The Chant of Savant

Wednesday 23 January 2008

Kondoo wanapogeuka mbuzi kwa mafisadi

HABARI kuwa wananchi wenye hasira walivamia shamba la aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali, haziwezi kupita bila kujadiliwa.

Januari 20, mwaka huu, tulishuhudia wananchi wenye hasira kwenye eneo la Mbweni-Maputo, Kinondoni, Dar es Salaam, wakivamia shamba la Ballali na kuanza kuligawana.

Walifanya hivyo, kwa kudai kuwa lile shamba lilipatikana kutokana na pesa yao iliyoibwa na wachache wakishirikiana na watendaji wa serikali akiwamo Ballali.

Hakika huu ni mwamko mpya licha ya kuwaonya mafisadi kuwa muda wao wa kutanua unaanza kuwatupa mkono.

Ni kauli na kitendo cha ukombozi cha kuukataa ukondoo na urambaji wa viatu vya wakubwa wasio na ukubwa wowote, isipokuwa ukubwa wa ovyo.

Kama wezi wetu wamebakiwa na ukubwa, basi si ukubwa chochote, bali ukubwa wa dume la nyani ambalo licha ya kuwa na maguvu, halina akili ya kulima bali kuongoza kushambulia mashamba ya binadamu.

Katika sakata hili, binadamu wameamua kwa dhati kupambana na manyani watu, waliovamia rasilimali na asasi zao hata serikali kwa ujumla.

Hili laweza kuonekana kama jambo dogo. Lakini ifahamike umma hauna dogo unapoamua. Hata kuchoma vibaka moto kulianza na watu wachache.

Tumekuwa tukiwahimiza wananchi waachane na kuwaua vibaka huku wakiwanyenyekea wanaotafuna mabilioni yetu na kusababisha ongezeko la vibaka.

Sasa wakati wa wananchi kuwasaka wabadhirifu umewadia.

Pamoja na sheria kuwa wazi, hakuna anayeruhusiwa kujitwalia mali halali ya mwenzake, sheria hiyo hiyo iko kimya kuhusiana na mali haramu kama hii ya Ballali.

Kilichofanyika ni somo kwa serikali, ikamate mali za watuhumiwa haraka kabla hakujatokea vurugu hata umwagikaji wa damu. Watawala wetu walizoea kutukoga na kututuliza kwa pesa zetu wenyewe.

Wamezoea kumkaanga samaki kwa mafuta yake. Sasa samaki ameshtuka. Ukiingia majini kwake anakugeuza asusa.

Hakuna nchi ambayo mafisadi wana jeuri kama Tanzania. Ni watuhumiwa wangapi wa ujambazi tunawajua sasa ni waheshimiwa?

Ni wangapi wameghushi nyaraka na vyeti na sasa ni waheshimiwa huku wakikingiwa vifua na serikali hiyo hiyo tuliyodhani ni yetu?

Inashangaza kuona mali zinazodaiwa kupatikana kwa dhuluma kama za kina Kagoda, Jeetu Patel, Tanpower, ANBEN (Anna and Benjamin Mkapa), na Fosnik (Foster and Nicholas Mkapa) na nyingine nyingi bado zimo mikononi mwa watuhumiwa!

Ni majumba mangapi na viwanja vya ubadhirifu vingapi vinaendelea kuwa mikononi mwa wamiliki kinyume cha sheria? Je, hii ndiyo siri ya serikali kusuasua kukamata na kufilisi watuhumiwa wanaojulikana, tena wakubwa?

Ziko wapi nyumba zetu zilizouzwa na Serikali ya Awamu ya Tatu? Je, serikali itaendelea kuwalinda wahalifu hawa dhidi ya wananchi ambao inaonekana kuwaacha kila mtu ajitafutie haki yake ajuavyo?

Ingawa tumekuwa tukiaminishwa na watawala wetu kuwa nchi yetu ni ya amani. Ijulikane wazi kuwa amani haiwezi kuwapo bila haki na uwajibikaji.

Ikiwepo imani ya amani na si amani kwa maana yake. Ikiwepo ni kejeli (mockery) kwa amani na wananchi kwa ujumla. Ni uongo wa mchana kusema kuna amani iwapo umma unaibiwa kila uchao, tena na wale watu uliowaamini kuwapa ofisi zake.

Sasa ndiyo wakati muafaka wa wananchi kuukiuka mwiko wa kugeuzwa nepi za kufutia uchafu wa watawala. Ni wakati muafaka kwa wananchi kuachana na kugeuzwa vichaka na mihuri ya kufichia mali za wizi zitokanazo nao.

Ni mara ngapi rais amekumbushwa kutaja mali na wenzake? Je, wananchi wataendelea kuwa ‘wajinga’ na kuruhusu watawala waendelee kufanya ubadhirifu kwenye fedha zao?

Serikali inayoficha mali za watumishi wake inaweza kujiepusha na shutuma za ubadhirifu? Hata chama kinachounda serikali hii si chama cha ubadhirifu?

Kama kuna wilaya imeonyesha mwamko wa kifikra, si nyingine bali Kinondoni, Dar es Salaam, ambayo ninaipongeza.

Tukio la kukamatwa mali ya Ballali si la kwanza. Nani amesahau mkuu wa wilaya hiyo aliponusurika kipigo baada ya kutaka kuwageuza wananchi kuwa ‘wajinga’ kusimamia ubadhirifu wa mali zao?

Ilitokea Wazo Hill, Kijiji cha Chasimba. Imeingia kwenye vitabu vya historia, wananchi wameukataa utawala usiowajali wala kuwafanyia lolote isipokuwa kuingia mikataba mibovu kama ilivyodaiwa kwenye sakata la Richmond, IPTL, ubinafsishaji na uuzwaji wa NBC.

Huu ni mwaka wa wananchi kujinasua kutoka mikononi mwa mafisadi hata kama watakuwa wanalindwa na serikali.

Tulionya kuwa serikali inaweza kufurushwa na wananchi wakijua kuyatumia vizuri madaraka yao kama ilivyotokea kwenye mifano hii miwili.

Hakika hata wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wanaoendelea kuzungushwa na kudhalilishwa na wamangi meza wachache nao wataamua kuamka usingizini na kudai hata kuchukua kilicho chao.

Hatua hii ya ukombozi itaondoa uongo na unafiki wa baadhi ya watawala kuwa wanaongoza kwa ajili ya wananchi, wakati ukweli ni kwamba wanatawala na kufanya ubadhirifu kwa ajili yao binafsi na marafiki zao.

Ingawa serikali imeshikilia ripoti ya ukaguzi ya Ernst and Young, ukweli ni kwamba kashfa nzima ya BoT haijawekwa ugani kama ilivyo. Tulicholetewa ni majani.

Bado shina na mizizi ya gogo zima liitwalo kashfa ya BoT, nani ataridhika na mbuzi wa shughuli (Ballali) wakati wenye shughuli wenyewe bado hawajaguswa? Je, rais anajua kuwa wananchi wanamfahamu zaidi ya anavyodhania?

Anayo habari kuwa wana hasira kuliko anavyojiridhisha au watapiga kelele halafu watanyamaza?

Kwa upande wa wananchi nao inabidi waongeze kasi. Maana inashangaza kuona walipigia kelele kulanguliwa umeme halafu taratibu wanaletewa kesi ya Ballali, nao kama ‘mbwa’ aitikiaye miito mingi, wanauingia mkenge wananyamazia kadhia na jinai ya kulanguliwa umeme, ilhali serikali ndiye mlimbikizaji mkuu wa madeni, ukiachilia mbali kuwa nyuma ya Tanesco.

Hata kama mbinu chafu za kuleta picha mpya kila inapozuka picha yenye kuweza kuwaamsha wananchi inainusuru serikali, ukweli unabaki pale pale kuwa wananchi wanaita mazingaombwe ya Rais Jakaya Kikwete na timu ya mawaziri wake waliotajwa kwenye ufisadi.

Leo, watu wangetaka kuona mawaziri kama Basil Mramba, Juma Ngasongwa, Andrew Chenge, Edward Lowassa, Zakhia Meghji, Ibrahim Msabaha na wengine wengineo, wanaotuhumiwa kuiingiza nchi kwenye matatizo ya kiuchumi wakichukuliwa hatua za kisheria.

Hakika kilichotokea kwenye shamba la Ballali ni ukweli kuwa kondoo wameanza kugeuka kuwa mbuzi dhidi ya mafisadi wanaowasumbua.



Source: Tanzania Daima Januari 23, 2008.

No comments: