Hivyo kikao cha leo ni kwa Beti muuza gongo maarufu. Mtaa sikwambii. Jamaa zetu wapendao dezo na kubughudhi umma wanaweza kututokea likawa zari. Si unawajua wanavyonyenyekea mafisadi na majambazi ilhali wanatuponyoa sie kitu kidogo.
Hivyo maongezi ya leo ni ulevi mtupu. Wanakijiwe wamepigika na kupagawa wanazoza bila kumjali mtu wala nini.
Mgosi akiwa ndiye anayeonekana kuukwaa mma vilivyo hata hivyo mma umempa nguvu ya kutoa mipwenti. "Wagosi, kwa nini tisiandamane kutaka mkuu avunje genge la hasara na ulaji la mawaziii? Mie natamani tife na mtu. Tisiogope kifo maana tiishakufa zamani. Hamioni watu akina Patei wanavyozidi kuchota njuuku BoT huku sisi tikiishia kulewa tu?"
Kabla ya kuendelea anatapika hivyo Mpemba anakula 'mic'. "Yakhe japo pombe haramu leo imenipa nguvu sina nfano! Niko tayari kwenda walipo pamoja na mkuu niwafikishie salamu Wallahi. Sie Pemba tushazoea. Mwaelewa Komandoo alivyotufanyia uhanithi nasi tukantimua."
Mkurupukaji anakurupuka akiwa anapiga mbwewe. Anasema kwa sauti ya ulevi. "Wewe yakhe kujifunza kukamata ulabu unataka tumtimue Chekacheka? Hujui naye ni mlevi kama sisi na Komandoo? Sisi tunalewa matapu tapu wao madaraka na mishiko kama ANBEN Richmond, Tanpower na mauzauza mengine." Kabla ya kuendelea mara anatapika!"
Anacheua. Harufu kali ya ulabu na mapupu vinajaa chumba kizima!
Nani anajali iwapo wote tumelewa kama jamaa zetu wa Idodomya wanaovumilia uoza wa akina Ballaliii na Jitu Patili na wenzao?
Mpemba anaendelea. "Walahi Kaya hii ya majuha tajiri ila wanaokufa kwa ukaapa! Juzi uliosoma walivotumia milioni 150 kwenye kuzomewa? Afu eti Nkuu atutia madole kusema mawizi na wabuge waache biashara ilhali weshachuma! Hii Kaya twaliwa hata kama hatutaki kukubali. Au twaingiliwa na Popo bawa Yarabi."
Mai mai mai! Naona mbwa mwitu kaangusha gari! Anavyokoroma na kutia huruma utadhani wadanganyika mbele ya maisha! Heri yake amelewa ulabu kuliko wadanga waliolewa uongo na mazingaombwe ya akina Kikwekwe na Pateli, Nambari wahedi na majambazi wengine!
Kwanza ngoja nicheke kwa huzuni. Nasikia radio ikitangaza kuwa jamaa yangu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Shoptalk ya vijiwe huru visivyo huru bali udhuru barani! Ama kweli wamejua kutuvisha kilemba cha ukoko.
Sasa ngoja mtasikia walevi watakavyoandama kujipongeza na kumpongeza utadhani uenyekiti wake dili. Sana sana atautumia kukwepa majukumu ya Kaya na anavyopenda safari ndiyo usiseme. Hapa nadhani bi mkubwa ndiyo anasherehekea kupatia nafasi ya kuondolea ushamba. Si unamjua na watu wetu walivyo limbukeni.
Wakati nikijisemea kilevi kumbe mambo yanazidi kuengezeka! Maana mzee Ndomo hangoji mlevi mwingine atie timu kabla yake. "Oya mama Beti, wapi jero yangu? We mama wa kichanaga naona ushanisachi! Nawe ni fisadi kama akina Patel. Hata kama ni mbongo mwenzetu we fisadi. Yaani huna aibu unaibia hata walevi kama mimi! Changamkia tenda BoTii siyo hapa au akina Rema si nduguzo?"
"Oya," Anachumpa Makengeza. "Kaya hii ya walevi. Kama hulewi pesa ya ufisadi utalewa ya udokozi. Kama hulewi ulabu utalewa ukondoo na ujuha. Ilmradi wote ni walevi. Kaya ya walevi kuanzia juu hadi chini kushoto kulia."
Akiwa anahema utadhani anataka kupasuka, Kapende anatia timu. "Nyie mnazungusha kwa woga wenu. Hii ni Kaya ya vibaka na mibaka. Huoni Chinga wetu na mbweha wengine walivyotuibia? Hamuoni Chekacheka alivyoshirikiana naye kiasi cha kuendelea kumlinda yeye na chama lao? Kwani hatujui? Waulize takrima waliyotembeza waliipata wapi kama siyo kukwiba."
Mchunguliaji naye hataki amaliziwe mipwenti. Na nyonde nyonde zake na ulevi anatia timu kiaina. "Wazee hapa mnantafuta Ngosi wa kamba. Kizee sijui kina makengeza ya ubongo! Bila aibu unaweza kukisikia kikipinga kuwa nambari wani siyo majambawazi wakati ni majambawazi watupu kuanzia juu hadi chini! Na kilaaniwe kama Ngumbaru Mwehu""
Kabla ya kuendelea Mzee Kidevu anakula Mic. "Watu wote wamesema, jamaa zangu wa majoho wamenkuna. Wametumbua jipu kuwa ufisadi na siri-kali imo hata ijibaraguze vipi."
"Wamekukuna wapi? Tiambie tiandastandi isiwe kama ya Tunituni na waivonkuna wawekezaji akajiwekeza na mkewe. Au umekunwa na yue kasisi wetu aliyekula nadhii Idodomya ambaye huwadanganya watu eti atawapa utajii wakati naye kapuku?" Alichomekea Machungi.
Kabla ya kukamilisha pwenti yake Mzee Maneno hangoji ujiko uwamwagikie watu wa Bwana. "Hawa nao wanafiki wakubwa. Walikuwa wapi wakati akina Tunituni wanahomola? Au ni kwa vile mkuu siyo miongoni mwa kundi lao? Au wanabembeleze misamaha ya mali wanazoiingiza kwa kumsingizia Mungu huku wengi wakiwaibia watu mchana kwa kuhubiri uganga wa kienyeji kama anayesema Mgosi?"
Kachokoza nyuki! Maana Msomi ambaye inaonekana pombe imemtia kigugumizi anamua kuingia bila taarifa.
"Hapa mzee wangu suala siyo udini. Ufisadi sawa na ukoma hauna dini. Kwanza katika ufisadi tajwa wote walikuwamo kuanzia Tunituni hadi Chekacheka na wote wana dini hata wengine huchangia ujenzi wa nyumba za Mungu.Isitoshe wao humuombea hata Kibaka ilmradi awape nao ulaji. Pia kulindani ni dili lao la kurithishana ulaji. Huoni wanavyolinda na kuapa kufa pamoja. Kama Chekacheka angekuwa ni tofauti na Tunituni asingechukua mizoga yake yote na kuihuisha."
"Hapa tunatembezewa uganga wa kienyeji kote kote. Kwa God wapo. Mapilato ndiyo usiseme. Wale askari wa Kirumi ndiyo hoi kabisa. Hili Kaya la majuha tajiri ambao kama Kenge hukimbia mvua kwa kujizamisha baharini. Ni kama mbuzi aogopaye maji akaoga michanga."
"Mzee umenena hili Kaya makenge watupu." Msomi anaamua kuondoa kigugumizi. Anaendelea, "Umemsikia Chekacheka na upuuzi wake eti jamaa zake wachague siasa au biashara! Hapa kuna siasa au ni biashara ya siasa na siasa za biashara. Yaani kaliona leo baada ya yeye kupata? Kwa nini angoje watu wachume ndipo aamie shamba?"
Anavuta mchupa wake wa gongo na kugida na kuendelea. Huu ni ujambazi. Mbona hataki kutaja mali zake na wenzake akina Richmonduli? Halafu mmesikia nambari zero wanavyotufanya sisi majuha kama wao? Eti ndiyo vinara wa kufichua mafisadi wakati ni wao! Wanasema mafisidi wafilisiwe utadhani wao sio! Waulize: pesa ya takrimu waliipata wapi kama si kwa akina Ballaliii? Wamejengea na wanatanulia nini kama si hiyo? Inaonekana hawa wapuuzi wamelewa kuliko sisi.
Acheni unafiki tuleteeni Ballalii amwage mtama kwa kuku muone kama hamtaumbuka. Na msiishie hapo. Hata huyu habithi anayejificha kwenye maulaji ilhali ndiye Richmond mfichueni na kumfungisha virago kama Ballalii. Tumemchoka tangu enzi za Mchonga aliyemtolea uvivu na kumpulizia laana inayozidi kumuandama. Jamaa ana tamaa utadhani fisi!
Akiwa anajiandaa 'kumwaga razi' mara pombe zilimzidi akaangusha gari. Kustuka; kumbe wote tulikuwa tumeangusha magari kama nyinyi! Tukiwa tunaendelea kuuchapa mara ndata wakatia timu kututoza kodi ya ulevi! Tim nilitimka hata nikashindwa kumalizia kikao na maazimio ya Kaya ya matajiri majuha!
Source: Tanzania Daima, Februari 6, 2008.
No comments:
Post a Comment