The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Tuesday, 14 February 2017

Mihadarati: Barua ya wazi kwa Kikwete

            















Mheshimiwa Luteni Kanali na rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete, naomba nisikuite dokta kwa vile sikumbuki wewe kusomea shahada ya juu ya PhD. Najua unazo PhD za heshima ambazo kisomi, huwa wanaopewa hawaruhusiwi kuzitumia hasa ikizingatiwa kuwa wewe ulipewa kama rais lakini si kama Kikwete.  Hivyo, tofauti na wengine wanaokuvisha kilemba cha ukoko, nimeamua kueleza kwa cheo chako ulichokisotea. Hayo tuyaache.
            Shikamoo; na habari za ustaafu? Unaendeleaje na matibabu ya ugonjwa ulisema uligundulika miaka michache iliyopitwa ambao nakupongeza kwa kuuweka wazi? Mimi ni mzima mwenye afya. Nakufahamisha; mimi ni shabiki wako na aliyefurahia kipindi cha utawala wako. Sina tofauti na wale uliokuwa ukiandamana nao ughaibuni kwenye ziara zako za mara kwa mara kwenda kwenye matanuzi hadi ukabatizwa jina la Vasco da Gama yule habithi wa kireno aliyesaidia ukoloni kuenea duniani.
            Mheshimwa Kikwete, leo nakuandika rasmi waraka huu wa wazi kwa lengo la kukuomba na kukusihi usaidie kuliokoa taifa letu toka kwenye hatari na mkwamo vitokanao na kushindwa kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya ambayo bila shaka unaijua vizuri. Hivyo, rasmi, nakuomba utoe orodha ya majina ya wauza madawa ya kulevya uliyotangazia umma kuwa unayo; na ulipewa na vyombo vya usalama. Nakumbuka ilikuwa mwaka 2006 ulipotoa kauli hii ya kuwa na orodha hii muhimu katika mapambano haya magumu dhidi ya midarati nchini. Hata wabunge bungeni wameomba hili lifanyike.  Ninapoongea, wale vijana wasanii uliozoea kukutana nao na kuwapa ujiko hadi ukaambiwa kuwa chama chako na serikali yako vilikuwa vya wasanii sasa baadhi yao wako mbele ya mahakama wakipmbana na kesi zihusianazo na mihadarati. Juzi juzi wengi walisweka kwenye vituo vya polisi wakidaiwa kuwa wanabwia unga jambo ambalo liliibua hisia tofauti miongoni mwa watanzania. Suala hili limewagawanya watanzania baina ya wale wanaounga mkono jitihada hizi za kupambana na mihadarati ambazo zimeanzishwa na kijana wako Paul Makonda mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam. Pia wapo walioona kama huu ni usanii mwingine wa baadhi ya wapambe wa rais kulinda ulaji wao. Wengine walisema kuwa hii ni danganya toto na nguvu ya soda ya kisiasa tokana na namna zoezi lenyewe linavyoendeshwa. Kama haitoshi, hata waheshimiwa wabunge bungeni walitoa pofu kweli kweli wengine wakilaani kitendo hiki cha kuonea watumiaji badala ya kukamata wasambazaji na wauzaji. Wengine walikipongeza wakisema ni mwanzo mzuri ingawa waliilamu serikali kwa kutotimiza wajibu wake hasa serikali zilizopita ikiwemo yako. Wapo waliokwenda mbali hadi kudai walioanzisha wimbi hili jipya la kupambana na mihadarati kwa wasanii kwa kukamata vidagaa wakati wakiacha mipapa kuwa walichagiwa na wauza unga kwenda kutanua Marekani, Ufaransa na kwingine.  Wengi wanahoji mantiki ya kukamata vijidagaa wakati mapapa wanajulikana.
            Naomba ufanya yafuatayo:
Mosi, nakuomba chonde chonde utoe ile orodha ya wauza madawa ya kulevya uliyosema ulipewa na vyombo vya usalama mabayo umekaa nayo kwa zaidi ya miaka kumi. Kwa vile ulipoondoka madarakani hukukabidhi madaraka rasmi, sikumbuki kusikia kuwa ulikabidhi orodha hiyo kwa rais Magufuli aliyechukua madaraka baada yako. Nakumbuka uliwaambia watanzania kuwa una orodha za wauza unga, majambazi, wala rushwa, hata wezi wa bandarini kutaja wachache.
            Kwa vile ushastaafu, nashauri ile orodha uitoe kwa rais John Pombe Magufuli aliyesema hana simile na biashara hii. Alikaririwa akisema kuwa hata kama mkewe akijihusisha akamatwe bila kujali ni mke wa rais. Hii maana yake ni kwamba rais–kama hafanyi usanii–hataki mchezo na mihadarati.
            Pili, kama utaweza, naomba ueleze ni kwanini uliamua kutowakamata watuhumiwa baada ya kupewa orodha uliyokiri kuwa nayo. Umma ungependa kujua sababu za kutofanya hivyo ili uweze kuzifanyia kazi na kuepuka wewe kugeuzwa kuwa sehemu ya jinai hii.
Tatu, naomba uelezee ni kwanini hukumpaulinzi marehemu Amina Chifupa alipoamua kuweka mambo hadharani kiasi cha kuhatarisha usalama na maisha jambo ambalo lilikuwa wazi. Je uliamua kuwasamehe wauza unga kama ulivyofanya kwa wezi wa EPA uliowaamuru warejeshe fedha na mambo yaishe wakati kufanya hivyo ni kinyume cha sheria jambo ambalo una bahati halikufika mbali. Kwani ingekuwa ughaibuni ungekuwa impeached kwa kuvunja katiba.
Nne, kama kiongozi mstaafu, nakuomba utoe kauli dhidi ya balaa hili kwa taifa ili lau watanzania waache kuishi kwa kudhani nawe ni sehemu ya tatizo badala ya kuwa suluhu. Kwa sasa ni rahisi kwako kufanya hivyo, hasa ikizingatiwa kuwa huna shughuli nyingi sawa na ulizokuwa nazo ukiwa kiongozi wa nchi. Hili ni muhimu hasa kwa sasa ambapo imejengeka imani kuwa wauza mihadarati wana serikali yao ndani ya serikali. Isitoshe, kujitokeza kwako kuelezea mapungufu ya utawala wako dhidi ya jinai hii kutaisaidia serikali ya sasa kupambana na kadhia hii kwa kuchota kwenye uzoefu wako hasa pale ulipoacha kuwakamata watuhumiwa ambao orodha ya majina yao unayo.
Naomba kutoa hoja na ombi kwako ili utusaidie kwenye vita hii kama mtanzania na kiongozi mstaafu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.

Saturday, 11 February 2017

Mlevi kuleta FBi kupambana na bwimbwi Bongo

          Baada ya Mkoa wa Dar-Si-Salama chini ya munene wake Po Makondakonda kujitutumua kupambana na biashara ya bwimbwi, mlevi niemeamua kuwaunga mkono. Nitatumia umaarufu wangu na elimu yangu ya juu sana ya mambo ya sheria na usalama kuwasaidia namna ya kushinda vita hii hatari na ngumu. Hivyo nitatoa mapendekezo yafuatayo kabla ya kuingiza the big gorilla, Federal Bureau of invasion (FBi).
            Kwanza, mapambano dhidi ya wauza bwimbwi al maaruf barons au kingpins kwa Kinyasa, yaanze kisayansi na si kisiasa, kukurupuka au kutafuta sifa. Mfano, lazima ufanyike uchunguzi wa kina na wa kitaalamu wa kubaini wauzaji ndipo wakamatwe. Hapa wale wanaoita vijidagaa kutafuta umaarufu na kuuridhisha umma wanapaswa kupata somo. Sina haja ya kuonekana kama nawakandia au kuwakong’ota. Iko wapi vita ya kupambana na shisha iliyoanzishwa kwa nguvu ya soda? Si bado watumia shisha wanaendelea kutesa. Mmeshindwa shisha; mtaweza bwimbwi?
            Pili, nguvu kubwa ielekezwe kwenye mapapa na si vidagaa vinavyogalagazwa mbele ya vyombo vya habari ili kuonekana mapambano ya kupambana na bwimbwi yapo na yanafanikiwa wakati si kweli. Juzi tuliltewa wasanii njaa wanaohangaishwa na njaa ya umaarufu na njuluku kiasi cha kugeuka kuwa taxi kisiasa. Maskini, wakati wakipiga kampeni tena baada ya kubwia bwimbwi hawakushughulikiwa. Sasa uchakachuaji umeisha. Jasho linawatoka. Wako wapi wanasiasa ambao microphone wa mjengo aliwahi kusema wanakula bwimbwi tena njengoni? Je ni wanasiasa wangapi na vyama vingapi vimekuwa vikifadhiliwa na wazungu wa bwimbwi? Kwani hii siri? Wako wapi wafanyabiashara mashuhuri wanaojulikana kuwa kingpins wa bwimbwi wanaosifika kufadhili wanasiasa na vilabu vya michezo?
            Tatu, zitungwe sheria kali dhidi ya kitu hii. Sijui kama zilizopo zina makali ya kuweza kupambana na kitu hiki hasa ikizingatiwa kuwa utawala uliopita ulihalalisha kila jinai. Naona yule anatoa mimacho akidhani nazua. Umesahau namna mashushu walivyofanya upelelezi na kukusanya orodha ya wauza bwimbwi wakubwa wakampa Njaa Kaya ambaye aliwahi kukiri alikuwa nayo asiifanyie kazi tokana na kuogopa kuvuruga ulaji? Kwanini asibanwe akatoa hii orodha ili kurahisisha kazi ya kuwasaka wauza bwimbwi? Au waliotangaza vita hii hawajui hii kitu ambayo hata kunguru wanaijua?
            Nne, ili kushinda vita dhidi ya bwimbwi tunapaswa kuwa wakweli kwa nafsi zetu. Mfano, huwezi ukapambana na biashara ya bwimbwi bila kuwa na sheria inayokupa mamlaka ya kukamata mali yoyote inayotuhumiwa kupatikana tokana na biashara hii haramu.  Ukiachana je mapilato wetu ni wasafi hasa ikizingatiwa kuwa wengi waliteuliwa na Njaa Kaya kwa kuangalia udini, urafiki na ushikaji? Anayebishia hili ajiulize wale mapilato vihiyo waliwezaje kuupata ujaji kama siyo kujuana? Je hawa wanaweza kutoa haki bila kununuliwa na wazungu wa unga? Naona yule anasonya. Sina maana kuwa majaji au mapilato wote ni makanjanja. Hasha. Ila wapo wengi ima feki, makanjanja, vihiyo na mafisadi tena wanaojulikana kwa majina.
            Tano, hakuna mashamba ya poppies Bongo. Hii maana yake ni kwamba bwimbwi linatoka ughaibuni hasa kule kwa Watalibani. Je linaingizwa kupitia wapi kama siyo kwenye viwanja vyetu vya ndege, mipakani na kwenye bahari zetu? Je hawa wanaosimamia maeneo haya wameshughulikiwa? Ni wangapi wanafahamika? Ukitaka kuwajua huna haja ya kuhangaika. Wapo vijana walioajiriwa jana lakini wana ukwasi wa kutisha. Unadhani wameupataje kama siyo kuruhusu bwimbwi lipite kwenye maeneo tajwa? Ukiachi hilo, inakuwaje wazungu wa bwimbwi wasijulikane wakati mateja yamejaa kila mtaa? Kamateni mateja yote yawapeleke yanakopata kago nako waeleze anayewasambazia kago. Ukiachia hilo, nenda Masaki na kwenye maeneo ya matajiri uone waja wenye kutia kila shaka walivyonunua mihekalu bila kuwa na historia ya njuluku. Kamata mahekalu haya na kuwabana wawambie walivyotengeza njuluku ya kuyanunua. Simpo. Hata wachovu mitaani wanawajua wauza bwimbwi ila wengine hawawataji kwa vile ni wafadhili wao. Mkikaa vizuri na wachovu wanaochukia kitu hii mtapata habari kibao. Je mtawahakikishia usalama dhidi ya wauzaji ambao ni wakatili hakuna mfano?
            Nimalizie kwa kuwapa mfano hai toka kwenye kaya ya nyayo pale jirani. Baada ya wauza bwimbwi waitwao Akasha kuwaweka mifukoni wanasiasa, polisi, majaji na kila yoyote mwenye nafasi, tokana na hofu ya kupoteza uchaguzi, lisirikali kule liliwaita FBi wakawategea ntego na kuwakamata na kuwasafirisha kwa Joji Kichaka. Nanyi kama mmeshindwa si mniambie niwaunganishe na FBi? Muve na zuva rakanaka.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

Tuesday, 7 February 2017

Mihadarati: Barua ya wazi wa Makonda

 Image result for makonda and wema sepetu
Kibonzo kwa hisani ya gazeti la Daily Nation, Feb., 8, 2017.
           Huwa nina mazoea ya kukosoa au kupongeza viongozi wa umma pale wanapokosea au kufanya yale yenye kuwaridhisha wananchi. Niseme kwanza. Nilishaandika makala huko nyuma za kumkosoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makamba. Ni pale alipowaweka ndani watendaji wa Halmashauri ya Kinondoni na alipomdhalilisha afisa mmoja wa ardhi kwa kumwita chizi.
            Hivyo, kwa waliosoma makala hizo wanaweza kushangaa kwa kusoma makala hii. Hata Makonda mwenyewe atashangaa kutokana na kutojua kuwa mimi sina chama zaidi ya Tanzania wala dini zaidi ya Haki na Ukweli. Hivyo, leo nachukua fursa hii kuandika barua hii rasmi kwa ndugu Makonda.
            Kwanza,  nakupongeza kwa hatua zako za hivi karibuni za kuthubutu kuwanyoshea kidole watuhumiwa wa biashara ya mihadarati bila kujali nafasi zao katika jamii. Hili ni jambo la kupigiwa mfano hasa ikizingatiwa: hakuna kiongozi awe mdogo au mkubwa aliyejaribu kufanya kama ulivyofanya hivi karibuni. Hongera sana ndugu Makonda na Mungu akulinde usafishe Dar es Salaam ili uwe mfano kwa  nchi nzima.
            Pili, nakupongeza kwa kujitoa mhanga kama ishara ya uzalendo na upendo kwa taifa tena vilivyotukuka. Kwani, ulisema wazi kuwa hugopi kufa ikibidi. Hii ni kuonyesha usivyobabaisha wala kuogopa. Tunakuunga mkono; hasa tukizingatia kuwa kadhia ya mihadarati, licha ya kuangamiza maisha ya vijana wetu ambao ndiyo nguvu kazi, inachafua heshima na sifa ya taifa letu.
            Tatu, umeonyesha ujasiri na kutokuwa mwoga ukiachia kuvunja mwiko kuwa biashara ya mihadarati inaongeleka na kuweza kushughulikiwa; kama atapatikana mtu wa aina yao ambaye tunashauri rais akupe ulinzi na usaidizi wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa vita uliyotangaza si lelemama, uwezekano wa kushinda ni mkubwa.  Laiti akina Lameck Mwigulu Nchemba, waziri wa mambo ya ndani, hata rais mwenyewe, wangekuwa na hata robo ya uthubutu yako; mihadarati ingekuwa historia. Hata hivyo, hatuwezi kumshuku rais hasa ikizingatiwa kuwa ndiye aliyekuteua kwa kujua ujasiri na ithibati vyako.
            Sasa nini kifanyike? Tunashauri ufanye yafuatayo ili kufanikisha vita hii adhimu na muhimu dhidi ya mihadarati:
            Mosi, kukubali kuwa vita hii ni hatari na si ya kawaida. Hivyo, inahitaji maandalizi na umakini wa juu kuweza kuishinda mfano kuwalinda watoa taarifa na kuhakikisha wanachunguzwa ili kuepuka kupokea taarifa zinazopotosha au kukomoana tena zinaweza kutengenezwa na wauza mihadarati wenyewe ili kukukatisha tamaa kama njia ya kujiponya.
            Pili,  mwendee rais mstaafu Kanali Jakaya Kikwete ambaye alikuteua mara ya kwanza kuwa mbunge wa Bunge la Katiba ili akupe ile orodha ya wauza unga aliyowahi kudai alipewa na vyombo vya usalama akagwaya kuishughulikia tokana na sababu ajuazo mwenyewe. Hivyo, kuna mahali pa kuanzia. Niliwahi kushauri rais Magufuli atumie mamlaka yake kumtaka mtangulizi wake atoe orodha ile hasa ikizingatiwa kuwa si mali binafsi ukiachia mbali kuikalia kuwa mchango mkubwa na motisha kwa wauza mihadarati.
            Tatu, anzisha utaratibu wa kuhakiki mali za watuhumiwa na wale wote wanaoonyesha kuwa na ukwasi wa haraka bila kuweza kueleza walivyoupata tena kwa muda mfupi. Ni bahati mbaya kuwa Tanzania inaruhusu watu kujitajirikia bila kuonyesha walivyochuma huo utajiri kiasi cha wezi na wauza wengi kuwa kero mitaani wakijidai na kununua mali kila mahali wakati wanajulikana walivyo wahalifu. Bila kubadili mfumo huu na kuwa na sheria inayomtaka kila Mtanzania kueleza alivyochuma utajiri wake kwa njia ya kujaza fomu za mali na kodi kila mwaka, uwezekano wa kushinda vita hii ni mdogo.
            Tatu, kamata watumiaji au wasambazaji wadogo wadogo na kuwahoji kwa kuwaahidi msamaha ili wawataje mabosi wao katika jinai hii. Inashangaza kuona watajwa wengi ni makoplo wa polisi na wasanii waganga njaa ambao kimsingi ni dagaa. Je hayo mapapa yanaachwa ili iweje? Inajulikana kuwa polisi wadogo hukusanya fedha na kuwapelekea wakubwa zao na si kwenye madawa tu hata kwenye rushwa kama vile za barabarani.
            Nne, kamata kimya kimya watuhumiwa wote kisha utangaze baada ya kukamata ili kuepusha kuwastua wengine. Hapa lazima kuitambua na kuiainisha mitandao ya biashara ukubwa na mbinu zake ili kuweza kuishughulikia vizuri kisayansi, vilivyo na kwa ufanisi.
            Tano, weka makachero bobezi na waaminifu watakaonunua au kuuza huku wakirekodi kila kitu ili kuwa na ushahidi wa wazi kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Kenya ambapo Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) liliweka mitego ya namna hii na kuwanasa vigogo maarufu wa unga wa famili ya Akasha hivi karibuni. Hawa jamaa walikuwa wamefanikiwa kuwahonga polisi, majaji na wanasiasa kiasi cha kutokamatika. Hivyo, ikibidi, tafuta msaada nje ya nchi ili kupambana na hawa wahalifu wanaoangamiza taifa kwa tamaa zao hata wawe ni wakubwa kiasi gani kama umedhamiria. Hapa ndipo rais anapaswa kukusaidia zaidi ili kuweza kushinda biashara hii ngumu na hatari ambayo inahusisha hata wale ambao huwezi kuwadhania tokana na hadhi zao katika jamii. Wapo wanaojifanya watu wa dini wakati ni wauzaji wakubwa wa mihadarati na wengine wengi kama vile wasanii tena maarufu na hata wanasiasa.
            Tumalizie kwa kukupongeza angalau kwa kutoa mfano wa kuanzia kupambana na kadhia hii ambayo imegeuzwa serikali ndani ya serikali na haramu iliyohalalishwa tokana na woga, tamaa na unafiki wa watendaji wanaopaswa kupambana nayo. Mungu akutangulie Makonda.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

Akina Mgoshi Machungu kujidai Hollyweed

          Baada ya rahis mpenda sifa na vimwana, Don Trumpet, kuipiga tafu Bongolalaland kwa kuruhusu wabongo kuingia kayani kwake bila visa, kijiwe kinapanga kwenda kule hasa Holyweed kujinoma kama hakina akili nzuri. Pamoja na upenyo huu, sijui kama magaidi hawataanza kutuonea wivu na kutaka kutunyotoa roho kwa wivu.
            Mgoshi Machungi anaingia yote 36 yakiwa nje kwa furaha. Anasalimia na kutujuza habari njema. Anasema “wagoshi mimesikia jinsi Tiampu aivouhusu wabongo kuingia Maikani bia visa? Sijui wenzangu mmeipokeaje hii habai njema?”
            Kapende anajibu “hapa hakuna cha kusherehekea hasa vinginevyo uwe mwanasiasa au muuza bwimbwi kama si fisadi anayeweza kuwa na  njuluku za kulipia pipa na hoteli kwenda kustarehe kule. Hii ni danganya toto. Huenda kuna kitu ameona anachotaka kuja kuchukua kwa kujifanya mwekezaji wakati ni mchukuaji.”
            Msomi Mkatatamaa anajibu “huenda anataka kudhibiti hii  urani iliyogunduliwa Kusini ili maadui zake wasiweze kuifaidi na kutishia woga ambao Marikani imekuwa ikitumia kutisha mataifa mengine hasa Irani ambayo imeshupaa kuwa haitishwi.”
            Mbwamwitu anamchomekea Msomi “nimesikia hii kitu ingawa sijui kama hata wamachinga wataruhusiwa kwenda kule kufanya biashara kama vile kuuza kanda na kununua kanda za wasanii wa kule.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea “bila shaka mama ntilie nao wajiandae kukwea pipa kwenda kuwapikia watasha waliochoshwa na kunyotolewa roho na Makidonald Janki yaani vyakula vibovu tokana na ujinga na uvivu wao. Nasikia watasha wanakula kila kitu hata nyanya chungu na mchunga. Ila wakija huku hujifanya hivi si vyakula anavyoweza kula mtasha wakati kwa wanavipwakia kama hawana akili nzuri.”
            Kabla ya kuendelea, Kapende anachomeke “ nadhani hapa na vyangu wa Bongo hao ndiyo usiseme wanajiandaa kutia timu hasa ikizingatiwa kuwa Don mwenyewe anapenda vimwana kama jamaa yangu Njaa Kaya. Wakiingia kule watapeta hasa ikizingatiwa kuwa uchangu kule unaruhusiwa kisheria. Jamaa yangu mmoja alinitonya kuwa machangu hulipia ndude zao kodi kama wafanyabiashara walipiavyo maduka na biashara zao nyingine halali.”
            Mipawa naye anaamua kutia timu na kusema “ hii kitu inaweza kushabikiwa sana na kuonekana nzuri tu bila kufikiri. Tangu lini Marikani ikapenda kaya yoyote duniani wakati falsafa yake inajulikana kuwa hakuna rafiki wala adui wa kudumu bali maslahi?. Wabongo–tokana na ujuha na ulimbukeni na upenda dezo–wanaweza kujisifia wamepata wasijue wamepatikana. Hapa lazima nitahadharishe. Wauza bwimbwi msithubutu. Kwani kwa Trumpet hawana mchezo na bwimbwi kama hapa kayani ambako bwimbwi lilihalalishwa baada ya kifo cha nzee Nchonga. Huoni walivyowakamata akina Akasha pale Kenya na El Chappo kule Mexico?”
            Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic “kama Tramp naruhusu Tanjania kwenda Amerikani mimi sasa kwenda fanya pango vekeza kule. Tafanya pango unganisa Bombey na Vashington ili fanya biasara kuba kuba. Kama veve natumia akili wizuri hapa naweza kuwa tajri veve na vatu vako vote.”
            “Wenzako tunashangilia wabongo kuruhusiwa kuingia kwa Joji Kichaka kama taifa kumbe mwenzetu unakamia kwenda kule kwa faida ya Ughabacholini na si kaya yetu. Ama kweli kunguru hafugiki walisema wahenga! Wakati sisi tukidhani wewe ni mwenzetu kwa kutudanganya na kutuita ndugu zako, kumbe bado roho yako iko Bombei!” anasema Mchunguliaji huku akipokea gazeti toka kwa mheshimiwa Bwege.         
            Mheshimiwa Bwege anakatua mic “dog achana na Kanji. Kwani ulikuwa hujui sera za hawa jamaa ambao alituletea mkoloni mwingereza halafu akatuachia wakazaana kama magugu? Mie hapa nafikiri kwenda kwa Joji Kichaka kuoa mitoto ya kitasha. Lazimanilipize kisasi. Kila mara naona mabinti zetu wakichezewa na watasha wanaojifanya watalii, acha nami niende kule niwachezee binti na dada zao hata mama zao. Maana naambiwa kuwa watasha si wabaguzi kama wamanga au magabacholi wa hapa. Nasikia kule wote wanaitwa wamakonde bila kujali nani alitoka wapi. Jamaa yangu anayeishi kule alisema kuwa watasha wakiamua kubagua wanabagua kila mtu ambaye si mtasha bila kujali ni gabacholi, mmanga au mjep au mchainizi.  Pia naambiwa akina mama wa kitasha wanapenda sana wanaume wa kiswahili kwa vile wanajua kupenda na kuwanyenyekea.”
            Kabla ya kuendelea Msomi anakatua tena mic “waswahili kwa kushobokea vya wengine. Kwani hapa wanawake wameisha au ni kutafuta matatizo? Hamjui kuwa mama wa kitasha anaoa Mswahili bali haoelewi kama mlivyozoea. Mgoshi Machungi najua udenda unakutoka kwa kuwazia mitoto ya kitasha. Hamjui mnachokimbilia kama kweli mtajaliwa kwenda zenu kwa Trampet. Sijui kama mtaweza kupewa vijibwa mvipeleke kujisaidia au kufanya mazoezi huku mkiviruhusu kulala vitandani mwenu na kulia kwenye vyombo vyenu kama watasha wafanyavyo. Kuchunga mbwa kwa mswahili wapi na wapi. Kubalini. Mmezoea kuchunga mbuzi na ng’ombe lakini si mbwa.”
            Mijjinga aliyerejea hivi karibuni toka kijiji anakula mic “mie wala sina mpango wa kwenda kwa Trampet hasa ikizingatiwa kuwa aliwahi kusema kuwa lazima Afrika itawaliwe zaidi. Aliendelea kusema kuwa waswahili hawana akili ya kuweza kujitawala.”
            Kabla ya kuendelea Kapende anakatua mic ‘kwani alikosea? Huoni tulivyoruhusu magabacholi kuja hapa kujiibia watakavyo na kutajirika wakati sisi tukiendelea kuwa makapuku? Hii ni nini kama si ujinga?”
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
 
 

Sunday, 5 February 2017

Hotuba ya Magufuli suto kwa Afrika

           Hivi karibuni rais John Pombe Magufuli alionyesha upekee kama kiongozi wa nchi kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa  Tanzania kuhutubia mkutano wa wakuu wa Nchi Huru za Kiafrika kwa Lugha ya Kiswahili jambo ambalo lilipokelewa kwa hisia tofauti. Wapo walioona kama ni kujidhalilisha au kukwepa kutumia Kiingereza Lugha ya mtawala wetu wa kikoloni wa zamani huku wengine–hasa wenye kujitambua na kupenda taifa lao–wakimsifu kwa ujasiri na uthubutu huu wa aina yake. Wale ambao bado mabakia ya ukoloni hayajawatoka vichwani walidiriki kusema kuwa rais hajui Kiswahili bila kujua kuwa andiko lake kwa ajili ya shahada yake ya uzamizi (PhD) aliliandika kwa lugha hiyo. Niliwasoma kwenye mitandao wakikejeli kitendo hiki cha kishujaa bila kujua kuwa walikuwa wakifichua ujinga na kujikana kwao.
            Hata hivyo, ujinga na ulimbukeni na woga wa kutumia lugha ya Kiswahili ambayo ni moja ya lugha kubwa za kimataifa kwa baadhi ya wenzetu havikuanza jana wala havitaisha kesho. Zipo nchi tena jirani ambazo watu wake wanaonea aibu Kiswahili kwa kushabikia Kiingereza ambacho nacho hawakijui zaidi ya kukiongea kwa lafudhi za lugha zao asilia.  Wengi hukwepa kutumia Kiswahili au kikionea aibu kutokana na imani mfu kuwa lugha hii ni ya wale ambao hawajaelimika jambo ambalo si kweli. Hivyo, tunampa moyo rais Magufuli asikate tamaa bali aendelee kukienzi na kukitumia Kiswahili popote aendapo ili kutangaza Kiswahili kama lugha ya taifa na ya Afrika yenye asili yake Tanzania.
             Hata hivyo, Magufuli si wa kwanza kukosolewa na kuonekana wa ajabu kwa kutumia Kiswahili kwenye jukwaa la kimataifa.  Kwa mfano, mwaka 1964 marehemu profesa Ali Mazrui gwiji wa sayansi ya jamii alipendekeza Kiswahili kitumike kuwa lugha ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU). Badala ya kuungwa mkono, pamoja na usomi wake wa kupindukia, alizomewa na kuonekana kama hakuwa ameelimika vilivyo. Ajabu ya maajabu ni kwamba wengi waliomzomea walikuwa na viwango vidogo vya elimu ikilinganishwa na Mazrui mwenyewe.  Watu wenye mawazo mgando, ya kikale na kikoloni wanaweza kuona kama rais Magufuli kuhutubia Umoja wa Afrika (AU) ni jambo la ajabu bila kujua kuwa ni njia moja ya kuonyesha kujitambua, kujithamini na kuchangia kwa Umoja wa Afrika na kuondokana na masalia ya ukoloni ukiachia mbali kukuza Kiswahili kama lugha ya  taifa na kimataifa ya kiafrika hata kama ina baadhi ya maneno ya lugha za kigeni.
            Kwanini viongozi wa mataifa makubwa kama China, Japan Urusi na mengine hutumia lugha zao hata kama viongozi hawa wanakimanya kiingereza? Wanafanya hivyo ili kuonyesha wanavyojitambua. Tunapaswa kujivunia hatua hii aliyofikia rais Magufuli kwa kupeperusha bendera ya Tanzania na lugha yetu ya taifa. 
            Wapo wanaokosoa hotuba ya Magufuli kwa kuangalia udhaifu uliojitokeza ambao si kosa la rais yaani kutotoa nafasi kwa mkalimani kutafsiri. Ikizingatiwa kuwa hii ni hotuba ya kwanza kwa rais Magufuli kwenye jukwaa kubwa kama hili, hivyo anaweza kujifunza na kushughulikia mapungufu haya. Hata hivyo, ukisikiliza namna wasikilizaji walivyokuwa wakimshangilia, ni wazi ujumbe ulikuwa ukiifikia hadhira yake barabara. Watanzania na waafrika walio wengi wana kasumba ya kujivunia vya wengine wakati vyao wakividhalilisha. Unaweza kuona udhaifu huu kwenye namna ya watu wetu wanavyotetea dini nyemelezi za kigeni huku wakitukana mila zao na kutukuza za wenzao hata kama zinafanana au ni mbovu kuliko zao.
            Lazima waafrika tufikie mahali tujikomboe kutoka kwenye kongwa za kikoloni kama vile kutumia lugha zao bila ulazima au kuamini kuwa sehemu takatifu duniani ziko ughaibuni ukiachia mbali kupachikwa majina ya kigeni na kuomba kwa baadhi ya lugha za kigeni kana kwamba Mungu hajui wala hakutupa maarifa ya kuunda lugha zetu. Wakati mwingine tunawalaumu wazungu na waarabu waliotuletea ukoloni wao tukaugeuza kuwa wetu wakati sisi wenyewe ndiyo tunauendeleza na kuutukuza tokana na kutojitambua, kutojiamini na ujinga.
            Tumalizie kwa kumpongeza rais kwa kuanza kujikomboa mwenyewe ili liwe somo kwa wengine hasa viongozi wenzake wa Umoja wa Afrika (AU) ambao walionyesha kongwa za ukoloni katika uchaguzi uliopita wa Mwenyekiti wa AU kwa kupiga kura kwa kulalia kwenye mgawanyiko wa kikoloni baina ya makoloni ya zamani ya kifaransa na kiingereza ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Chad Moussa Fakhi Mahamat alimshinda mwenzie wa Kenya Amina Mohamed.
            Tunawasihi watanzania wajenge mazoea ya kuithamini lugha yao kama tunu yao. Kwani si mataifa mengi ya kiafrika yenye lugha zenye hadhi na kusambaa kijiografia kama Tanzania. Rais Magufuli ameanza. Naamini hata majirani zetu wanaoona Kiswahili kama ni lugha ya wasiosoma, watabadilika na kuanza kujiamini na kujithamini na kutumia Kiswahili kama Waafrika. Hakika hotuba ya Magufuli kwa AU ni suto kwa Waafrika walio wengi ukiachia mbali kuwa jambo la kupongezwa na kupigiwa mfano.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

Saturday, 4 February 2017

UDARt na mwendo kasi wa kupunyua mali za walevi

          Alipozindua mradi wa mabasi ya mwendo kasi jijini Bongo hivi karibuni, rahis alionyesha shaka ya kutojua faida ambayo kaya itapata au imeishapata tokana na mradi wenyewe ambao ni mazonge na madudu matupu kama tutaidurusu historia ya mbia katika mradi huu. Kwa tunaojua historia ya mradi, tunajua fika kuwa imekula kwa walevi. Najua wengi watashangaa kusikia habari mbaya hii ambayo ni ukweli mtupu. Hakuna kilichonichefua kama jina la mradi wenyewe yaani UDART. Jina hili linanikumbusha lile Shirika la Walevi la Usafari Dar (UDa) ambalo lilianzishwa na mzee Nchonga wa Burito kuondoa msongamano kwenye jiji hili la salama isiyo salama.
          Leo nataka nihoji baadhi ya masaala hata kama kilevi kama ifuatavyo:
          Mosi, je sakata la kashfa ya unyakuliwaji UDa limeishia wapi hadi sasa? Kwa kumbukumbu za kilevi ni kwamba aliyekuwa waziri ndogo wa njuluku Adama  (siyo yule wa Gambia) Milima aliwahi kuutonya mjengo kuwa hisa za lisirikali hazikuwa zimeuzwa kwa kampuni la Simian Group; na zile zilizokuwa zimedaiwa kuuzwa zilikuwa zimeuzwa kwa bei ya kichaa au kutolewa bwerere baada ya wahusika kutembeza mlungula kwa waliokuwa wakubwa wa shirika hili mfu. Bado nakumbuka. Milima alikuwa ima akijibu swali la bi Iron lady Halimaaa Mdzee au Joni mwana wa Nyika wote wahisimiwa wa Chakudema tena njengoni.
          Pili, inakuwaje lisirikali linatoa sadaka shirika na njuluku za umma kana kwamba mradi ni mali yake binafsi bila kutaka kutumia asasi zake kuchunguza na kufikishwa kwa pilato waliojitwalia UDa yetu kama alivyoshauri Mdhibiti na Mkaguzi wa njuluku za lisirikali? Nashauri lisirikali liitumbue UDa kwanza kabla ya kujisifu kuwa imefanya makubwa kwa kuleta mradi wa kipekee wakati upekee wake unaonekana ni wizi kasi na si mwendo kasi. Je dokta Kanywaji hayajui haya madudu na majipu yote haya tena yanayojulikana na kunuka wakati alikuwapo wakati yakifanyika? Hivi lisirikali halijui kuwa UDa ilianzishwa kwa njuluku za walevi ukiachia mbali huu mradi mpya lililozawadia hiyo kampuni ya Simian nao umegharimu mabilioni ya dola tena za nkopo toka Benki ya Dunia ya mabwanyenye na mabepari? Hii akili au matope?
          Tatu, je kwanini lisirikali limefanya siri hii ndoa haramu baina ya UDa na Dati iliyotengeneza kitu kinaitwa UDATA? Kwa nchezo huu sitashangaa kusikia kuwa siku moja Simian Group imegawiwa Air Bongolalalander.
          Nne, nani wako nyuma ya hujuma hii inayohalalishwa kwa mlango wa nyuma huku walevi wakishangilia wasijue haya ni mauti yao? Sasa nawaambieni hata kama ni kwa nguvu ya kanywaji na majani kuwa hii UDAT ni bomu na jipu linalopaswa kutumbuliwa haraka badala ya kuwekewa utuli. Hivi nyie walevi, nani aliwaroga hadi mkaaminishwa kuwa UDAT ni big deal wakati ni wizi mtupu? Je hamjui kuwa watasha watakapotaka njuluku zao mtalipa nyinyi au vizazi vyenu?
          Tano, tujalie kuwa Simian Group walilipa cash na kuuziwa UDa. Je walichunguzwa kujua walivyotengeneza hiyo njuluku? Nauliza swali hili kuepuka ushenzi wa wenye mamlaka kuwatumia waramba makalio wao kulinda na kuendesha miradi yao itakanayo na kuwaliza walevi. Pili, nahofia kuwa tusipokuwa makini, tutajikuta tukiwasaidia watakatishaji njuluku za bwimbwi na ujambazi mwingine.
          Nimalizie kwa kuwaonya walevi kuwa kama wataendelea kulishwa kila urongo na takataka watakuja kustukia siku moja nao wametwaliwa kama UDa na kubinafsishwa kwa mafisi watakaowachuuza watakavyo. Huwezi kuridhia ndoa ya ya UDAT bila kuuliza najisi na usharmuta (ukahaba) ulioendelea hadi kufikia ndoa hii ya haramu. Kinachopaswa kufanyika ni kujibu maswali ambayo wahishimiwa wenye uchungu na kaya wamekuwa wakiuliza kuhusiana na kashfa hii. Hakuna aliyeniacha hoi kama mstahiki wa jiji la Bongo aliyeapa kufumua uchafu wa UDa kusikia kuwa juzi amepiga kura kuunga mkono kutumia madafu bilioni 5 yanayodaiwa kulipwa na Simian Group kuitwaa UDa bila kueleza namna ulipofikiwa uamuzi wa kupewa njuluku kidogo wakati thamani ya UDa ilikuwa kubwa kuliko haya madafu. Kama haitoshi, leo tunaambiwa mradi wa mandinga yaendayo kasi ni wa mabilioni lukuki lakini unakasimiwa kwa  wale wale waliotuchomolea UDa yetu. Tieni akilini;msimame na kuhakikisha ndoa ya UDAT inabatilishwa na UDa yetu inarejeshwa na kuuzwa kisheria.
Nipashe Jumamosi leo.

Wednesday, 1 February 2017

Why AU needs to be decolonised

Chad's Moussa Faki Mahamat, the new chairperson of the African Union Commission, at the African Union headquarters in Addis Ababa, Ethiopia on January 31, 2017. PHOTO | ZACHARIAS ABUBEKER | AFP
            The just-ended conference of the African Union (AU) in Addis Ababa, once again exhumed Africa’s endemic glitches revolving around the colonial dregs.
            This was displayed during the election of the AU Commission’s new chairperson. Seven candidates battled it out for the position, including Kenya’s Foreign Affairs Cabinet secretary, Ms Amina Mohamed, and Chadian Foreign Minister Moussa Faki Mahamat, who carried the day after some horse trading, threw Ms Mohamed out.
            The Nation reported that Burundi, Djibouti and Uganda were to blame for Ms Mohamed’s defeat, not to mention Tanzania that abstained with other members of South African Development Community (Sadc).
            Essentially, this two-horse race epitomised Africa’s colonial past and present revolving around the obscurities of its former colonial masters, mainly Britain and France.
            Despite priding themselves about being free and independent, the African countries in these two blocs still vote along colonial lines. Those whom French colonial monsters ruled will vote for any francophone candidate, while those who were under the British also go for an anglo candidate.
            Since 2002, francophone Africa has produced four out of the five AUC chairpersons. Apart from voting along colonial and linguistic lines, African countries, under their union umbrella, still use colonial languages in their business.
            Prof Ali Mazrui was once jeered at and scorned in 1964, when he proposed Swahili to be used as the language of the defunct Organisation of African Unity (OAU). The AU is not an emancipatory organ for Africa. It is an embodiment of colonial extension.
            The AU’s treaty stipulates clearly that it must treat the sovereignty of member states as sacrosanct. It also states that there must be a “general recognition of the exclusive sovereignty of each party over its lands, people, and agents abroad, and each and several responsibility for the warlike acts of any of its citizens or agents.”
            This acts as a stumbling block for the total reunification or unification of Africa. The way the AU vote is the exegesis, if not a replica, of how Africa is still pregnant with toxic colonial legacies.
            You wonder why Burundi would vote against a candidate from the East African Community simply because it is francophone. Djibouti is purely Arabic, while Uganda is despotic just like Burundi and Chad, which they fully supported.
            Did Burundi revenge against Kenya for its opposition during the waiting time for joining the EAC? Kenya and Tanzania opposed the speedy admission of Burundi and Rwanda that Uganda had proposed. Tanzania, a Sadc member, abstained.
             What does this say about the EAC? Was it a display of hidden antipathy between the intra-rifts of the EAC, namely the Coalition of the Willing (CoW) and the Burundi-DRC-Tanzania Community (BDTC) that seem to still simmer despite being pushed under the carpet? Arguably, for a true pan-Africanist, what transpired in Addis shows the artificiality of the EAC and the division of Africa, in general.
            Yes, the friend in need is the friend indeed. Ms Mohamed’s defeat is the loss of the EAC, given that her victory would not only have been beneficial to Kenya, but also the EAC.  
            Another colonial legacy that displays how toxic African countries are can be seen in the regional groupings. The 15 countries from the southern Africa bloc, Sadc, abstained and made Mr Mahamat’s victory easy.
            Apart from Angola and Mozambique, the rest are anglophone countries but they didn’t vote. However, doing so was like voting for Mr Mahamat as it denied Ms Mohamed the votes she deserved.
            One may argue that the Sadc members felt they had nothing to lose given that one of their own, Dr Nkosazana Dlamini- Zuma was just relinquishing the post. Again, many will recall that francophone countries backed Gabonese Jean Ping, whom Dr Dlamini-Zuma defeated after being supported by all the anglophone countries. 
            You wonder why the Sadc members decided to abstain instead of voting for Ms Mohamed. What a betrayal and a divisive stance for Africa!
Looking at how fractured Africa is, it needs to be decolonised and detoxified in order to unite instead of operating along colonial lines.
            Going on like this is nothing but internalising and reinforcing colonialism and the victims are the African countries themselves.
Source: Daily Nation Kenya, February 1, 2017.

Serikali inaposhindwa kujua faida ya mradi wa DRT

Image result for photos mabasi ya mwendo kasi
            Hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli  akiwa ameandamana na makamu wa rais wa Benki ya Dunia (WB) kwa Afrika, Makhtar Diop alizindua awamu ya kwanza ya magari yaendayo kwa kasi jijini Dar es Salaam (DRT). Mradi huu wa kipekee katika Afrika Mashariki na Kati ni jambo la kujivunia kama litaleta faida na kukidhi matarajio ya watanzania.
            Pamoja na hadhi ya mradi husika ambao umejengwa kwa mkopo toka Benki ya dunia, wapo wanaooanza kushuku uwezekano wake wa kufikia malengo. Mmojawapo ni rais mwenyewe ambaye vyombo vya habari vilimkariri akimtaka waziri wa usafirishaji amueleze faida itakayopata serikali kutokana na mradi wa husika. Hili liliwashangaza wengi hasa wanaojua namna taifa letu lilivyofikishwa lilipo kifisisadi. Kama rais, nasi tunauliza, je huu mradi unaweza kuwa na faida kisiasa japo si kiuchumi? Tunaweza kujivuna kuwa tuna mradi mkubwa na wa pekee barani Afrika. Je hilo ndilo wanalotaka watanzania ambao ndiyo wenye fedha inayokopwa kwani watailipa siku moja?
            Tukiangalia waliopewa kuendesha mradi huu ambao sasa unaitwa UDART mbali na utata unaoghubika zoezi zima, tunapata shaka kama watanzania watapata faida waliyotarajia tokana na mradi huu unaojengwa kwa fedha yao. UDART ni muunganiko wa kampuni ya iliyokuwa ya Usafiri Dar Es Salaam (UDA) pamoja na  Dar Es Salaam Rapid Transit (DART).  Kuungana si jambo geni. Ila inapokuja kuwa muungano huu ni wa watuhumiwa na asasi ya kiserikali, unapata taabu na kushindwa kuelewa mantiki ya muungano huu rangi mbili.
            Kwa wanaojua historia ya namna UDA ilivyouawa na kutwaliwa kifisadi huku serikali zilizopita na hata ya sasa zikiendelea kupiga dana dana, watakuwa wanashangaa mantiki ya watwaaji wa UDA kuaminiwa kuendesha mradi mkubwa wa umma kama huu wakati hawana hata chembe ya imani tokana na kashfa ya utwaliwaji wa UDA. Ni vigezo gani vilitumika kuteua UDA kuendesha mradi wakati ni watuhumiwa  wa kuhujumu umma ambao hawajawahi kukanusha kwa kutoa ushahidi unaoingia akilini kuwa walijitwalia iliyokuwa shirka la Usafirishaji Dar Es Salaam (UDA)? Kwa vile walioua UDA; na hatimaye kuitwaa bado wako pale pale, je hii haiwezi kujenga dhana kuwa hata DART itauawa na kutwaliwa kama UDA hasa ikizingatiwa kuwa walioko nyuma ya hujuma hii si hawa tunaowaona wakijiita wamilki na wakubwa wa UDA wakati historia zao hazionyeshi chembe ya ujasiriamali wala namna ambavyo wangeweza kuwa na mtaji wa kununua UDA kama wanavyodai. Kama ukimdurusu Simon Kisena, hupati historia yoyote inayoonyesha ana uwezo wa kuwa na fedha zinazodaiwa kulipwa kwa serikali kama manunuzi ya hisa zake ambazo nazo ni utata mtupu. Tunapaswa kujua mchakato na namna watuhumiwa kama hawa walivyopata tenda ya kuendesha mradi wa wananachi wale wale waliowaibia shirika lao. Tunapaswa kujua na vyanzo vya fedha iliyotumiwa kununua hisa kama kweli ziliuzwa.
            UDA ni bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote kama serikali itaamua kutimiza wajibu wake. UDA ni jipu linalopaswa kutumbuliwa haraka bila kujali ni nani wako nyuma ya hujuma hii kwa taifa. Huu si wakati wa kulindana na kuoneana aibu. Najua rais alisema kuna makaburi hatayafukua kwa kushindwa kuyafukia. Pamoja na msimamo huu, nadhani kelele za waathirika–yaani wananchi–zitaendelea kumuandama hadi atende haki kama alivyoapa kufanya. Na hakika; umma unaotaka haki na kuchukia maovu, hautanyamaza kumkumbusha rais na serikali yake kutekeleza wajibu wao bila upendeleo wala uonevu.  Inashangaza kwa taifa kuendelea kuchukua mikopo toka kwenye taasisi za kimataifa na nchi mbali mbali na kuishia kuwapa mafisadi wanaojulikana miradi itokanayo na fedha hii waihujumu kwa kisingizio cha kuiendesha. Wezi wa UDA hawana udhu wa kuweza kusimamia mradi wowote wa taifa.  Historia ya utwaliwaji wa UDA inaonyesha uchafu sawa na kashfa nyingine kama vile IPTL, Kagoda, EPA, ESCROW, Lugumi na nyingine nyingi ambazo serikali inaonekana kuzigwaya kutokana na vigogo walioshiriki kuzitenda. Mbunge wa Kawe Halima Mdee alinukuriwa hivi karibuni akipinga wizi wa UDA akisema “naliambia Bunge msije mkathubutu, maana nimesikia mara zile Sh bilioni 5 alizolipa Simon Group zipangiwe matumizi, naomba niwaambie sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu, sasa kama hatujitambui na Serikali inataka kuingilia, hatuwezi kutumia hii shilingi bilioni 5 kuhalalisha haramu kuwa kitu kitakatifu.”
            Mwisho, inashangaza mantiki ya serikali kutumia jumla ya shilingi 39.6bn ambazo zililipwa kwa kampuni ya kichina Beijing International Engineering Group (BCEG) kujenga miundo mbinu ya mradi na kuruhusu kampuni yenye thamani ya blioni 5 kuwa mbia katika kuendesha mradi huu. Je mgawanyo wa hisa baina ya UDA na DART ni upi? Je ni UDA hii hii ambayo Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali (CAG) alishauri hisa zake zirejeshwe kwa serikali na kuchunguza namna UDA ilivyotwaliwa kifisadi?. Kashfa ya UDA imegeuka donda ndugu kwa taifa letu. Alipoingia rais Magufuli na tumbuatumbua yake, wengi walidhani angekuwa na ujasiri na uzalendo wa kutumbua jipu hili. Ukweli ni kwamba hatafanya hivyo. Ushahidi uko wazi kuwa kitendo cha serikali yake kuridhia waliohujumu umma kwa kuiba Shirika lake la UDA ndiiyo hao hao walioaminiwa kuendesha mradi tena mkubwa kuliko ilivyokuwa UDA yenyewe. Swali muhimu hapa ni: Kama serikali haijui faida ya mradi wa DRT, nani anajua sasa?
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

Mpayukaji Ahudhuria Kikao cha Wanene Addis Ababa

          Baada ya wanga na woga wengi kudai kuwa nina woga wa kusafiri ughaibuni, nimeamua kuwatoa nishai ili waaibike na kushushuka. Si wapo waliosema kuwa sitakwenda kwenye kuhudhuria genge la wanene wenzangu barani kwa vile ni mwoga wasijue nilikuwa nasukuti na kujipa shule kabla ya kwenda kule na kuchemsha. Mie siyo kama vimbelembele waliozoea kukesha kwenye madege wakienda ughaibuni kutia aibu na kujiaibisha hadi wengine kupewa nishani uchwara na matapeli ukiachia mbali wengine kupewa udaktari uchwara wakautumia kana kwamba wamesomea wakati ni vihiyo wa kawaida.
            Mwenzenu baada ya kumtimua Yaya Jammeh, nimeamua kupitia zangu Addis lau kutia tafu wenzangu kuhakikisha tunaandaa mkakati wa kuwatimua wanene wa wachovu hasa marahis wanaogeuza ikulu kuwa mali binafsi. Haiwezekani watasha wakaendelea kutucheka kwa kukumbatia maimla wakati tunao uwezo wa kuwatoa nkuku kama alivyofanyia Jammeh ambaye huko aliko mafichoni atakuwa anamiss shoptalk ya Addis aliyozoea kuhudhuria na kujidai huku akimwaga pumba zake na kujivisha kama mmanga wakati nimmakonde wa kawaida tena asiye na hata hiyo dini anayopwakia. Atakuwa akitoatoa mimacho na kujilaumu kwa kushindwa kuchakachua uchaguzi uliomtupa nje bila yeye wala dunia kutegemea. Ama kweli kila chenye mwanzo shurti kiwe na mwisho. Hata hivyo, anabahati hakunyotolewa roho kama swahiba yake Kashafi wa Libya aliyekufa akilia kama kichanga baada ya wachovu wa kule kumgeuzia kibao.
            Napanga kutoa mada juu ya demokrasia, uwajibikaji na uchaguzi huru na wa haki bila kusahamu kuheshimu katiba za kaya ambazo sasa zinadhalilishwa na marahis wengi kwa kutaka ulai rahisi utokanao na kung’ang’ania urahis na kubadili katiba. Nakwenda kuwapasha wanene wote waliochakachua ima katiba au uchaguzi na kuendelea kuwa maulajini kinyume cha sheria. Hapa sitajali nani tunatoka ukanda mmoja au rafiki bali kutoa dozi kama sina akili nzuri. Hapa ni mipasho tu kama kazi au vipi?
            Japo wakubwa wezi walionitangulia kuongoza kaya hii ya Danganyika walizoea kuandamana na utitiri wa walaji huku wakiifanya misafara yao kuwa siri, mie sifichi. Nasikia hali ilikuwa mbaya hadi kufikia hata vigagula kuwa kwenye msafara wa munene. Kwa kazi gani kama siyo ujinga na ujuha wa mwaka? Kufanikisha ujinga na ufisadi wao wengi walizoea kuondoka usiku ili kuficha yale mabomu waliyokuwa wakiandamana nayo. Kuonyesha nisivyo na cha kuficha nimeondoka mchan nikiwa nimeandamana na waziri wangu wa Mambo ya Ughaibuni Mghoshi  Machungi na maafisa wachache ili kubana matumizi. Vikao kama hivi siyo sehemu ya kufanyia sherehe na kupeleka washamba kwenda kutoa tongotongo.  Huwa sipendi kutumia njuluku za wadaganyika kwenye  mambo ya kilimbukeni na kishamba wakati wanaihitaji kwa ajili ya mambo mhimu kama vile Afya, Elimu na mambo mengine muhimu. Mie si mchoyo wala sina roho mbaya kama wale walionitangulia ambao walisumbuliwa na roho mbaya na ushamba wakidhani wangeweza kuizunguka dunia nzima. Hata kama walifanya hivyo, ili wapate nini zaidi ya kuendelea kuwa waja kama wadanganyika wengine? Kuoneyesha nilivyo serious, hata bi mkubwa sikuandamana naye hasa ikizingatiwa kuwa hana anachokwenda kufanya kule. Huu ni mkutano wa wakuu na si wake wa wakuu wala waramba makalio ya wakuu.
            Pili,  sikusafiri kwenye business class kama wale washenzi na washamba waliozoa kutumia daraja hili wakati walikuwa wakiongoza kaya kapuku. Huu nao ni ufisadi ambao ulipaswa kufumliwa na walioutenda kuwajibishwa kama siyo kuogopana na kulindana vinavyoanza kuchipuka kimya kimya. Mijitu mingine kwa ulimbukeni sina mfano. Ukienda huko madongo ilikozaliwa usafiri wao ni wa punda na mikokoteni. Lakini ikishapata ulaji hujisahau na kujifanya siyo ile iliyozaliwa na kulelewa kwenye vitanda vya kamba na kulalia ngozi za mbuzi na kondoo. Hawa nao nitawapasha bila huruma wala aibu.
            Tatu, baada ya kumaliza kutoa mada yangu ya demokrasia, uwajibikaji na uchaguzi huru na wa haki, nina mpango wa kutoa pendekezo kuwa ving’ang’anizi wote waliomo maulajini waanze kufungasha virago ili kupisha mawazo mapya yatawale kaya ambazo wamezibaka kwa miaka. Kabla ya kuendelea, hivi juzi mlimsikia M7 akiwazodoa  Wagandaji kuwa yeye si mtumishi wa yeyote utadhani kaya ni mali yake binafsi?  Ana bahati mjivuni huyu. Ingekuwa majuu angefungashiwa virago siku hiyo hiyo ili wachovu wapate kiongozi mtumishi na si bwana kama huyu jamaa aliyeng’ang’ania ofisi kwa zaidi ya miongo mitatu. Inaonekana madaraka yamamempanda kichwani kiasi cha kuanza kujichanganya kutokana na kuchanganyikiwa na kuchanganya mambo. Inawezekana anaanza kutabiri anguko lake kama Jammeh litakalotokea bila kutegemewa na kwa namna isiyotarajiwa. Kwani akina Compaore, Jammeh hata Kashafi walitegemea kung’oka? We ngoja tu. Jamaa yangu Msomi anasema huyu jamaa anaweweseka baada ya kuondolewa maimla wawili japo kwa njia tofauti yaani Blaise Compaore na Jammeh. Anahofia Wagandaji wanaweza kuamka na kumfanyia kitu mbaya kama ambavyo amekuwa akiwafanyia kwa miongo zaidi ya mitatu.
            Kwa vile nina ishu nyingi za kushughulikia, acha niachie hapa ili niende kuwapasha waduwanzi wanaotumia njuluku za wachovu vibaya kwa kujilisha pepo na kutoa tongotongo. Special greetings to all Vasco da Gamas of this world. Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.