The Chant of Savant

Wednesday 30 January 2008

Kwanini kila ufisadi wa kaya hii yumo Gabacholi?

NIMEJILAWA leo. Nautafakari unafiki wa wakubwa. Nimechukizwa na baadhi ya wachumia tumbo waliojaa kwenye majoho wakivichafua vitabu na nyumba za Mungu. Wapo wengi. Wanaojifanya wanakipenda kijiwe, ilhali ni mbweha wa kawaida.

Yupo mbweha mmoja, aliyedai tumsaidie mkuu wa kaya kupambana na ufisadi wakati kufanya hivyo ni kupambana na yeye mwenyewe.

Leo nina mada: Kwanini kaya na kijiwe chetu vimegeuka nyumba ndogo ya magabacholi? Na kwanini tunaridhika na uongo wa Cheka cheka kumlinda kibaka Tunituni na genge lake?

Nikiwa nimejiinamia, nasikia salamu toka kwa Mpemba.

Anasalimia: "Salaamaaleko jamia."

Mzee Kidevu anamjibu haraka huku akipokea kipisi cha sigara toka kwa mzee Ndomo.

Mara Msomi anaingia akiwa anabofya ki-Nokia chake. Akiwa anatafuta mahali pa kukaa, Mkurupukaji anaingia na gazeti. Kichwa cha habari ni, 'Yule mwizi wa pesa ya rada kumbe bado anatanua!'

Utadhani kamwaga jivu kwenye siafu!

Mgosi Machungi analamba mic. "Jamani hali hii inatishangaza. Yaani kia wizi wapo magabachoi! Hivi huu ndiyo ubinafsishaji hata kaya?"

Akiwa anashangaashangaa, Mkurupukaji analamba mic. "Mgosi hujui kwanini kaya hii imewekwa kimada na magabacholi? Hujui baada ya kuondoka Mchonga ziliingia sirikali za kijiweni zinazotumiwa na magabacholi kujineemesha huku sisi tukiteketea?"

Kabla ya kujibu, kwa mara ya kwanza, gabacholi Kanji anayeishi mtaa jirani, anatia timu kupata gahawa. Inaonekana katumwa na wenzake baada ya kusoma habari za kijiwe hiki mama wa siasa kutuchunguza.

Mzee Kidevu anaamua kumchokoza. Anauliza swali la nyodo. "Jamani kaya hii hivi ni ya Wadanganyika au ya magabacholi?"

Kanji kapata upenyo! Analamba mic bila kutoa hata taarifa. "Swahili napenda laumu Hindi. Kwanini silaumu ongozi yenu? Sisi nakuja na fuko tupu natoka na fuko jaa kwenda Bombay."

Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anakwanyua mic kwa hasira. "Kanji acha kututia madole machoni. Yaani huna aibu unatutukana, tena kwenye kijiwe chetu!"

Kanji halazi damu. "Wewe toka. Iko na jiwe wapi we jusi? Sisi taka ondoa mbea yenu naweza honga city, kazi kwisa. Kama taka salama acha sisi. Nyinyi iko na lengo dogo dio maana ongozi yenu natumia sisi kuibia nyinyi. Kwanza nyinyi haiko na secret. Kama nakamatwa nasema siri yote. Lakini sisi nakimbilia London, Canada au Bombay. Pia sisi haiko na bibi nyingi. Sisi nazaa kama panya, lakini hapana lala na jumba dogo."

"Kanji acha nyodo, huo ni wizi hata kama mnashirikiana na baadhi ya wachumia tumbo wetu, mna lawama. Kwanza mmekujaje hapa kama siyo kuletwa na malkia mkoloni?" anauliza Makengeza kwa hasira.

Kanji halazi damu, anajitetea. "Hata kama letwa na Queen sisi iko raia sasa. Nenda laumu ongozi yenu kutumia pesa jumbani dogo."

Kabla ya kuendelea, Mbwa mwitu anamzodoa Kanji. "Nyie raia au kunguru! Angalia wenzenu walivyoitelekeza Kenya baada ya kuanza vagi. Nyie ni raia wa karatasi sawa na chui wa karatasi, hamna sera, ni wezi watupu, rudini kwenu mkafe kwa umaskini uliotamalaki."

Kanji anajibu. "Hiyo dua ya kuku haipati mewe dugu yangu. Wewe sida nini? Kwanini siseme sisi jumuia yetu kachangia wewe pesa kidogo ya kula na mama toto yako?"

Kapende anapandwa ghadhabu. Anamkwida shati Kanji ampe dispilini.

Anasema. "Kawatie madole akina Tunituni na Cheka cheka siyo sisi. Unapata wapi jeuri kutunyea tena hadharani mbwa we!"

Kapende anamtembezea kichapo Kanji hadi tunaanza kumuonea huruma.

Mzee mzima naingilia kati kuwaachanisha huku Kapende akitweta na Kanji akitetemeka utadhani kiama chake! Maana bila kufanya hivyo polisi wetu waabudiao magabacholi wakitukuta tunampa displini ponjoro watatutia ndani na kutubambikizia kesi za bange hata mada.

Mzee Maneno anaingilia kuokoa jahazi. "Kapende unamuonea Kanji bure. Hawa ni kama inzi, hawawezi kuacha kidonda bila kuchokonolewa. Hapa wa kulaumu ni vyangudoa wetu anaoongelea mzee. Huko nyuma walikuwa hawatumiwi hovyo hivi." Anamtazama Mkurupukaji.

Kanji hana imani na kijiwe tena. Anaamua kutimka mbio kwenda zake asipate kichapo.

Kijiwe kinamzomea hadi wapita njia wanashangaa.

"Huyo gabacholi. Huyo!" Yanasikika makelele.

Msomi anaamua kuingilia. "Wazee, japo hakuna mzinzi mmoja bali awe na mzinzi mwenzie, Kanji mmemuonea. Tumeshindwa kuwatia adabu vyangudoa wetu tunawaandama malaya wenzao! Hebu muangalie Tunituni. Eti bado anaalikwa akasuluhishe akina Kibaka wakati naye zigo la ufisadi linamlemea."

Anavuta kombe lake la kahawa na kupiga funda na kuendelea kutoa mapwenti.

"Mie nina wasiwasi na usomi wetu. Hivi inakuwaje afisa tena mzima kama Tunituni bwana kujua anaingizwa mjini na tapeli kama Jitu au Shaileshi Visirani?"

Kabla ya kuendelea, Makengeza anamjibu. "Msomi usishangae. Hukusikia vizuri maneno ya Kanji? Jamaa wanawatumia magabacholi kuficha siri zao. Huoni wanavyohangaika na Ballaliii kutaka kumnyotoa roho ili awafichie siri? Usishangae kuona tunaowalilia watende haki ndiyo wezi wenyewe."

"Du!" Anasema Msomi Mkatatamaa na kuendelea. "Mzee umenifumbua macho. Kumbe ndiyo maana Chekacheka kaamua kututoa kafara kumlinda Tunituni! Hakika kaya hii si huru, ina maadui aina mbili; magabacholi na vyangudoa wetu wachumia tumbo. Angalia mabaki ya nyumba za Mchonga, viwanda, maduka, mabenki, maduka ya kubadilisha na kutoroshea pesa na sasa kimebakia kijiwe kama pango la wezi kama alivyoonya Mchonga. Kwanini tusianzishe chama cha kudai uhuru upya?"

Akiwa anajiandaa kukomelea pointi nyingine, Mpemba anadandia. "Yakhe, hawa dawa yao kupigwa mawe. Adhabu ya mzinzi yeyote kupigwa mawe hadi kufa bila kujali nasaba wala cheo. Hivi naye Ntikila kaishia wapi? Maana naona magobacholi wazidi sasa hadi waingia kwenye mjengo wetu Idodompya!"

Msomi anaendelea. "Ami umesema vyema. Tumewekwa mabaya hadi kuruhusu kunguru wa mzee Karumekenge watutawale na kutuibia. Napata taabu kuamini hata bidhaa wanazotengeneza kwenye viwanda vyao. Kama wanaweza kuwa na influence kiasi hiki kwanini wasitulishe sumu, uchafu na bidhaa zilizopo chini ya kiwango? Nani atawakamata iwapo hata kijiwe ni chao? Anayebishia hili arejee utawala uliopita wa mfanyabiashara Tunituni na mkewe mama moneybags."

Kabla ya kuendelea simu yake inalia. Anaipokea na kuongea kwa kifupi na kuendelea na lecture.

"Hawa jamaa si bure. Wanapata jeuri kutokana na kuibeba sirikali iliyomo mifukoni mwao tokana na tamaa, upofu na nyongea ya jamaa zetu. Hata chama kimeishaingiliwa muda mrefu. Ogopa kiama cha walaji kinachopata ruzuku isikitoshe kikaamua hata kuwachuuza watu wake. Chama ilikuwa zama za Mchonga sasa ni kiama chetu.

"Ni genge la wachumia tumbo. Hakuna aliye safi wala mwenye nafuu. Hata hawa mnaowadhania ndio siyo. Juzi jamaa wa intelligence alinitonya, kama ukweli wa ufisadi wote kijiweni na kayani ukiwekwa hadharani, wa kwanza kuadhirika na kuathirika kama Wadanganyika wataamka ni kiama chao cha walaji. Wa pili ni mkuu wa kijiwe mwenyewe. Huoni kila uchao anakuja na mazingaombwe! Kwanini hawakamati Tunituni na magabacholi wake?

"Anafahamu akiwakamata nao watamkamatisha. Laiti kijiwe kingekuwa na watu wenye akili, dawa hapa ilikuwa kumkoma nyani bila kuangaliana usoni. Maana kijiwe kimewashinda kiasi cha kuwaachia magabacholi wakichezee wanavyotaka. Kama alivyobainisha Kanji, usishangae siku moja tukawa na mkuu wa kijiwe gabacholi kama alivyowahi kuotea mbweha mmoja gabacholi kule Zenji. Mnamkumbuka ya Zenji? Hakina wataalamu hii huiita Gabacholization of Kaya and Kijiwe."

Alipokuwa akijiandaa kuendelea, mara ndata walivamia kama upupu ili watunase kwa kumtia adabu mteule gabacholi Kanji. Mie nilitimkia zangu Ilala kwenye ofisi ya DP ya Ntikila.



Source: Tanzania Daima Januari 30, 2008.

No comments: