How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 7 May 2024

Fyatu Awataja ‘Wanamtusi’ Rahis


Mpendwa Dada mkubwa,
 Pole kwa majukumu hata majungu. Naamini ulisoma waraka wangu kwako wa ripoti ya CAG. Naomba, kwa mara nyingine, tuwasiliane bila kufyatua wala kufyatuka. Juzi ‘mwanao wa pekee’––––kama kweli na siyo chawa, msakatonge, na msanii anayetaka kukuingiza mkenge––––alitutangazia kuwa ifikapo tarehe 15 Aprili, angetaja ‘wanaokutukana’ mitandaoni.                 Ajabu ya maajabu, hakutaja! Kama yeye ‘mwana wa pekee’ basi wewe Mungu. Wanaokuhadaa kwa kukugeuza Mungu wanakuchulia, kukulaani, na kukuwangia. Waogope ja ukoma. Watakuponza. Jiulize. Walioitwa Mungu wakakubali wako wapi? Wasemayo yatoka tumboni si rohoni.  Mie si chawa, kidhabu, mwoga wala mmbea, nataja.
        Kabla ya kutaja, naomba nielimishwe maana ya kutukana. Nashauri, aliyetoa madai abanwe atutajie majina ya hao watukanaji, mitandao wanayotumia, matusi gani, ili iweje, kwanini, na wachukuliwe hatua gani. Akishindwa, timua usiendekeze uoza. Je kweli unatukanwa au ukosefu ubunifu na uchawa wa kutafuta tonge? Nini majibu, mawazo, au ushauri wako?  Je huyu afanyaye haya hakutukani? Naomba, kwa heshima na taadhima, tufuatane. Nikujuze wanaokutukana.
Kwa vile ‘mwana pekee’ amegwaya kutaja ‘wanaokutukana’, Fyatu Mfyatuzi, bila   kificho, uchawa, unafiki woga wala kumung’unya maneno nawataja ifuatavyo kuwa ni wale:
        Mosi, wananaomkuhadaa kukuita mama yao wakati wanakusanifu na kutaka kukuzidi akili. Wakitoka hapo baada ya kukuita mama, wanakwenda kwa mama zao na kusema yule ni mama wa ulaji usichukie mama yangu. Wewe ni mama wa Abduli, aliyewahi kumtuma kufanya kazi za kiserikali kwa Yowe M7i sawa na kitegemezi chake kifanyavyo kwenye ufalme wa dingi wake, Wani, na wengine wawili ambao majina yamenipiga chenga. Hivyo, yeyote anayejiita mtoto wako wa pekee ima anawaua, kuwaficha watoto wako halali, au kutuaminisha kuwa ulizaa nje ya ndoa jambo ambalo ni matusi yasiyosameheka kwako na kwetu. Sikumbuki wewe kuasili mtoto hata pet wala kuwahi kuishi Kolomije. Pia, kama M7i, anatwambia kuwa unatawala kiukoo na kifamilia.
Pili, binadamu wanaojidhalilisha kwa kujiita au kukubali kuitwa machawa. Ukiwa na chawa hata kuwafuga, unaanisha wewe ni mchafu. Tunakujua wewe ni msafi tu. Hivyo, kataa chawa hata wakuabudie na kukusifia vipi. Lengo lao, kama huyu mwenzao, ni kukunyonya damu hata kukuambukiza magonjwa. Kama hukulijua hili, lijue.
Tatu, wapigaji njuluku za umma, wasanii, wasakatonge, na matapeli wa kisiasa wanaopayuka bila kufikiri wakiendeshwa kwa matumbo. Wanakutukana, kwa sababu wanataka kukudanganya, kukutumia, na kukudhalilisha kwa matendo yao machafu.
Nne, wanaokusifia hata ukiboronga mfano kutofanyia kazi ripoti ya CAG au kutotumbua zaidi ya kupenda kuteua na kutengua wenye madoa au ndugu zako na wanaotaka uwateue. Wewe siyo M7i kuteua vitegemezi vyako, wakwe, mashoga, hata wapambe machawa wasio na sifa yoyote bali kujipendekeza na uchawa. Huu ni uchafu ambao atakayeuita hivyo hatukani bali kusema ukweli mtupu. Kama ukweli ni kutukana, basi, hao wanakutukana.
Tano, wanaoficha au kuteua na kuwakingia kifua wahalifu hata wengine wenye tuhuma za kuua. Rejea wasiojulikana waliofyatua mafyatu kama akina Azori Gwanda na wengine zama zile za ubabe na utukutu uliotukuzwa hadi ukaitwa utukufu. Muulize rafiki yako Tunda Lishe. Atakwambia habithi aliyeongoza waliotaka kumdedisha.
Sita, wanaokuambia umbea na uongo kwenye mitandao kama vile TwT na mingine yenye majina makubwa tena mbele ya wanene wenzako kama yule kidhabu aliyekuahidi asitaje. Kama hakukutana au kukuhadaa ili kupata ujiko, nini kimemzuia kutaja? Je alisukumwa na uongo na umbea ili kuwatisha wenzake?
Saba, wanaokuchonganisha na wasaidizi wako kwa faidi fichi binafsi. Hawajui kuwa kaya ina vyombo vya upelelezi, usalama, na mifumo ya ndani ya kushughulikia madai ya kweli na si umbea? Hawajui kuwa kaya haiendeshiwa kwa umbea japo kuna dalili za kujipendekeza na uchawa kuhalalishwa kwa maangamizi ya kaya baadaye.
Mwisho, wale wanaojifanya wanakujali, kukupenda wakati ukweli ni kwamba wanakuchukia kukulamba kichogo, na kukuponda. Wanachopenda ni maslahi yao binafsi hata kwa kuwaangamiza wengine wasijue kuwa mafanikio ya wengine hayazuii yao. Ni roho mbaya tu, uzwazwa, na umbea vinavyosumbua. Ukitaka kujua, kujifunza, na kuzingatia nisemayo, jikumbushe. Kuna fyatu alisifiwa kama Chuma mwendazake akaingia mkenge? Angalia waliokuwa wakimsifia hadi kumuita Mungu wako wapi. Hawakumsifia, kumshukuru, na kumtukuza hadi wote wakakufuru wasijue walikuwa wanahadaana na kulaaniana. Si wapo kwako wanajikesha na kujipendekeza ili tonge liingie mdomoni. Hawa ni hatari na na hovyo. Wako tayari hata kulisaka tonge chooni au kwa kuwatilia wenzao sumu. Waepuke.
 Shukran sana kwa kunisoma na kunishabikia. Heri wanaokwambia ukweli maana wanakupenda kuliko wanaokudanganya kwani wanakuponda na kujifanya kukuzi akili. Waogope kama ukoma. Akina Yuda wako wengi na wengi unao kwenye ulaji wako. Kwenye msafara wa mamba na kenge wamo. Utawajua. Kumbe nimeshapata kanywaji!
Chanzo: Mwananchi J'tatu iliyopita.


No comments: