haramu, ulisema wazi, atakayetaka kula nyoka au nguruwe ruksa, atakayepiga ulabu ruksa. Hukujifanya msafi na mhafidhina kutumia dini yako inayopingana na mambo haya kuwapendelea waliojiona ni wenzako wakati hawakuwa. Ulijua mipaka ya dhamana ya urais. Kwa mawazo, maneno, na vitendo ulithibitisha kuwa ulikuwa rais wa wote waumini na wasioamini. Hukuyumba wala kuyumbishwa hasa ulipoweka historia ya kuwa kiongozi muislamu ambaye hakupendelea msikiti wala kuchukia kanisa. Ulikuwa mtanzania kwanza na muislam mwisho jambo ambalo ni gumu wengi kulifanya. Na hii ni mojawapo sababu za mafyatu kukupenda. Nani mara hii kasahau kipindi kigumu na mtihani kwako Zanzibar ilipotaka kujiunga na jumuia ya kimatiafa ya kiislamu (OIC) mwaka 1992 bila kusahau kuibuka kwa kundi la G55 lililotishia muungano? Baada ya kusoma katiba na sheria, ulisimama kidete na kushughulikia kadhia hii kwa busara na haki na kuiondoa nchi kwenye mtatange, mtanziko, na mtihani vilivotishia kutugawanya na kuutikisa hata kuuvunja muungano wetu. Wewe ulikuwa muungano maana ulizaliwa bara na kukulia na kutawala visiwani bila upendeleo wala uonevu.
Ndugu Mwinyi, makala au kitabu kimoja haviwezi kueleza mema nengi uliyolifanyia taifa kuanzia darasani, madarasat, ubalozini, hata ikulu uliyoifanya kuwa sehemu na nyumba ya watanzania bila kujali nafasi zao kijamii. Kukukariri, wewe ni hadithi nzuri.
Tunaaswa kuwa كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْت kullu nafsin zaikatul maut bimaana kila nafsi itaonja mauti. Pumzika baada ya kazi nzito na tukufu. Lala salama Ndugu yetu alhaj Ali Nzasa Hassan Mwinyichande Mangandi. Tusalimie wapendwa Julius Nyerere, Abeid Karume, Aboud Jumbe Mwinyi, Benjamin Mkapa, John Kanywaji Magufuli, Edward Sokoine, Idris Wakil, shehe Thabit Kombo na wengine waliotangulia. Waambe. Tunawamiss na kuwakumbuka sana.
Hamba kahle mfowethu.
Chanzo: Mwananchi leo.
No comments:
Post a Comment