Nilicheka na kuhuzunika sana kutokana na ukweli kuwa ni upuuzi, uzushi na kutapatapa kwa CCM kutoa madai ya kitoto kama haya bila aibu.
Nilicheka zaidi niliposoma kuwa CCM inasema mafisadi wafilisiwe! Nilicheka kwa sababu tuendako CCM haiwezi kukwepa kuhusika na ufisadi uliotikisa taifa letu. Kwa mujibu wa taarifa zilizomkariri John Chiligati, Katibu wa Uenezi wa CCM, kamati kuu ya chama eti imetaka wote watakaobainika kuwa waliopora pesa BoT wafilisiwe!
Kwanza ifahamike kuwa CCM inajua kuwa watakaopatikana ni mbuzi wa shughuli na dagaa wachache watakaobeba msalaba wa vigogo wa CCM na serikali.
Mbona vyombo vya habari vimeishafichua njama hii? Rejea habari kubwa ya gazeti la Raia Mwema la Januari 31 kuwa mashahidi watakaojitokeza mbele ya tume ya rais ya kuchunguza kadhia hii wasiwataje vigogo wa chama na serikali.
Hivi CCM inadhani Watanzania wana makengeza kiasi cha kutoona zengwe linalotembezwa?
Nani hajui kuwa kashfa hii inashughulikiwa kinamna namna kwa kutafuta kusukuma muda na kuwahadaa wananchi? Kwanini serikali ya CCM imeshindwa hata kuiomba rasmi Marekani kumrejesha nchini Ballali?
Rejea taarifa ya Balozi Mark Green wa Marekani kwa wanahabari siku chache kabla ya CCM kuja na usanii huu. Mbona rais anapata kigugumizi kuomba Ballali arejeshwe haraka? Badala yake serikali imepata kisingizio kwa kupigia upatu ujio wa Rais George Bush wa Marekani utadhani ndiyo tatizo la nchi!
Nina sababu mahususi kwa hili.
Kwanza, CCM ndiyo inayounda serikali zote tangu uhuru. Ukiondoa serikali ya awamu ya kwanza na kidogo awamu ya pili, serikali zilizobaki ni balaa tupu. Je, hapa CCM itakwepaje kuwajibika na uchafu wa serikali na watendaji wake? Anayebishia hili ajikumbushe kashfa zinazomkabili rais mstaafu, Benjamin Mkapa na marafiki zake huku mwenyekiti wa CCM hii hii akimkingia kifua kuwa hawezi kuchunguzwa.
Tulishasema kinga ya urais inatumiwa vibaya kulinda wezi. Tulishahoji kutochukuliwa hatua kwa Anna Mkapa, Nicholaus Mkapa na Daniel Yona, ambao ni washirika wakuu wa Mkapa. Je, nao walikuwa marais nyuma ya pazia?
Pili, CCM na serikali zake ndiyo iliyoasisi na kuneemesha mfumo mfu wa watawala kujiibia watakavyo.
Hapa napo CCM haiwezi kukwepa lawama na kuwajibika. Hebu rejea kuendelea kufichwa kwa kigogo wa serikali anayejulikana kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond. Rejea kuendelea kulipwa pesa kwa kampuni kama IPTL, Richmond na nyingine nyingi hewa kama Deep Green.
Tatu, CCM kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilidiriki hata kuzuia Bunge kujadili ufisadi wa BoT hadi upinzani uliposimama kidete na kuuibua upya kupitia majukwaani. Kwanini CCM inasahau iliyosema jana? Mbona CCM na serikali, mwanzoni zilizisema: madai ya ufisadi yaliyokuwa yakitolewa na wapinzani ulikuwa umbea na uongo mtupu?
Yaani CCM ilivyotembeza zengwe hadi mhusika mkuu, mbuzi wa kafara Dk. Daudi Ballali, akawaita waandishi wa habari na kuwaambia: "Sina wasi wasi na morali ya kazi iko juu!" CCM mara hii imeishasahau yote haya!
Nne, CCM ndicho chama tajiri barani Afrika kikimiliki mali nyingi isivyo halali, kama viwanja vya wazi vya umma vitumikavyo kama maegesho ya magari ukiachia mbali viwanja vya michezo kama vile CCM- Kirumba.
CCM haiishii hapa, inamiliki miradi iliyojengwa kwa fedha ya umma kama makao makuu Dodoma, Chuo cha CCM Kivukoni na mali nyingine nyingi.
Tano, CCM ndiyo inayotamkwa sana kunufaika na chumo la wizi la Benki Kuu lililotumbukizwa kwenye uchaguzi ghali kwa viwango vyote. Ukitaka kujua ninamaanisha nini hebu jaribu kujumlisha gharama za kununulia kanga, vibandiko, T-shirts, mabango, matangazo, nauli za kuzunguka nchi nzima, pesa ya malazi mahotelini, posho zilizolipwa kwa wajumbe na wapiga kampeni wa CCM nchi nzima, magari na vikorombwezo vingine halafu ulinganishe na pato halali la CCM.
Utapata pesa kubwa kiasi cha kutisha. Hii maana yake ni kwamba ufisadi unaoongelewa ni mkubwa kuliko huu kiduchu tunaopewa.
Hapo bado hatujaangalia mali za vigogo wa serikali wanaoishi kama wafalme kwenye bahari ya umaskini wa kutupwa. Hapa bado hujagusia ile pesa inayotoroshewa nje na wageni wa CCM na serikali zake, yaani kina Chavda, Patel na wengine.
CCM kwa kutoa kauli hii, inaonekana bado ina mawazo kuwa Watanzania ni wajinga wa miaka ya 60, ambapo wangeweza kukaa na kubishania milioni moja ina sufuri ngapi! Imesahau kuwa Watanzania sasa ni mabingwa wa kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya internet kiasi cha kuwa taifa la kwanza duniani kuutumia mtandao kufichua kashfa kubwa ya kifedha kuliko zote nchini!
Sasa tuangalie taarifa kuwa kuna baadhi ya wana CCM safi wenye uchungu na nchi yao wanaotaka mafisadi wote watajwe bila kuangalia sura zao.
Hawa wakishikiria msimamo huu wanaweza kurejesha chama chao kwa wanachama toka mikononi mwa wezi na wasaka ngawira. Kabla ya kifo chake, mwanzilishi wa CCM Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutishia hata kujitoa kwenye chama alichosema si mama yake.
Hii ni baada ya chama kuporwa na wachuuzi wa roho na miili ya watu walioua azimio la Arusha kwa kuanzisha la Zanzibar.
Hadi Nyerere anafariki alikuwa mtu aliyekata tamaa sana. Rejea maneno yake, "Nawaombea Watanzania wangu." Hii licha ya kuwa laana ni kauli ya kukata tamaa. Tunamshukuru Mungu: maneno ya gwiji hili yamedhihirika. Rejea aibu na kihoro vinavyompata rais mstaafu Mkapa ambaye licha ya kumvua nguo Nyerere aliyemuwezesha kuwa rais asijue alikuwa bomu, ameifuja nchi yake na misingi yote aliyoiweka, akaipigania na kuifia.
Na bado. Mkapa anaweza kukwepa kifungo leo, kwa kuwa Kikwete kwa sababu anazozijua mwenyewe amemkingia kifua. Lakini ajue nchi hii si ya Kikwete wala Kikwete hataishi milele akiwa rais wa nchi. Na isitoshe yeye akiponyoka hawa wengine arobaini yao itafika.
Huenda utabiri wa Nyerere kuwa CCM itakuja kufa kama haitaacha kuwakumbatia matajiri kwa kuwatelekeza wanyonge.
Nani haoni wafanyabiashara wachoyo waliojipenyeza kwenye chama na kupata vyeo wanavyoipeleka CCM kuzimu?
Ukitaka kujua hatari hii chunguza ni wabunge wangapi wako bungeni kulinda himaya zao za biashara kwa mgongo wa CCM, ambayo nayo imewapokea na kuwapa madaraka makubwa, isijue nia ni matumbo yao, na si taifa kama ilivyokuwa agenda ya kuanzishwa kwa CCM.
Hivyo wana CCM wenye uchungu na nchi hii wanaweza kushirikiana na upinzani na vyombo vya habari kuwafichua manyang'au waliomo chamani walioshiriki kwenye uchafu wa BoT ili umma uwape adhabu wanayostahili.
Kama alivyosema Mwalimu Nyerere, wasichelee lolote. Kwani CCM si mama zao wala Mungu wao.
Kuna haja ya kuanza kuchimba kaburi la CCM. Maana kaka na dada zake iliozaliwa nao wote wameishakufa kuanzia Ghana, Kenya, Zambia, Malawi, Senegal, Uganda, Nigeria na kwingineko.
Umefika wakati wa ama CCM kuuawa na mafisadi au wana CCM wazalendo na wasafi kuinyakua CCM kutoka kwenye pango la wezi wanaoichuuza yenyewe na watu wake.
Tuhitimishe. Kama CCM inataka mafisadi wafilisiwe, wa kwanza kama haki itatendeka itakuwa CCM yenyewe.
Nihitimishe na kituko. Rais Jakaya Kikwete amekaririwa akiwataka mawaziri na wabunge ama kuchagua biashara au siasa ili kuondoa mgongano wa kimasilahi. Nina maswali madogo. Kwanini angoje wawe matajiri ndipo aseme? Mbona anakataa kutaja mali zake na wenzake? Je, hii nayo ni kamba nyingine? Je, waliokwishaneemeka na jinai hii wafanywe nini na ni wangapi? Je, umefika wakati wa kuinusuru CCM kutoka kwa wafanyabiashara?
Mwisho atatoa lini ombi kwa Marekani kumrudisha Ballali? Na je, ataanza lini kuwashughulikia mafisadi, wala unga, wala rushwa bila kusahau nyumba zetu?
Mungu ibariki Tanzania.
Iepushe na mafisadi, iondoe kwenye mizengwe na usanii.
Source: Tanzania Daima Februari 6, 2008.
No comments:
Post a Comment