Nadhani mmemaliza mwaka kwa kushuhudia wenzangu kwenye vyama vya siasia wakimenyana kugombea ulaji. Kwenye chama chetu cha mafyatu na si cha siasa, huwa hatugombea ulaji. Ukishawaingiza laini mafyatu na kuwapumbaza, unaula kwa vipindi vibee. Baada ya hapo unafunga virago na kutokomea kwenye ustaafu utake usitake. Kama ulikuwa umeona mbali, unaanda kitegemezi au rafiki yako kuendelea kuwa kwenye maulaji ili kulinda ulaji wako, familia yako, na maswahiba zako.
Kwa vile mwakani ni msimu wa uchafuzi, sorry, uchakachuaji, sorry, uchaguzi mkubwa, nitatia timu kimakwelini na kinomi ili nishike dola na kutengeza midola tena bila kutoa jasho au vipi? Usicheze na dola. Unashika dola, kutengeneza, na kupiga midola kama huna akili nzuri. Lazima kieleweke. Niitwe mheshimiwa hata kama muishiwa. Niitwe mtukufu hata kama mtukutu. Nani asiyependa kuwa juu ya kila kitu hata sharia au asiyependa misifa hata asiyostahiki, na kunyenyekewa na kupendwa hata kama wanaofanya hivyo nyoyo zinawacheketa na kutamani nawe wawe wateule kama wewe? Nani asiyependa ujiko kama huu tena yeye, familia, marafiki, hata waramba manonihino? Unene wa kaya ni sawa na uungu nguru mbili ambapo mhusika hawezi kutenda kosa lolote kisheria hata kama kimakwelini ni mkosefu kama mafyatu wengine. Nani asiyependa ukuu wa kimungu na ulaji wa dezo yeye na ukoo na maswahiba zake? Mshaambwa. Mali ya umma huwa haiumi hata ukiila au kuiuma. Nami, familia, na marafiki tunataka kuuma mali ya umma tena kwa mikono na miguu na siyo kwa uma na vijiko. Kwani hatuwaoni wanaokula na kubukanya wakati mafyatu wakifyatuliwa na njaa na utapiamlo?
Kwa vile kupewa kura ya kula kunahitaji sera na ushawishi hata usanii, somewhat, nami naleta sera zangu tukufu za kuwakomboa mafyatu kwenye ufyatuliwaji ili wajifunze ufyatuzi na kufyatua wale ambao wameshindwa kuwafyatua. Sera zangu, licha ya kuwafundisha mafyatu ufyatuzi, zinalenga kuhakikisha kuwa hakuna anayemnyonya au kumfyatua mwenzake kama ilivyo kwenye usawa huu wa vurugu. Zilenga kuhakikisha kuwa kila fyatu anakuwa na uhakika wa kufyatua milo kumi kwa siku. Hivyo, rasmi, naleta sera zangu kwa mafyatu ili wazichunguze na kuzidurusu ili wanipe kura ya kula tule pamoja badala ya kuwala wao kama ilivyo.
Kiurahisi, sera yangu kuu itakuwa UUU yaani, Unyigu, Unyuki, na Usiafu. Kwa wanaojua ukali na unoko wa wadudu hawa, watakubaliana nami kuwa––––ninapanga kutenda kama wao––––sitaruhusu ujambazi uchwara wa kufyatuana ili kuneemesha wachache na kuacha mafyatu wengi wakifyatuliwa na matatizo yanayoweza kuzuilika. Kwa kutumia unyuki, nitatengeneza asali na kuhakikisha kila mtu anaramba asali. Kwa kutumia manyigu, nyuki, na siafu, nitahakikisha fyatu wote wanalindwa na kuwa salama. Kwanza, hawa jamaa hawahitaji mshahara wala hawaombi kitu kidogo. Pili, ni waaminifu. Wako tayari kufa na adui kuliko kumgwaya au kushirikiana naye kufanya hujuma. Si rahisi kuwateka wala kuwaletea mambo ya kijingajinga. Hawa jamaa wakianza ulinzi wa kaya, mambo ya kuteka na kutekana yatabaki historia kama nitachaguliwa na kushika dola. Mpaka hapa, sera yangu ya UUU si inapendeza?
Nimesikia mafyatu wengi wakilalamikia uchawa, ufunza, ukiroboto, na ukunguni. Mie sitafuga wadudu zaidi ya kuwafyatua. Ili kuondoa chawa, kwanza, nitasafisha kaya na kuhakikisha kuwa kila fyatu anakuwa msafi kimwili, kiroho, na kimaadili kuanzia wanene, wanono, hadi wanuni. Kwa kusafisha kaya, nitahakikisha kila fyatu hata wanyama anatendewa haki vilivyo. Hivyo, hatua ya kwanza ya UUU ni kuhakikisha uchafu wote, uwe wa kimwili au kiroho, kimaadili au kitaaluma, vinakomeshwa mara moja. Kama manyigu, nyuki au siafu wafyatuavyo maadui au yeyote anayewachoza, nami nitatumia UUU kutenda zaidi ya hawa jamaa mara mia.
Kwanza, chini ya UUU, nitaunda sirkal ndogo yenye mafyatu wasafi kimaadili hata kitaalumana si wapiga madili wala wenye tabia za kunyonyana kama chawa. Nitateua mafyatu wakali kama manyingu, nyuki, na siafu ili tutumie UUU kuwakomboa mafyatu toka kwenye kongwa zinazofanya walalamike bila majibu. Nitapambana na udokozi, ujambazi, wizi, upigaji, na kila aina ya jinai. Nitafanya kile ambacho wanyakyusa huita lifestyle audit ambapo, kila mwaka, kila fyatu anajaza taarifa za mapato na matumizi yake ili kubaini wanaofyatua mali na njuluku za mafyatu. Majambazi na vidokozi waliozoea kulala maskini na kuamka wakwasi nitawanyonga sawa na mafisi na mafisadi wa mali za mafyatu.
Pili, kama walivyo wadudu wangu jasiri na wapendwa, nitahakikisha kila fyatu anachapa kazi kama mdudu ili ale na asiyechapa kazi atakula mafi yake kkkkk.
Kwa vile huu ni utambulisho, mengi mtayasikia nitakaposimama majukwaani kuanza kumwaga sera na kutetea UUU. Hivyo, leo sitaki niandike mengi kwa vile naenda kuandaa rasimu rasmi tayari kuwania urahis ili niwafyatue, sorry, niwatumie, sorry, niwatumikie mafyatu.
Chanzo: Mwananchi leo.