How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 27 February 2008

Kijiwe kilivyosherehekea kukaangwa Richimondul

WIKI hii ni ya sherehe mtindo mmoja kwa Kijiwe. Ni wiki ya kupongezana na kuzidi kudurusu jinsi ya kuliendeleza vagi na valangati dhidi ya mafisidi, mabangusilo na marichimondul.

Kwa mara ya kwanza Kijiwe chetu kimekipelekea salamu za pongezi Kijiwe pinzani cha Idodomya kwa kumtolea uvivu na kumkaanga jamaa yetu Richimondul. Tunawataka watuletee Richimondul wote na BoT na si mabangusilo-kafara.

Tunaita nambari wani msalabani badala ya kuiruhusu yenyewe iwasulubu wachache ili inusurike.

Naona wanakijiwe wanaingia kwa nyodo, mashamsham na kila aina ya bashasha.

Mzee mzima leo nimetilia suti yangu niliyonunua duka moja na yule jamaa daktari Mwakiembe. Ni suti ya mapilato.

Naona Mgosi Machungi kanitilia bonge ya tarabushi na darzi kali sana huku chini akinimaliza na tarawanda. Yu mtribu maridadi kweli kweli Msambaa yule. Utadhani Mgosi wa nambari. wani.

Msomi naona ana mabuku na magazeti yote ya wiki akidurusu na kudurusua hili na lile. Ama kweli ni siku adhimu na maalumu!

Macho yote yameelekezwa kwangu mzee mzima kwa kufanikiwa kumnanga na hatimaye kumdedisha.

Mara Mgosi ananichokoza huku akitabasamu.

"Mgoshi naona Richimondul wako ametimuiwa aende zake Mondui. Timeona vitu vyako. Akini nasi azima tijipongeze. Maana Kijiwe kimichangia sana."

Mie sijibu nabaki kutabasamu na kutikisa kichwa nikila maujiko.

Wakati Mgosi akijiandaa kuendelea kulonga mara Mpemba anakwanyua mic.

“Yakhe uliona watu wakikaangana? Wallahi mie naona yule Mwakiembe sijui Mwakinazi siyo CCM ni Kaafu Wallahi huyu! Hata hivyo jipu halijatumbuka yakhe! Maskini nikikumbuka Richimondul alivyoadhirika na kufedhehaka wakati mwingine naona huruma," anasema.

Mbwa ameudhiwa na Mpemba kumhurumia jamaa. Anatuguna mic. “Yakhe na huruma zako! Unamuonea huruma mwizi tena jibaka kubwa! Heri ungewaonea huruma vibaka waliozalishwa na mibaka kama huu. Mie sijaridhika. Nitaridhika nitakapoona mtu lupango, vinginevyo naona kama zengwe tu. Nitaridhika nitakapoona watoa takrima wote wakisulubiwa badala ya haya mauza uza,” anasema.

Kapende anamdandia Mbwa. “Mbwa umenena. Kwanini atoke mmoja badala ya genge lote? Kwani wakati anasuka lile dili alikuwa ametumwa na nani kama si bosi wake? Kwanini atumie kampuni ya yule Mwarabu kama si kumlipa fadhila kwa kumuwezesha bosi wake? Yaani jamaa kajua kuwaweka kimada. Hadi chama!”

Mzee Ndomo naye anaingia bila taarifa. “Ulimwengu tulioambiwa kuja kwa youm kiam, umewadia ambapo simba atazaa mbwa. Alijisemea Mchonga tukamuona mwongo, yako wapi sasa?” Anatema mate chini kwa dharau ya mafisadi na kuendelea.

“Kilichotokea ni watu kuchoka kutumiwa kama ambavyo tumekuwa tukiwaonya. Wengine wanasema walinyimana na kuzidiana kete kwenye mitandao yao ya ulaji. Mradi kila mtu na lake. Ila kikaka kimoja kimedondo si haba.”

Leo ni bandika bandua. Msomi anaamua kuingia hata kabla ya wakati wake kutokana na furaha yake juu ya mkuki wa Richimondul. Anaanza. "Kwanza nikupongeze mzee mzima." Ananigeukia akiwa anatabasamu na kuendelea. “Kwanza muuzaji mmwagie kahawa hadi azimie. Nakupongeza sana kwa cheche zako hasa na usanii wa kuteua jina lililokuwa lina kila jibu. Ulizoea kuiita kashfa ya Richimondul …. Je, ulimaanisha nini?" Ananigeukia tena.

Mpayukaji sijivungi nakatua mic. “Wazee, mimi nilitonywa na wasomaji wangu ambao wengi ni wa usalama na wengine ni wahusika waliotumikishwa na jamaa hawa. Hivyo, nilipokuwa nikiandika Richimondul nilitaka umma uunganishe Richimondul naniino upate jibu lenyewe kama alivyofanya rafiki yangu Daktari son of Kyembe, ambaye alikuwa mwalimu wako Msomi. Simple hilo ndilo nilifanya na alhamdullillahi hatimaye mambo yamejipa. Niwekee kahawa kwanza’"

Msomi anaendelea. “Je, huu ndiyo mwisho au ndiyo mwanzo? Je, hamuoni kuwa jamaa kaamua kubwaga manyanga kuwaokoa wenzake hasa genge lao liitwalo nambari wani? Je, turidhike na usanii huu au tudai zaidi wote wafichuke kuanzia Richmond, IPTL, Green Finance, ANBEN, Tanpower, Fosnik, Mifuko ya Bima, NBC, Air Tanzania, Tanesco, Bandari, TRA, Uhamiaji, BoT na kwingineko."

Kabla ya kumaliza, Mbwa mwitu anadakia. “Du jamaa alivyoyakariri haya madudu utadhani msahafu ama kweli wewe ni msomi na mwanafunzi wa kweli wa Mwakye!”

Msomi kasifiwa na anaonekana wazi kupagawa kiasi cha kuendelea kutoa lecture. “Mie naona ni kama mwanzo wa mwisho wa kugeuzwa kile mzee aitacho nepi na sindano. Je, Lu-washa alikuwa peke yake? Mbona sijasikia tamko kuhusu huyo mmanga wake aliyejichimbia kwenye chama lao?

Mbona sijasikia chanzo au vyanzo vya takrima iliyompa mbawa Chekacheka hadi akapaa na kukwanyua kiti cha ufalme? Tujiulize na kujiuliza na kujiuliza ili kuhakikisha kila jiwe linageuzwa?”

Kabla ya kuendelea Mzee Maneno naye anatia buti. “Nyie hamjui. Mie nilionya maneno ya Mchonga yatakuja kufufuka na kuondoka na mtu mkaniona kama natania. Yako wapi sasa? Huwezi kuufanya umma vipofu wakati una macho tena mawili na hauvai mawani kama wewe. Hapa la msingi ni kwa wasomi kugeuka na kuanza kutumia usomi kama daktari Kyembe kusaidia nchi kutoka kwenye ufisadi."

Msomi anaendelea. “You’re very right mzee wangu. Kimsingi sisi wasomi ndiyo tatizo. Lakini siyo wote. Ni wale waliosoma wakashindwa kuelimika. Ni wale wanaotumia makamasi kufikiri badala ya ubongo.

Mie nikipata hata ukuu wa wilaya mshahara na marupurupu yake yanatosha. Nani atakufa na pesa zaidi ya aibu kama jamaa yetu? Bado sasa watoto wao waliojazana pale BoTii. Nao tutawafungashia virago siku si nyingi.

Mie naona wingu analitia Chekacheka kwa kutatua matatizo nusu nusu. We muache naye tutamchenjia kama alivyosema Arawa shauri yake. Tungoje tuone wa kupinda pinda naye atatupindisha au kutunyoosha vipi."

Kabla ya Msomi kuendelea mara Makengeza ndiyo anaingia. Hasalimii bali anaanza kutoa stori za jana. "Wazee jana mtaani hatukulala. Tulikuwa tukisherehekea kuanguka kwa Richmonduli wa mzee. Tulikunywa na kula kufuru. Maana kumbe watu wanakulimbika ukiwa unafanya vitu vyako. Sikujua kuwa watu walikuwa wanamchukia jamaa hivyo! Kwanza niwape stori toka redio mbao. Ni kwamba atateuliwa waziri mkuu kutoka usalama wa taifa ingawa nao si usalama chochote."

Kabla ya kuendelea, Msomi anadakia. “Je, ni jibu:walikuwa wapi wakati mambo yanaharibika? Mie sioni usalama bali uhasara sawa na TAKULA ya daktari fulani anayetuhumiwa kuwa swahiba wa Jamaa. Naye sijui anangoja nini? Watu wote wanaweza kujidanganya na kujipa moyo sijui rafiki yangu Enderea Chenga kweli atanusirika mara hii? Hata Miramba, Meng-ji, M7ha Bangusilo, Msulwa, Kingungo, Wakupuya, Ngasongora na wengine nao lazima watimke. Mie naona kutimua siyo jibu. Wapelekwe mbele ya sheria ili haki itendeke.

Ukiachia Richimondul, wapi majumba yetu? Wapi wala rushwa na wauza unga? Wapi wapi wapi? Hapa ndipo Chekacheka anacheza kama paa. Ameufungulia uji wa moto bombani lazima umuunguze naye kwa uzembe na kulindana kwake."

Anachukua kombe lake la kahawa na kulibusu na kuendelea. "Ingawa huwa tunawabeza kijiwe cha Idodomya, leo nawapa heko kwa kuachana na unepi na utaulo. Vichwa vimeshinda matumbo. Walikuwa wanatia kinyaa kugeuzwa nyumba ndogo ya mafisadi.

Tuwashinikize washikilie hapo hapo kudai wahusika wote wafilisiwe, wakamatwe na kufungwa. This is the answer vinginevyo tunapotezeana muda. Hapa ni wanakijiwe kuachana na sherehe za kina Makengeza na kusimama kidete kutumia fursa hii adhimu na adimu vinginevyo watapozwa na libeneke itaendelezwa. Wazee mmeona kiroja cha Mwajabu kukosa adabu? Eti na Enderea Chenga amerejeshwa kwenye kigwena. Hivyo huyu jamaa ana matatizo gani au ndiyo la kufa?”

Akiwa anajiandaa kutwanga manyundo mara tuliona gari Jei Wi likielekea Dawasco kutoa dispilini ya uonevu. Tulidhani wanatuijia sisi hivyo tulitimka kila mtu kivyake! Na hili gesi lisipodhibitiwa linaanza ufisadi mwingine wa kutupiga piga utadhani tu ngoma.

Source: Tanzania Daima Feb. 27, 2008.


mpayukaji@yahoo.com

No comments: