Waswahili wana msemo kuwa muosha naye huosha. Pia husema kuwa ukijua huu wenzio wanajua ule. Baada ya mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda kuwatuhumu wenzake kuwa walikuwa wakipokea rushwa kwenye sakata la shisha jijini Dar, sasa amegeuziwa kibao na wabunge wanaotaka achunguzwe ili kubaini ukweli wa mambo yake hasa umilki wa mali zenye thamani ya mamilioni na kuweza kwenda nje kutanua.
Mbunge wa Kawe, mheshimiwa Halima Mdee alisikika bungeni akihoji waliomfadhili Makonda kwenda kutanua ughaibuni kwa muda mrefu tofauti na kipato chake. Tokana na shutuma hizi, wengi tunajiuliza; je ni wakuu wangapi wa mikoa wamekwenda nje kutanua kama Makonda? Yeye ana nini cha mno? Mdee alikwenda mbele na kudai kuwa huenda Makonda alifadhiliwa na wauza unga kwenye safari yake ya ughaibuni hivi karibuni. Je ni kweli alikwenda ughaibuni kutanua tena kwa kufadhiliwa na fedha chafu? Je alijilipia mwenyewe? Wabunge walitaka kujua kama mshahara wake, kwa muda mfupi aliokuwa ofisini, ungemewezesha kufanya hayo.
Mbali na Mdee, Mbunge wa Geita Vijijini, mhesimiwa Joseph Msukuma (CCM), aliongoza mashambulizi alipokaririwa akisema “RC wa Dar es Salaam anamiliki ma-V8 na Mwanza amejenga maghorofa ndani ya mwaka mmoja. Je, ni akina nani hao wanaomfadhili kupata mali hizo?” Kama haitoshi, Msukuma alionekana kuungana na Mdee kuhusiana na safari ya Makonda ughaibuni na nani walimfadhili akisema “wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.” Makonda hakwenda Marekani tu. Msukuma anasema “kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshahara upi alionao?” Msukuma anaonekana kujua mengi kuhusiana na Makonda. Kwani aliongeza kusema kuwa “kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janet anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?”
Tuhuma hizi, licha ya kuwa nzito, zimetolewa na watu wazito wanaowakilisha watanzania wengi tokana na nafasi zao. Hivyo, haziwezi kuchukuliwa kivyepesi. Zinapaswa kupewa uzito na kuchunguzwa na matokeo ya uchunguzi wake kuwekwa hadharani. Kwa namna hiyo, Makonda anapaswa kuwekwa kando kupisha uchunguzi ili aweze kusafishwa au kukutwa na hatia. Huu ndiyo uongozi bora; na hakuna anayepeswa kuwa juu ya sheria.
Tunaomba yafayike yafuatayo haraka:
Mosi, mamlaka husika kuchunguza madai dhidi ya Makonda yawe ni ya kushirikiana na au kunufaika toka kwa wauza unga au kumilki mali nyingi tofauti na uwezo wake kisheria. Tungependa haki itendeke kwa kumhoji na kushughulikia mhusika kama alivyosema rais John Magufuli kuwa hata kama akiwa ni mkewe akamatwe. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha, kama alivyodai Mdee, kuna baadhi ya watendaji wa serikali wanasikilizwa zaidi ya wengine kiasi cha kuaminiwa bila sababu ya msingi au kutoshughulikiwa wanapotuhumiwa. Mfano rahisi ni pale Makonda alipowatuhumu Makamanda wa polisi Simon Sirro na Suzana Kaganda kupokea rushwa toka kwa wauza shisha. Hakuitwa na vyombo husika kumhoji wala kutoa taarifa ya matokeo ya mahojiano na uchunguzi wa sakata husika. Hii ni tofauti na ni kinyume na dhana nzima ya utawala bora na wa sheria. Na rais Magufuli asipoangalia, hili litamkwamisha na kuweza hata kumchafulia. Kwani amekuwa akiunga mkono kila anachofanya Makonda kiasi cha kujengeka dhana kuwa yeye ndiye anayemtuma. Je anamtuma kweli? Sidhani kama Magufuli anahitaji kujificha nyuma ya Makonda hasa ikizingatiwa kuwa si mwoga. Je Makonda anapata wapi au kinga hii dhidi ya madai anayotoa? Jibu au majibu yatapatikana kutokana na namna serikali itakavyoshughulikia tuhuma hizi zilizotokewa na wabunge tena nyingi zikitolewa na wabunge wa CCM. Hakika, huu ni mtihani mwingine kwa Magufuli.
Pili, kama Makonda yu safi na tuhuma zinazoelekezwa kwake ima ni za uongo au zinalenga kumkatisha tamaa na kumwamisha, atafurahia ushauri huu na kuwa wa kwanza, kupisha uchunguzi na kutaka achunguzwe ili ukweli ujulikane ili aendelee na vita hii aliyoanzisha ambayo imewashinda wengi. Maana, kwenye shughuli za umma hakuna cha kuaminiana ukiachia mbali kuwa tetesi mara nyingi huelekea kwenye ukweli. Tusimhukumu Makonda kabla ya kufanyika uchunguzi hasa ikizingatiwa kuwa mitandao ya wauza mihadarati inajuana na kupigana vita.
Je mwanzo wa mwisho wa Makonda ndiyo unaanza? Je yanayosema juu ya Makonda ni kweli au siasa? Je ni yale ya ivumayo haidumu? Je Makonda ataendelea kuwa kitendawili au mamlaka zitazinduka toka usingizini na kumtendea sawa na watuhumiwa wengine?
Tumalizie kwa kumtaka Makonda na serikali kuanza uchunguzi mara moja ili mbivu na mbichi zilijulikana na kuendelea na mapambano yetu dhidi ya janga hili la kitaifa. Pamoja na mapungufu yatakayojikeza, tuseme wazi; Makonda angalau amethubutu na kujaribu pale wengi waliposhindwa. Atusaidia katika hili ili kukata mizizi ya fitina. Naomba kutoa hoja.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment