How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 12 December 2007

Lowassa; uhuru wanaoutaka Watanzania ni huu

NILISOMA taarifa kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, licha ya kuchukizwa, amesikitishwa na kutoandikwa makala za kutosha kuhusiana na uhuru wa Tanzania. Lowassa amekwenda hatua nyingi mbele kwa kuwashangaa wachambuzi walioonyesha wazi kutoridhika na uhuru wa Tanzania wenye umri wa miaka 46. Japo ni haki yake kikatiba, hata wapingaji ni haki yao kadhalika.

Lowassa alikaririwa akisema: "Hivi kweli mtu mmoja anaandika katika makala yake kuwa miaka 46 ya Uhuru iliyopita ni bure, je, kweli hakuna kilichofanyika?’ alihoji.

“Hali hii imenisikitisha sana kama Uhuru huu usipoelezewa vizuri historia yake na sisi wenyewe nani atauelezea,”` alisema Lowassa.

Kwa Lowassa uhuru wa Tanzania una mengi na ya maana kiasi cha kushangaa ni kwa nini wenzake hawayaoni. Lowassa na wenzake wanaofaidi matunda ya uhuru wana kila sababu na haki ya kushangaa.

Maana mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Kwa mtu wa kada ya Lowassa ambaye amekulia na sasa kuanza kuzeekea serikalini, uhuru wa Tanzania ni wa maana sana. Kwa Lowassa na wenzake ambao wao na watoto wao ndiyo serikali, wana kila sababu ya kushangaa hata kusikitika.

Nani anatarajia mtoto wa kigogo kama Lowassa anayefanya kazi Benki Kuu na watoto wengine lukuki wa vigogo, uhuru wa Tanzania una kila maana na umuhimu. Je, kwa wale wanaotumika badala ya kutumikiwa na uhuru anatarajia nini?

Badala ya Lowassa kulalamikia na kushangaa, inabidi ajiulize ni kwa nini watu wameandika makala zenye mawazo na misimamo tofauti na yake. Walichoandika wachambuzi wengi kuwa uhuru wa Tanzania si chochote si lolote wana sababu tosha na zenye siha.

Kwa mtu anayeshuhudia madudu yaliyofanyika baada ya Mwalimu Nyerere kuachia ngazi, hawezi kuona maana ya uhuru. Maana uhuru haujakidhi matarajio ya wananchi. Utayakidhije iwapo watanzania wengi wanazidi kuwa maskini huku mafisadi wachache wakishirikiana na wawekezaji wameiteketeza na kuitelekeza nchi yetu?

Ni mtu gain, kwa mfano, anayeshuhudia malori ya mchanga uliojaa madini yakikatiza nchi kwenda Tanga bandarini kuusafirisha nje anaweza kuonyesha matunda ya uhuru? Ni ‘mjinga’ gani ambaye mtoto wake anazungushwa kila uchao akihangaishwa kupata mkopo wa kusomea anaweza kusema uhuru umefana?

Kwa akina Lowassa waliosoma bure wakatunga sheria za kulipisha elimu iliyosahauliwa, uhuru ni mafanikio yasiyo kifani.

Kwa akina Lowassa ambao serikali yao imekuwa bingwa wa kashfa na ahadi zizotekelezeka bila kuadhibiwa uhuru ni kila kitu. Wapo wenye uhuru wa kufanya watakavyo bila kushughulikiwa. Rejea kashfa kama zile za BoT, Buzwagi, Richmond, IPTL, Deep Green, Takrima, ununuzi wa rada na ndege feki ya rais, utoroshwaji wa mitaji na wafanyabiashara wa kigeni na uchafu mwingine.

Leo sitashangaa Wahindi na Wachina waliotamalaki nchini wakiwa na utajiri mkubwa kwa kusherehekea na kushangilia uhuru ilhali watanzania wazawa wakiendelea kuwa vibarua.

Ni Mtanzania gani anayepandishiwa bei ya maji na umeme huku serikali na wafanyabiashara wezi kama ilivyotokea Tanga Cement wakifaidi vitu hivi bure, atashangilia uhuru? Hebu arejee kiwanda kimoja cha Dar es Salaam cha kusindika mafuta kilichobainika kujiunganishia maji bila kulipa na kisifanywe kitu.

Hivi Lowassa anatarajia Watanzania ‘wanaoganga njaa’ wauone uhuru? Uhuru siyo hotuba za watawala. Uhuru ni shibe, uwajibikaji, maendeleo na mabadiliko. Hivi kweli wazanzibari waliopoteza ndugu zao kwenye vipigo vya FFU wakati wa chaguzi za kubambikiwa watawala wanaweza kuuhisi uhuru?

Hivi wanafunzi wanaokalia mawe karne ya 21 wanaweza kuuona uhuru? Je, wajawazito na wagonjwa wanaolazwa kitanda kimoja wanne Mwananyamala, Amana, Temeke na kwingineko nao ni huru? Je wale waliopasuliwa vichwa badala ya miguu na miguu badala ya vichwa nao ni huru?

Je, wachimbaji wadogo wadogo wanaofukuzwa kwenye ardhi ya nchi yao kama wakimbizi nao ni huru? Wakulima wanaotumiwa walanguzi wa mazao yao au kulazimika kuyauza kimagendo au wavuvi wanaokula mapanki nao ni huru? Kama wako huru basi uhuru huu ni kejeli na fedheha. Bila haki uhuru unakuwa sawa na wendawazimu. Bila nidhamu ya matumizi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, uhuru ni matusi.

Tumsaidie Lowassa kuelewa wale anaowaona kama wamekejeli uhuru wanachomaanisha. Leo tuna serikali inayotumia pesa yetu vibaya huku ikishindwa wazi wazi kusimamia raslimali zetu. Je, kwa kuendelea na kuwa serikali zigo iliyojaa mafisadi wanaojulikana tunaweza kujisifu tuko huru? Wako wapi waliotuhumiwa kuliibia taifa pesa na kuwekeza kwenye kuchaguliwa?

Japo tunadanganyana kuwa wanachunguzwa na wenzao, ukweli ni kwamba hakuna la maana la kutarajiwa iwapo watuhumiwa wale wale wamo maofisini wakiharibu ushahidi na kuvuta kamba wajuavyo. Kwao uhuru wa kuharibu na kuneemeka ni jambo la maana wakati kwetu ni hatari na hasara.

Miaka 46 tangu tupate uhuru tunazidiwa hata na nchi tulizozikomboa wenyewe. Hebu Lowassa aangalie Angola na Msumbiji atajua ninachomaanisha. Hebu Lowassa atafute sababu ya shilingi yetu kupitwa na sarafu kama ya Kenya, Rwanda hata Burundi atajua ni kwanini kuna watu tusioona mantiki ya uhuru.

Lowassa inabidi aambiwe hata kama atachukia au kutokubaliana kuwa baada ya kung’atuka kwa Mwalimu watanzania walitumiwa na wasaka ngawira wachache walioalikana na hata kurithishana madaraka kwa mbinu chafu kama ilivyokuja kubainika kuwa uongozi nchini umekuwa ukitafutwa kwa rushwa na kuendeshwa kwa kujuana huku umma ukihujumiwa na kusahaulika.

Hivi Lowassa anaweza kueleza ni kwa nini yeye na wenzake wameshikwa na kigugumizi kutaja mali zao? Anaweza kuelezea pesa wanazotoa kwenye kuchangia miradi mbali mbali huku wakiishi maisha ya kifahari walizipataje? Lowassa atusaidie kueleza ni kwanini tofauti kati ya walionacho na wasionacho inazidi kuongezeka kama kweli uhuru wetu tulioaminishwa ungeleta usawa na maendeleo una maana.

Huwezi kuwa na nchi inayoishi kwa kukopa na kutegemea wafadhili kuendesha maisha yake kwa zaidi ya asilimia 40 ukadai uko huru kwa maana sahihi. Nchi inayogawa hovyo hovyo raslimali zake siyo huru. Nchi inayoendeshwa na sera za kukopa na kuamriwa na Washington na London si huru. Nchi isiyo na sera wala falsafa inayoelewaka kiungozi si huru hata kama itajidanganya na kuwadanganya wengine kuwa iko huru.

Uhuru ni wananchi kuendesha nchi yao kwa kanuni na sera zitokanazo na wao. Uhuru ni kuwa na serikali inayowajibika kwa umma na siyo kwa watu wachache.

Huwezi ukawa na umma wa wananchi zaidi ya nusu uishio chini ya dola moja ya Kimarekani ukajidanganya kuwa uhuru umeleta mafanikio au kukidhi yalitorajiwa. Huwezi ukawa na watawala wasiokwenda na wakati ukasema uko huru. Kama huu ni uhuru basi ni udhuru si kingine.

Wanaokula na kusaza, kupora watakavyo bila kushughulikiwa ni huru. Lakini wale wasiokuwamo kwenye genge hili si huru bali mateka wa genge hili.

Nafasi haitoshi.

Nkwazigatsha@yahoo.com

No comments: