How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 2 February 2025

Mpumbavu aliyevunja ndoa akiamini anaihami


Kuna kisa cha mwanandoa Gilombo (si jinale) tulichoshuhudia.  Gilo hakujaliwa sura wala tabia nzuri. Alikuwa mzinzi wa kutisha aliyelazimisha ndoa kwa kijana handsome na mwenye nazo asiye na uzoefu. Alibahatika kupata mtoto wa kike katika ndoa ya kulazimisha iliyoduma miaka miwili tu.
            Baada ya kuishi na mumewe kwa mwaka mmoja na kulazimisha kubeba mimba bila ya makubaliano, jambo ambalo lililomstua muwe, Gilo aliamini mumewe bwege asiyeweza kustuka wala kushuku. Hivyo, mazabe yake yasingefumka. Taratibu, mambo yalianza kutifuka na kufumka. Mumewe alianza kumshuku kwa kila jambo. Mfano, kuna wanaume waliokuwa wakiwatembelea aliowatambulisha kama ndugu zake. Bahati mbaya, mmojawapo alikuwa akifahamika kwa rafiki wa mumewe waliyekutana JKT. Siku moja, Gilo akiwa ametembelewa na huyu ndugu yake ambaye pia alikuwa mshikaji wake jeshini, alifika rafiki wa mumewe aliyewajua wawili hawa.
            Mume aliporejea na kuwakuta wageni hawa, alimtambulisha ndugu mshikaji wa mkewe kama shemeji yake aliyekuwa amempa mtaji kuanzisha biashara. Rafiki yake alishangaa na kuchukia tokana na aliyojua. Hivyo, alishindwa kuvumilia. Wakati wakiagana, alimuomba rafiki yake awe na kifua amwambie jambo. Jamaa alipasua mbarika na kuweka kila kitu wazi. Baada ya kupita miezi kadhaa, jamaa mshikaji wa Gilo alirejea akitaka fedha zaidi toka kwa mumewe ambaye alimkatalia zamu hii. Baada ya mwizi wake kuondoka, alimbana mkewe aliyekiri kuwa na udugu na uhusiano wa kingono. Tangu siku hiyo, mapenzi yalitoweka.
            Kuona kitumbua kinaingia mchanga, Gilo alianza harakati za kuhami ndoa yake. Alikwenda kwa wachungaji kuomba ushauri na kuombewa. Mambo yalizidi kuwa mabaya. Mwishowe, aliamua kwenda kwa mganga wa kienyeji aliyemwambia kuwa alikuwa na nuksi na alikuwa amerogwa via vya uzazi na shangazi yake. Hivyo, alipaswa kutumia dawa kuingiza ukeni ili kutibu nuksi. Sharti kubwa alilopewa ni kutafuta mwanaume ambaye si mumewe ajipake dawa na kumuingilia mara moja tu. Kwa kutapatapa na upumbavu, Gilo alikubaliana na sharti. Tatizo, ni nani angempata ajipake hiyo ‘dawa?’
            Jibu lilikuwa rahisi. Alimwambia mganga wa kienyeji kuwa hana mtu. Mganga alimwambia kuwa kama angempa fedha, angefanya kazi hiyo. Walikubaliana na Gilo wakajifungia ndani wakafanya ngono. Baada ya kumaliza, mganga wa kienyeji aliongeza sharti jingine kuwa lazima wafanye ngono kwa wiki nzima kila jioni. Gilo alistuka lakini alikuwa ameishaingia mkenge. Alikataa katakata. Mganga kuona hivyo, aliamua kumtishia angemwambia mumewe. Gilo ilibidi akubali. Wakaendelea kufanya mapenzi. Kabla ya wiki kupita, mume alistuka na kuamua kumfuata mkewe pindipo alipoaga jioni anakwenda kwenye maombi. Kimyakimya alimfuata hadi akiingia nyumba ya kulala wageni na mganga. Alifanya harakaharaka akawafuma na kumuacha hapohapo bila hata kurusha ngumi wala tusi.
Katika kushuhudia na baadaye kudurusu sababu za kuvunjika kwa ndoa hii, tuligundua vitu kadhaa. Mosi, ndoa hailazimishwi. Pili, maisha ya kabla ya ndoa yanaaweza kuimarisha, kuyumbisha hata kuvunja ndoa. Tatu, kutokujiamini, ubabaishaji, kutafuta ushauri bila kufikiri na kutahadhari, na kuamini kila ushauri vinaweza kuvunja ndoa. Nne, kutafuta tatizo kwa kutapatapa ni hatari kwa ndoa. Wanadoa wanapaswa kuendana. Kwani, wawili hawa hwakuendana kwa sura na tabia. Japo hili si tatizo, licha ya kulazimisha ndoa, Gilo aligeuka ‘chuma ulete.’ Kwanza, baada ya kuhamia kwa kulazimisha ndoa, Gilo aliwasomba ndugu zake ukiachia kukmtoa fedha mumewe ili kuwatumia wazazi wake kwao. Pili, Gilo, licha ya kumficha mumewe ukweli kuhusiana na maisha yake yaliyosababisha alazimishe ndoa kwa, hakuwa muwazi juu ya maisha yake ya awali.
            Je unajifunza nini hapa? Mosi, ndoa inataka uaminifu na ukweli. Pili, siyo kila ushauri unafaa. Tatu, ndoa haina daktari wala mchungaji isipokuwa wanandoa wenyewe. Nne, hakuna siri ya milele. Tano, usiamini kila mtu na kila kitu. Sita, ndoa inataka kujiamini. Saba, waganga wa kienyeji na wachungaji matapeli ni maadui wakubwa wa ndoa. Nane, katika ndoa, wanawake wana maadui wengi kuliko wanaume. Tisa, mchawi au mlinzi wa ndoa yako ni wewe mwenyewe. Kumi, unapopta tatizo, tumia njia sahihi ukiwa umetulia kufikiri na kufanya utatifiti ukiepuka kufanya maamuzi kwa msongo wa mawazo na hofu.
Chanzo: Mwananchi leo.

Saturday, 25 January 2025

KATIKA NDOA, USIHUKUMU KABLA YA KUJIHUKUMU


Tutaanza na kisa ambacho tulishuhudia kwa ndugu yetu mmoja. Huyu bwana, kuna kipindi alichishwa kazi. Hivyo, alianza kuamka kila asubuhi akielekea mjini kusaka vibarua ili mkono uende kinywani. Mambo hayakwenda kama alivyotaka wala kupanga. Hivyo, ulipita muda bila kuwa na namna ya kujiingizia kipato. Hata hivyo, alifanikiwa kumtafutia mkewe kibarua kwa ndugu yake. Mama alifurahi kupata kibarua na kuingiza lau kipato. Hata hivyo, yule mama ambaye tunasema ni mpumbavu, alianza kumuona mumewe kama hamnazo na asiye na ujanja wa kuhangaika na kupata kipato.
         Siku moja alidamka, kama kawaida yake akijiandaa kwenda kwenye kituo cha daladala ili aende zake mjini kuchakalika. Kwa bahati mbaya, siku ile hakuwa hata na nauli. Hivyo, alimuomba mkewe nauli. Badala ya mama kumpa nauli, alimjibu “mwanamme mzima unaomba nauli kwa mkeo! Mwanaume gani suruali.” Kwa busara na upendo, yule bwana hakukasirika wala kujibu zaidi ya kuumia ndani na kufunika kombe mwanaharamu apite.
        Kwa vile tabia ile ilituudhi, tulimwita jamaa kando na kumpa nauli bila hata kumpa pole kwa kuhofia tungeamsha uchungu hata kumwaga mafuta kwenye moto. Pamoja na kumhifadhi ndugu yetu huyu, kile kitendo kilituudhi na kutufedhehesha. Cha mno, kile kitendo kilitupa somo kuwa, katika ndoa, kuna wanandoa wengine wanabomoa ndoa zao kwa mikono yao. 
        Badala ya mama kujiuliza angekuwa yeye angefanya nini, aliamua kujivua na kumvua mumewe nguo tena mbele ya watu. Katika hali hii, mume akipata fursa ya kutosha, je hawezi kulipiza kisasi kiasi cha kuanza unyanyasaji katika ndoa. Je hapa chanzo na wa kumlaumu zaidi ya mkewe ni nani japo naye, kama mume, anapaswa kupima mambo. Je ni wangapi wanatumia lugha chafu kama hizi dhidi ya wenzi wao? Je wanafaidikaje na tabia hii chafu?
        Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza. 
        Mosi, kupata na kukosa, yote ni majaliwa na aliye nacho leo anaweza asiwe nacho kesho na asiye nacho akawa nacho.
        Pili, kuna haja ya kuvumiliana hasa wanandoa wanapopata mitihani ya kimaisha ambayo ni mambo ya kawaida yanayoweza kuwajenga au kuwabomoa.
        Tatu, kupata si ujanja na kukosa siyo uzembe au ujinga. Kwanin watu wa namna hii hawahoji ni kwanini watu wengine wanaishi kwa muda mrefu wakati wengine wanaishi kwa muda mfupi?
Nne, upendo baina ya wanandoa unapaswa kuvuka vitu vidogo kama vile kipato, elimu, na mengine kama haya. Kwani, kila mmoja anaweza kuwa nayo au asiwe nayo. 
        Tuliwahi kudurusu kisa cha mwanandoa mmoja aliyesoma akaishia form four failure aliyejiona msomi sana kuliko mumewe ambaye hakumaliza hata la saba. Huyu mama toka familia maskini, alianzishiwa biashara na mumewe huyo huyo asiyesoma na kufikia hata kumilki biashara yake na gari.
         Baada ya kujiona kapata, alianza kumdharau mumewe hadi kufikia kumtamkia “wewe hukusoma.” Ajabu ya maajabu, wakati wanakubaliana kuoana, alijua fika kuwa mumewe alikuwa kaishia darasa na tano. Kwa waliosikia kisa hiki cha hovyo, walijiuliza ni kwanini hakumkataa alipomchumbia tokana na kutokuwa na elimu aliyotaka ijapokuwa naye hakuwa nayo? 
        Ukiunganisha kisa cha ‘mume suruali’ na cha ‘wewe hukusoma’ unagundua mambo mengi ambayo ni hatarishi na sumu katika ndoa.  Mfano, mwanandoa aliyemwambia mwenzie ni mume suruali, naye alikuwa katokea kwenye familia maskini. Je kwanini hakujiuliza kuwa hata baba yake alikuwa mume suruali na hata mama yake mke gauni? 
        Kwa yule aliyemwambia mume hakusoma, utakuta wazazi wake pia hawakuwa wamesoma ukiachia mbali kuwa hata naye hakuwa amesoma. Katika ndoa, epukeni tabia ya nyani kutoona nonihino lake. Epuka kuwa kama mbwa chihuahua (chiwawa) kiumbe mwenye kubweka sana asishambulie wala kujihami anapokabiliwa na adui. Kwenye ndoa, epuka kumhukumu mwenzio kabla ya kujihukumu.
        Kama mmejaliwa au mmoja wenu kajaliwa talanta fulani, zitumieni kwa upendo na usawa bila kudhalilishana, kunyanyasana, kutukanana, na kuvunjiana heshima.  Leo, unaweza kumuona mwenzio hafai wakati nawe hufai na kesho mkaachana ukajikuta umemkimbia mjuzi na kumkumbatia mamba. Hivyo, kabla ya kuhukumu au kutuhumu, fanya hivyo kwako mwenyewe kwanza. Hiyo ndiyo busara ya leo.
Chanzo: Mwananchi Jpili iliyopita.

Wednesday, 15 January 2025

Hamisheni mafisi, mafisadi au waanimo na si akina Yero


Kejaa enteipa inno? Jibuni  kasidai endama, ai, maata enyemali. Keje ninye eninno. Kwanza, nimshukuru mheshimiwa Rais kwa kutuliza joto la NrongonrongoHuwa nashangaa mafyatu wanavyofikiri kinyumenyume. Leo, nitafyatua kasheshe ya kuwaonea akina Yero sobai wanaohamishwa kwenye ardhi ya mababu zao utadhani waanimo toka Serengeti kwenda Burigi-Chato zama zile za Geitalite aka Gbadolite na sasa Kizimikadolite kwenye maonyesho ambako simba aliitwa Tunda Lishe. Inavyonekana, amependa na kulishobokea bila kujua kanaweza kuwa kamtego. Kama siyo, basi expect the unexpected and the unexpectable where the impossible will be possible and the possible impossible. Kwa uzoefu wangu wa kifyatu, hata wanyama wanapohamisha au kuwa relocated (kimakonde), hupelekwa kwenye mazingira sawa na yanayofanana na yale walimotolewa kuepuka kuwaua kisaikolojia na kuhatarisha maisha yao. Je wanyama wakishamaliza kushiriki maonyesho wanarejeshwa mbugani au ndo wanakitoa zao kuelekea ughaibuni kwenye zoos huko Du buy, Tailendi, n.k.? Kwanini kupeleka wanyama sehemu isiyo na wanyama badala ya kumotisha watalii kwenda mbugani kutalii kama kweli lengo ni kuvutia utalii? Kaya yetu si vibaya kusema, ni ajabu jipya duniani kwa tunavyoboronga mambo tukidhani tunajenga hata kwa kubomoa. Inakuwaje, mfano, ndata wanakuwa na kila zana za fujo na maangamizi lakini wagonjwa wanakosa ambulances? Nadhani wanaosababisha haya ndiyo wanafaa kuhamishwa kuelekea mkoa wa lupango ili wawapishe mafyatu wazalendo na weledi wachape mzigo au siyo?
            Nizame kwenye sekeseke na sheshe la akina Yero wa kule Nrongonrongo. Kwanza, mpaka sasa, hatujupewa sababu kuntu za kuwahamisha. Je hii ndiyo njia pekee iliyopo? Je tumechemsha bongo na kushindwa au kuishiwa majibu? Je tumejaribu njia nyingine zikashindikana na kwanini? Je kuna namna?
 Kuna fyatu mmoja alinitonya, sijui kama ni kweli au umbea kuwa wanahamishwa eti kupisha uwekezaji ambao mara zote ni upigaji!  Kwanini kuhangaika na kuhamisha mafyatu wasio na hatia ili kutengeneza njuluku badala ya kuhamisha hawa wanaopiga njuluku iliyokwisha tengenezwa kuliko hiyo ambayo bado? Ni kutumia commonsense badala ya uncommonsense
Kama haiwezekani tokana na unene wao basi, hamisha waanimo. Tunakosa ubunifu hadi kuzidiwa na wahalifu kama Chauda mpigaji ambaye ameng’ang’ania kwetu kwa kuogopa kurejeshwa kwao akasote!
        Turejee kwa akina Yero. Yaani unamtoa morani mbugani na kumpeleka pwani! Huku siyo kumdhalilisha na kutaka kumnyotoa roho taratibu mbali na kuua na kuzima utamanduni na mila zake? Mayero huwa hawali samaki kwa sababu hawawatofautishi na nyoka. Leo, mwawapeleka kwa akina waja leo waondoka leo ili iweje? Kwanini hamkuwapeleka Manyara lau wawe karibu na mazingira yao badala ya huko mlikowatupa ili waangamie taratibu? Mnafanya hivi kwa faida ya nani?
            Kama imeshindikana basi waombe majirani zetu wa Kenya wawapokee huko Kajiado na Oloitokot ambako, kama siyo wakoloni kuligawa bara la Afrika, ndiko ilipo nchi yao ya asili? Akina Yeor siyo kama akina shakaza wanaoweza kushamiri mahali popote tena bila kula cha mtu maana wao ni kama mbegha. Huwa hawali cha mtu na ndima zose wanagoshoa bila kinyongo wala mbwaiTate nane tate nane. Naanza kulikoroga! Anyways, nini kifanyike? Simpo. Hamisheni waanimo. Sababu zifuatazo zinaniaminsha wanene watakubaliana nami kutowahamisha akina Yero kupisha wachukuaji:
        Kwanza, ni mafyatu si wanyama na wanyama si mafyatu wala hawana hata uhusiano.
        Pili, ni wanakaya. Waanimo hawana uraia wowote. Leo, wako bongo. Kesho wako Kenya. Hawana fungamano wala uwezo wa kujua au kuamua wapi wasimamie. Wao wanafuata mlo.
        Tatu, ni wamiliki wa waanimo ambao lisrikal liliwakuta nao likawanyang’anya na kuwawekea masharti namna ya kuishi nao badala ya kujifunza toka kwao. Sasa, limenogewa. Linataka kuwang’oa kabisa tena si kwa faida yake bali wachukuaji waliopewa jina zuri la wawekezaji.
        Nne, wanalipa kodi japo waanimo nao wanaingiza madolari mengi tu. Hata hivyo, waanimo hawanunui wala kuuza. Hivyo, mchango wao ni mdogo ikilinganishwa na wahyuman.
        Tano, hawana udugu na waanimo japo wana uhusiano wa mamilioni ya miaka wakiishi pamoja kwa amani na furaha.
    Sita, walipigania uhuru na kukataa ukoloni wakati waanimo hawawezi kutofautisha kitu.
Kumi, tuage kiYero, Olesere Yero.

    Saba, waanimo siyo walalamishi na hawamilki chochote bali humilkiwa.
            Nane, wana haki ya kufaidi haki za binadamu ila si waanimo ingawa wana watetezi wa kimataifa wateteao waanimo kuliko mafyatu.
    Tisa, thamani yao ni kubwa kuliko waanimo ambao thamani yao inafahamika. Nani anafahamu thamani yangu au ya doktari maza?
Kumi, gharama ya kuhamisha waanimo ni ndogo kuliko mafyatu. Rejea jiwe alivyohamisha wanyama kwenda Burigi-Chato ambako hawajengewi majumba. Kwanini ,wasihamishiwe hawa wahayawani huko na kuachana na akina Yero?
    Kumi na moja, waanimo hawana historia na mali zisizohamishika wala kufidiwa kama vile makaburi, vilipozikwa vitovu na mengine kama hayo. 
    Kumi na mbili, nashauri bi mkubwa atumie mantiki aliyotumia kuenzi Kizimkwaja huku asiwafyatue akina Yero. Nao ni mafyatu kama yeye. Wana historia, hisia, na mapenzi na kwao kama alivyo yeye.
Chanzo: Mwananchi leo J'tano.

Uhuru na usiri ni siri za mafanikio ya ndoa


Ndoa inapaswa kuwa huru na isiyotegemea au kuingiliwa na watu wengine katika uendeshaji wenu. Mliapishwa wawili tu na si mia mbili. Hivyo, jukumu na wajibu wa kutunza kiapo chenu ni lenu. Si la watoto wenu, marafiki, wazazi, mashoga, na wengine hata muwapende, kuwathamini, na kuwaamini vipi. Ndoa ni kama sehemu zenu za siri au siri asiyopaswa  kujua yeyote isipokuwa wanandoa. Hivyo, mna jukumu la kuilinda, kuitunza, na kuiimarisha au kuiachia ibomoke tokana na kushindwa kutimiza wajibu wenu. Hakuna apaswaye kuziona au kuzihudumia siri na sehemu zenu za siri isipokuwa wanandoa wenyewe. Nani mpambavu huanika chupi zake hadharani?
        Binadamu tumeumbwa na kujipenda na kujipendelea kuliko wengine hata kama kufanya hivyo kunaweza kuwaudhi au kuwaumiza wengine. Hivyo, unapaswa kujua kuwa mafanikio yako ni yako siyo ya kuwasimulia wenzako. Kitanda usicholalia, hupaswi kujua kunguni wake. Kama ilivyo kwenye siri ya mtungi, muachie kata pekee ajue siri za mtungi. Unawambia wenzio habari na siri za mwenzi wako ili iweje? Unategemea nini? Je wakikuumiza utamlaumu mwenzio au mwenyewe? Japo mfano wa hapo juu mwenzi wa mmbea aliyewapa siri za mwenzi wake ana makosa, na mumewe pia ana makosa. Ukilinganisha makosa ya wawili, utagundua kuwa mama ana makosa makubwa kuliko mumewe ingawa wote wana makosa.
        Japo kuna kipindi mambo huzidi kiasi cha waliotanzwa kutafuta msaada. Katika ndoa, linapotokea tatizo, ni muhimu likashughulikiwa na wahusika peke yao tena kwa usiri. Ndiyo mana tunasema siri za ndani ziishie chumbani. Zisivushwe hata kuchungulia sebuleni. Kama ikizidi sana, basi wahusishe wazazi wenuwa pande zote. Wao, wana uzoefu na uchungu na ndoa na mafanikio yenu kama wazazi. Na hata mkiwahusisha, mpime  michango na ushauri wao. Maana, wao hawajui thamani na umuhimu wa ndoa yenu kama nyinyi wenyewe. Ajuaye thamani ya mkonga ni tembo aliyeubeba. Na ndoa ni mkonga wenu. Wengine wanaweza kuukata wakauuza mkauawa au kuumia.
        Wakati mkikumbana na mitihani katika ndoa na kutaka msaada au ushauri, mnapaswa kujua kuwa hao mnaowafuata nao wana changamoto, kasoro, na matatizo yao. Kama ikizidi sana, turudie na kusisitiza wahusisheni wazazi wa pande mbili japo nalo hili linataka utafiti na umakini vya hali ya juu. Hata hivyo, kuna angalizo. Kuna baadhi yetu wamezaliwa kwenye ndoa za mitala au zilizoharibika.             Hivyo, unapowahusisha wazazi, pia uzingatie ithibati, ubora, au udhaifu wa ndoa yao mbali na uwezo wao wa kujadili matatizo na kuyatafutia suluhu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ndoa yako ni yako na si yao kama ambavyo ndoa yao si yako bali yao. Mnapozoea kuwapelekea watu matatizo yenu, mnayazidisha na kuyafanya yawe magumu zaidi kuliko mkiyashughulikia wenyewe. Hii ni kutokana na namna mnavyoyaeleza kwao na namna wanavyoyaelewa au hata kutoyaelewa. 
Mlipoamua kufunga ndoa mlikuwa peke yenu na wengine walikuwa mashahidi tu. Mjue baada ya kukubaliana na kufunga ndoa, mlitoa taarifa kwao kama sehemu ya hitajio la kijamii na kisheria. Kwenye changamoto, matatizo, na migogoro ya ndoa, msiwahusishe hata wapambe au mashahidi wenu. Wanaweza wasiwe na utashi, uzoefu, hata nia njema nanyi.
        Mwisho, jikumbusheni. Ni ndoa ngapi zimevunjwa na mashahidi wake? Hakimu wa kwanza wa kushgulikia changamoto na matatizo ya ndoa ni wanandoa wenyewe na mahakama yao ni chumba cha kulala.
         Hivyo, ndoa inapaswa kuwa taasisi huru ambapo uhuru huu ulindwa kwa wivu na tahadhari kubwa. Tunaposema uhuru, tunamaanisha uhuru wa kutoingiliwa na yeyote. Hakuna apaswaye kuwa na uwezo wa kuamua lolote kwenye ndoa isipokuwa wanandoa wenyewe. Tutoe mfano. Mwanandoa mmoja mzembe na hatari kwa ndoa yake alizoea kuwapa marafiki zake siri za mwenzi wake. Moja ya siri alizotoa ilikuwa ni ukubwa wa maumbile yake na namna alivyojua shughuli. Katika hao marafiki, walikuwamo wakware waliokuwa wakimmezea mate mwenzi wake. Hivyo, kutotunza na kulinda siri za ndoa yake kuligeuka angamizi la ndoa yenyewe hasa wahusika walipokula njama kumuandamana mhusika na wakampata kirahisi.
Chanzo: Mwananchi, J'pili.


Wednesday, 8 January 2025

Mliomba, mnaomba, mtaomba mjue si jibu


Nashukuru. Nilimaliza mwaka uzuri. Nawatakieni mwaka mpya wenye heri wote wapenzi wangu na mafyatu wote. Niende kwenye inshu. Kuna mchezo hatari unaanza kufyatua mafyatu hadi baadhi yao wanawafyatua mafyatu waliokataa kufyatuka hadi wakafyatuliwa kirahisirahisi. 
        Kuna kaugonjwa ka kuombaomba na kukupokopa njuluku toka kwa wachina, wamanga, na watasha. Wapo wanaoomba baraka wanapokwenda kukopa! Huduma za kijamii, lazima mafyatu waombe. Wakizipata, wanasifia hata wale wanaotimiza wajibu wao. Kabla ya kula, kuna mafyatu wanaomba. Ila wakati wa kuanza kulima hawaombi!
         Kamchezo/kagonjwa kengine ni kuamini aukutemea miujiza feki na uchwara. Juzi nilisikia fyatu aliyekuwa amekwama kituo cha ngwarangwara kule Kawee akisema eti alitoka mikoani kwenda kwa mchunaji, sorry, mchungaji, habithi, sorry, nabii Dar aombewe amalize mgogoro wa kiwanja! Hii ni akili au utaahira?
            Tokana na kuazoeleka kamchezo ka kuombaomba na kuamini miujiza feki na uchwara, kuna wanjanja wachache wanaotaka kuwa karibu na wanene wa kisiasa ili wawafyatue mafyatu wanaokuja na gea ya kuombea kaya. Mfano, wanaomba mvua wakati wanaharibu mazingira wasijue suluhu ni kutunza mazingira. 
        Wanaomba amani katikati ya dhuluma, utekaji, na vurugu wakati suluhu ni kutenda haki na kupambana na ukapuku wa kutengenezwa na ufisadi. Wanaomba furaha wakati kila kitu ni karaha. Wanaomba utajiri bila kutaka kuchapa kazi na kutetea haki zao. 
        Wanaombea kaya badala ya kuiambia ukweli kuwa iendavyo sivyo! Nawaambieni. Mtaomba hata uchi, hayo mnayoomba hamtapata. Bwana God siyo njinga mjue. Kawapa uchumi mnaukalia halafu mnaendekeza kubomu na kukopa, na isirafu. Kawapa madini bwerere. Mnashuhudia yakivushwa kila uchao halafu mnakwenda kuomba hukohuko yapelekwako. Mafyatu hawachapi kazi. Wameshikilia ushirikina wa kuomba, halafu wanategemea waletewe maendeleo. Kivipi?
            Majizi manene yanafyatua njuluku ndefu. Yakifa tunaomba yaingie peponi. Mengine yanapiga soga makazini badala ya kuchapa kazi. kuna uzururaji na matumizi mabaya ya raslimali za kaya yanayofanywa na baadhi ya mafyatu wapaswao kuwafyatua wasifyatuliwe. Halafu eti mnategemea kaya itajirike. Vipi? 
        Acheni kujigeuza ombaomba bila sababu za msingi wala ulazima. Mnachohitaji si kuombewa bali kuambiwa ukweli. Hamhitaji dua na sala bali uadilifu na ukweli. Wanaowafyatua wakiwaaminisha wanaweza kuwaombea, wanahitaji kuombewa sana tu. Sasa mie siwaombei. Nawaambia. Mnajichelewesha kwa ushirikina wenu mnaoita imani.
            Waliobukua historia wanajua. Walipokuja watasha na vitabu vyao vya kuomba, walituambia tufumbe macho tuombe. Tulipoyafumbua, tulijikuta wametufyatua kwa kutupa vitabu wakafyatua ardhi na mali zetu. Hawa wanaotufundisha kuomba kwa kila kitu, kwao hawaombi. Walituletea ukoloni na utumwa hivi hivi tokana na ujinga na uzwazwa wetu. Mnadhani akina Mkwawa, Mirambo, Nyungu ya Mawe, na Mchonga wangeomba, mngekuwa huru leo?
            Hata kama kuomba kunalipa, si kwa wale wanaoombewa bali wanawaombea. Hamjaona biashara ya neno na miujiza vilivyogeuka dili? Badala ya kujihangaisha na kuchapa kazi, waombaji wanawaibia mazwazwa waliokata tamaa wanaoamini miujiza uchwara. Japo wanaiba kihalali, wizi ni wizi tatizo ni kuufumbia macho na kuubariki tokana na ugonjwa wa kuomba na ushirikina. 
        Jitu linaanza kijikanisa uchwara tena kwenye banda la tope. Punde si punde linaangusha mahekalu. Ukiuliza miujiza gani, unaambiwa neema za God. Mingine inatuhumiwa kuuza bwibwi au kusaidia wafanyabiashara wakwepa kodi kupitisha bidhaa bila kulipa kodi kwa sababu dini zimesamehewa. Huu nao ni udhaifu wa kimfumo. Mnawasamehe kulipa kodi, kwani, nyinyi ndo mliwalazimisha wafanya biashara ya kuuza neno? Au ni kwa vile mmerithi tabia hii ambapo wakoloni walizawadia dini kodi kwa sababu zilizowasaidia kututawala kirahisi baada ya kutupeleleza na kutoa siri zetu kwa wakoloni? 
        Kwa mujibu wa Madison Trust Company, Kanisa la Roma linashikilia nafasi ya kwanza kuwa na ardhi kuliko taasisi yeyote duniani. Lina heka zipatazo 177,000,000. Kwa kulinganisha, ukubwa wa ardhi inayomilkiwa na Vatican, ni kubwa kuliko taifa la Ufaransa ambalo lina ukubwa wa heka 166, 757,337.  Ni zaidi ya nusu ya eneo la Tanzania yenye ukubwa wa heka 234,108,380. 
        Kuonyesha mnyororo na ukoloni, familia ya kifalme ya Uingereza nayo inaongoza kwa kuwa na hekali 6,600,000,000. Kinachostua, ni kwamba mamilioni yote ya ardhi yanayomilkiwa na wakoloni hawa, licha ya kuingizia mabilioni ya dola, yalinyakuliwa bila kulipa chochote hasa kwa bara la Afrika.
            Kwa waliosoma historia na kuielewa wanajua namna wamisionari walifyotufyatua. Walitwambia tutubu dhambi halafu wakajua udhaifu wetu na kuwapa taarifa mataifa ya kikoloni yaliyowatuma ikawa rahisi kututawala. Mbali na hili, ukiangalia namna makanisa hasa ya Kirumi yalivyo na ardhi chekwa, unagundua kuwa hakuna kitu walifanya kama kunyakua ardhi.
            Tumalizie. Mliomba, mnaomba, mtaomba ila mjue mnakwepa tatizo kwa kutafuta suluhu ya tatizo lisolokuwapo. Mtaomba hata uchi. Matatizo yenu yatabaki palepale na sanasana yataongezeka. Kwa wanaoipenda kaya na wenye kutaka kuisaidia, waiambie ukweli badala ya kupoteza muda na kuomba. Hakuna kaya iliyowahi kujengwa kwa maombi.
Chanzo: Mwananchi leo J'tano.


Tuesday, 7 January 2025

Udhaifu katika ndoa ni sehemu ya ndoa


Kwanza, kila binadamu ana ubora na udhaifu hata awe mzuri au mbaya kiasi gani. Hivyo, wanandoa wanaposhughulikia ubora au udhaifu wao, wanapaswa kukumbuka kuwa wote ni binadamu wenye mapungufu. Unaweza kuwa msomi mkubwa tu, tajiri, mwelewa si kawaida, mkarimu hata katili vipi, bado una ubora na udhaifu wako. Hivyo, tukubali na tujue haya yanatuhusu wote. Hivyo, kuwa au kuonyesha udhaifu katika ndoa, sawa na maisha, ni jambo la kawaida. Kisicho cha kawaida ni namna ya kuukubali, kuurekebisha, au kuupunguza udhaifu huku wahusika wakijitahidi kuujua, kuutumia ubora wao huku wakijitahidi wawezavyo, kuishi na madhaifu yao.

            Pili, udhaifu mwingine ima unaweza kuwa ubora au kuchochea ubora hasa wahusika wanapoamua kuushughulikia. Hata hivyo, tukubaliane. Kuna udhaifu usiokubalika hasa unapogeuka donda ndugu. Kwa upande wa ubora, hauna tatizo katika ndoa. Kwani, unaweza kutumika kama kichocheo na nyenzo ya mafanikio ya ndoa. Tutatoa mifano. Ni wanandoa wangapi wana wenzi wakoromao walalapo? Je hufanya nini kupambana na kurekebisha udhaifu huu? Ni wangapi wana udhaifu wa kutosikiliza au kuwahukumu wenzao bila kuwasiliza? Je udhaifu huu hauna tiba? Ipo tiba. Kama ukigundua au mkigundua kuwa kuna tatizo hili, kwanza, ni kuliweka wazi kwa lugha na namna nzuri inayojenga na siyo kubomoa. Badala ya kuitana wabishi na wasiojali, elezaneni hisia zenu kwa ukweli na uwazi kuhusiana na tatizo hili. Kama mmojawapo ana tatizo la kutosikiliza, anapaswa kujifunza namna ya kumsikiliza mwenzake.
            Kila mnapoongea au kusemezana, mwishoni, ulizaneni kama mmesikilizana na kuelewana. Maana, kuna kusikiliza ilimradi kumridhisha mwenzako wakati ukweli ni kwamba unajua unafanya hivyo kumlidhisha wala si kumsikiliza. Kuna kusikiliza bila kuelewa ukutoa michango isiyotegemewa wala kuleta maana. Hivyo, hatua ya kwanza ni kuujua udhaifu. Hatua ya pili ni kuukubali na kuutafutia suluhu. Hatua ya tatu ni kufanya mazoezi ya kutatua tatizo. Na mwisho, ni kutathmiana kwa kuulizana na kutathminiana pasina kuridhishana au kudanganyana. 
        Hili halihitaji shahada. Kwani, binadamu yeyote amejaliwa uwezo wa kisaikolojia wa kumuelewa, japo wakati mwingine anaweza asimuelewe mwenzake kulingana na namna alivyopokea anachopokea. Hatutazama kwenye saikolojia. Tumetumia mfano wa kusikiliza na kusikilizana kuwakilisha mifano mingine mingi. Mfano, mnaombana ushauri? Je huu ushauri mnaufanyia kazi au kuudharau? Je mnapoombwa au kuomba ushauri, mnaupokea na kuufanyia kazi? Maswali haya hayawezi kupatikana au hata kufikirika kama mtakiuka hatua ya kwanza ya kukubali ubora na udhaifu vyenu. Pili, lazima mjue kuwa mna uwezo na welewa tofauti wa mambo. Wanandoa wengi wanaharibiwa na kidudu kiitwacho kujihami. Linapotokea tatizo au kutoelewana, kinga ya kwanza ni kuepuka kujihami. Badala yake, mjitahidi kuelewa tatizo. Kama mna au mmojawapo ana wasiwasi wa kutoeleweka au kueleweka vibaya, amuulize mwenzake kama amemuelewa na amemuelewaje.
            Baada ya kuomba maelezo, mhusika awe tayari kusikiliza maelezo, utetezi, au welewa wa mwenzake. Mruhusu aseme bila kuingilia ili apate fursa ya kujieleza eleweke nawe umewelewe. Kama bado kuna kutoelewa/kueleweka au hofu ya kutoeleweka, si vibaya kuuliza upya ili kupata maelezo ya kina ili muweze kuelewa tatizo na kulisuluhusha. Hapa, kuna ubora au udhaifu kimawasiliano. Katika maisha, mawasiliano ni muhimu na hayaepukiki. Si kila mawasiliano ni mawasiliano. Hapa, tunamaanisha mawasiliano chanya si hasi. Mfano, mkisikilizana, kuheshimiana, hata kudharauliana, mnakuwa mnawasiliana ingawa matokeo yake yanaweza kukinzana hata kutofautiana. 
        Kwa vile nafasi haitoshi, tungetaka kumalizia kwa kuwapa nyenzo nyingine. Jengeni lugha maalumu ya mawasiliano. Wana ndoa karibu wote wana aina fulani ya lugha hata mawasiliano ambayo kwa wasiohusika ni vigumu kuielewa. Kadhalika, hata namna yao ya kuwasiliana ni tofauti na ya pekee kulingana wanawasiliana vizuri au vibaya na kwa muda mrefu. 
    Hakika, kila mtu ana ubora na udhaifu. La muhimu ni kutafuta na kuvijua vitu hivi na kuvifanyia kazi. Tunaishi mara moja. Kila mtu sawa na ndoa, ana udhaifu. Hata njiwa wana udhaifu pamoja na kusifika kwa mapenzi yao kemkem.
Chanzo: Mwananchi, J'pili.

Wednesday, 1 January 2025

Sera yangu ni unyigu unyuki na usiafu


 Nadhani mmemaliza mwaka kwa kushuhudia wenzangu kwenye vyama vya siasia wakimenyana kugombea ulaji. Kwenye chama chetu cha mafyatu na si cha siasa, huwa hatugombea ulaji. Ukishawaingiza laini mafyatu na kuwapumbaza, unaula kwa vipindi vibee. Baada ya hapo unafunga virago na kutokomea kwenye ustaafu utake usitake. Kama ulikuwa umeona mbali, unaanda kitegemezi au rafiki yako kuendelea kuwa kwenye maulaji ili kulinda ulaji wako, familia yako, na maswahiba zako.

            Kwa vile mwakani ni msimu wa uchafuzi, sorry, uchakachuaji, sorry, uchaguzi mkubwa, nitatia timu kimakwelini na kinomi ili nishike dola na kutengeza midola tena bila kutoa jasho au vipi? Usicheze na dola. Unashika dola, kutengeneza, na kupiga midola kama huna akili nzuri. Lazima kieleweke. Niitwe mheshimiwa hata kama muishiwa. Niitwe mtukufu hata kama mtukutu. Nani asiyependa kuwa juu ya kila kitu hata sharia au asiyependa misifa hata asiyostahiki, na kunyenyekewa na kupendwa hata kama wanaofanya hivyo nyoyo zinawacheketa na kutamani nawe wawe wateule kama wewe? Nani asiyependa ujiko kama huu tena yeye, familia, marafiki, hata waramba manonihino? Unene wa kaya ni sawa na uungu nguru mbili ambapo mhusika hawezi kutenda kosa lolote kisheria hata kama kimakwelini ni mkosefu kama mafyatu wengine. Nani asiyependa ukuu wa kimungu na ulaji wa dezo yeye na ukoo na maswahiba zake? Mshaambwa. Mali ya umma huwa haiumi hata ukiila au kuiuma. Nami, familia, na marafiki tunataka kuuma mali ya umma tena kwa mikono na miguu na siyo kwa uma na vijiko. Kwani hatuwaoni wanaokula na kubukanya wakati mafyatu wakifyatuliwa na njaa na utapiamlo?

            Kwa vile kupewa kura ya kula kunahitaji sera na ushawishi hata usanii, somewhat, nami naleta sera zangu tukufu za kuwakomboa mafyatu kwenye ufyatuliwaji ili wajifunze ufyatuzi na kufyatua wale ambao wameshindwa kuwafyatua. Sera zangu, licha ya kuwafundisha mafyatu ufyatuzi, zinalenga kuhakikisha kuwa hakuna anayemnyonya au kumfyatua mwenzake kama ilivyo kwenye usawa huu wa vurugu. Zilenga kuhakikisha kuwa kila fyatu anakuwa na uhakika wa kufyatua milo kumi kwa siku. Hivyo, rasmi, naleta sera zangu kwa mafyatu ili wazichunguze na kuzidurusu ili wanipe kura ya kula tule pamoja badala ya kuwala wao kama ilivyo.

            Kiurahisi, sera yangu kuu itakuwa UUU yaani, Unyigu, Unyuki, na Usiafu. Kwa wanaojua ukali na unoko wa wadudu hawa, watakubaliana nami kuwa––––ninapanga kutenda kama wao––––sitaruhusu ujambazi uchwara wa kufyatuana ili kuneemesha wachache na kuacha mafyatu wengi wakifyatuliwa na matatizo yanayoweza kuzuilika. Kwa kutumia unyuki, nitatengeneza asali na kuhakikisha kila mtu anaramba asali. Kwa kutumia manyigu, nyuki, na siafu, nitahakikisha fyatu wote wanalindwa na kuwa salama. Kwanza, hawa jamaa hawahitaji mshahara wala hawaombi kitu kidogo. Pili, ni waaminifu. Wako tayari kufa na adui kuliko kumgwaya au kushirikiana naye kufanya hujuma. Si rahisi kuwateka wala kuwaletea mambo ya kijingajinga. Hawa jamaa wakianza ulinzi wa kaya, mambo ya kuteka na kutekana yatabaki historia kama nitachaguliwa na kushika dola. Mpaka hapa, sera yangu ya UUU si inapendeza?

 Nimesikia mafyatu wengi wakilalamikia uchawa, ufunza, ukiroboto, na ukunguni. Mie sitafuga wadudu zaidi ya kuwafyatua. Ili kuondoa chawa, kwanza, nitasafisha kaya na kuhakikisha kuwa kila fyatu anakuwa msafi kimwili, kiroho, na kimaadili kuanzia wanene, wanono, hadi wanuni. Kwa kusafisha kaya, nitahakikisha kila fyatu hata wanyama anatendewa haki vilivyo. Hivyo, hatua ya kwanza ya UUU ni kuhakikisha uchafu wote, uwe wa kimwili au kiroho, kimaadili au kitaaluma, vinakomeshwa mara moja. Kama manyigu, nyuki au siafu wafyatuavyo maadui au yeyote anayewachoza, nami nitatumia UUU kutenda zaidi ya hawa jamaa mara mia.

            Kwanza, chini ya UUU, nitaunda sirkal ndogo yenye mafyatu wasafi kimaadili  hata kitaalumana si wapiga madili wala wenye tabia za kunyonyana kama chawa. Nitateua mafyatu wakali kama manyingu, nyuki, na siafu ili tutumie UUU kuwakomboa mafyatu toka kwenye kongwa zinazofanya walalamike bila majibu. Nitapambana na udokozi, ujambazi, wizi, upigaji, na kila aina ya jinai. Nitafanya kile ambacho wanyakyusa huita lifestyle audit ambapo, kila mwaka, kila fyatu anajaza taarifa za mapato na matumizi yake ili kubaini wanaofyatua mali na njuluku za mafyatu. Majambazi na vidokozi waliozoea kulala maskini na kuamka wakwasi nitawanyonga sawa na mafisi na mafisadi wa mali za mafyatu.

            Pili, kama walivyo wadudu wangu jasiri na wapendwa, nitahakikisha kila fyatu anachapa  kazi kama mdudu ili ale na asiyechapa kazi atakula mafi yake kkkkk.

            Kwa vile huu ni utambulisho, mengi mtayasikia nitakaposimama majukwaani kuanza kumwaga sera na kutetea UUU. Hivyo, leo sitaki niandike mengi kwa vile naenda kuandaa rasimu rasmi tayari kuwania urahis ili niwafyatue, sorry, niwatumie, sorry, niwatumikie mafyatu.

Chanzo: Mwananchi leo.