Baada ya dogo Po kuwatibuliwa wanene, wasanii na ndata kwa kuwatuhumu baadhi yao kuwa wanasepa na mibwimbwi nimesikia walevi wengine wakilalamika kuwa walishukiwa kuuza bwimbwi; na hivyo kuchafuliwa majina yao na kuvunjiwa heshima katika dugudwa hili. Tangu lini kumshuku mlevi ikawa kumvunjia heshia? Kwani kaya ya walevi imegeuka ya malaika? Huwa sielewi madai ya namna hii hasa ikizingatiwa kuwa chini ya sheria ya kaya wanakaya wote ni sawa isipokuwa mtukufu rahis ambaye yuko juu ya sharia. Ajabu ya maajabu, wale wanaolalamika kuwa wamedhalilishwa walidhalilika zamani kutokana na shughuli zao za kutia kila aina ya shaka katika jamii. Hivi jitu linalokurupuka na kutangaza kuwa linatenda miujiza wakati ni uongo mtupu halijadhalilika? Nani anaweza kutenda miujiza usawa huu? Kama kweli mnatenda miujiza, basi itendeni sasa mnapokabiliwa na shutuma za kuuza bwimbwi.
Tuache utani jamani na kuchunguza dafina za mioyo yetu. Hivi mwanakaya kapuku ambaye hata kazi zake hazieleweki kulala maskini na kuamka tajiri si alama na ushahidi kuwa kuna tatizo hasa njia haramu za kupata utajiri? Wanagapi wanakula haramu itokanayo na kuwaibia au kuwarubuni walevi waliokwama kimaisha na kuukata huku waathirika wao wakiendelea kuhangaika? Mnajipachika vyeo na kufanya mambo ya hovyo halafu tuwaache siyo? Huwezi kuwa tajiri bila maelezo na ukakubalika katika jamii. Kama mlizoea utawala wa kijambazi sasa mtakoma na kukomaa. Ni wangapi wanamilki mindinga mikali hata mapipa wakati hawana kazi yoyote ya maana zaidi ya kuwapigia kelele walevi kwa kisingizio cha dini? Nani anahitaji dini usawa huu ambapo kila mlevi anajua anachopaswa kufanya kama kiumbe wa Mwenyewe aliye juu? Unafiki na ubabaishaji mtupu. Baadhi ya walevi wanajipachika vyeo vikubwa na vitukufu huku wakifanya usanii wazi wazi na kijinga kama kuponya wagonjwa na kutenda miujiza ya uongo na ukweli. Narudia tena. Fanyeni hiyo miujiza yenu ili tuhuma za kuuza bwimbwi ziwatoke badala ya kulalamika. Kwani hatuwaoni wala kuwajua? Juzi juzi mtuhumiwa wa bwimbwi mmojawapo alijifanya kuwa amepooza na kujiombea na kupona. Ukimwambia nenda Muhimbili ukawaponye wenye ulemavu anaanza stori za kuwa hadi uponywe lazima uwe na imani. Ni mgonjwa gani asiye na imani wakati ana shida ya kupona? Tumegeuza kaya kuwa ya washirikina na wababaishaji tokana na ujinga wa kimfumo. Hapa lazima rais Kanywaji afanye kweli kuhakikisha kaya inaondokana na upuuzi na ujinga huu wa ajabu. Napendekeza akamate mali zote za wale walioukata bila maelezo ili tuanze kuheshimiana na kufanya kazi badala ya kupiga politiki na kuhubiri ujinga. Tangu lini mganga akajiganga kama si ujinga na upuuzi? Mlizoea mfumo wa hovyo wa kukwapua. Sasa mtakoma na mkomae. Tunataka kila mlevi aeleze alivyochuma ukwasi wake kwa wale wenye ukwasi wa ghafla bin vu tena wa kutia shaka.
Inakuwa shaka zaidi kwa wale wanaodai wameokoka kuwa matajiri wakati yule wanayedai kumhubiri alikuwa kapuku wa kutupwa hadi kushindwa hata senti tano ya kulipa kodi hadi alipomkopa samaki. Wapo waliosema kuwa walipaswa kupigiwa simu. Sheria gani hii iwapo kila mwanakaya anaweza kutuhumiwa? Mbona Yesu alipotakiwa kwa Pilato hakupigiwa simu? Wao ni nani zaidi ya kutapatapa? Kama huuzi bwimbwi si uende ueleze na kuwasuta waliokutuhumu badala ya kutupigia mikelele?
Nadhani baadhi ya wana kaya walisahau kuwa mfumo wa kijambazi uliokuwa umeanzishwa na tawala uchwara zilizopita ambapo kila mhalifu alikuwa akijihudumia ungefikia mwisho. Well, kila kilicho na mwanzo shurti kiwe na mwisho ndugu zanguni. Kubalini mmefulia; na imekula kwenu usawa huu wa dokta mtumbua majipu ambaye hana mchezo na mtu. Kwanini hamkubali kuwa hakuna kasma wala bajeti ya kuwapigia simu watuhumiwa? Kama hutaki kuchafuliwa au kushukiwa basi fanya mambo yanayoeleweka kama mimi ambaye nimeokoka kweli kweli na hivyo situhumiwi kwa vile maisha yangu ni mambo hadharani?
Juzi jamaa yangu anayejidai kaokoka katoa mpya pale tulipokuwa tukikamata kanywaji pale uwanja wa Hyena. Baada ya kumpa pole kwa kutuhumiwa na kusema ni kwanini yeye na si wengine si alijibu “hata kama nauza bwimbwi wewe yakuhusu nini wakati nimeishakwambia kuwa nimeokoka? Nikishasema nimeokoka kila kitu kinasamehewa. Hivyo, hakuna anayepaswa kufuatilia misele na mishemishe zangu isipokuwa bwana mwenyewe aliyeniokoa.” Upuuzi kiasi gani? Yaani kila mmoja akisema ameokoka wakati anahitaji kuokolewa tumwamini? Lalamikeni pale mnaponyimwa nafasi ya kujitetea; kutuhumiwa si kosa wala uonevu bali utaratibu wa kisheria.
Nimalizie kwa kusema wazi; mie siuzi wala kubwia bwimbwi. Hivyo, nikituhumiwa sitalalamika bali kwenda kumwaga nondo za kuthibitisha kuwa tuhuma zangu si za kweli badala ya kujificha kwenye kuokoka. Simpo.
Chanzo: Nipashe Jumamosi kesho.
No comments:
Post a Comment