Kibonzo kwa hisani ya gazeti la Daily Nation, Feb., 8, 2017. |
Hivyo, kwa waliosoma makala hizo wanaweza kushangaa kwa kusoma makala hii. Hata Makonda mwenyewe atashangaa kutokana na kutojua kuwa mimi sina chama zaidi ya Tanzania wala dini zaidi ya Haki na Ukweli. Hivyo, leo nachukua fursa hii kuandika barua hii rasmi kwa ndugu Makonda.
Kwanza, nakupongeza kwa hatua zako za hivi karibuni za kuthubutu kuwanyoshea kidole watuhumiwa wa biashara ya mihadarati bila kujali nafasi zao katika jamii. Hili ni jambo la kupigiwa mfano hasa ikizingatiwa: hakuna kiongozi awe mdogo au mkubwa aliyejaribu kufanya kama ulivyofanya hivi karibuni. Hongera sana ndugu Makonda na Mungu akulinde usafishe Dar es Salaam ili uwe mfano kwa nchi nzima.
Pili, nakupongeza kwa kujitoa mhanga kama ishara ya uzalendo na upendo kwa taifa tena vilivyotukuka. Kwani, ulisema wazi kuwa hugopi kufa ikibidi. Hii ni kuonyesha usivyobabaisha wala kuogopa. Tunakuunga mkono; hasa tukizingatia kuwa kadhia ya mihadarati, licha ya kuangamiza maisha ya vijana wetu ambao ndiyo nguvu kazi, inachafua heshima na sifa ya taifa letu.
Tatu, umeonyesha ujasiri na kutokuwa mwoga ukiachia kuvunja mwiko kuwa biashara ya mihadarati inaongeleka na kuweza kushughulikiwa; kama atapatikana mtu wa aina yao ambaye tunashauri rais akupe ulinzi na usaidizi wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa vita uliyotangaza si lelemama, uwezekano wa kushinda ni mkubwa. Laiti akina Lameck Mwigulu Nchemba, waziri wa mambo ya ndani, hata rais mwenyewe, wangekuwa na hata robo ya uthubutu yako; mihadarati ingekuwa historia. Hata hivyo, hatuwezi kumshuku rais hasa ikizingatiwa kuwa ndiye aliyekuteua kwa kujua ujasiri na ithibati vyako.
Sasa nini kifanyike? Tunashauri ufanye yafuatayo ili kufanikisha vita hii adhimu na muhimu dhidi ya mihadarati:
Mosi, kukubali kuwa vita hii ni hatari na si ya kawaida. Hivyo, inahitaji maandalizi na umakini wa juu kuweza kuishinda mfano kuwalinda watoa taarifa na kuhakikisha wanachunguzwa ili kuepuka kupokea taarifa zinazopotosha au kukomoana tena zinaweza kutengenezwa na wauza mihadarati wenyewe ili kukukatisha tamaa kama njia ya kujiponya.
Pili, mwendee rais mstaafu Kanali Jakaya Kikwete ambaye alikuteua mara ya kwanza kuwa mbunge wa Bunge la Katiba ili akupe ile orodha ya wauza unga aliyowahi kudai alipewa na vyombo vya usalama akagwaya kuishughulikia tokana na sababu ajuazo mwenyewe. Hivyo, kuna mahali pa kuanzia. Niliwahi kushauri rais Magufuli atumie mamlaka yake kumtaka mtangulizi wake atoe orodha ile hasa ikizingatiwa kuwa si mali binafsi ukiachia mbali kuikalia kuwa mchango mkubwa na motisha kwa wauza mihadarati.
Tatu, anzisha utaratibu wa kuhakiki mali za watuhumiwa na wale wote wanaoonyesha kuwa na ukwasi wa haraka bila kuweza kueleza walivyoupata tena kwa muda mfupi. Ni bahati mbaya kuwa Tanzania inaruhusu watu kujitajirikia bila kuonyesha walivyochuma huo utajiri kiasi cha wezi na wauza wengi kuwa kero mitaani wakijidai na kununua mali kila mahali wakati wanajulikana walivyo wahalifu. Bila kubadili mfumo huu na kuwa na sheria inayomtaka kila Mtanzania kueleza alivyochuma utajiri wake kwa njia ya kujaza fomu za mali na kodi kila mwaka, uwezekano wa kushinda vita hii ni mdogo.
Tatu, kamata watumiaji au wasambazaji wadogo wadogo na kuwahoji kwa kuwaahidi msamaha ili wawataje mabosi wao katika jinai hii. Inashangaza kuona watajwa wengi ni makoplo wa polisi na wasanii waganga njaa ambao kimsingi ni dagaa. Je hayo mapapa yanaachwa ili iweje? Inajulikana kuwa polisi wadogo hukusanya fedha na kuwapelekea wakubwa zao na si kwenye madawa tu hata kwenye rushwa kama vile za barabarani.
Nne, kamata kimya kimya watuhumiwa wote kisha utangaze baada ya kukamata ili kuepusha kuwastua wengine. Hapa lazima kuitambua na kuiainisha mitandao ya biashara ukubwa na mbinu zake ili kuweza kuishughulikia vizuri kisayansi, vilivyo na kwa ufanisi.
Tano, weka makachero bobezi na waaminifu watakaonunua au kuuza huku wakirekodi kila kitu ili kuwa na ushahidi wa wazi kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Kenya ambapo Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) liliweka mitego ya namna hii na kuwanasa vigogo maarufu wa unga wa famili ya Akasha hivi karibuni. Hawa jamaa walikuwa wamefanikiwa kuwahonga polisi, majaji na wanasiasa kiasi cha kutokamatika. Hivyo, ikibidi, tafuta msaada nje ya nchi ili kupambana na hawa wahalifu wanaoangamiza taifa kwa tamaa zao hata wawe ni wakubwa kiasi gani kama umedhamiria. Hapa ndipo rais anapaswa kukusaidia zaidi ili kuweza kushinda biashara hii ngumu na hatari ambayo inahusisha hata wale ambao huwezi kuwadhania tokana na hadhi zao katika jamii. Wapo wanaojifanya watu wa dini wakati ni wauzaji wakubwa wa mihadarati na wengine wengi kama vile wasanii tena maarufu na hata wanasiasa.
Tumalizie kwa kukupongeza angalau kwa kutoa mfano wa kuanzia kupambana na kadhia hii ambayo imegeuzwa serikali ndani ya serikali na haramu iliyohalalishwa tokana na woga, tamaa na unafiki wa watendaji wanaopaswa kupambana nayo. Mungu akutangulie Makonda.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
No comments:
Post a Comment