The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 26 November 2025

Rasmi natangaza Ufalme wa Fyatuland


Kuanzia sasa, Fyatuland si jamhuri tena. Ni ufalme wa Fyatu Mfyatuaji awafyatuaye mafyatu atakavyo wasifyatuke wakamfyatua. Kuwafyatua vilivyo, juzi niliwafyatua mafyatu mkenge. Walinipigia kelele wanataka domoghasia aka demokrasia. Sikusita. Kwangu, hii ilikuwa fursa ya kuwafyatua vilivyo tena bila aibu wala huruma. Niliitisha uchaguzi ambao wapinzani wangu waliuita uchafuzi. Nilishangaa. Nani alimchafua nani wakati nilichofanya ni kufyatua? Ajabu, wengi wanaolalamika na kupiga zegele ni wale waliosusa sisi tukachukua na kuweka mwaa. Sasa twala. Viroho vinawauma kwa ngoa na wivu. Mshindwe kama mlivyoshindwa kwenye uchaguzi kumbaffuni kabisa. Kuanzia sasa, hakuna uchaguzi. Sitaki presha.

            Juzi, nilisikia mafyatu wakizoza na kuzodoa kuwa hakuna haki! Ebo! Nani kawafyatua mkenge na kuwadanganya? Guniani hakuna haki. Ukitaka haki, nenda kaichukue ilivyo. Nani kakwambia haki inaombwa? Haki huwa haiombwi bali kupokwa mafyatu wangu.
            Mafyatu bila kujua nitawafyatua, si waliingia mkenge nikawafyatua kwa kushinda kwa aslimia 1000. Ngoja walalamike wengine wakitishia kufyatuka na kunifyatua. Nami sikujivunga. Niliwafyatulia mbali viherehere waliojitoa ufahamau. Niliamrisha migambo yangu kumfyatua yeyote ajitieaye kunihoji au kunipinga wakati sihojiwi wala sipingwi. Wacha mafyatu waipate. We! Walifyatuliwa kwa mamia hadi wakatia akili. Natangaza rasmi. Kwanza, sichezewi. Pili, sijali. Tatu, kuwakomesha na kuwaonyesha kuwa mie sifyatuliwi, natangaza ufalme. Mambo ya demokrasia naona yanatuletea ghasia bila sababu. Tangu lini eti vitoto vilivyofyatuliwa jana vinahoji ulaji na unene wa wanene wakati vyenyewe si vinene? Vitanenaje na nini wakati vyenyewe si vinene? Sijui kwanini havielewi. Mshaambwa vitoi ni taifa la kesho. Ila siku hizi vinasema kuwa vyenyewe ni taifa la leo, kesho, na kesho kutwa! Mnataka mibuyu tule polishi? Vingine vinahoji hata uteuzi wangu? Vinalalamika eti nateua vitegemezi vyangu na shahiba yangu. Ebo!
            Kwa kuhofia ufyatu wa mafyatu, natangaza ufamilia, sorry, ufalme ili kuwa na uhakika kwa kuula na kufyatua bila bughudha. Hivyo basi, kuanzia sasa, sirkal yangu itakuwa ya kifalme ambapo ni vitegemezi vyangu, wake au waume zao ndiyo watakaounda lisirkal la mafyatu. Pia, nitateua vitegemezi vya washikaji wangu ili kuondoa wasi wasi wa kufyatuliwa nikajikuta pakanga bila sababu. Kwani ni kosa kutangaza ufalme wa ukoo wa kifalme hata kama ni kwa mlango wa nyuma? Kuanzia sasa, mtoi wangu Moja aka Wanune kwa kitasha, atakuwa waziri kwenye sirkal pamoja na hubby wake Moha we! Koma. Namaanisha Modicai Nchengeta ili kulinda ulaji wa familia ya kifalme. Hii ni sayansi ya siasa ya kisasa alonifunza dugu yangu kaka Joe Mseventy. Kama surname yako ni ya kichovu, unataka nani akuteue na ili iweje? Jamani, ngojeni zamu yenyu. Kutesa mshaambwa ni kwa zamu. Jamani, Nadhani watasha wa Ushoto mtanisamehe msije niambia mani ja mwenye
            Kama kwa Joji Kichaka Tarampu ameteua vitegemezi, wakwe, na maswahiba zake, kosa langu liko wapi? Mbona kule Equtorial Guinea dingi ni prezo na kitegemezi chake ni makamu wake? Kwanini kwangu iwe nongwa wakati siku hizi mambo ni kula kifamilia? Kwa wasiojua mantiki ya kufyatua niliyofyatua, kama daktari mwenye shahada kali sana, nataka kuonyesha kuwa demokrasia ya kitasha haina nafasi hapa. Huku ndiko kujikomboa kisiasa kusikokubaliana na kujikomba. Kufyatua zaidi, kuanzia sasa, hakuna kukopa wala kubomu. Tutakula njuluku za hapa hapa liwalo na liwe.
            Ili kutowaacha patupu maswahiba zangu, Mamadou kitegemezi cha Thubutu Kombania kitakuwa kwenye sirkal yangu pamoja na Riziki kitegemezi cha rafiki yangu yule Kiwete nacho kinaula. Kuwaudhi na kukomesha kidomodomo na ushakunaku vya mashakunaku na mashambenga, ninapanua sirkal yangu ambayo lazima waikubali watake wasitake wafyatuke wasifyatuke. Mie kisiasa ni alpha na omega. Ukijitia kufyatuka, nakumega na kukufyatua kama siyo kukuteka, kukupoteza, na kukunyotoa roho. Msinijaribu wala kunitania. Sijaribiwi, kutania, wala kutaniwa.
            Jambo jingine, ili kuhakikisha kila mshikaji anafyatua, natangaza kupanua sirkal yangu. Najua wanoko watazoza. Sasa bila sirkal kuwa kubwa ukubwa utakuwa na maana gani? Kwanini mnahangaishwa na ukubwa wa sirkal kana kwamba hakuna njuluku za kuiendesha? Hapa lazima niongeze kodi ili kuongeza mapato ya sirkal ya kuwawezesha washikaji zangu nami kujinomi kinomi au siyo? Nitatengeza nafasi kwa ajili ya maswahiba zangu na maswahiba zao. Nitahakikisha kila mshikaji anapata pa kushika ili tule kwa kujinafasi. Mwenye wivu si ajinyonge tu. Nani aliwambia mfyatuliwe kwenye familia maskini zisizojua kushika patamu na kula utamu? Utamu si wa kila fyatu. Una wenyewe na wenyewe ni sisi. Si mnisifie kidogo jamanini.
            Nimalizie kwa onyo kali. Kuanzia leo, hakuna fyatu anaruhusiwa kuhoji, kukosoa, kupinga, kulalamika, kulaani bali kusifia. Atakayekaidi amri hii ya kifalme, ajue. Atakuwa anatenda uhaini. Na adhabu yake mnaijua. Hivyo, kaeni chonjo, saa mbaya. Kumbe naweweseka usingizini. Ukisoma hii puuzia ni ndoto tu.
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

No comments: