Mpemba anaingia akiwa na bashasha. Lazima ana jambo la kutujuza lau tulidurusu na kutongoa huku tukitoa mapendekezo ya nini kifanyike kama suluhu ya tatizo liwe la kibinafsi au kitaifa.
Baada ya kuamkua, Mpemba anamwaga pwenti “jamani mmesikia kilivoumana kuhusiana na biashara haramu ya bwimbwi? Maana naona pachimbika bila jembe ati. Kila ntu asamaka Makonda hadi watuchanganya. Iweje leo ndiyo waamue kuanika siri za Makonda au nao wameguswa pabaya? Huko nyuma mbona hawakuwa hivyo. Au wote ni wale wale?”
Kapende anampoka mic na kuronga “wewe unaamini kuwa vita hii dhidi ya wauza bwimbwi inaweza kufanikiwa wakati inaonekana kufanyika kienyeji na kisiasa?”
Mpemba anajibu “wamaanishani kusema eti vita yapiganwa kisiasa na kienyeji?”
Kapende anajibu “uliona wapi watuhumiwa wanaitwa kwa ndata na kuachiwa wakati siku zote wezi wa kuku wanapotuhumiwa huozea lupango; sijui nani anataka kumdanganya nani katika sanaa hizi?”
Mipawa anakwanyua mic “hata mimi nilidhani ni usanii hasa pale walipokamatwa dagaa huku mipapa ikipeta. Lakini baada ya kuona na watukufu wakiitwa kwenda kujieleza, nilianza kujenga imani ingawa bado nina shaka na utaratibu mzima unaotumika wa kishikaji.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia daluga. Anakohoa kidogo na kudema “ yote yanawezekana hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mwanzo. Nadhani wengi mnashuku zoezi hili tokana na udogo wa aliyetanga na wale waliokamatwa mwanzo na namna walivyoshughulikiwa. Mie nafurahi kuwa angalau wanene wameamua kusema kitu hata kama si jibu. Maana ilifikia mahali bwimbwi na ufisadi vilihalalishwa. Napenda nitoe ushauri kuwa lisirikali linapaswa kuangalia mfumo mzima ulioweza kumotisha na kuruhusu baadhi ya wahalifu kumaliza vijana wetu kwa bwimbwi. Hivyo ningependa yafanyike yafuatayo: kila mwanakaya aeleze alivyochuma ukwasi wake huku wale watakaoshindwa kutoa maelezo mali zao zikamatwe na watupwe lupango.”
Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi anakula mic “hapa Msomi umenena. Tingependa wae wote tinaowajua kuwa wana ukwasi wa haamu lazimu tiwataje na washikwe kwanza haafu mengine yafuate.hapa bia shaka wanapaswa kutieeza waivotengeneza ukwasi huu kama hakuna kitu nyuma ya pazia.”
Msomi anaendelea, “ukiachia mbali kukamata mali haramu, nashauri lisirikali lipige marufuku mianya yote ya uchumaji utajiri haramu kama vile baadhi ya wenzetu kujipachika vyeo vikubwa vikubwa vya kidini huku wakivitumia kuwaibia wachovu wetu kwa vile wana matatizo na ni wajinga. Hamjaona uchunaji ulivyogeuka uchochoro wa kutengeneza njuluku haraka? Nijuavyo, Yesu alikuwa kapuku. Sasa inakuwaje mtu anahubiri tu na kugeuka milionea hata bilionea ghafla bin vu wakati kazi anayofanya haina kipato kikubwa kama hakuna namna?”
Kanji anamchomekea “Somi mimi kubali veve sana dugu yangu. Iko vatu tajiri sana. Kama nauliza veve iko fanya kazi gani, hapana jibu zuri. Kama piga kelele naingiza juluku haraka sana mimi iko anza hubiri ili nipate juluku haraka.”
Mijjinga anakatua mic “mimi ni mchumi. Huwa sielewi namna ambavyo jamii inaweza kuruhusu jinai hii halafu isikumbwe na hatari kama hii ya kuuza bwimbwi na ujambazi mwingine bila kusahau ufisadi. Anayeiba sadaka au kuwatoza wachovu njuluku ili awahudumie hana tofauti na mwizi. Kwanza hawa wezi hawalipi kodi. Nashauri watozwe kodi na kuwekewa mfumo wa kuhakikisha wanaonyesha vyeti vya taaluma ya hayo wanayosema wanaweza kufanya kama vile kutenda miujiza na ujambazi mwingine ulioanza kuhalalalishwa kwa mlango wa nyuma tokana na kuwa na tawala uchwara zilizopita ambazo ziliruhusu kila mmoja ajiibie wakati wakubwa nao wakihomola na kufuja.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anabusu mic “mie naunga mkono mapambano dhidi ya bwimbwi. Kwani hapa tunapoongea kaka yangu ni teja. Alikuwa amesoma vizuri na kazi nzuri lakini ameharibiwa na mibwimbwi kiasi cha kugeuka mzigo kwa familia. Hapa lazima kila mmoja wetu ashiriki vita hii kwa kutaja anaowajua ilmradi asiseme uongo wala kuonea mtu. Nafurahi kuwa wamethubutu hata kama ni kwa njia za kutia shaka.”
Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic. Ansema “da Sofia tafadhali niruhusu nikuchomekee kidogo hapa. Nakubaliana nawe ingawa napingana na baadhi ya mawazo yako. Napendekeza kuwepo na utaratibu wa kisheria unaoeleweka ili kuepuka uwezekano wa baadhi ya wanene kuwamaliza maadui zao kisiasa au kuwaachia washirika wao kwenye balaa hili. Hii vita ni kubwa kuliko tunavyodhania. Hivyo, ningeshauri rahis mwenyewe awe taskforce yake ya kushughulikia balaa hili kwa mujibu wa sheria na kwa haki na usawa bila kujali cheo au jina la mhusika.”
“Hakuna kilichoniacha hoi kama waheshimiwa wa njengoni. Wanashangaa kwanini Makonda asafiri na kwenda kutanua ughaibuni na nkewe tena kwenye business class wakati Dk Kanywaji alipiga marufuku kwenda kutanua nje? Je ni wakubwa wangapi wa mikoa wamekwishakufanya hivyo? Hapa napo kuna so washikaji. Wengine wanasema jamaa ana ukwasi kama Bill Gates. Sijui hapa muongo na mkweli ni nani na kwanini sasa?” anakula mic Mijjinga.
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapia Humvee la Makonda. Acha tulikate shingo kwa mshangao namna jamaa alivyochanganya njuluku haraka!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment