The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Tuesday, 3 March 2026

Nitapiga marufuku kuzaa fyatuland


 Siku hizi, mambo kuwa si mambo. Maisha yamekuwa magumu. Napanga kutangaza sera ya kuzuia mafyatu kufyatua watoi japo kwa muda. Naona yule anatikisa kichwa akidhani mibangi imenifyatua hadi nikafyatua kitu hiki kifyatufyatu. Hapana. Nina sababu nuzuhu za kufanya hivyo. Twende kwenye hoja. Napanga kupiga marufuku kufyatua watoi hadi mambo yatakaporekebika na kufaa. Hivyo, zifuatazo ni sababu za kufanya hivyo.

Mosi, hakuna uhuru wa kufikiri kwa sasa. Hivyo, sitaki mafyatu wafyatue watoi mazezeta au wakaokataa uzezeta na kuishia kupatilizwa kama siyo kutekwa, kupotezwa, na kunyotolewa roho. Nani anataka mtoi wake atekwe au kupotezwa kwa kujiingiza kwenye dhambi ya kufikiri hadi anaishia kupinga?
        Pili, katika utafiti wangu binafsi wa kifyatu, nimegundua kuwa watoi wanazaliwa na msongo wa mawazo ambao huwazeesha hata kabla ya kuacha ziwa tokana na misongamano ya karibu kila kitu. Wanaamka usiku wa manane na kwenda skuli na kurejea home. Pia, wanabanwa kwenye ngwarangwara, madarasani, na kila mahali. Hapa, sijagusia wanavyobanwa kwenye mbavu za mbwa za kupanga. Funga kazi ni pale wengi wanapobanana hata vitandani au kwenye makochi walalamo. Kwani, hayapo? 
Hii huwasababishia woga wanapoona ngwarangwara na tukutuku vikivunja sheria mchana kweupe. Wanapata msongo wa mawazo zaidi wanapovuka barabara kwa kuogopa kugongwa na hawa wavunja sheria wasioshikishwa adabu. Hii inawaathiri kiakili na kimwili. Hivyo, kuendelea kuwafyatua ni kufyatua kaya yenye changamoto kubwa kiakili na kimwili. Nani analitaka hili? 
    Mfano, katika pitapita yangu kwenye miji mingi ya Fyatuland, niligundua kuwa kuna makelele ya kuua fyatu. Bahati mbaya yameruhusiwa chini ya visingizio kama vile biashara, kuburudisha, kuhubiri, kupayuka tu, ving’ora, na uhuru wa kila fyatu kuwa navyo.
        Tatu, sitaki mafyatu wafyatue vitoi vitakavyobanwa kama wao. Zamani tukifyatuka na kupayuka tulivyotaka. Siku hizi, fanya hivyo, ufyatuliwe kama siyo na maisha, basi watoi wenyewe hasa usawa huu ambapo adabu na maadili vimetoweka kama siyo kutekwa, kupotezwa, na kufishwa.
        Mbali na mibanano ya kimiwili, ipo ya kiakili. Usipojikomba, kusifu, na kuabudia, unakuwa hatarini. Dawa ni kukaa kimya. Nayo ni ugonjwa. Maana, mawazo hujaa na kuvia kichwani kiasi cha kuchizika taratibu. Maisha gani haya? Sijui kwanini hawa wanaotubana hawajui kuwa tusipoongea tunaishia kuchanganyikiwa baada ya kuchanganywa na wachanganyaji tokana na kuchanganya mambo!
        Nne, kwanini kufyatua watoi watakaofyatuliwa na umaskini usababishwao na upigaji njuluku za mafyatu ambao husababisha msongo wa chuki, hasira, na kichaa hata kutaka kujinyotoa roho? Wakati tukiminywa tusiongee, wapo wanaotupigia makelele wakitutisha au kuwasifia watubanao! Siku hizi, hata mimba zinabanwa ima tokana na ukosefu wa madawa, vifaa, na rushua. Hakiji kitegemezi hadi njuluku ikutoke!
        Tano, utafiti umegundua kuwa sababu na shida zote vimeungana. Baada ya hizo sababu hapo juu, kuna hili suala la msuguano wa kimawazo ambapo kutofautiana kumegeuka kosa la jinai. Huu nao huchangia sana matatizo tajwa hapo juu. Cha mno, hili husababisha matatizo mengi kiasi cha waathirika kuishi kwa kutegemea visungura kama njia ya kujiliwaza, kujipoza, na kusahau matatizo. 
Hili nalo limeongeza matatizo mengine kama utegemezi wa urahibu, udokozi, wizi, jinai, ukosefu wa maadili, adabu, aibu na mengine kama hayo. Hii imefanya nifyatuke ahead of time. Katika kufanya hivyo, nimegundua kuwa baada ya hayo matatizo na mazabe hapo juu, waathirika wataanza kutegemea vipanya hadi paka wawachukie kwa kusababisha ushindani pale bei ya visungura itakapopaa. 
Hii pia ina madhara yake. Watoi na waathirika wengine wataanza kubet ili watengeneze njuluku wasijue wajinga ndiyo waliwao! Nani aliwahi kuukwaa kwa kubet kama siyo kuishiwa akili na ubunifu? Baya zaidi, jinai hii imehalalishwa na kuonekana kama uwekaji wakati ni uchukuaji utokanao na uoza na uzwazwa wa kimfumo?
        Sita, nimeamua kuchukua uamuzi huu ili kuwaepusha mafyatu kufyatua vitoi vilivyojaa chuki, hasira, kukata tamaa, na mengine mengi tena yasiyo na sababu za msingi zaidi ya ubinafsi, uchoyo, upofu, na uzwazwa? Nani anapenda ajenge jamii ya woga kiasi cha mafyatu kufikia hata kuogopa vivuli vyao kama kule kwa wadanganyika? Nani anapenda kuwa na jamii hata inayoogopa wasiojulikana wala visivyojulikana? Nani anapenda kujenga jamii ambayo haina utaratibu unaoeleweka hadi fyatu akiona ndata wanaopaswa kumlinda anazimia kwa mashaka na woga?
        Saba, nimegundua kuwa hali tajwa hapo juu hufanya mafyatu ima wageuke au wafikiri kama wadudu. Hujasikia wanaojiita chawa, funza, kunguni, hadi luba? Kesho, sitashangaa wakijiita au kuitwa minyoo kama siyo virusi.
        Nane, wale wasioweza kugeuzwa wadudu, waweza kuwa majambawazi. Tokana na kukosa matumaini, mipango bora, na ubunifu, watoi ima hujiingiza kwenye uchangu hata ushoga kama siyo jinai za kila aina. Nani anataka ajenge kaya ya jinai usawa huu ambapo mapilato nao wamesongwa kiasi cha kutoa adhabu kama hawana akili nzuri? Hapa, sijaongelea ndata ambao nao siku hizi wamegeuka miungu tokana na kuwalinda miungu wanene kwenye jinai yao.
        Du! Nimesemaje! Kama ninabanwa na kusongwa na jinamizi!
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

No comments: