INGAWA shamra shamra za kuanguka mbuyu katika utawala wa Awamu ya Nne maarufu kama Kasi Mpya hazijatulia, wenye vichwa wanajiuliza maswali mengi.
Hii ni baada ya mtu aliyeonekana kama King Maker, rafiki na mpambanaji mwenzake Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, kudondoka bila kutarajiwa na kwa staili ambayo haikutarajiwa ukiachia mbali kutowahi kutokea!
Ulikuwa kama mchezo wa kuigiza kwenye filamu za Holywood au tuseme visa kwenye hekaya za Abunwasi. Kwa waliomjua Lowassa na nguvu na jeuri alivyokuwa navyo, hakika hawakutarajia kama angedondoka kirahisi na haraka kama ilivyotokea.
Hakuwa wa kwanza kukumbwa na misukosuko ya kisiasa hasa kwenye kiti moto cha Uwaziri Mkuu. Mtangulizi wake, Fredrick Sumaye anaweza kutoa somo na sura halisi ya kilichotokea.
Lowassa kama Sumaye, alikumbwa na kashfa zihusianazo na kusaka ngawira. Bahati mbaya bosi wake, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kutokana na ubabe wake alizima kila wimbi lililotaka kumsomba mteule huyo, rafiki na mshirika wake ambaye alimaliza ngwe zote mbili akiwa majeruhi kiasi cha kukosa udhu wa kurithi kiti cha Mkapa (urais).
Hii ni baada ya kambi ya Kikwete akiwa na Lowassa na mshirika wao mwingine, Rostam Aziz, Mbunge wa Igunga kumchafua na kumuundia kila njama na hatimaye kumzuia asimrithi Mkapa. Sasa hiyo ni historia.
Kilichomtokea Lowassa na namna kilivyotokea, hakina tofauti na kile kilichomtokea dikteta wa zamani wa Iraq, marehemu Saddam Hussein, ambaye aliogopwa na dunia nzima kutokana na tambo na aina ya ukandamizaji wake.
Hakuna aliyeamini kuwa angeangushwa ndani ya wiki moja! Ndivyo ilivyokuwa hadi kunyongwa akikutwa kajichimbia shimoni kama mhanga, huku picha ya aibu hii ikirushwa dunia nzima, sawa na ya Lowassa.
Hakuna ubishi. Kuondoka kwa Lowassa ni nafuu ya Kikwete kwa muda. Ni nafuu kwanza kutokana na Lowassa kuwa na rekodi chafu, hasa baada ya kutuhumiwa na mtu aliyeaminiwa na kuendelea kuaminiwa na Watanzania - Mwalimu Julius Nyerere.
Nyerere kama ni laana, basi aliiacha. Na kama ni kuona mbali kutokana na tahadhari yake, basi aliona mbali zaidi ya Kikwete, Lowassa hata na Watanzania wote. Aliyosema yamedhihirika.
Pili, alikuwa mzigo kutokana na kutopendwa. Hili nalo siwezi kulitolea maelezo, ama ni kutokana na kariba ya mtu au athari za maneno ya mwanzilishi wa taifa hili ambaye amebaki kuwa mfano na kipenzi kwa Watanzania hata baada ya kufariki dunia.
Tatu, alikuwa akikabiliwa na shutuma nyingi zihusianazo na fedha kama alivyokuwa Sumaye.
Kitu kingine, Kikwete hakujaliwa Wazungu waitacho ‘a gift of gab’ au utaalamu wa kubishana na kujenga na kuharibu hoja kama Mkapa ambaye pamoja na ujanja wake, kadhalika umeshindwa kumsaidia kipindi hiki anapokabiliwa na tuhuma za ufisadi akishirikiana na mkewe, mwanawe na marafiki zake.
Kuondoka kwa Lowassa kwaweza kuonekana kama nafuu kwa Kikwete. Lakini ni kwa muda. Kwa sababu ufisadi bado haujashughulikiwa na ni mwingi na mkubwa ajabu.
Hebu fikiria kama kashfa moja, tena ndogo ya Richmond imeweza kumuondoa waziri mkuu, na hizi nyingine hasa ya Benki Kuu inaweza kuangusha wangapi na wakubwa kiasi gani?
Lowassa pamoja na upungufu alionao, alikuwa ni ubongo kwa Kikwete kiasi cha baadhi ya wachambuzi kumlinganisha na mkono wa kuume wa Kikwete.
Sasa umekatwa. Je, ataweza kuyakabili mawingu ya bahari iliyokwisha kuchafuka na aogelee hadi ng’ambo salama? Hili ni suala la wakati.
Kwa kumtoa kafara, nadhani, Kikwete alidhania angekuwa amefuta swali. Hii ingekuwa hivyo kama wadadisi na wananchi wasingeona mbali wakaridhika na hili. Lakini hali ilivyo ni kwamba wananchi wangetaka mambo yote yawekwe hadharani.
Haiwezekani wananchi wakawa na uchungu dhidi ya ufujaji na wa Richmond, halafu wananchi hao hao wawe kama mfanyabiashara juha, wasamehe wizi mkubwa kama wa BoT, mikataba mibovu ya uwekezaji kwenye nishati na madini, uuzaji wa hasara wa mashirika ya umma kama NBC na mengine mengi.
Hawawezi kufanya kama kwenye kisa cha Mpare, mpenda kesi ambaye aliuza ng’ombe kutetea kesi ya kuku. Hakuna shaka: wameishaonja asali watataka kuchonga mzinga.
Hapa ndipo Kikwete na Chama chake Cha Mapinduzi watajikuta kwenye joto zaidi ya hili la Richmond lililowaacha majeruhi. Na bahati mbaya sana, CCM haina bongo zinazochemka kuweza kuliepusha hili ambalo ni tukio linalongoja wakati muafaka.
Kwa maneno mengine, hapa kuna ugomvi wa kitaasisi baina ya Bunge na utawala ambao kwa muda mrefu umekuwa ukilitumia Bunge kama nyumba ndogo badala ya mshirika sawa.
Bunge linaweza kulaza damu likaridhika. Je, wananchi wataridhika ilhali ugumu wa maisha unazidi kukatua zaidi huku vyombo vya habari vikimwaga habari nyingi juu ya ulaji wa kifisi wa mabilioni?
Tuliwahi kuonya CCM kuwa inaelekea ukingoni mwa enzi na zama zake. Hakika kwa hali ilivyo, kama tochi itamulika vizuri walioko nyuma ya wizi mkubwa wa BoT, Lolote linawezekana.
Ingawa Kikwete ameripotiwa kuwa aliridhia kujiuzulu kwa Lowassa, hii ni kumpa sifa asizostahili. Ukweli ni kwamba Lowassa alifukuzwa na wabunge baada ya kuchoshwa na ubabe wa kikundi kidogo cha watu waliomzunguka na kumbinafsisha rais.
Hakuna pigo kama alilopata Kikwete na Lowassa. Watajikongoja kwa nyonde nyonde ili waepushe shari kamili baada ya kutembelewa na nusu shari. Je, wataweza?
Tuuangalie ukweli hata kama unauma. Mwalimu alionya: wanaotumia pesa kwenda Ikulu wanafuata nini Ikulu na watarudishaje pesa hiyo na walinunuliwa na nani kwa makubaliano gani?
Leo tunaambiwa habari za ndoa ya Dowan na Caspian Construction ya Rostam Aziz ambaye amekuwa akitajwa kama mfadhili mkuu wa Kikwete. Je, hii inaleta picha gani?
Mwalimu alionya: ‘CCM imetekwa na wafanyabiashara’. Hili si uzushi. Tunao wabunge, tena wasio na mshipa hata mmoja wa siasa walioko bungeni kutokana ama na pesa zao au za baba zao.
Wapo tena wengine watoto wadogo watokao kwenye familia zenye biashara ya kutia shaka linapokuja suala la kulipa kodi. Kwanini na hawa tusiwatake waachie ngazi mara moja? Je, tutaridhika na ushauri wa maneno usio na vitendo wa rais kuwa wanasiasa waamue kufanya biashara au siasa?
Nasema ni wazo au ushauri wa longo longo kutokana na kilichoripotiwa hivi karibuni kuwa rais ataandamana na wafanyabiashara zaidi ya 60 kwenye ziara yake ya Ujerumani.
Tukirejea kwa Kikwete ambaye chama chake chini ya kampuni ya chama iitwayo Deep Green imehusishwa kwenye ufisadi wa BoT, yeye na chama chake hawana upenyo wa kuepuka kuwajibika.
Leo watu bado wanashangaa ni kwanini rais hatoi ombi rasmi kwa mamlaka za Marekani kumrejesha Gavana wa zamani wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali.
Bahati mbaya kashfa ya BoT, kwa kitambo imemezwa na anguko la Lowassa. Je, si wakati muafaka kwa Bunge na wananchi kwenda mbele na kutaka walioko nyuma ya BoT waletwe mbele ya hadhira na kupata stahili yao?
Je, ni nani hao? Kwanini tusitake kuambiwa gharama za uchaguzi hasa matumizi ya wagombea na jinsi walivyopata hiyo pesa, tukajua la kufanya?
Tuhitimishe kwa kusema wazi kuwa Tanzania ipo njia panda na katikati ya mafisadi na wananchi wenye mapenzi mema na nchi yao.
Je, katika kipute hiki ni nani atafuata kutoka kwenye majeruhi wetu? Japo kila jicho na sikio linataka kusikia na kuona muarobaini wa hali hii, ukweli ni kwamba muarobaini pekee uliopo ni kuwajibishana bila kuangaliana usoni. Je Kikwete na chama chake watanusurika?
Source: Tanzania Daima Februari 13,2008.
No comments:
Post a Comment