Pamoja na kutolewa kwenye famÃlia maskini na umaskini unaonuka mbali na kukosa hata hizo sifa za chini kabisa kufaa kuolewa, huyu mama tunayemouna mpumbavu, alijiona msomi wa kupigiwa mfano wakati alikuwa mjinga asiyemithilika kama tutaangalia dhana ya usomi ni nini. Kwa ufupi, usomi siyo wingi wa shahada au miaka mingi darasani bali unyenyekevu na utayari kusaidia wengine. Ni kama mtu aliyebahatika kufumbuliwa macho anayeishi na vipofu au vyongo. Ni sawa na tembo anayeishi na wanyama wadogo wanaotegemea awasaidie maadui zao wanapowazengea. Usomi ni kujua udhaifu wako na kutambua ubora wa wengine hata kama unawazidi elimu. Huu ndiyo usomi tunaomaanisha hapa.
Maisha na ndoa havina shahada zake bali unyenyekevu na kuwa tayari kunyenyekea na kuujua ubora na udhaifu wako na wa wengine. Hivyo, hata kama wewe umesoma kweli kuliko mwenzio, kisiwe kibali au nyenzo kumdhalilisha, kumdhulumu, na kumdhalilisha mwenzi wako hata wengine. Usomi si ubabe na majivuno bali unyenyekevu.
Turejee kwenye kisa chetu. Mama huyu mjinga wa mwisho na failure, alijiona msomi si kwa sababu alikuwa amesoma bali kwa sababu hakuwa amesoma wala kuelimika. Usomi unapaswa kuchochea kumbukumbu na heshima kwa wengine. Tokana na ujinga hata upumbavu wa mama huyu, alikosa kumbukumbu mbali na wizi wa fadhila, uchumia tumbo, na ukatili vilivyotamalaki. Hata kama kweli mwenzio hakusoma, kwanini hukumwambia kabla ya kuoana? Kama usomi ilikuwa ni sifa uliyotaka mwenza wako awe nayo, kwanini hakusema mapema kabla ya kuingia makubaliano ya kufunga ndoa? Jibu ni rahisi. Alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo ila alifuata utajiri wa ‘mjinga’ huyu aliyetaka kumdhalilisha na kumnyanyasa, kumwibia mbali na kumdhulumu.
Iwe mwanamke au mwanaume, hupaswi kutumia usomi, utajiri, uzuri, ubora, na chochote kumdhalilisha, kumuumiza, na kumdhulumu mwenzako. Kabla ya kumuumiza, kumdhalilisha hata kumkatisha tamaa mwenzako, jiulize. “Kama unasema mumeo au mkeo hakusoma, je baba na mama, babu na bibi zako wamesoma?” Hata kama ungekuwa umesoma au wazazi wako wamesoma, bado huna haki wala haja ya kuutumia usomi wako dhidi ya mwenzio. Kabla ya kufanya hivyo, vaa viatu vyake. Jiulize “ingekuwa mimi, ningetaka nitenzwe vipi?” Kwa wanaotumia ujinga na upumbavu huu waambiwe. “Nyinyi si wajinga na wapumbavu tu bali mafisi ambao wako tayari kula hata watoto wao au fisi wenzao kwa sababu ya tamaa na upumbavu wao.” Kama mlitaka kuoa au kuolewa na wasomi, au matajiri si mngechagua maprofesa au vyuo vikuu au mabenki. Mbona haya madai wahusika hawakuyatoa wakati wakiwabembeleza hao “wajinga’ wawaoe au kuolewa nao? Kimsingi, wote wanaokuja na visingizio kama hivi, si wajinga na wapumbavu tu bali matapeli na wavivu wa kutafuta wanaotumia ndoa kama sehemu ya kujipatia maisha tena kinyume cha maadili na utu. Tunasema hivi kwa sababu kabla ya kuingia makubaliano ya kuoana hasa kipindi cha uchumba, wahusika walikuwa na muda na sababu za kutosha kutoa mapendekezo, mapendeleo yao na ushauri kuhusiana na wanayetaka kuoa au kuolewa nao. Ni aibu kwa mtu mwenye akili kutumia upumbavu kama huu ili ima apate sababu ya kuvunja ndoa, kukomoa, kuumiza, au kumdhalilisha mwenzake.
Tunashauri wenye tabia hizi mbaya waache. Pia, tunashauri wahanga wasimame na kuwauliza maswali magumu hawa ‘wasomi’ wao kama wazazi na ndugu zao hata nyumba zao wamesoma. Kwani, hata kama kweli wangekuwa wamesoma, usomi si majivuno wala manyanyaso bali msaada na unyenyekevu.
Chanzo: Mwananchi leo.