Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Monday 16 September 2024

Ndoa ni darasa jifunze na ufunze


Tuanze na kisa cha wanandoa wawili marafiki na wageni waliotutembelea hapa nyumbani. Walitoka Toronto kuja Manitoba. Hivyo, ilibidi walale lau tujadili hili na lile. Baba ni kutoka nchi jirani ya Tanzania. Mama ni mkanada mzaliwa wa Toronto. Ilipofika wakati wa kulala, tuliwakumbusha watoto wetu kwenda kupiga miswaki na kwenda vyumbani kwao. Baada ya hapo, na sie tuliwaaga wageni wetu kuwa tulikuwa tunawenda maliwatoni kupiga mswaki. Hawakuamini kama ambavyo nasi hatukuamini baada ya kueleza mshangao wao. Wale wanandoa walitushangaa kwanini tunapiga miswaki kabla ya kulala. Nasi, tuliwashangaa. Mama alisema kuwa akipiga mswaki wakati anakwenda kulala, asingeweza kupata usingizi mbali na kinyaa cha kufanya hivyo! Nesaa naye alimwambia kuwa akilala bila kupiga mswaki, asingepata usingizi. Hivyo, tulishangaana kama ambavyo hushangaana kwenye mbalimbali ambapo huishia kujisuta wakidhani wanawasuta wenzao.

Sasa unaweza kujiuliza. Kama una mazoea safi ya kupiga mswaki kila ulalapo , utajiuliza hata kushangaa inakuwaje walale bila kupiga miswaki. Ukiangalia kisa hiki, kinahusu jambo dogo lakini lenye umuhimu mkubwa na la binafsi lakini kinaweza kukufunza mengi. Je ni mangapi wanandoa hawayajui japo ni muhimu?

            Mnapofunga ndoa, kila mmoja anakuja na mambo yake, yawe mazuri au mabaya. Kila mmoja anakuja na mazoea yatokanayo na malezi, mazingira hata uchaguzi na utashi wake. Ni kapu mchanganyiko. Hivyo, mnapoanza kuishi kama wanandoa, jambo kubwa na la muhimu ni kuwa tayari kujifunza na kufundisha. Ndoa ni kama darasa au shule isiyokuwa na mwisho. Ili kuifanikisha, wanandoa, bila kujali viwango vya elimu au umri, lazima wawe tayari kuwa wanafunzi na walimu kwa wakati mmoja. Ukiangalia hili la kutopiga mswaki wakati wa kulala, pia laweza kuwapo la kulala bila hata kuoga. Binadamu ni viumbe wachafu. Unapalala mchafu, unategemea kweli mambo yaende vizuri? Umeshinda unakula, kujisaidia, kutoa jasho na mengine. Sasa inakuwaje unalala m chafu? Je kwa wale waliozoea kulala bila kupiga mswaki au kuoga hawajapata la kujifunza hapa? Je wale wenye utamaduni wa kuyafanya haya hawana la kuwafundisha wasioyafanya?

            Binadamu tuna mazoea na mila tofauti na saa nyingine kinzani kiasi cha kuchekana na kuishia kujicheka bila kujua. Mfano, kuna jamii huko bara Asia ambayo huamini kuwa kuramba vidole ni kuonyesha kuwa chakula kilicholiwa ni kitamu! Ukila na kumaliza bila kuramba vidole wanakushangaa kama unavyowashangaa kwa kuramba vidole. Pia, huko huko, wapo wanaokula kwa kupwakia na wengine wakiongea. Ukila kimya, bila shaka watakushangaa kama utakavyowashangaa. 

        Pia, kuna mazoea mabaya zaidi kwa wanandoa kula chakula cha usiku (wakubwa mnatuelewa) kwa kupigishana makelele bila kujali watoto hata kama wapo chumba cha pili hasa kwenye jamii za kibinafsi za Magharibi. Wakati kwa Waafrika hili ni mwiko, kwa wenzetu hutushangaa inawezekanaje kula chakula cha usiku cha baba na mama bila kupigishana makelele. Nasi huwashangaa inakuwaje wapige makelele kama nguruwe kiasi cha kuharibu watoto wao.

 Kwa watu hasa wa Pwani, haya ni makufuru. Je wanapooana watu toka kwenye hizi jamii tofauti, kweli hawana la kujifunza na kufundisha? Inakuwaje mtu ule kama mbwa, kuramba vidole, au kupwakia kama fisi? Unaweza kuhoji.

Turejee kwenye ndoa kama darasa hata shule. Je wewe au mwenzako alishawahi kukutana na mazoea, mila, au tabia ambazo ni tofauti hata kinzani na za mwenzako. Je huwa mnafanya nini mnapojikuta kwenye hali kama hii? Kama hamjawahi, mkijikuta kwenye hali kama hii, mtafanya nini? Hapa hakuna jibu moja. La muhimu, ni wote wawili kuwa tayari kujifunza na kufundishana bila kila mmoja kushikilia lake ndiyo sahihi. Mfano, katika kisa cha kutopiga mswaki, kupiga mswaki wakati wa kulala ni bora kuliko kutofanya hivyo. 

       Pia, katika kisa cha kupwakia kama wanyama na kuongea wakati wa kula, kukaa kimya ni bora kuliko kutofanya hivyo. Hata hivyo, tuonye. Mazoea ni magumu kuyaacha hasa yanapokuwa sehemu ya makuzi na malezi ya binadamu.

Tumalize kwa kushauri kuwa, katika kutatua matatizo kama hayo, wanandoa wanapaswa kuwa flexible (hatuna Kiswahili chake). Wawe tayari kujifunza na kufundisha na si mara moja bali miaka yao yote.

Chanzo: Mwananchi jana.

Thursday 12 September 2024

Tumekuwa Mateka wa Watekaji


Hapo zamani kaya ikiwa kaya, tulizoea kusikia utekaji na uuaji wa watu kisiasa kwa majirani zetu. Majirani zetu wa kaskazini mashariki walisifika kwa mchezo huu mchafu uliofyatua vigogo wengi wa kisiasa wakiwamo mwaziri kabla ya wale wa Kaskazini magharibi kuchukua ukanda. Ni pale nduli alipompoka madaraka Oboto ambaye naye alimpoka madaraka kabaka tena kwa kumtumia nduli huyuhuyu.
        Sasa inavyoonekana ni zamu yetu. Zamani tukiitana ndugu. Kila fyatu alikuwa ndugu wa mafyatu wote zama za mzee Nchonga (RIP SANA Nguli). Baadaye alikuja mzee Ruxa (RIP SANA Mwamba) kabla ya kuja kwa mzee Ben Nkapa (RIP SANA BRO). Baada yah apo alikuja BoysIIMen, na baadaye Jiwe (RIP). Katika awamu zote tano, mambo ya mafyatu kutekwa na kufyatuliwa na mafyatu wasiojulikana yalianza zama za jiwe. Hapa ndipo ulipomzizi wa kadhia hii ya ajabu na aibu kwa kaya iliyosifika kwa udugu, upendo, usawa, na mshikamano tena vya kupigiwa mfano. 
        Pamoja na mazuri yake kivitu, jiwe hakufanikiwa kiutu pamoja na kujiita mtetezi wa mafyatu wanyonge. Ni bahati mbaya, pamoja na ukali wake, Jiwe aliondoka bila hata kumnyaka mmoja wa wale waliojulikana kama wasiojulikana ingawa walikuwa wakijulikana. Kama wanaharakati huru ambao hawakuwa huru bali udhuru walijulikana, iweje wauaji wasiojulikana wasijulikane kwa lisrikal lenye kila aina ya wataalamu wa uchunguzi na udukuzi.
        Sina haja ya kumlaumu marehemu. Cha mno, historia huwa haina huruma wala upendeleo. Huripoti kitu kama kilivyofanyika au kutokea. Kwa muktadha huu, sasa najikita kwenye jinai, uchafu, na unyama wa kutekana na kutoana roho kwa mambo ya kidunia kana kwamba kuna atayeishi milele. 
            Ni kama tumekubali kutekwa na kugeuka mateka wa watekaji wetu. Je hawa ni nani, wanatoka wapi, kwanini wanaua mafyatu hovyo, wanatumwa, wanajituma, na nani anawalea hawa maafriti nduli wakubwa? Je vyombo vyetu vya uhasama, sorry, usalama, navyo viko wapi? Ndata wetu ambao mara nyingi wemejionyesha kushabikia na kutumiwa na chata fulani nao wako wapi? Je tunaanza kuwa na utawala wa kimafia bila kujua? Je tutaendelea kukubali kuwa mateka wa wahuni wachache hata kama wanaowatuma wanaweza kuwa na maulaji? Maana haieleweki mafyatu wanyotolewe roho mchana kweupe na hakuna anayeshikwa. 
            Je lisrikal liko wapi? Je nalo linahusika? Kwanini wanaotekwa na kunyatuliwa roho ni wa chata kimoja kati ya utitiri wa vyata vya upingaji? Je huu ni mchezo mchafu wa siasa? Je mafyatu wa kaya hii wakimbilie wapi? Je kasi ya lisrikal walilochagua na kulipa kodi kila siku ni nini? Je tuanze kulichunguza? Kwani, likijichunguza, hakuna atakayepatikana wala kujulikana. Kwa taarifa zilizopo ni kwamba kaya ishapoteza takriban mafyatu 80. Je wafe wangapi ndo wahusika wastuke na kutenda haki hata kusitisha kadhia hii?  Maswali ni mengi kuliko majibu.
            Yeyote anayewatuma, sababu zozote zinazowasukuma, yeyote anayewalea anapaswa kujua kitu kimoja. Wanaweza kumgeuka naye akajikuta kwenye wahanga sawa na wahanga wengine. Kabla ya kupinduliwa, Obote hakudhani kuwa uhuni lingekuwa tatizo lake wala jambo ambalo lingemfyatua na kumtemesha ulaji. Hivyo, nasi, tunapaswa kuwa makini kama mafyatu wenye akili timamu na tunduizi wanaoisoma historia na kujifunza namna ya kutatua baadhi ya matatizo kama hili la utekaji wa kaya na mafyatu wake. 
Haiwezekani mafyatu wafyatuliwe kila uchao halafu tunaambwa mambo poa. Hivi hawa wahanga wa utekaji huu siku watakapokengeuka hali itakuwaje? Mafyatu si wanyama, wadudu wala mataahira. Ni viumbe wanaobadilika na wasiotabirika. Hata hawa waliobadirikiana na kugeuziana kibao ni mafyatu kama hawa wanaofyatuliwa na hawa wahuni.
         Kwa vile huwa nasikia kuwa rahis wetu ni msikivu, si vibaya kumpa ushauri wa bure kuwa hali hii isipokomeshwa, uwezekano wa kuwachochea mafyatu ambao wanajiona kama wahanga wasio na mtetezi wala pa kwenda, kuamua kufyatuka na kuwatafuta hao wanaowateka ili nao wawateke waonje ladha ya dawa yao. Nadhani wanachosahau hawa watekaji, watesaji, na wauaji ni kwamba wao ni mafyatu tena wenye familia, ndugu, jamaa ambao wanaweza kujikuta katika ulipizaji visasi mbali na kutaka kukomesha hii jinai na dhuluma.
Kwanini tunaweza kupata ndata wa kuzuia maandamano au kukamata ng’ombe kwenye mbuga za wanyama lakini hawapo wakukamata watekaji au nao wametekwa bila kujijua? Uadui hata ugomvi wa kisiasa humalizwa kisiasa na si kihuni na kikatili hivi. Hii ni aibu kwa kaya yote. Je tumeishiwa kiasi hiki hadi tunatekwa na watekaji kiasi cha kugeuka mateka wa wawatekaji!?
Tumalizie. Chonde chonde msiharibu sifa nzuri ya kaya yetu. Maulaji yana mwisho. Na isitoshe, hakuna anatayeyafaidi wala kuishi milele. Kuna haja ya kujirudi na kuachana na uhuni wakati huu ambapo mnaweza kuwapa sababu ya baadhi ya wahuni na maadui wasiotakia kaya yetu mema kuanzisha machafuko na vita uchwara kama kule Somaliya. Tunfahamiana hapa? Hivi ni asubuhi au usiku? 
Chanzo: Mwananchi jana.

Friday 6 September 2024

Tumechatwa Hadi Tumechakatika Haswa


Juzi, mtukufu doktari rahis alipofyatua na kuchakata, viherehere, vibwengo, na visebengo waso adabu wenye wivu waliawashwa midomo wakafyatua yasopaswa. Alipowaweka kando njemba wawili waliozoea kupayuka bila midomo kuwasiliana na bongo, wapo waliompongeza na kulaumu kwa kutumbua majipu, kujivua magamba, na kutua mizigo. Hakika, mafyatu si binadamu kama wajumbe! 
        Alipochakatua na kuchakata kwarejesha wakongwe wabee, vibabu tena chakatwa badala ya gen Z. walianza, mara “anatuletea Gen Zees makapi.” Jamani, mnataka afanye nini mfurahi au kuridhika? Akiteua wakweze, mnasema ufamilia na ufalme. Akinyamaza kama chura, mnasema mwoga!
            Ukizungukwa na jalala, kila kikufaacho ni uchafu tokana na kuwa nyenzo pekee jalalani. Jikumbusheni profedheha mwenye jina kama kabundi kadogo aliyechemolewa jalalani na aliyemfinyanga kisiasa. Ukitumia nyundo, kila tatizo ni msumari. Ukizoea kunyonga, yanini kuchinja?
            Mnafyatuka eti kazi sasa ni kuchakata na kuchakatua hata maiti. Kazi ya urahisi ni nini? Akisafiri, mnazoza. Afanye nini wakati urahisi ni uungu mtu unaompa madaraka yaso mipaka kufanya atakalo akasifiwa hata akikosea? Akirejesha vibabu, yawahusuni? Mwataka ateue wajukuu zake au wapingaji kama Looter kule kwa jirani? Kwani, hamuoni?
        Nawashangaa.  Mshindwe na waregee. Kitu gani siyo recycled? Mmesahau, uchakachuaji, sorry, uchaguzi uliopita uliochakata hawa mnaowaita recycled materials? Ebo! Nani, mara hii, kasahau mchakato wa bao la mkono? Je huku siyo kuchakata tena kisiasa ambako nyie huita uchakachuaji? Ni uchakataji kuanzia chini hadi juu, juu hadi chini na kila kitu kimechakatwa. Sera hazitoki majuu? Shopping na wachukuaji siyo majuu?
        Kwanini tumegeuka kaya ya uchakataji aka recycled kaya? Mosi, ni ukosefu wa nyenzo aka materials zifaazo. Jiulize. Kisiasa, maadili yamegeuka madili na siasa sasa ni sanaa na usanii bila kusahau misifa na usifiaji hadi njemba nzima zinampigia magoti mja utadhani Mungu.                         Tumeishiwa sera nini? Sifa zinageuka sera na sera zinageuka maudhi, uongozi umegeuka uongo, ukale umegeuzwa usasa na usasa ukale. Tunazalisha pamba. Tunavaa mitumba. Tunasomesha na kuzalisha mitumba. 
        Hizi ni zama za kujihudumia badala ya kuhudumu, na kutumikisha badala ya kutumikia. Haki na stahiki vimegeuzwa hisani, ukweli umegeuka uongo, ubangaizaji umegeuka kazi, haramu imehalalishwa na halali imeharamishwa. Akina Yero wamegeuzwa wakimbizi Kayani mwao. Kwani, hamuyaoni jamani? Mnasema ujanja kupata? Mwataka nifyatuke vipi mnielewe muache kulalama mfanye kweli?
        Pia, kijamii, ni kuchakata kwenda mbele. Jitu jeusi ja mkaa linatoja tojo (tattoos) nyeusi likiigiza watasha. Mingine mibwabwa na misagaji. Kama haitoshi, siku hizi, imbaba mizima inavaa hereni, vipuri, miregezo, kuonyesha ‘undaweya’ chafu bila aibu, kusuka na kutoboa masikio mbali na miziki recycled na wanamuziki walochakatwa kiubunifu waharibuo maadili nasi tukishuhudia kana kwamba haituhusu? Mwachakatuliwa na kuchakatwa bila chekeche. Mwacheza chakacha!
            Kiuchumi, zamani ulikuwapo uchumi si uchumiatumbo. Tulikuwa na wachumi si wachumaji, wawekezaji wamegeuka wachukuaji, watawaliwa wamegeuka watu waliwao, wafadhiliwa wamegeuka wafadhili. Wezi wanalinda fedha na mbwa kulinda nyama. Mnalalamika nini wakipiga njuluku na kutajirika mkageuzwa makapuku na walalamikaji wasiochukua hatua? Mnadhani kuna wafadhili watakuja kuwakomboa? Thubutu yenu!                             
Jikomboeni. Uchumi mmeugenisha. Mmegeuzwa manamba kwa kisingizio cha kutengeza vibarua muitavyo ajira. Kwanini kutegemea ajira? Kuweni wabunifu mjiajiri na kuwaajiri hao wageni wanaowaajiri? Imefikia mahali Afrika inakodisha ardhi kwa wageni kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wao kukwepa kukinunua kwa bei mbaya wakati inaagiza hata nyanya na mayai visa toka ughaibuni halafu inasema iko huru. Uhuru au udhuru?                                     Wanene  watanuaji wanatanua sirkal na mikanda wakati nyie mkiambwa mfunge mikanda. Mtakula lini au mwangoja muingie peponi ambako hamna uhakika mbali na kuingia bila midomo wala matumbo? Mla kala leo kesho kalani.
        Siku hizi, uchatakataji umevamia hata anga za kiroho na kugeuza uroho kuwa dili na dini. Zamani, tulikuwa na mashehe kwelikweli siyo mashehena waliosheheni uroho hadi wanauza mali za wakfu au kugeuka wapiga ramli na waganganjaa wa kienyeji. Msiseme nazusha. Kumbuka mwendazake alivyoshupalia kurejesha baadhi ya mali za baadhi ya wale ambao siwataji. Wamejaa wachungaji waliogeuka wachunaji kondoo waliopaswa kuwachunga. 
            Wanawatoza njuluku eti kuwapa huduma wakati ni hujuma tupu. Kwani hawapo? Hamkusikia zile kashfa za ngono? Hamuoni kuibuka utitiri wa manabii na mitume uchwara?             
    Zamani, dini ilikuwa huduma si hujuma. Siku hizi, imechakatwa nasi tukiangalia tu na kugeuzwa biashara ya mabilioni. Utapeli na mauzauza vinaiitwa miujiza wakati ni wizi itumiayo mijizi iliyojificha nyuma ya imani sawa na ile imani ya amani katikati ya vurugu, utekaji, ujambazi, upigaji njuluku za umma n.k. Kwani, hayapo? Nasi tumevamiwa.Tuna makanjanja wanaosaka bahasha badala ya habari wajaze mitumbo yao isiyotosheka.
            Nimalize. Muacheni bibie achape kazi, kutanua hasa usawa huu anapokwenda kusaka kura ya kula ili kuendelea kukamua. Mwenye wivu ajinyonge. Msitupigie kelele vinginevyo tutawasweka lupango kama akina Tunda Lishe aka lion na wenzake. Juzi, nilisikia akichangisha njuluku kutengeza gari lake. Kwani halikuwa na bima? Nimesemaje?
Chanzo: Mwananchi Jumatano juzi.


Sunday 1 September 2024

Hakuna Daktari, Mchungaji/Mganga wa Ndoa

Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na wanandoa kutojiamini na badala yake wakaamini miujiza au ushirikina. Hakuna muujiza kwenye ndoa zaidi ya wanandoa wenyewe. Hakuna ushirikina unaoweza kuimarisha ndoa. Wahenga walisema; hakuna dawa ya mapenzi. Kama ipo si nyingine ni uaminifu, upendo, utayari, usiri, uwajibikaji, matendo, na maneno mema baina ya wahusika. 
        Tumeweka ushirikina na ushauri pamoja kutokana na uzoefu wetu. Tunajua. Kuna wanandoa walioishiwa hadi kuamini kuwa maombi, tunguli, n.k. vinaweza kuokoa ndoa ambazo wameziua tokana na ujinga na upumbavu wao. Tangu tumeoana, hakuna kitu tulichojiepusha nacho kama kuweka mambo yetu ya ndani siyo nje tu ya nyumba yetu bali nje ya chumba chetu cha kulala ambayo ndiyo makao makuu ya ndoa yetu. 
        Haiingii mtu yeyote humo isipokuwa watoto wetu wachanga tu. Siri za humo hazitoki hata kwa viboko. Hivyo, unapoanza kuingiza mashoga kwenye chumba chako cha kulala na baadaye kwenye kitanda chako ujue unamtafuta na kumtengeneza mchawi au wachawi wa ndoa yako. Tusisitize mambo makuu yafuatayo:

            Mosi, ndoa yako ni siri yako binafsi asiyopaswa kujua mtu yeyote. Ndoa siyo gazeti wala kitabu ambacho unaweza kusoma na wenzako. Ndoa yako ni siri kuliko hata nguo zako za ndani, maana huwa unazinunua au wengine kuzianika zikaonekana. Ndo ani kama moyo wako. Anayeweza kuuona ni daktari wako pekee na Mungu aliyeuumba.

Pili, chumba chenu cha kulala ni sehemu ya siri asiyopaswa kuijua wala kuingia mtu yeyote isipokuwa wawili nyinyi. Hivyo, wale wanaowaruhusu mashoga au wasichana wao wa kazi kuingia kwenye chumba chao cha kulala ni makosa makubwa.

Tatu, matatizo yako ya ndoa yanapaswa kutatuliwa na wawili. Kwanini iwezekane kuyatengeneza mshindwe kuyatatua? Ushauri wa mashoga na marafiki hausadii. Hawajui thamani ya ndoa yako. Na lolote baya likitokea, wao hawatakuwapo. Kitanda usicholala hujui kunguni wake. Hapa lazima usiri uwepo na si usiri tu bali hata hofu na kutomwamini mtu yeyote. Hata inapotokea ukapata ushauri, lazima uupime kwa kuangalia thamani ya ndoa yako na si mawazo ya aliyekupa ushauri. Kupewa ushauri ni jambo moja na kulifanyia kazi ni jambo jingine.

Hakuna anayefungwa na ushauri wa mtu yeyote. Kupanga–––tujue–––ni kuchagua. Unapopanga au kuchagua, fanya hivyo vizuri ukijua wazi. Ndoa yako ni sawa na kaburi. Tunatoa mfano huu siyo kwa sababu ya kukutisha. Tunataka upate ujumbe kama ulivyokusudiwa. Hebu piga picha mtu anapokufa. Kuna mtu anaweza kumsaidia kukaa kwenye kaburi lake? Msaada pekee hapa ni kumchimbia kaburi na kumuingiza wakimuacha mhusika aingie na kuishi kwenye kaburi lake. Unaweza kuugua au kuhisi njaa na kupata msaada lakini si kwenye kaburi. Samahani kwa kutoa mfano wenye majonzi ingawa ndiyo hali halisi.

Kitu kingine wanachopaswa kufahamu wanandoa ni mategemeo au matarajio yao. Wengi wanapofunga ndoa huangalia upande mmoja yaani wa kufaidi. Wanasahau kuwa­­­–––kama ilivyo katika nyanja nyingine za maisha–––kila kitu lazima kiwe na majaribu na mitihani mbalimbali yenye changamoto juu ya kujifunza namna ya kutatua matatizo. Hivyo, unapoingia kwenye ndoa, lazima uangalie pande zote. Ndiyo maana baadhi ya dini na mila hufundisha kuwa ndoa ni kifungo ambamo mhusika asitegemee vinono tu hata machungu. Hata hivyo, ikitokea mitihani, dawa si kuachana wala kukimbiana. Kwani unaweza kumkimbia mjuzi ukajikuta uso kwa uso na mamba. Hii maana yake ni nini? 

    Ni kwamba mwanandoa mzuri unaweza kudhani ni wa mwenzako kwa sababu kitanda usicholalia hujui kunguni wake. Kila binadamu ana matatizo awe hata rais au msomi wa kiwango cha juu. Huu ndiyo ubinadamu tunaopaswa kuukubali na kuufanyia kazi si katika ndoa tu bali katika maisha yetu yote. Maisha ni safari ndefu yenye kona, mabonde, mito, milima, vikwazo na hata lift.

Ni bora kuhitimisha tukisema wazi. Pig aua. Jua. Hakuna Daktari, mchungaji, mganga, fundi wa ndoa wala mwalimu bali wanandoa wenyewe kuwa tayari kuilinda ndoa yao, kujifunza, kufundisha, kujielimisha, na kuelimishana. Tumeyaona. Tumeyapitia.

Chanzo: Mwananchi leo.