The Chant of Savant

Thursday 20 December 2007

Mwaka 2008 tukatae utumwa wa fikra

WATANZANIA tunahitaji kupigania uhuru upya toka kwa wakoloni wa kila aina. Tunao wakoloni aina kama mbili ama tatu.

Wale wa kutoka nje na wale wa kutoka ndani wanaotumiwa na wale wa nje kutunyonya na kututawala na wao wakitawaliwa.

Kimsingi hata wakoloni wanahitaji ukombozi. Hatuwezi kuwakomboa wakoloni wa nje. Lakini tunaweza kuwakomboa wa ndani. Kuwashupalia na kuwaambia hivyo sivyo.

Hivyo nguzo ya kwanza ni kujikomboa wenyewe halafu tuwakomboe na wenzetu. Tutaanzaje? Kwa kuukataa na kuuchukia ukoloni hata kama itatulazimu kufa. Na baya zaidi ukoloni wa kutawalana sisi kwa sisi.

Tunaishi kama panya! Mifumo yetu inatawaliwa na upanya. Lakini panya wana afadhali. Maana hawana nchi ya kuita yao wakaitawala na kuimiliki. Ndiyo maana siku zote panya hata akipata chakula cha kutosha, lazima ataficha kama baadhi yetu wanavyoiba kwenye mali za umma na kuficha ama ndani kwa kutumia kila mbinu au nje na kurejea na kujikausha wakiwinda nyingine wakafiche. Huu hakika ni utumwa.

Hata kama nimesoma, nina mali hata madaraka, kama ndugu, jirani, wananchi wenzangu wanalala njaa wakati nikivimbiwa, mie na hao wanaoteseka ni watumwa wa njaa hiyo hiyo. Maana uroho wangu na ukondoo wao wa ama kulalamika bila kupambana au kuridhika huku wakimuachia Mungu utadhani Mungu anaishi hapa, ni utumwa tena mchafu kuliko ule wa kufungwa kamba.

Je, tatizo letu ni nini? Ni mali au maarifa? Je, umaskini wetu ni wa mali au ubongo? Kwanini sisi? Huo ni utumwa wa fikra na lazima mwaka mpya wa 2008 tuseme hapana.

Kuna haja ya kujikomboa kutokana na upofu ambapo mtu anamnyonya mwenzie anayekubali kunyonywa kutokana na utumwa wa fikra. Hawa wawili wanahitaji ukombozi. Watu watafanyaje mambo kwa kupapasa kama wadudu wasio na macho? Hata wadudu ni afadhali. Maana hakuna mchwa anayemguguna mwenzie.

Tunahitaji ukombozi toka kwenye ukupe wa kutegemea wafadhili au ujanja ujanja wa kimifumo. Kupe na ng’ombe wote ni watumwa. Wanahitaji ukombozi. Kupe hata anenepe vipi bado ni kupe. Ukupe haumfai mtu wala jamii ya watu.

Tunahitaji ukombozi toka kwenye uchangudoa. Je, sisi siyo changudoa wanaotegemea wafadhili kwa fedha hata maadili? Je, hatuna watu tena wanaojiita wakubwa wanaofakamia kila uchafu ilimradi umetoka Ulaya? Hawa nao wanahitaji kukombolewa kutoka kwenye kichaa cha kujikana na kujikinai wakiwaneemesha wengine wakati kama paa wakijipalia mkaa. Je, hatuna watu tena waongo wanaotwambia tunakimbia wakati tumekatwa miguu? Je, na sisi tunaodanganywa na kukubali si watumwa? Je, wanaotudanganya si watumwa?

Tunahitaji kujikomboa kutoka kwenye woga. Je, sisi hatuogopani? Tajiri anamuogopa maskini anayemnyonya ili asimuibie au kumdhuru na maskini anamchukia na kumuogopa tajiri asizidi kumnyonya na kumdhulumu. Hawa wote ni watumwa. Chama tawala kinaogopa upinzani. Wanaogopana! Huu nao ni utumwa. Hatuaminiani!

Leo hii nchi za Kiafrika zinaimba nyimbo za ubinafsishaji ambao umevuka mipaka kiasi cha kubinafsisha miili na roho za watu! Ni utumwa kiasi gani?

Sipendi ubinafsishaji. Maana ni utumwa, tena wa hiari. Na kama ningeupenda basi nisingeanzia kuueneza kwa kuuza na kuiba mali za umma, bali ningebinafsisha mzizi wake ambao ni madaraka. Siogopi kusema kuwa ni heri kubinafsisha Ikulu kuliko kiwanda. Maana kiwanda huzalisha bidhaa tukazitumia kuliko Ikulu. Je, Ikulu huzalisha nini? Serikali kubwa? Na serikali huzalisha nini?

Sisi ni watumwa, tena wanaonuka hata kama tunaoga na kujitia uturi. Tutashindwaje kunuka iwapo tumejaliwa kila aina ya vinono na vya thamani, lakini kwa kichaa chetu tunajisifu kuwaita watu waje kujichotea wakati watu wetu wakichotwa na magonjwa, ujinga, umaskini, dhuluma na kila aina ya udhalili?

Tutashindwaje iwapo tunaendekeza mifumo inayotukwamisha badala ya kutukwamua. Tutashindwaje kuoza hata kugaga iwapo tunapingana na ukweli tena mchana kweupe? Nani kipofu na taahira asiyejua kuwa katiba yetu ni bomu? Je, tuko tayari kuibadili ili kila mtu awajibike na kupata haki yake? Nani atafanya hivi iwapo kuna baadhi yetu ni watumwa wa ukubwa usio ukubwa? Ni watumwa wa mali, matabaka, itikadi, vyama na woga?

Tutakuwaje huru iwapo tunauchukia na kuuogopa ukweli? Nani atakuwa huru bila kuukubali na kuukumbatia ukweli? Je, sisi siyo sawa na panya na fisi hata samaki tunaokulana utadhani vyakula vimeisha?

Inakuwaje nchi tena yenye kila aina ya mali na watu iridhike na umatonya isiwe kichaa na mtumwa? Hata kama mabwana wanatulipa kwa utumwa wetu, tukubali kuwa wengi wa watu wetu wanaumia.

Je, tutashindwa kutungiwa majina yote mabaya iwapo tunawaaminisha watu wetu kuwa tutawakomboa ilhali tunawauza? Basi tuwaambie ukweli badala ya kujidanganya na kuwadanganya. Kusema ukweli ni ukombozi namba moja na kuukubali ukweli ni ukombozi wa hali ya juu.

Mie ningekuwa rais wa nchi hii nisingefunga safari kwenda kuomba. Nisingethubutu hata kujidhalilisha na kuwadhalilisha watu wangu kutenda jinai hii.

Wenzetu wanatucheka na kuambizana kuwa vichwa vyetu vifanyiwe uchunguzi. Kwani tunamalizana wenyewe kwa wenyewe kwa kutumiwa na wakoloni wa nje.

Hakika tumegeuka wa hovyo. Hujaona kasa akimcheka kobe? Leo Afrika Mashariki kwa mfano imeshindwa kuungana kwa sababu ya ukondoo, ufisi na uchangudoa. Itaunganaje iwapo hatujiamini na kuaminiana?

Tutaunganaje iwapo wapo wanaofanya wenzao wa hovyo wasijue kuwa wao ni wa hovyo zaidi? Uzinzi ni mchafu. Wazinzi wawili wote ni wachafu hata mmoja awe anajisifu kumpata mwenzie.

Je, tumeridhika na uhayawani na umsukule wa kuendeshwa na kutumiwa huku tukijua, lakini tukajidanganya kuwa tu huru? Leo utashangaa kuona watu wanatishana na kufungana kwa kisingizio eti cha usalama wa taifa. Ni taifa gani liko salama iwapo lina mamilioni ya raia maskini? Je, adui ni yule anayetupinga kwa jinai hii au sisi tunaoikubali na kuwaaminisha watu wetu kuwa haya ndiyo maisha?

Leo kuna watu hawatakiwi kusimama mbele ya wenzao na wakaongoza kwa sababu hawafai. Lakini ukiwaambia, ugomvi! Je, wewe na wao nani adui na mtumwa mbaya?

Kusema mengi si kufikisha ujumbe. Ujumbe, Watanzania bado tuko utumwani. Hata uwe msomi, rais, mchungaji, sheikh au tajiri. Kama umezungukwa na maadui niliowaorodhesha hapo juu, ukiwa unawatumikia ilmradi upate chako, wewe ni hayawani. Maana unawajua na unawaona na umepewa akili kupambana nao kama utakubali kuukana utumwa wa fikra na kuacha kuukimbia ukweli hata kama unauma.

1 comment:

Anonymous said...

NN mimi nakubaliana moja kwa moja na yote uliyoyaongea, infact kuna kipindi nasikia kulia na yale yanayotokea nchini. JK yuko busy kuwatafuta mabepari waje wachukue rasilimali zetu eti kisa hatuna technology sasa si afadhali watuachie hayo madini basi kuliko kuja kuchimba na kutuachia mashimo? Lakini pia kuna nchi kama Botswana hawana nyenzo kama cc ila wameingia mikataba mizuri nao wanenjoy cake c mgeni aichukue yote atuache watupu kama hapa kwetu

Napata bahati ya kuzunguka nchini, at times napata hasira ya ajabu. Juzi nilikuwa Njombe, wakenya niliowakuta huko hawana idadi, wamekwenda kuchukua mbao ambazo zikifika kenya zinapigwa stamp 'product of kenya' zinapelekwa ulaya wanakula dola tunabaki na madafu. Sidhani kama hata hiyo kdi wanalipa kwa jinsi TRA walivyocorrupt kufuru.

Baharini kwetu nina ushahidi wa factory ships zisizokuwa na idadi zinazovua samaki wetu idadi isiyomithilika pasipokuwa na kibali wala kulipa kodi na no one cares.

Kwenye uwindaji nako ni kiama, bei zetu nyingi ni robo ya zile wanazotoza majirani zetu na hao wanyama wanopelekwa uarabuni kila wiki wakiwa hai Mungu anajua. Wajukuu zetu itabidi wawe wanakwenda uarabuni kuangalia wanyama kwani by then hapa itakuwa ni history kwamba tuliwahi kuwa na mbuga.

Huyu mjinga JK jamani asiyechoka kuzunguka dunia nzima na bakuli lake eti kuomba misaada kwanini asingeanza na haya maeneo ambayo yako wazi kabisa jamani? Wala huhitaji kuwa genius kuona namna ambavyo TZ haina rais kama tunaye basi ni rahisi. Na kinachoniuma zaidi na zaidi ni kwamba pamoja na kuchemka kote huku tutampa tena nchi 2010-Oh my God. NN unajuwa sababu ya hili ambayo ni HATUNA WAPIGA KURA MAKINI,tulionao ni wale unaoweza kuwapa kofia na tshirt wakasahau machungu yote YA MIAKA MIAKA MI5 na ahadi ulizoshindwa kutekeleza still wakakupa miaka mingine mi5. What do we do jamani kuondokana na hili?