Tunaona bibi wa kizungu na kijana MwAfrika uwanja wa ndege–––hatuutaji–––wakibusiana. Tumeamua kuandika haya juu utumwa kimapenzi ambamo waafrika ndiyo wahanga. Utumwa huu umejikita kwenye mapenzi bandia ambapo mmoja wa ‘wapendanao’ humtumia mwenzake kulingana malengo na hadhi na rangi yake. Htuzushi. Utaona vibabu/bibi vya kizungu vikifunga ndoa na wavulana/wasichana wa kiafrika mtawalia. Bila kupoteza muda–––hapa kuna tamaa, ujinga, na umaskini–––kama vyanzo vya ukoloni na utumwa huu wa kimapenzi.
Katika mila za kiafrika, mwanaume hutegemewa kuoa mtu ima wa umri wake au anayemzidi umri japo si kwa mbali sana. Inapotokea mwanaume akaoa mwanamke sawa ua zaidi ya mama yake au binti akaolewa na kibabu sawa na babu yake, jamii hustuka, kuhuzunika, kushangaa, kuchukuia, hata kulaani. Hakuna kitu muhimu katika ndoa kama tegemeo la kuzaa watoto ambao ndiyo malipo kwa jamii na wazazi. Ndoa bila mtoto, kwa muafrika, ni janga. Tujiulize. Inakuwaje wahusika wanaweka kando hitajio hili muhimu? Kuna cha mno? Inakuwaje kijana wa kiafrika kufunga ndoa na zee lisiloweza kumzalia au kumzalisha au kumuachia ujane? Je ni tamaa, ujinga, au umaskini ukiachia mbali kuabudia rangi ambapo mweupe, hasa mzungu, anaonekana mali japo si mali kitu?
Katika ndoa hizi, kama kweli ni ndoa, wazungu hutumia waAfrika. Hatujawahi kuona MuAfrika mzee akioa msichana mzungu au kijana mzungu akioa bibi muAfrika. Kuna tatizo. Si rahisi kupata majibu sahihi bila kudurusu. Kwa akili ya kawaida, hili si jambo la kawaida, hasa kwa waswahili. Kimsingi, katika ndoa hizi, mweupe ana mamlaka na mswahili hana. Si vibaya kusema kuwa mswahili anaolewa katika mahusiano haya.
Kiafrika, mwanaume huoa na mwanamke huolewa. Ila katika uhusiano tunaojadili, mwanamke/mwanaume wa kiAfrika huolewa na mzungu ambaye humuoa bila kujali jinsia. Hata katika utumwa huu, mswahili hutegemea akiolewa na mzungu ataukata kwenda majuu na kuchuma madola. Hapa thamani ya maisha ya binadamu ambayo ni kubwa kuliko chochote, huwekwa kwenye vitu vya hovyo tokana na ujinga au umaskini kama masalia ya ukoloni wa kimila ambapo mtu mweupe ni mkombozi wa mtu mweusi ni mkombolewa–––hata kama dhana hii ni hovyo na ushahidi wa utumwa wa kiakili, kimaadili, na kimila.
Tuweni wakweli. Hivi kuna mapenzi ya kweli kati ya kizee cha miaka–––tuseme miaka 60, 70 au zaidi kuoa kijana wa miaka 30, 35 hata 40 au babu kuoa kigoli umri wa mjukuuwe? Hapa tunapata dhana ya ubaguzi wa kujitakia ambapo muathirika hujiona dhaifu mbele ya mkoloni wake bila kujali jinsia. Je kuolewa na mzungu ni kuukata au kupatikana licha ya kudhihirisha ujinga, umaskini, na tamaa ya wahusika? Tumeisha Ulaya kitambo si haba. Kuna kitu wanacho yaani ubinafsi/umimi (individualism) ambapo mtu kujiona kama huru na asiyejali wengine isipokuwa yeye. Hapa ndipo chanzo cha kwanza cha balaa hili kilipo mbali na ukoloni ambapo waafrika wameaminishwa na wakaamini–––iwe ni kwa kupitia dini au siasa–––kuwa wazungu ni wakombozi wakati ni waangamizaji. Utamuona Yesu mweupe wakati hakuwa mzungu. Mitume wote siyo waafrika. Maandiko matakatifu yote ni ya kigeni na lugha zinazotumika kuyaeneza. Huu ndiyo mzizi wa kila kitu. Waligundua, kutengeneza, na kueneza ‘weupe’ kuwa ukombozi na wengine wenye dhambi. Unashawishikaji kuwa kila mtu anazaliwa na dhambi wakati mtoto mdogo ni malaika?
Utumwa kwa waafrika ulianza tulipohujumiwa na kurubuniwa kuacha mila zetu tukakumbatia mila hatari za kigeni ziitwazo dini na ustaarabu japo si chochote wala lolote bali maafa kwetu. Mzazi unajisikiaje kijana wako wa kike/kiume anapoolewa na bi kizee kuliko hata baba au mama yake kwa kisingizio cha ‘mapenzi hayana macho.’ Mapenzi yana macho. Ndiyo maana, hayaishi bila kuwa na uhuru na utashi wa kuchagua, ambao katika balaa hili jipya haupo. Binadamu anapotumia njaa, tamaa, ujinga na umaskini kama nyenzo za kufikiri, anaweza kufanya jambo ambalo hata mnyama hawezi kufanya.
Tumalize kwa kuwashauri vijana wa kiafrika kuacha kuuza utu wao eti kwa tamaa na ujinga wa kwenda majuu. Wakishafikishwa ‘majuu’, huumizwa na kuwa watumwa zaidi wakaishia kujuta kama mmoja niliyekutana naye kwenye mji jirani aliyenyofolewa Arusha na kuishia kwenye utumwa.
Chanzo: Mwananchi leo.
No comments:
Post a Comment